Thursday, February 27, 2014

Matukio mbalimbali ya ziara ya Mhe. Membe nchini China


...Mhe. Membe alipokutana na Makamu wa Rais wa China mjini Beijing
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Li Yuanchao alipokutana nae kwa mazungumzo kwenye Jumba la Mikutano la Kitaifa la China maarufu kama People's Great Hall mjini Beijing, China. Mhe. Membe yupo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tano kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari, 2014.
Mhe. Membe na Mhe. Yuanchao wakiendelea na mazungumzo.
Mhe. Membe akiagana na Mhe. Yuanchao mara baada ya mazungumzo yao.


....Mhe. Membe alipokutana na Makamu Waziri wa Usalama wa Raia wa China



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa katika mazungumzo na Mhe. Wang Hanning, Makamu Waziri wa Usalama wa Raia wa Jamhuri ya Watu wa China alipokutana nae mjini Beijing wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Membe nchini China tarehe 26 Februari, 2014.
Mhe. Membe akiendelea na mazungumzo na Mhe. Hanning huku Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Abdulrahman Shimbo (kulia kwa Mhe. Membe) na wajumbe waliofuatana na Mhe. Hanning wakisikiliza.

.....Mhe. Membe alipokutana na Makamu Waziri wa Biashara wa China

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akisalimiana na Mhe. Li Jinzao, Makamu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China kabla ya kufanya mazungumzo rasmi na Waziri huyo wakati wa ziara yake nchini China.
Mhe. Membe (kulia) na Ujumbe wake wakiwa kwenye mkutano wa pamoja na Mhe. Jinzao (kushoto) na ujumbe wake.



Tuesday, February 25, 2014

Mhe. Membe akutana kwa mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.)  akipokelewa na mwenyeji wake Mhe. wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China mara baada ya kuwasili kwenye  Wizara ya Mambo ya Nje ya China.  
Mhe. Membe na Mhe. Wang Yi katika picha ya pamoja.
Mhe. Membe akiongozana na Mhe. Wang Yi mara baada ya kupokelewa.
Mhe. Membe akisalimiana na aliyewahi kuwa Balozi wa China nchini Tanzania miaka kadhaa iliyopita.Anayeshuhudia pembeni ni Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.







Mhe. Membe awasili nchini China kwa ziara ya kikazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Makamu Mkurugenzi wa masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Bi. Sun Baohong mara baada ya Mhe. Membe kuwasili nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tano.
Mhe. Membe akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika Ubalozi wa Tanzania nchini China. Kulia ni Mhe. Lt. Jen. (Mstaafu) Abdulrahaman Shimbo, Balozi wa Tanzania nchini China.
Mhe. Membe katika mazungumzo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki. 

Na Mwandishi Wetu, Beijing, China

MHE. BERNARD K. MEMBE (MB.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amewasili nchini China tarehe 24 Februari 2014 nchini China kwa ziara ya siku tano, na kulakiwa na Bi. Sun Baohong, Makamu Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje China. 

Baada ya kuwasili Mhe. Membe alipokea taarifa ya maendeleo ya shuguli za ubalozi kutoka kwa Lt. Jen. (Mstaafu) Abdulrahaman Shimbo, Balozi wa Tanzania hapa China ambapo pia iligusia maeneo ambayo Mhe. Waziri atayatembelea yaani Shenzhen na Guangzhou.  Baadaye Mhe. Membe na ujumbe wake walipata chakula cha usiku na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi Beijing China kuhusu ziara yake na masuala mengine yahusuyo Tanzania. 

Katika salamu zake kwa Watanzania hao ambao walijumuika na wafanyakazi wa Ubalozi na Familia zao, Mhe. Membe alieleza baadhi ya mambo yaliomleta kwenye ziara hii ikiwa ni pamoja na maandalizi ya ziara ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete nchini hapa kufuatia mualiko wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. 

