Sunday, February 12, 2017

Rais Magufuli awaapisha Mabalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Uganda na Algeria

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Joseph Edward Sokoine. Hafla za uapisho huo zimefanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Sokoine.

Mhe. Rais Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Grace Aaron Mgovano.
Mhe. Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Mgovano.

Mhe. Rais Magufuli akimuapisha Balozi wa kwanza wa Tanzia nchini Algeria, Mhe. Omar Yussuf Mzee.

Mhe. Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Mzee

Waheshimiwa Mabalozi wakila kiapo cha Maadili ya Viongozi wa Umma, pembeni yao ni Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala (wa kwanza kulia)  na  Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bw. Rogers William Sianga ( wa pili kutoka kulia) ambao pia waliapishwa pamoja na Waheshimiwa Mabalozi.

Kutoka kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma wakishuhudia hafla ya kuapishwa kwa waheshimiwa Mabalozi na Makamishna Wakuu wa Uhamiaji na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Sehemu ya Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Waziri, viongozi waandamizi kutoka katika wizara mbalimbali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda wakifuatilia hafla ya kuapishwa. 

Sehemu nyingine ya Mawaziri na viongozi wa Mamlaka ya kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya wakifuatilia hafla ya uapisho, wa pili kutoka kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb). 

Hafla ikiendelea, wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb).

Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakishuhudia kuapishwa kwa mabalozi na Makamishna Wakuu, Kutoka Kulia ni Balozi Innocent Shio, Balozi Abdallah Kilima na Balozi Anisa Mbega. 

Sehemu nyingine ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa Ikulu katika hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi na Makamishna Wakuu, Kutoka kushoto ni Bw. Osward Kyamani, Bw. Bernard Haule na Bw. Nigel Msangi.

Picha ya pamoja meza kuu, Waheshimiwa Mabalozi na Makamishna Wakuu walioapishwa .

Picha ya pamoja meza kuu, Waheshimiwa Mabalozi na Makamishna Wakuu walioapishwa pamoja na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Taarifa kwa vyombo vya Habari


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MABALOZI WATATU WAPANGIWA VITUO VYA KAZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wapya watatu ambao aliwateua tarehe 3 Disemba 2016.

Mabalozi hao waliopangiwa vituo ni Mhe. Joseph Sokoine anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Omar Yussuf Mzee anayekuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Algeria na Mhe. Grace Mgovano anayekwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Dkt. Ladislausi Komba nchini Uganda ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Balozi Sokoine ambaye anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Deodorus Kamala ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Mzee kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo alishawahi kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nafasi ya mwisho alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika awamu ya kwanza ya Mhe.  Rais Dkt. Ali Mohammed Shein.

Kwa upande wa Balozi Mgavano kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Ubalozi alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Rais, Ikulu.

Mabalozi wote waliopangiwa vituo vipya vya kazi wataapishwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho siku ya Jumapili tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu jijini Dar Es Salaam saa tano asubuhi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki,
Tarehe 11 Februari 2017

Friday, February 10, 2017

Rais Magufuli akutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Mabalozi wanaziwakilisha nchi mbalimbali nchi Tanzania na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kuanza mwaka mpya iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam
Kutoka kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Katibu Mkuu wa Wizara Balozi Dkt.Aziz P. Mlima wakifuatilia hotuba ya Mhe. Rais Magufuli 



Sehemu ya Waheshimiwa Mabalozi wakifuatilia hotuba
Sehemu nyingine ya Waheshimiwa Mabalozi wakifuatilia hotuba
Hotuba ikiendelea

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe.Lu Youqing

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem 

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mratibu Mkazi wa Mashika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maaendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)  nchini Tanzania, Bw. Alvaro Rodriguez

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo nchini Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Joseph Sokoine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Celestine Mushy

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Baraka Luvanda
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Daspora, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Anisa Mbega


Mkuu wa Kitengo cha Mawaliano Serikalini na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga akizungumza katika hafla hiyo


Bi. Mindi Kasiga akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Mawasiliani Ya Ikulu Mhe. Gerison Msigwa
Rais Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mhiga wakiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Mabalozi

Rais Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga wakiwa katika picha ya pamoja Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa nchini Tanzania

Rais Mhe. Dkt. Magufuli na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Magufuli akutana na Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa ushirikiano na mchango wao kwa Serikali ya Tanzania ambao umesaidia kufikia malengo ya Serikali kwa mwaka uliopita wa 2016. Rais Magufuli aliwasihi Waheshimiwa Mabalozi waendelee kuisaidia Serikali ili kufikia malengo iliyojiwekea kwa mwaka 2017.

Mhe. Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu,  Dar es Salaam kati yake, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa  yaliyopo nchini.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa mwaka 2016 ambao ulikuwa mwaka wake wa kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano umekuwa wa mafanikio makubwa ambapo nchi imendelea kudumisha amani, mshikamano, umoja na Muungano umeimarika. Aidha katika mwaka huo,  Serikali  imeongeza jitihada za kuimarisha demokrasia, kupiga vita rushwa, ujangili na ufisadi.

