Sunday, June 16, 2024

DKT. MPANGO AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MAZISHI YA KITAIFA YA MAKAMU WA RAIS WA MALAWI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Hayati Dkt. Saulos Klaus Chilima. Ibada ya Mazishi hayo imefanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi leo Jumapili tarehe 16 Juni 2024.

Akitoa salamu za rambirambi, Dkt. Mpango amesema Tanzania inatoa salamu za pole na kuungana na waombolezaji wote walioguswa na musiba katika kipindi hiki kigumu.

Dkt. Mpango amesema Hayati Dkt. Chilima alikuwa kiongozi imara, mwanamajumui wa kweli wa Afrika ambaye wakati wote alitanguliza mbele masilahi ya wananchi anaowaongoza na Afrika kwa ujumla.

Ametoa wito kwa wananchi wa Malawi na Afrika kwa ujumla kuenzi mambo ambayo Hayati Dkt. Chilima aliyaamini na kiyasimamia. 

Katika safari hiyo Dkt. Mpango ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.), pamoja na Balozi wa Tanzania, Mhe. Agnes Richard Kayola.

Hayati Dkt. Chilima alifariki dunia katika ajali ya ndege na watu wengine nane iliyotokea tarehe 10 Juni 2024 kutokana na hali mbaya ya hewa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akitoa heshima kwenye jeneza la mwili wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Hayati Dkt. Saulos Klaus Chilima, katika Ibada ya Mazishi iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu jijini Lilongwe, Malawi tarehe 16 Juni 2024.








Saturday, June 15, 2024

NAIBU KATIBU MKUU MAMBIO YA NJE ATOA SALAMU ZA POLE KWA FAMILIA YA MAREHEMU DKT. SHOGO


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ameungana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kutoa salamu za pole kwa familia ya aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Marehemu Dkt. Shogo Mlozi tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa familia ya Marehemu Dkt. Shogo Mlozi  tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa familia ya Marehemu Dkt. Shogo Mlozi  tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.

Balozi Mussa na Mhe. Kawawa wakimfariji Prof. Eliamani Sedoyoka ambaye ni mume wa aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Marehemu Dkt. Shogo Mlozi.

Balozi Mussa na Mhe. Kawawa wakitoa faraja kwa wazazi wa marehemu.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama walipoungana na waombolezaji wengine katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Marehemu Dkt. Shogo Mlozi tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.

 

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA YATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imefanya ziara jijini Arusha leo tarehe 15 Juni, 2024 ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.


Baada ya kuwasili Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Vita Kawawa aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa walipokelewa na  Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Modibo Sacko.


Kufuatia umuhimu wa ziara hiyo kamati ilianza ziara kwa kufanya kikao na menejimenti ya Mahakama kilichoongozwa na Mhe. Jaji Sacko akiwa na mwenyekiti mwenza Mhe. Vita Kawawa.


Akiongea katika kikao hicho Mhe. Jaji Modibo Sacko ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kuendelea kuipigania Bungeni Mahakama hiyo hususan katika kupata fedha za Maendeleo zinazowezesha kuendelea kwa ujenzi na kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.


Naye Naibu Katibu Mkuu Mambo ya Nje, Balozi Mussa ameipongeza Mahakama kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia Haki za Watu kila inapotakiwa kufanya hivyo kulingana na itifaki ya uanzishwaji wake.


"Kamati imefanya ziara ili kujionea hatua iliyofikiwa katika ujenzi na pia tunashukuru kwa kuwa na kamati imara katika usimamizi wa majukumu hivyo, niwaondoe hofu kuwa Wizara itaendelea kusimamia ujenzi unaoendelea pamoja na kuzingatia thamani ya fedha," alisema Balozi Mussa .


Akiwasilisha salamu za  shukrani Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Kawawa ameeleza kuwa Kamati yake inatambua umuhimu na majukumu makubwa yanayolotekelezwa na Mahakama hiyo katika kuimarisha haki barani Afrika, hivyo Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.


Mara ya mwisho Kamati ya Mambo ya Nje, ulinzi na Usalama kutembelea ujenzi wa mradi wa Mahakama hiyo ilikuwa mwezi Machi, 2023. Hata hivyo, wabunge hao kwa umoja wao wametoa pongezi kwa hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa na kusisitiza usimamizi makini.


Mradi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ulianza ujenzi mwezi Agosti, 2023 na unatarajiwa kumalizika mwezi Februari, 2025 na utagharimu takriban shilingi za Kitanzania Millioni 22.97.

