Thursday, February 15, 2024

RAIS SAMIA AWATAKA DIASPORA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUITANGAZA TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehamasisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi yaa Diaspora kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuitangaza nchi kwenye maeneo waliyopo ili kuvutia watalii, wawekezaji na wafanyabishara kwa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.

 

Mhe. Rais Samia ametoa wito huo kwenye Mkutano wake na Watanzania waishio Norway na nchi nyingine za jirani uliofanyika hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kitaifa nchini humo.

 

Mhe. Samia amesema Serikali inatambua na kutahamini mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa na kuwahimiza kuendelea kuitangaza nchi kwa kusema yale mazuri yanayopatikana nchini ikiwemo vivutio vya utalii na fursa za biashara na uwekezaji.

 

Pia amewahimiza Diaspora hao kuendelea kuweka akiba nyumbani, kufundisha watoto wao mila na desturi nzuri za Tanzania ikiwemo Lugha ya Kiswahili, kupendana na kushirikiana na kufuata sheria na taratibu za nchi walizopo ili kujiepusha na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwasababishia matatizo wao binafsi na kuiabisha nchi.

 

Akizungumzia hali ya siasa na uchumi nchini, Mhe. Rais Samia amewaeleza Diaspora hao kuwa, hali ya uchumi ni nzuri na inaendelea kuimarika baada ya kushuka katika kipindi cha janga la ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo kwa sasa uchumi umekua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4 miaka mitatu iliyopita na unatarajiwa kukua hadi asilimia 6.5 ifikapo mwaka 2027.

 

“Tunaendelea na jitihada mbalimbali za kukuza uchumi wetu hata ziara yangu nchini Norway ni kati ya jitihada hizo za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Tanzania inapiga hatua katika maendeleo na tayai imetajwa na Shirika la Fedha la Kimataifa kuwa ni kati ya Nchi 20 zinazokua vizuri kiuchumi duniani” amesema Mhe. Rais Samia.

 

Kuhusu siasa, Mhe. Rais Samia amesema kuwa hali nchini ni shwari ambapo vyama vyote vya siasa vinaendelea na shughuli zao za kichama kwa uhuru na nchi ina amani na utulivu.

 

Kuhusu ajira,   Mhe. Rais Samia amesema bado ni tatizo hata hivyo Serikali yake imeendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuwasaidia vijana na wanawake wa mijini na vijijini ili kuwawezesha kujiajiri na kujipatia kipato kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo biashara ndogondogo.

 

Amesema, kwa upande wa mijini, Serikali imeendelea kuwajengea masoko bora vijana ambao wengi wanajishughulisha na biashara ndogondogo maarufu kama machinga,  kuwatafutia mfuko wa kupata mitaji na kuanzisha taasisi yao ambayo inafanya vizuri na hata wameweza kuanzisha gazeti na Televisheni yao.

 

Kuhusu vijana wa vijijini, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imeanzisha program inayoitwa Jenga Kesho Bora (BBT) ambayo imejikita kuwwezesha vijana hao katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji. Amesema tayari kundi la kwanza la zaidi ya vijana 800 wamepewa Ekari 10 kila mmoja yenye miundombinu ya umwagiliaji na kuwakopesha mitaji na ruzuku kwa ajili ya pembejeo za kilimo.

 

Kuhusu sekta ya elimu na afya nchini, Mhe. Rais Samia amewaeleza Diaspora hao kuwa, hali ni nzuri ambapo kwa sasa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi kidato cha sita wanasoma bure huku Serikali pia ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi.

 

Akizungumzia Hadhi Maalum, Mhe. Rais Samia amesema anatambua umuhimu wake kwa Diaspora na kwamba  Serikali inafanyia kazi baadhi ya taratibu za kisheria kwenye masuala ya ardhi na uhamiaji ili kukamilisha suala hilo.

 

Awali akizungumza, Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden anayewakilisha pia  Nchi za Scandinavia na Baltic, Mhe. Grace Olotu amesema Diaspora katika eneo lake la uwakilishi wapo 3,973 ambapo kwa upande wa Norway ni Diaspora 1,407, Sweden 1,815, Denmark 1,001, Finland, 725, Iceland 11, Estonia 11 na Ukraine 4. Diaspora hao wamegawanyika katika makundi ya wafanyabiashara, wafanyakazi na wanafunzi.