Mhe. Membe alielezea pia nia yake na Wizara anayoiongoza ya kukuza na kuendeleza Diplomasia ya Michezo na kusema anaamini Serikali ya China itaridhia ombi la Tanzania la kufundisha wanamichezo thelathini wa Kitanzania kwenye michezo mbalimbali kabla ya Mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Madola katikati ya mwaka huu.

Mwishoni Mhe. Membe aliwaelezea Watanzania hao mchakato unaoendelea Tanzania wa kupitia Katiba na hoja kuu ya Wizara ya Mambo ya Nje inayowagusa Watanzania wengi waishio ughaibuni ya Uraia wa Nchi Mbili.

Kesho Mhe. Membe na Ujumbe wake wanatazamia kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa China, Mawaziri wa Mambo ya Nje,  Biashara na Naibu Waziri wa Usalama kabla ya kuendelea na ziara yake kwneye Jimbo la Shenzhen na Guangzhou.

Kwenye ziara hii, Mhe. Membe ameongozana na Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Nakuala Senzia Mkurugenzi  Kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bi. Mindi Kasiga Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje.


Meya wa Mji wa Vallejo wa Marekani awasili nchini

Meya wa Mji wa Vallejo nchini Marekani, Mhe. Osby Davis (kushoto) akisalimiana na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Didas Masaburi mara baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi. Mji wa Vallejo una uhusiano wa udada na Mji wa Bagamoyo
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu akisalimiana na mmoja wa wajumbe waliofuatana na Meya Davis kutoka Vallejo nchini Marekani.
Meya Davis na ujumbe wake wakimsikiliza Balozi Msechu wakati  akifafanua jambo kwao huku Mhe. Masaburi nae akisikiliza.
Mhe. Masaburi akiwapatia maelezo Mhe. Davis na ujumbe wake.

Sunday, February 23, 2014

MHE. MEMBE ZIARANI NCHINI CHINA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atafanya ziara ya kikazi ya siku tano katika Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari, 2014. Ziara ya Mhe. Membe inakuja kufuatia mwaliko kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi.

Mhe. Membe anafanya ziara hiyo nchini China kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya Tanzania na China. Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Membe atafuatana na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Ziara hii pia ni muendelezo wa maeneo ya utekelezaji baada ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping aliyoifanya hapa nchini tarehe 24 na 25 Machi, 2013 na baadaye ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda nchini China mwezi Oktoba, 2013.

Akiwa nchini China, Mhe. Membe atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China tarehe 25 Februari 2014. Siku hiyo hiyo Mhe. Membe atamtembelea Makamu wa Rais wa China, Mhe. Li Yuanchao kwa lengo la kumsalimia na baadaye atafanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Biashara wa China, Mhe. Gao Hucheng.

Aidha, tarehe 26 Februari, 2014 Mhe. Membe atatembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Poly Technologies yaliyopo katika mji wa Shenzhen na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa  na Kampuni hiyo kabla ya kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya China Merchant Holdings International ambako atapokea taarifa ya maandalizi ya kuanza kwa mradi wa Ujenzi wa Bandari katika eneo la Mbegani huko Bagamoyo.

Mhe. Membe pia atapata fursa ya kutembelea Kampuni ya HUAWEI ili kujionea shughuli mbalimbali. Kampuni ya HUAWEI ina Mkataba na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya hapa nchini kuhusu Elimu kwa Njia ya Mtandao (e-Education) kwa Shule za Sekondari.

Vile vile tarehe 27 Februari, 2014, Mhe. Membe atautembelea Mji maarufu wa biashara wa Guangzhou na kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi mjini hapo. Mhe. Membe atatoa taarifa kuhusu hali ya uchumi, siasa na masuala ya jamii yalivyo hapa nchini kwa sasa pamoja na  kutoa taarifa ya maendeleo ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.

Waziri Membe pia atatembelea Eneo la Viwanda la Huadu tarehe 28 Februari, 2014 kabla ya kurejea nchini tarehe 1 Machi, 2014.

IMETOLEWA NA: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.

