Thursday, March 23, 2017

Katibu Mkuu Mambo ya Nje apokea vifaa vya kuendesha mikutano kwa njia ya Video


Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (Kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kuendeshea Mikutano kwa njia ya Video Wizarani Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Machi, 2017. Makabidhiano yanakamilisha sehemu ya vifaa vilivyotolewa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Awa Dabo ambavyo vilikabidhiwa tarehe 2 Februari, 2017 ili kuiwezesha Wizara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi.
Katibu Mkuu akimpongeza Balozi Mushy kwa jitihada zake za kuimarisha mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo sambamba na kuhakikisha shughuli za kiutendaji za Wizara zinaenda na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Katibu Mkuu na Balozi Mushy wakipokea maelezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eric Kombe kuhusu namna vifaa hivyo vinavyoweza kurahisisha Mawasiliano.

Mhe. Rais Magufuli apokea Hati za Utambulisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Hungary nchini, Mhe. Laszlo Eduard Mathe mwenye makazi yake Nairobi, Kenya. Hafla hiyo fupi imefanyika tarehe 23 Machi, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Mathe akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Aziz Mlima huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa kwanza kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Mary Matari wakishuhudia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Guinea nchini, Mhe. Sidibe Fatoumata KABA mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia. Hafla hiyo fupi imefanyika tarehe 23 Machi, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.
Mhe. Sidibe Fatoumata KABA (katikati) akiwa ameongozana na Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Balozi Grace Martin (kushoto) na Mnikulu, Bw. Ngusa Samike.
Mhe. Rais Magufuli akimtambulisha Balozi Kaba kwa Waziri Mahiga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Belarus nchini, Mhe. Dmitry Kuptel mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia. Hafla hiyo fupi imefanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 23 Machi, 2017.
Mhe. Dmitry Kuptel akisikiliza wimbo wa taifa lake kutoka Bendi ya Polisi kabla ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Mhe. Rais Magufuli
Mhe. Dmitry Kuptel akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Botswana nchini, Mhe. Lebonaamang Thanda Mokalake mwenye makazi yake Lusaka, Zambia. Hafla hiyo fupi imefanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 23 Machi, 2017
Balozi Mokalake akisikiliza wimbo wa taifa lake kutoka Bendi ya Polisi kabla ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Mhe. Rais. Kulia ni Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Balozi Grace Martin na kushoto ni Mnikulu, Bw. Ngusa Samike
Mhe. Rais Magufuli akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi Mokalake, Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ikulu na Maafisa kutoka Ubalozi wa Botswana.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho  kutoka kwa Balozi Mteule wa Niger nchini, Mhe. Adam Maiga ZAKAKARIAOU mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia.
Balozi ZAKAKARIAOU akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho  kutoka kwa Balozi  wa Mauritius nchini, Mhe. Jean Pierre Jhumun mwenye makazi yake Maputo, Msumbiji.
Bendi ya Polisi ikipiga wimbo wa taifa wa Mauritius kwa heshima ya Mhe. Balozi Jean Pierre Jhumun.

Wednesday, March 22, 2017

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho za Mabalozi Wateule

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Mauritius nchini, Mhe. Jean Pierre Jhumun mwenye makazi yake Maputo, Msumbiji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Nepal nchini, Mhe. Amrit Rai mwenye makazi yake Pretoria, Afrika Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ecuador nchini, Mhe. Benys Toscano Amores mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Congo Brazaville nchini, Mhe. Guy Nestor Itoua mwenye makazi yake Kigali, Rwanda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa New Zealand nchini, Mhe. Michael Gerrard Burrel mwenye makazi yake Pretoria, Afrika Kusini.

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Balozi Mteule wa Oman nchini


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (kulia) akizungumza na Balozi Mteule wa Oman nchini, Mhe. Ali Abdullah Mahruqi alipomtembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo yao yalijikita katika suala la Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma na namna Ofisi za Ubalozi huo zinavyoweza kutumia fursa hiyo kuwashauri wafanyabiashara wa Oman kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu pamoja na huduma nyingine za biashara ambazo bado hazijawa za uhakika katika mji huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Bi. Zainab Angovi (kushoto) akiwa na Bi. Patricia Kiswaga, Afisa Mambo ya Nje.
Mazungumzo yakiendelea.
Balozi Mlima akiagana na Balozi Al Mahruqi