 

Kwa upande wao Diaspora ambao waliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi, Bi. Margaret Adaa wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada mbalimbali anazozifanya nchini katika kujenga umoja na mshikamano nchini na kuinua uchumi kwa kuitangaza nchi kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Jumuiya ya Diaspora wa Tanzania wanaoishi Norway alipokutana nao wakati wa ziara yake ya kitaifa ya siku tatu nchini humo kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari 2024

Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe, Grace Olotu akizungumza wakati wa mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora

Mwakilishi wa Diaspora na Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano kati ya Mhe. Rais Samia na Diaspora akisoma risala ya Jumuiya ya Diaspora mbele ya Mhe. Rais Samia (hayupo pichani)
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya viongozi wa Serikali wakishiriki Mkutano wa Mhe. Rais  Samia na Diaspora. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Mhe. Selemani Jafo na kulia ni Katibu wa Rais, Bw. Waziri
Mhe. Balozi Olotu akiwana Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (kushoto)
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya Viongozi kutoka Serikalini walioshiriki mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diapora wa Norway.
Sehemu ya ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki mkutano wa Mhe. Rais na Samia na Diaspora. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bw. Justine Kisoka akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani, Balozi Swahiba Mndeme na Mkurugezni wa Idara ya Sheria, Dkt. Kweka

Mkurugezni wa Idara ya Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akishiriki mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu nyingine ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu nyingine ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Norway wakishiriki mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora
Sehemu ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Sehemu nyingine ya Diaspora walioshiriki Mkutano na Mhe. Rais Samia
Mhe. Rais Samia akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wake na Diaspora nchini Norway
Mhe. Rais Samia akiwa katika picha ya pamoja na wajukuu ambao ni watoto wa wana Diaspora walioshiriki mkutano wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi akimkabidhi zawadi Mhe. Rais Samia kwa kutambua mchangio wake katika maendeleo ya kiuchumi nchini

Mhe. Rais Samia akipokea zawadi ya jezi namba 10 kutoka kwa kiongozi wa Timu ya Diaspora ya Kilimanjaro FF kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini

Kikundi cha burudani kinachojiita Wamasai wa Norway kikitumbuiza wakati wa mkutano wa Mhe. Rais Samia na Diaspora.
















 

Wednesday, February 14, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO NA MAONESHO YA 11 YA PETROLI AFRIKA MASHARIKI

Viongozi wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC (walioketi) wakisaini  taarifa ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 14 Februari 2024. Waliosimama ni Watendaji mbalimbali kutoka nchi wanachama wakishuhudia zoezi hilo.

Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeipitisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Machi 2025.

Mbali na hayo mkutano huo umepitisha bajeti ya kiasi cha Dola za Marekani 1,842,467 kwa ajili ya maandalizi ya kongamano na maonesho hayo.

Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya, na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia. 

Katika hatua nyingine mkutano huo umetoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya na watu wake.


Aidha, katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye pia ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar umependekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji.

Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara ameeleza kuwa Jumuiya itaweza kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na biashara endapo, pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikana wa nishati ya uhakika na salama. 


“Sekta ya Nishati ina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya. Hivyo umuhimu wa upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama na gharama nafuu ni jambo la lazima na sio la hiyari kwani ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji na kufanya bidhaa na huduma zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la ndani na kimataifa”. Alieleza Waziri Kaduara


Vilevile Mhe. Kaduara alitumia fursa ya mkutano huo kutoa mwaliko kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuja nchini, kushuhudia na kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Maji wa Bwawa la Julius Nyerere, unaotarajia kuzalisha Megawatts 2115 utakaofanyika tarehe 25 Februari 2024.


Mkutano huo wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika kwa siku tatu kuanzia 12-14 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, ulitanguliwa na Mkutano wa Wataalam na Makatibu Wakuu.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye akifurahia jambo wakati akiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Viongozi na Watendaji wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumazika kwa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 14 Februari 2024, jijini Arusha.
Meza Kuu wakiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya ujumbe kutoka Nchi Wanachama wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha

ASKOFU DKT. MALASUSA AONGOZA IBADA YA KUMUAGA LOWASSA

 

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa ameongoza ibada ya kumuaga Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam tarehe 14 Februari, 2024.

Akihubiri katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi Dkt. Malasusa ameeleza kuwa Hayati Lowassa pamoja na familia yake walipenda sana ibada katika maisha yao ya kila siku.