24 FEBRUARI, 2014

Friday, February 21, 2014

Tanzania na Misri kuimarisha ushirikiano


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Mhe. Nabil Fahmy  wakizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu  ziara ya siku tatu ya Mhe. Fahmy hapa nchini kuanzia tarehe 21 hadi 23 Februari, 2014. Mhe. Fahmy yupo nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan katika nyanja za afya, elimu, uwekezaji na siasa. 
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwasikiza Mhe. Membe na Mhe. Fahmy (hawapo pichani) walipozungumza nao

Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Vincent Kibwana (kushoto waliokaa)  na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga wakinukuu mazungumzo kati ya Mhe. Membe na Mhe. Fahmy (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wao na Waandishi wa Habari. 
Mhe. Fahmy nae akizungumza wakati wa mkutano huo.
Waandishi na Maafisa kazini.

Mhe. Membe akutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Nabil  Fahmy (hayupo pichani) katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency (Kilimanjaro) Jijini Dar es Salaam. Mhe. Fahmy yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 21 hadi 23 Februari, 2014. Wakati wa mazungumzo hayo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan katika nyanja za elimu, afya na uwekezaji. Kulia kwa Mhe. Membe ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Vincent Kibwana.
Mhe. Fahmy (wa nne kutoka kushoto) kwa pamoja na ujumbe wake  wakimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) wakati wa mkutano wao.
Mhe. Membe akizungumza.
Mhe. Fahmy akieleza jambo wakati wa mazungumzo.
Mhe. Membe na ujumbe wake wakimsikiliza Mhe. Fahmy (hayupo pichani)
Ujumbe wa Tanzania wakati wa mazungumzo kati ya Mhe. Membe na Mhe. Fahmy (hawapo pichani)
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Membe na Mhe. Fahmy (hawapo pichani).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri awasili nchini kwa ziara ya kikazi

Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Vincent Kibwana (kushoto) akiwa na Balozi wa Misri hapa nchini, Mhe. Hossam Moharam wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakisubiri kumpokea Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Nabil Fahmy ambaye anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 21 hadi 23 Februari, 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Nabil Fahmy (kulia) akiongozana na Mhe. Balozi Moharam mara baada ya kuwasili nchini.
Mhe. Fahmy akisalimiana na Maafisa kutoka Ubalozi wa Misri waliopo hapa nchini

Mhe. Fahmy akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili nchini.
Mhe. Fahmy akimsikiliza Balozi Kibwana wakati akifafanua jambo kwake mara baada ya kuwasili nchini
Mhe. Fahmy akizungumza na Balozi Moharam
Balozi Moharam akijadili jambo na Balozi Kibwana mara baada ya kumpokea Mhe. Fahmy.

Thursday, February 20, 2014

Waziri Membe azungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waandishi wa Habari ( hawapo pichani) juu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kiamataifa katika Ofisi za Idara ya Habari (Maelezo). Wakati wa Mkutano huo Mhe. Membe alizungumzia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutetea suala la Uraia wa Nchi mbili kwa Watanzania waishio ughaibuni kupitia Bunge Maalum la Katiba, Kuchaguliwa tena kwa Tanzania kwenye Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, Nafasi ya Tanzania katika Ulinzi wa Amani duniani na kuendelea kudumisha  Uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Rwanda. Wengine katika ni  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Rajabu Gamaha (wa pili kutoka kushoto), Balozi Simba Yahya (wa kwanza kushoto),  Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati na Bw. Assah Mwambene Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki (wa kwanza kushoto) akisikiliza kwa makini mkutano kati ya Mhe. Waziri Membe na Waandishi wa Habari (hawapo pichani). Katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya  Habari, Bi Zamaradi Kawawa na  Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga.
Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati yao na Mhe. Membe.
Mhe. Waziri Membe akisikiliza maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) alipozungumza nao. Mkurugenzi wa Afrika, Balozi Vincent Kibwana (wa pili kulia) na Bibi Rosemary Jairo (wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora wakati wa mkutano huo.