======================================

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kamati yake na menejimenti ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu wakati walipofanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama hiyo tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.
Naibu Katibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akieleza nia ya dhati ya Wizara ya kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaoendelea jijini Arusha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara katika Mahakama hiyo tarehe 15 Juni, 2024 jijini Arusha.

Makamu wa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Jaji Modibo Sacko akiishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara katika Mahakama hiyo jijini Arusha tarehe 15 Juni, 2024.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi John Kiswaga akiwasilisha taarifa ya hali ya utekekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Mahakama katika kikao hicho.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakipata ufafanuzi kutoka kwa msiamamizi wa ujenzi wa mradi huo.

Mhe. Kawawa akitoa ufafanuzi kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Mahakama baada ya kukamilisha kupata taarifa ya hali ya utekelezaji wa mradi huo.

Mhe. Jaji Sacko akimvisha Mhe. Kawawa nembo ya Mahakama hiyo ikiwa ni ishara ya shukrani kwa mchango mkubwa unaotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama hiyo.
Mhe. Jaji Sacko akimvisha Balozi Said Shaib Mussa nembo ya Mahakama hiyo ikiwa ishara ya shukrani kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kufanikisha majukumu ya Mahakama hiyo.


Picha ya Pamoja





Friday, June 14, 2024

MAKATIBU WAKUU WA EAC WAFANYA MASHAURIANO KUHUSU UANZISHWAJI WA VITUO VYA UMAHIRI

Makatibu Wakuu wa sekta ya afya kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana leo, tarehe 14 Juni, 2024, jijini Arusha kwa kikao cha mashauriano.


Kikao hicho ni maandalizi ya Mkutano wa 7 wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri, unaotarajiwa kuitishwa katika tarehe itakayopangwa baada ya kukamilika kwa mashauriano hayo. 


Mashauriano haya yanafanyika kufuatia wasilisho la pendekezo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuanzisha vituo vya umahiri, ambavyo ni Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.


Akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ameeleza kuwa kuanzishwa kwa vituo hivyo vya kikanda kutasaidia kuinua uwezo katika matibabu ya kibingwa, mafunzo ya kibobezi, utafiti, na utoaji wa huduma maalum za afya.


Aidha, amefafanua kuwa kuanzishwa kwa vituo hivyo ni ushahidi wa nia ya dhati ya kukuza ushirikiano wa kikanda, hususan katika masuala ya afya na elimu. Vilevile, vituo hivyo vitatumika kama maeneo ya kukuza ubunifu, vipaji, na utaalamu wa kikanda na katika maeneo mengine.


Naye Mwenyekiti wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Afya wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Dkt. Ader Macar Aclek ambaye alishiriki mashauriano kwa njia ya mtandao ameipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kufanikisha kuwasilisha andiko dhana la kuanzishwa kwa vituo vya umahiri. Pia, ameonyesha umuhimu wa kushirikiana katika kupambana na changamoto za kidunia, hususan mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakileta mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayohitaji jitihada za pamoja kukabiliana nayo.


Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu, Sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitumia wasaa huo wa ufunguzi wa kikao kuwaeleza wajumbe kuwa ana matumaini majadiliano ya kikao hicho yatafanyika kwa tija na masilahi mapana ya kikanda. 


Kadhalika, alishauri kuwa ni vyema Nchi Wanachama zikatoa ushirikiano katika uanzishwaji wa vituo hivyo vipya ili viweze kufikia malengo ya utendaji yanayotarajiwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazoendelea kikanda na ulimwenguni kwa ujumla.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu wa Makatibu Wakuu umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe, pamoja na maafisa waandamizi kutoka wizara na taasisi za afya na elimu nchini.

[18:15, 14/06/2024] Judith Ngoda: The EAC Permanent Secretaries held a consultative meeting at the EAC HQs in Arusha. The main agenda of the discussion was the considerations of the concept note for the two proposed  EAC Regional Centers of Excellence to be hosted by the United Republic of Tanzania.

===============================

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe akiwasilisha hotuba ya ufunguzi katika kikao cha Mashauriano cha Makatibu Wakuu kilichofanyika jijini Arusha, tarehe 14 Juni, 2024.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akifuatilia majadiliano katika kikao cha Makatibu Wakuu.