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho za Mabalozi Wateule nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) leo tarehe 22 Machi, 2017 amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi Wateule 7 wanaowakilisha nchi zao nchini kutoka Hungary, Belarus, Guinea, Botswana, Niger, Cyprus na Bangladesh. Pichani Balozi Mahiga akipokea nakala za hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Hungary nchini, Mhe. Laszlo Eduard Mathe mwenye makazi yake Nairobi, Kenya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akipokea nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Belarus nchini, Mhe. Dmitry Kuptel mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa na Balozi Mteule wa Guinea nchini Mhe. Sidibe Fatoumata KABA mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia mara baada ya kupokea Nakala zake za Hati za Utambulisho.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Botswana nchini, Mhe. Lebonaamang Thanda Mokalake mwenye makazi yake Lusaka, Zambia.
Waziri Mahiga akizungumza na Mhe. Mokalake mara baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho. Kulia ni Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Martin.
Mazungumzo yakiendelea kushoto ni Maafisa wa Ubalozi wa Botswana ambao waliambatana na Mhe. Mokalake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Niger nchini, Mhe. Adam Maiga ZAKAKARIAOU mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia. 
Waziri Mahiga akiagana na Mhe. ZAKAKARIAOU mara baada ya kuwasilisha Nakala za Utambulisho.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Cyprus nchini, Mhe. Andreas Panayiotou mwenye makazi yake Muscat, Oman.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Bangladesh nchini, Mhe. Meja Jenerali Abul Kalam Mohammad ahaumayun KABIR mwenye makazi yake Nairobi, Kenya. 
Waziri Mahiga akizungumza na Mhe. KABIR.Kulia ni Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Grace Martin na kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi wa Bangladesh ambaye aliambatana na Mhe. KABIR.

Balozi Mero awasilisha Hati za Utambulisho

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Mhe. Modest J. Mero akitoa maelezo mafupi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres kabla ya kuwasilisha rasmi Hati za Utambulisho.

Balozi. Modest J. Mero akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres.

Balozi. Modest J. Mero na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres wakipeana mikono baada ya zoezi la kuwasilisha Hati za Utambulisho kukamilika
Balozi. Modest J. Mero na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres wakisalimiana na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa waliokuwepo kushuhudia tukio la kukabidhi Hati za Utambulisho (pichani wakisalimiana na Bw. Songelael Shilla, Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, New York).
Akizungumza baada ya makabidhiano ya Hati za Utambulisho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Guterres alisema Umoja wa Mataifa unaishukuru Tanzania kwa jinsi inavyojitolea kwa hali na mali katika jitihada za kumaliza migogoro ya kisiasa katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Alitaja hatua zinazochukuliwa na Tanzania kurejesha amani DRC, Burundi na Sudan Kusini kuwa ni mfano wa kuigwa na kwamba anayo imani kwamba jitihada hizo hazitakoma mpaka nchi za SADC na EAC zote ziwe na utulivu wa kisiasa.Naye Balozi Mero akitoa neno la shukurani, alimuahidi Bw. Guterres ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa katika kufanikisha malengo ya maendeleo na ulinzi wa amani. Aidha, alimwonyesha matarajio iliyonayo Tanzania kwake kwa kuzingatia ushirikiano mzuri aliounesha wakati alipokuwa akishughulikia masuala ya wakimbizi duniani, ambapo kwa pamoja na serikali ya Tanzania waliweza kutekeleza mengi kwa mafanikio makubwa

Tuesday, March 21, 2017

Timu ya Everton ya Uingereza kutua nchini hivi karibuni

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Bw. Luca Neghesti kutoka SportPesa Tanzania leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Bw. Neghesti amefuatana na wawakilishi wa timu ya Mpira wa Miguu ya Everton ya nchini Uingereza kumpa taarifa Mhe. Waziri kuhusu maandalizi ya kuileta timu hiyo kucheza mechi za kirafiki nchini Tanzania hivi karibuni.


Mhe. Waziri Mahiga akiwa katika mazungumzo na wawakilishi wa timu ya mpira ya Everton ya nchini Uingereza. Timu hiyo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuja Tanzania kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki. Mhe. Waziri alisema ziara hiyo itasaidia kuitangaza Tanzania duniani pamoja na kuhamasisha mchezo wa mpira wa miguu kwa vijana wa Kitanzania. Anaozungumza nao kutoka kulia ni Mkuu wa Uendeshaji wa Mpira wa Miguu (Head of Football Operations) wa timu hiyo, Bw. David Harrison; Mkuu wa Ulinzi na Usalama (Head of Safety and Security) wa timu, Bw. Dave Lewis na Bw. Alan Chisholm kutoka Thomas Cook.


Waziri Mahiga akifurahia zawadi ya jezi aliyokabidhiwa na Mkuu wa Uendeshaji wa Mpira wa Miguu (Head of Football Operations) wa timu ya Everton, Bw. David Harrison. Jezi hiyo ni ya Mchezaji wa Timu hiyo ambaye pia ni Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ireland, Bw. Coleman.

Picha ya pamoja.

Friday, March 17, 2017

Taarifa kuhusu Ziara ya Rais wa Benki ya Dunia nchini Tanzania



Taarifa kuhusu Ziara ya Rais wa Benki ya Dunia nchini Tanzania

Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim, atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 19 hadi 21 Machi 2017. Akiwa nchini, Dkt. Kim atafanya mazungumzo na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu Jijini Dar Es Salaam siku ya Jumatatu, tarehe 20 Machi 2017 pamoja na kushiriki uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara za Juu katika eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).



Katika mazungumzo yao, Viongozi hao watajadili namna bora ya kuimarisha zaidi uhusiano uliopo kati ya Tanzania na benki hiyo. Vilevile, watazungumzia miradi mikubwa inayotarajiwa kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika kipindi kijacho.