"Kuleta mwili wa mtu asiyependa ibada Kanisani ni kuutesa mwili wa mhusika na hivyo Hayati Lowassa amestahili kuletwa hapa kwakuwa ni sehemu aliyokuwa ameipenda kuja" alisema Dkt. Malasusa

Pia ameeleza ni muhimu kwa viongozi wenye wafuasi nyuma yao kuwa na utaratibu wa kusikiliza neno la Mungu kwa ajili ya kuendelea kuongoza watu wao vizuri na kuleta tija katika yale waliyopewa nafasi ya kuyasimamia.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Sinde Warioba, Waziri Ofisi ya Rais- Kazi Maalum, Mhe. George Mkuchika, Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene,  Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonaz, Kaimu Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu Tatu, Mama Anna Mkapa, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mama Esther Sumaye, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Viongozi wengine Waandamizi wa Serikali na  Kanisa.







 

RAIS SAMIA AINISHA MAENEO MUHIMU YA UWEKEZAJI NCHINI KWA WAWEKEZAJI WA NORWAY

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza nchini kwenye sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi na kukuza uchumi wa nchi ikiwemo nishati mbadala, kilimo, gesi na mafuta, mifuko ya uwekezaji na usafirishaji.


Mhe. Rais Samia ametoa wito huo alipohutubia Wajumbe walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway liliofanyika jijini Oslo, tarehe 13 Februari 2024


Mhe. Dkt. Samia ambaye aliongozana na Mwana Mfalme wa Norway Haakon kwenye Kongamano hilo amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wenye nia thabiti kuja kuwekeza  mitaji yao nchini  kwenye sekta  ambazo kwa kiasi kikubwa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama vile chakula, umeme, mafuta na usafirishaji.


Amesema Tanzania ni sehemu salama kwa wawekezaji kutoka Norway kuwekeza mitaji yao kwakuwa Serikali imeboresha sheria mbalimbali za uwekezaji na kwamba kijografia Tanzania inafikika kwa urahisi na inapakana na nchi nane ambazo ni soko kubwa kwa wawekezaji na pia Tanzania ni nchi ya amani inayoamini katika usawa na utawala wa sheria.

Akizungumzia kilimo, Mhe. Rais Samia amewaeleza wawekezaji hao kwamba  bado sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania haijatumika ipasavyo kwenye sekta ya kilimo ambapo zipo Hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo na kati ya hizo Hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji 

Ameongeza kuwa, Tanzania ni nchi ya 10 duniani kwa uzalishaji wa zao la Alizeti na ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa zao hilo ambalo bidhaa zake ikiwemo mafuta zinahitajika kwa wingi nchini na nchi jirani.

Kuhusu nishati mbadala, Mhe. Rais Samia amewahamasisha wawekezaji hao kuchangamkia fursa za umeme wa jua na upepo kwani bado Tanzania inahitaji kuwa na uhakika wa upatikaji wa nishati mbalimbali ikiwemo umeme wa uhakika.


Awali akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuhamasisha wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi na namna ambavyo ameendelea kutambua mchango wa sekta binafsi kwenye uchumi na maendeleo ya nchi.


Mhe. Rais Samia yuko katika ziara ya kitaifa ya  siku tatu nchini Norway,  amefuatana na Mawaziri mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nci, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Fedha, Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi mbalimbali.

Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya Wawekezaji na Wafanyabiashara 150 kutoka Norway na Tanzania. 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika jijini Oslo. Mhe. Rais Samia yupo nchini Norway kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari 2024 kwa mwaliko wa Mfalme wa Norway Herald V.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway lililofanyika Oslo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu
Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa Kongamano hilo.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Jan Christian Vestre naye akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway
Kongamano likiendelea
Mhe. Rais Samia akizungumza kwenye Majadiliano ya Ngazi ya Juu kuhusu  Usawa wa Kijinsia na Siasa katika Biashara wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway
Mshauri wa Rais, Siasa na Uhusiano na Jamii, Mhe. William Lukuvi nae akishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji jijini Oslo. Wengine ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Gift Kweka (aliyesuka nywele)


Mratibu wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga akifuatilia Kongamano hilo
Mhe. Balozi Grace Olotu akishiriki Kongamano hilo na wajumbe wengine kutoka Norway
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi. Latifa M.Khamis akishiriki Kongamano hilo
Sehemu ya Washiriki kutoka Tanzania
Afisa Mambo ya Nje Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Bw. Magabilo Murobi akishiriki Kongamano hilo
Sehemu ya ujumbe kutoka Norway wakishiriki Kongamano