Mhe. Rais Magufuli aliongeza kusema kuwa, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kiuchumi na kuwa nchi ya pili yenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika ikitanguliwa na Ivory Coast. Uchumi wa Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotangulia. Pia kiwango cha mfumuko wa bei kilipungua kutoka asilimia 6.5 mwezi Januari 2016 hadi kufikia asilimia 2.5 mwezi Oktoba mwaka huohuo.

Akizungumzia suala la ukusanyaji mapato, Mhe. Rais Magufuli alisema kwamba Serikali inasimamia kikamilifu suala hilo ambapo kwa sasa  kiwango cha ukusanyaji wa mapato kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi.

Kuhusu mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/2021, Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi hao kuwa, mpango huu unalenga kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyoelekeza.

Alieleza kuwa katika kutekeleza Mpango huo kiasi cha shilingi Trilioni 107 kinahitajika na kati ya hizo  Serikali itatoa shilingi trilioni 59 ambazo ni wastani wa shilingi trilioni 11.8 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Utekelezaji wa mpango huo umeshaanza ambapo Serikali katika Bajeti yake ya mwaka 2016 imetenga kiasi cha shilingi trilioni 29.5  ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo. Kiwango hicho ni cha juu zaidi kuwahi kutengwa kwenye bajeti ya maendeleo katika historia ya Tanzania.

Fedha hizo zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kama vile nishati, barabara, reli  na maji. Aliongeza kusema kuwa Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 5.5 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya usafirishaji na shilingi trilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya nishati ya umeme. “Hii imetuwezesha kuendelea au kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga, maji pamoja na miradi ya umeme. Tuliweza pia kununua ndege mpya sita ambazo bila shaka zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini”

Kwa muktadha huo, Rais Magufuli aliwaomba Mabalozi kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika ujenzi wa Reli wa kiwango cha kimataifa kutoka Dar Es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kuunganisha hadi nchi za Burundi, DRC na Rwanda. Serikali kwa kutumia fedha zake za ndani itaanza kujenga kilomita 300 kuanzia Dar  Es Salaam hadi Morogoro.

Vile vile, Serikali imeweka kipaumbele kwenye kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu iliyotengewa trilioni 4.8  na sekta ya afya kiasi cha trilioni 1.9. Kupitia mpango huu wa kuboresha sekta ya elimu, kiwango cha udahili kwa watoto wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza na wale wanaopokea ufadhili wa masomo ya juu kimeongezeka mara dufu ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Akizungumzia masuala ya Diplomasia, Mhe. Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi na Wawakilishi hao wa Mashirika ya Kimatifa kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi ningine  yameimarika ambapo Viongozi Wakuu kutoka nchi mbalimbali wamefanya ziara nchini Tanzania. Aidha, yeye binafsi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Viongozi wengine Serikalini wamefanya ziara za kuimarisha ushirikiano kwenye nchi mbalimbali. Katika ziara hizo, Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano. Mhe. Rais aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwenye Mashirika ya Kimataifa na Kikanda ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na mengine.

“Tunawashukuru sana Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda kwa kazi nzuri mnayoifanya hapa nchini kwetu. Mafanikio yote haya niliyoainisha yamewezeshwa na ushirikiano wenu na naahidi Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwenu ili muweze kufanya kazi zenu vizuri” alisema Rais Magufuli.

Vilevile aliwaomba Mabalozi hao kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuiwezesha kufikia malengo yake na aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa za malighafi, nguvukazi na soko kubwa lililopo nchini.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli alianisha changamoto zinazochangia kukwamisha jitihada mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hii ili kuziwezesha jamii zetu kufikia maendeleo na ustawi. Pia kupitia Mabalozi hao alizipongeza nchi zilizoridhia Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na kueleza kuwa Tanzania imeanza mchakato wa kuridhia Mkataba huo tangu mwezi Aprili, 2016.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais aliwaeleza rasmi Mabalozi hao azma ya Serikali ya kuhamishia Makao Makuu mjini Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake na kuwaomba Mabalozi hao nao waanze mchakato wa kuhamia Dodoma.

“Mwaka jana wakati nakabidhiwa uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi niliahidi ndani ya miaka mitano Serikali itahamia Dodoma. Tayari Waziri Mkuu na baadhi ya Wizara zipo Dodoma. Nawaomba Mabalozi nanyi muanze kufikiria kuhamia Dodoma kwani Serikali imekwishatenga viwanja kwa ajili yenu, alisisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Edzai Chimonyo alisema kuwa anaipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa hatua kubwa  ya maendeleo iliyopiga katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake. Alisema kuwa katika kipindi hiki wameshuhudia uchumi ukikua, nidhamu katika utumishi wa umma, ukusanyaji wa mapato kuongezeka, na kiwango cha mfumuko wa bei kupungua.