Kutoka kushoto Mwenyekiti wa kikao wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Rut ambaye Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka na Mkuu wa Idara ya Afya katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Eric Nzeyimana wakiongoza majadiliano ya kikao hicho.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe (kulia) na Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya Shirikishi cha  Muhimbili, Prof. Bruno Sunguya  wakifuatilia majadiliano ya kikao.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano.

Ujumbe wa Tanzania.


Thursday, June 13, 2024

WAATALAM WA SEKTA YA AFYA KUTOKA NCHI ZA EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Wataalam wa sekta ya afya kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika kikao cha maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika kesho tarehe 14 Juni, 2024 na kutanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu.

 

Mkutano huu wa wataalamu pamoja na masuala mengine utapitia na kujadili  pendekezo la Tanzania la kuanzisha vituo  viwili vya umahiri ambavyo ni: Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

 

Akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka ameeleza kuwa kupitia mkutano huu wajumbe watachangia na kushauri juu ya umuhimu wa vituo hivyo viwili vya umahiri ambavyo vinachangia utoaji wa huduma za kibingwa za afya pamoja na mafunzo katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Naye Mwenyekiti wa mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Dut katika hotuba yake ya ufunguzi ameeleza kuwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 kumeleta somo katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan katika suala la kujijengea uwezo wa kujitegemea katika masuala ya huduma za afya, uanzishaji wa programu saidizi na uimarishwaji wa miundombinu katika sekta hiyo.

 

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka ambaye ameambatana na Wataalamu Waandamizi kutoka sekta ya Afya na Elimu.

 

Katika hotuba yake ya ufunguzi Mhandisi amesisitiza umuhimu wa mkutano huo, akibainisha kuwa andiko dhana ya kuanzisha vituo vya umahiri vilivyopendekezwa na Tanzania vitaleta mabadiliko muhimu katika mifumo ya afya, huduma za kibingwa, mafunzo, na kujengea uwezo.

 

Pia, amewahimiza wajumbe kujadili na kushiriki katika mijadala ya wazi na yenye kujenga ili kuboresha afya kwa ustawi wa watu wa EAC, huku akitoa shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika kuandaa maandiko haya ya dhana.

============================================

Mwenyekiti wa Mkutano wa Wataalam kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhandisi Ring Rut (wa pili kushoto) akifungua Mkutano Ngazi ya Wataalamu kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Saba (7) wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya utakaofanyika tarehe 14 Juni, 2024 jijini Arusha. Kulia kwake ni: Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka, Mkuu wa Idara ya Afya kutoka kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Eric Nzeyimana na kushoto ni Mnukuu (Rapportuer) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Dkt. Dieumerci Kaseso.
Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka (kati) akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano Ngazi ya Wataalam unaofanyika tarehe 13 Juni, 2024 jijini Arusha.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akitoa neno la ufunguzi katika Mkutano Ngazi wa Wataalam unaofanyika jijini Arusha tarehe 13 Juni, 2024.
Ujumbe kutoka Tanzania

Ujumbe kutoka Uganda

Ujumbe kutoka Tanzania

Sehemu nyingine ya Ujumbe kutoka Tanzania


Picha ya pamoja

 

Monday, June 10, 2024

BALOZI MUSSA AWAASA VIJANA KUWA MABALOZI WAZURI NJE YA NCHI


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amewaasa vijana waliochaguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana maarufu kwa jina la “Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders” kuwa mabalozi wazuri katika mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 18 Juni, 2024 jijini Washington, Marekani.

Nasaha hizo zimetolewa katika hafla fupi ya kuwaaga vijana hao 26 ambayo ilihusisha makabidhiano ya bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni ishara ya kuitangaza na kuiwakilisha nchi katika heshima inayostahili iliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mtumba, Dodoma tarehe 10 Juni, 2024.

Balozi Mussa aliwapongeza vijana hao kwa kuonesha uwezo na jitihada binafsi kuchukua nafasi ya kuomba na kufanikiwa kupita katika mchujo wa vijana wengi walioihitaji fursa hiyo. Hivyo, ni wema wakazingatia mafunzo na kuhakikisha ujuzi na elimu watakayoipata inaleta manufaa kwao na kuwajengea uwezo vijana wengine waliopo nchini.

"Hii ni programu maalum ambayo itawajengea uwezo katika masuala ya uongozi hususani, uongozi katika masuala ya usimamizi wa umma, uongozi katika usimamizi wa biashara na uongozi katika masuala ya ushirikishwaji wa jamii yakiwa ni maeneo mtambuka katika ukuaji wa nchi za Afrika.” alisema Balozi Mussa.