Aidha, baada ya mazungumzo hayo, Rais Magufuli na mgeni wake watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba mitatu:  (i) Uboreshaji Miundombinu ya Usafiri Jijini Dar es Salaam ikiwemo awamu ya tatu na ya nne ya mradi wa DART pamoja na ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la Ubungo (Dar es Salaam Urban Transport Project (DUTP); (ii) Awamu ya pili ya mradi wa Uboreshaji wa Upatikanaji wa Maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya maji taka (Water and Sanitation Project) na (iii) Uboreshaji wa Miundombinu na Huduma za msingi katika baadhi ya miji (Tanzania Strategic Cities Project).



Wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kim atapata pia fursa ya kutembelea Shule ya Msingi Zanaki ambayo ni moja ya Shule zinazonufaika na mpango wa kuboresha elimu ya msingi unaogharamiwa na Benki ya Dunia.



Ziara ya Dkt. Kim inafuatia ziara iliyofanywa nchini na Makamu wa Rais wa Benki hiyo wa Kanda ya Afrika, Bw. Makhtar Diop mwezi Januari 2017 ambapo alishiriki uzinduzi wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi (BRT) uliofanyika kwenye kituo kikuu cha mabasi hayo kilichopo Kariakoo jijini Dar Es Salaam.



-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 17 Machi, 2017


Sunday, March 12, 2017

Waziri Mahiga ampokea Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akizungumza na Mjumbe Maalum, Balozi Harro Adt aliyewasilisha Ujumbe Maalum kutoka kwa Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwenda kwa  Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Pamoja na mambo mengine walizungumzia pia namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Deus Kaganda wakifuatilia  mazungumzo kati ya Waziri Mahiga na Balozi Adt (Hawapo pichani).
Sehemu ya Wajumbe waliofuatana na Balozi Adt (hayupo pichani) nao wakifuatilia mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea
Waziri Mahiga akiagana na Balozi Adt mara baada ya kumaliza mazungumzo.
Waziri Mahiga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe Maalum, Balozi Adt (wa nne kushoto) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizarani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani nchini.
===================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa Tanzania na Ujerumani zitaendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo yale yanayohusu kudumisha amani na usalama duniani pamoja na kuheshimu misingi ya haki za binadamu kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.

Mhe. Waziri Mahiga  ameyesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi Harro Adt, Mjumbe Maalum wa Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli alipofika Wizarani kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe huo.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa, Ujerumani na Tanzania zina mahusiano ya kihistoria tangu enzi za ukoloni hadi sasa. Katika  masuala ambayo Tanzania inanufaika na ushirikiano huo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, maboresho katika sekta ya elimu na mchango katika uhifadhi wa wanayamapori.

“Uhusiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria tangu ukoloni. Hata hivyo Ujerumani  wamejaribu kutafsiri ushirikiano wetu katika misingi bora sasa kuliko ile ya kikoloni. Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania moja kwa moja  katika sekta mbalimbali kama elimu, wanyamapori na miundombinu na misaada mingine imekuwa ikipitia Umoja wa Ulaya” alisema Waziri Mahiga.

Akizungumzia ziara ya Balozi Adt nchini, Mhe. Waziri Mahiga alisema Mjumbe huyo Maalum wa Kansela wa Ujerumani ameleta ombi kwa Mhe. Rais na kwa Watanzania la kuiunga mkono Ujerumani kwenye nafasi ya  Mjumbe asiye wa Kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  wakati wa uchaguzi utakaofanyika mwaka 2018. Aliongeza kusema kuwa, Ujerumani imedhamiria kugombea nafasi hiyo ikiwa na dhamira ya kuunga mkono mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo kuziunga mkono nchi za Afrika kwenye harakati za kupatiwa nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza hilo.

Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alifafanua kwamba, katika kufikia malengo hayo Ujerumani imejiwekea misingi mikuu minne ambayo ni:- Kusaidia jitihada za amani na usalama duniani; Kusimamia Haki ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Kuhamasisha mageuzi ya Teknolojia na Kuhimiza ushirikiano na Ubia wa Kimataifa.

Mhe. Mahiga alieleza kuwa kwa kuzingatia misingi hiyo, amemueleza Balozi Adt azma ya Tanzania kuiomba Ujerumani iisadie Afrika kujenga Jengo la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambapo Tanzania ndio Makao yake Makuu huko Mjini Arusha.

Mhe. Mahiga pia alimhakikishia Balozi Adt kuwa ameupokea ujumbe wa Kansela wa Ujerumani na atauwasilisha kwa Mhe. Rais.

Kwa upande wake Balozi Adt, Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata baada ya kuwasili nchini. Pia ana imani kuwa Tanzania ambao ni rafiki wa kihistoria wa Ujerumani itawaunga mkono kwenye nafasi hiyo ili kuwawezesha kutekeleza malengo waliyojiwekea ikiwemo kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 12 Machi, 2017