Aidha, aliongeza kuwa wanaunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo Reli kwa vile kutawezesha kukuza biashara na nchi jirani na mataifa mengine kwa ujumla. Pia alipongeza jitihada za Serikali katika kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi ambayo ina mchango mkubwa kwenye maendeleo na kupongeza juhudi za Tanzania kwenye usuluhishi wa migogoro kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na kuitaja Tanzania kuwa ni Kisiwa cha Amani.

Kuhusu Mabalozi kuhamia Dodoma, Balozi Chimonyo alisema Jumuiya ya Mabalozi inaunga mkono wazo hilo na wapo tayari kuhamia Dodoma kama ilivyopangwa.

                                                             -Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 10 Februari, 2017

Katibu Mkuu akutana na Kansela wa Ubalozi wa Afrika ya Kusini nchini Tanzania


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akisalimiana Kansela wa Ubalozi wa Afrika ya Kusini nchini Tanzania, Bw. Frans Van Aardit walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo Kansela wa Ubalozi wa Afrika ya Kusini amekabidhi msaada wa kiasi cha Randi milioni 10 (Fedha ya Afrika ya Kusini), sawa na Dola za Kimarekani laki 7 ikiwa ni mchango wa Serikali ya Afrika ya Kusini kwa wahanga wa tetemeko la Ardhi wa Mkoa wa Kagera lililotokea Septemba 2016.

Waziri Mahiga atembelewa na wageni mjini Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika mazungumzo na Mbunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya, Mhe. David Martin katika Ofisi za Wizara mjini Dodoma.


Mazungumzo yanaendelea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Sarah Cooke katika ofisi za Wizara mjini Dodoma

Mhe. Waziri Mahiga akiagana na Balozi Cooke baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao.

Thursday, February 9, 2017

Wizara yapokea msaada wa vifaa vya kufanyia mkutano kwa njia ya video.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akipokea baadhi ya vifaa vya kuwezesha kufanya Mkutano kwa njia ya video kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Awa Dabo Wizarani Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima akiwa katika mzungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja Bi. Awa Dabo mara baada ya makabidhiano ya vifaa vya kufanyia mkutano kwa njia ya video  
Kutoka kulia, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kisiga, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ugavi Bw. Manyama M. Mapesi na Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy wakifuatilia zoezi la makabidhiano



Zoezi la Makabidhiano likiendelea





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara yapokea msaada wa vifaa vya kufanyia mkutano kwa njia ya video.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima leo amepokea msaada wa vifaa vya kufanyia mkutano kwa njia ya video (Video Conference Facilities) kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (United Nations Development Programme – UNDP).

Baada ya kupokea msaada huo, Balozi Mlima aliishukuru UNDP kwa msaada huo ambao alieleza kuwa utasaidia shughuli za Wizara katika ofisi mpya ya Wizara mjini Dodoma. Alisema msaada huo ni wa pili kwa Wizara katika muda mfupi ambapo awali UNDP ilitoa ngamizi, printers na cameras.

“Tunamshukuru Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy ambaye ndio alianzisha suala hili na kuongea nanyi na kulisimamia bila kuchoka hadi leo vifaa vinapatikana”  “Kwa kweli ni mtu ambaye wakati wote anapenda mambo anayoyasimamia yanatokea” Katibu Mkuu alimwambia Mkurugenzi wa UNDP nchini Tanzania, Bi. Awa Dabo.

Kwa upande wake Bi. Dabo baada ya kukabidhi msaada huo, alisema kuwa mazungumzo kuhusu maombi ya msaada huo yalianza tokea mwaka 2014 lakini kwa uwezo wa mungu vifaa hivyo leo vimekabidhiwa rasmi Wizarani. Alielezea matumani yake kuwa vifaa hivyo vitachangia kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa Wizara na pia utaboresha na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali na UNDP.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 09 Februari  2017.



Chuo cha Diplomasia chapokea ufadhili wa Kompyuta 150 kutoka Serikali ya Korea


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Diplomasia Mhe. Balozi Ombeni Sefue (katikati) wakipokea kompyuta kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Song Geum Young.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika tarehe 8 Februari, 2017 chuo cha Diplomasia Kurasini Jijini Dar es Salaam

Mhe. Balozi Sefue akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Bodi na Uongozi wa Chuo cha Diplomasia mara baada ya kupokea ufadhili huo kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Korea.
Balozi Mwinyi akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kuwa mdau wa maendeleo katika sekta mbalimbali nchini hususan sekta ya Elimu.



Sehemu ya Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia wakimsikiliza Balozi Sefue (hayupo pichani) wakati alipokuwa anatoa neno la shukrani.
Sehemu nyingine ya watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakishuhudia makabidhiano.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Bernard Archiula (wa kwanza kushoto), akifafanua jambo kwa Balozi Sefue na Balozi Mwinyi.
Balozi Ombeni Sefue akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga.
Wakiwa katika picha ya pamoja.