Pia akawaeleza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za nchi husika pamoja na kujikita katika malengo yanayowapeleka nchini Marekani ili kufanikisha kutumia fursa hiyo kujenga uwezo katika maoneo yao husika ya kiutendaji sambamba na kuijengea nchi sifa nzuri.

Aidha, amewasisitiza kuzingatia tamaduni na mila za kitanzania wawapo nchini humo kwakuwa mafunzo hayo yanahusisha mataifa tofauti hivyo ni vema kuepuka changamoto mbalimbalii za kimaadili zinazoweza kuwaharibia sifa binafsi na taifa kwa ujumla. Vilevile, katika hilo akasisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi za ubalozi zilizopo jijini Washington.

Nao vijana wanaoenda kushiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendeleza kuimarisha ushirikiano mzuri na Serikali ya Marekani na hivyo kuwawezesha kushiriki kwa wingi katika mafunzo hayo ambayo pamoja na masuala mengine yatawajengea na kukuza uwezo katika teknolojia inayopatikana katika taifa hilo kubwa lililopiga hatua kimaendeleo sambamba na kukutana na wadau katika sekta husika.

Programu hii inatarajiwa kutimiza miaka 10 tangu ianzishwe mwaka 2014 ambapo imekuwa ikitoa mafunzo kwa washiriki kwa njia ya vitendo na kuingia darasani na hivyo, kuwawezesha kushiriki katika majukumu ya kijamii pamoja na kufanya ziara katika ofisi mbalimbali za umma na mashirika nchini Marekani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisisitiza jambo alipokuwa akiwaaga washiriki wa programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana(Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program)yatakayofanyika nchini Marekani.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwa katika mazungumzo na vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akikabidhi Bendera ya Taifa kwa vijana waliochanguliwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa vijana (Mandela Washington Fellowship for Young African Leaders is the flagship program) kwenye hafla fupi ya kuwaaga vijana hao iliyofanyika Mtumba, jijini Dodoma.
Picha ya pamoja. 

KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KIKAO CHA SADC MASUALA YA SIASA NA DIPLOMASIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024.


Akifungua kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ngazi ya Makatibu Wakuu , Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia,  Bi. Etambuyu Gundersen aliwataka wajumbe kujadili na kutoa mapendekezo katika agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ili hatimaye mapendekezo hayo yawasilishwe kwenye kikao cha Mawaziri kitakachofanyika mwezi Julai 2024 kwa ajili ya kuridhiwa.

 

Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Balozi Shelukindo amezishukuru na kuzipongeza Nchi Wanachama wa SADC kwa kufanikisha uundwaji na uzinduzi wa Sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliofanyika mwezi Februari 2024 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

 

Amesema  uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa  ya wakuu wa nchi  wa Afrika  ulidhihirisha namna ambavyo  wanaenzi mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Mwalimu Nyerere kwenye Ukombozi wa  Nchi za Kusini mwa Afrika.

 

Kadhalika amesema  Tanzania inaendelea na mawasilianao ya ndani ili kukamilisha Mpango  wa Taifa  wa Utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 1325 kuhusu kuwawezesha Wanawake kushiriki  katika juhudi  za  kutatua, kuzuia na kudhibiti migogoro duniani huku akizipongeza nchi zilizokamilisha Mpango huo ikiwemo Zimbawe na Madagascar.

 

Vilevile, ametumia fursa hiyo kuzipongeza Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Madagascar kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika kwenye nchi hizo kwa amani na utulivu  tarehe 29 Mei 2024 mtawalia.

 

Amesema, kikanda uchaguzi katika nchi hizi mbili umeakisi viwango vya kimataifa vya demokrasia pamoja na kanuni na miongozo ya SADC kuhusu uchaguzi unaofuata misingi ya demokrasia.

 

Kikao hicho ambacho kimefanyika kwa ajili ya kuandaa mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2024,  kimehudhuriwa na Nchi za Tanzania, Lesotho, Eswatini, Botswana, Angola, Namibia, Afrika Kusini, Shelisheli ,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Zimbabwe.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024
Katibu Mkuu, Balozi Shelukindo akichangia hoja wakati wa Kikao cha Pamoja cha Kamati Ndogo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu masuala ya Siasa na Diplomasia kilichofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 Juni 2024. Kulia ni Afisa Mambo ya Nje anayeshughulikia Dawati la SADC, Bi. Shazma Msuya akinukuu taarifa ya kikao hicho. 

 
Kikao kikiendelea