Picha na Reginald Kisaka 

Naibu Katibu Mkuu ashiriki maadhimisho ya mwaka mpya wa China

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha akizungumza kwenye halfa ya kuadhimisha mwaka mpya wa China, iliyoandaliwa na Benki ya Standard Chartered na kufanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam. Wakati wa hafla hiyo Balozi Gamaha aliupongeza Ubalozi wa China katika kusaidia na kuchangia maendeleo ya Tanzania. Pia Balozi Gamaha aliipongeza Benki ya Standard Chartered kwa kushirikiana na Ubalozi wa China nchini katika kurahisisha  biashara kati ya Tanzania na China. 
Balozi wa  Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Lv Youqing akitoa neno la shukrani kwa Benki ya Standard Chartered kwa kuandaa hafla hiyo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Bi. Lizzy Lloyd akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo.
Balozi Gamaha (kulia) akimsikiliza Bw. Nathaniel Kaaya,  Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa hafla hiyo. Wengine wanaosikiliza  kutoka kushoto ni Bw. Iman Njalikai na Bw. Emmanuel Luangisa, Maafisa Mambo ya Nje.
Balozi Gamaha akizungumza na Waandishi wa Habari.




Picha na Reginald Kisaka

Wednesday, February 19, 2014

Makatibu Wakuu Zanzibar wapigwa msasa kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Balozi Celestine Mushy (wa kwanza kushoto kwa waliokaa), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa katika picha ya Pamoja na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Serikali ya Zanzibar baada ya kikao cha IMTC. Balozi Mushy alitumia kikao hicho kuwasilisha mada kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yatachukuwa nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia


Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mushy (kulia) na Balozi Silima Haji, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar mara baada ya kukamilika kikao cha IMTC.


Monday, February 10, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha taarifa za uvumi zinaosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari kuwa kuna Watanzania wapatao 160 wamenyongwa nchini China kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya.

Wizara inapenda kuujulisha Umma kuwa hakuna Mtanzania yeyote aliyenyongwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao na vyombo vya habari.

Aidha, taarifa hiyo ya uvumi imedai kuwa ndugu wa mmoja wa Watanzania hao ambaye kwa jina anajulikana kama Bw. Rajab Mohamed Ismail Mapusa wamekaa matanga kuomboleza kifo chake.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Serikali ya China, Bw. Mapusa yupo hai gerezani akitumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kuingiza madawa ya kulevya nchini humo, na hivi karibuni alishiriki kuandaa maonyesho ya utamaduni wa Kiafrika wakati wa kuadhimisha sherehe za Mwaka Mpya wa China.

Wizara inapenda kuwakumbusha Wanahabari kuandika taarifa ambazo ni sahihi zisizopotosha Umma kwa kuzingatia weledi, maadili na ukweli kutoka mamlaka zote husika.

 

Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam

10 Februari, 2014

Friday, February 7, 2014

Wizara kutengeneza Database ya Diaspora kwa kushirikiana na IOM

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Rosemary Jairo akizungumza wakati wa kikao kuhusu uundwaji wa Database na Tovuti kuhusu masuala ya Diaspora. Kikao hicho kiliwashirikisha Wajumbe kutoka Ofisi ya Rais Zanzibar, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uhamiaji na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji hapa nchini (IOM).
Wajumbe kutoka IOM, Ofisi ya Rais Zanzibar na Uhamiaji wakimsikiliza Bibi Jairo (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho
Mwakilishi kutoka IOM, Bi. Mia Immelback akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Bibi Jairo (wa pili kulia) akiwa na Wajumbe wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Mwakilishi wa IOM (hayupo pichani). Kutoka kushoto ni Bw. Mkumbwa Ally, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasialiano katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Kalumuna, Mkuu wa Kitengo cha ICT, Wizara ya Mambo ya Nje na Bi. Susan kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Bw. Kalumuna akichangia jambo wakati wa kikao hicho.

Picha na Reginald Kisaka.