Friday, April 27, 2018

Tanzania yajikita kutumia fursa za soko la Afrika Mashariki

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiongea na wawakilishi kutoka kampuni ya Agricom Afrika Ltd walioshiriki maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta Jijini Nairobi, Kenya tarehe 27 Aprili 2018.

=======================================

Tanzania yajikita kutumia fursa za soko la Afrika Mashariki.

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesisitiza kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali za Tanzania na Kenya ili kuhakikisha bidhaa na mazao ya kilimo yanayozalishwa na wananchi yanapata soko la kuaminika katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan Kenya.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda alipotembelea maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya, yaliyofunguliwa rasmi na Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Mhe. Mwangi Kiunjuri tarehe 25 April, 2018 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) Jijini Nairobi, Kenya.

Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo imeambatana na maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Kenya ambapo lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa mataifa hayo ili waweza kufanya makubaliano ya kibiashara, kupeana uzoefu na kuwezesha bidhaa za viwanda vya Tanzania kupenyeza katika soko la Kenya kama ambavyo bidhaa na huduma za wakenya zilivyoingia katika soko la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Aidha, aliongeza ushirikiano huo utasaidia kukuza biashara na uwekezaji na hivyo kuongeza ajira, kuinua pato la taifa na kipato cha mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla. ‘’ Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa yote na itaendelea kufata taratibu na kanuni za biashara zilizokubaliwa kimataifa” alisema Prof. Mkenda

Vilevile Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji alipata fursa ya kutembelea maonesho hayo ya bidhaa ambapo alisisitiza  umuhimu wa kuthamini bidhaa zetu na kwamba Serikali ya Tanzania na Kenya zitaendelea kuimarisha undugu na mshikamano uliopo kama ilivyokubaliwa na marais wa Tanzania na Kenya walipokutana Kampala, Uganda katika Mkutano wa 19 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo waliwataka viongozi katika nchi zao kumaliza vikwazo vya kibiashara.  “ Serikali itaendelea kuweka mazingira wezesha kwa wafanyabiashara hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wote kufuata taratibu na masharti katika kufanya biashara zao” alisema Prof. Ole Gabriel

Wiki ya Tanzania nchini Kenya imeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia ubalozi wake wa Nairobi, Kenya kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Bara), Wizara ya Viwanda na Biashara (Serikari ya Mapinduzi Zanzibar), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Taasisi ya Sekta Binafsi, Wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Tanzania ambao walijitoa kwa hali mali katika kudhamini ili kufanikisha Wiki ya Tanzania nchini Kenya.

Prof. Adolf Mkenda pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wakipata ufafanuzi wa biashara ya matunda na mboga mboga kutoka kampuni ya Agricom.



Prof. Mkenda akipata ufafanuzi wa ubora na matumizi ya mabomba yanayotengenezwa na kampuni ya kitanzania ya PLASCO LTD kutoka kwa Mhandisi Elisaria Aminiel.

Mmoja wa Mabalozi wanaowakilisha nchini Kenya akinunua mkanda kutoka banda la kampuni ya kitanzania inayozalisha bidhaa za ngozi WOISO Original Products, Pembeni ni mwakilishi kutoka kampuni hiyo, Bw. Justine Msigwa.

Ubalozi wa Tanzania, Uingereza waadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanzania kwa Ibada Maalum

Juu na Chini ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha Rose-Migiro (katikati) akiwa na Watumishi wa Ubalozi pamoja na Watanzania waishio nchini Uingereza mara baada ya kumaliza Ibada Maalum ya kuadhimisha Miaka 54 ya Muungano wa Tanzania ambayo ilifanyika kwenye Kanisa la Westminster Abbey Jijini London.


Naibu Waziri akutana na kufanya mazungumzo na mshindi wa shindano la 28 la urembo katika taji la World Miss University Africa 2017

Mhe. Dkt. Susan Kolimba Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akizunguza na Bi. Queen Elizabeth Manule mshindi wa shindano la 28 la urembo katika taji la World Miss University Africa (2017) lililofanyika Cambodia tarehe 20 Desemba, 2017.Membo Bi. Queen Elizabeth alikuja kumsalimu Naibu Waziri na kuomba ushirikiano kutoka Wizarani na Serikalini kwa ujumla katika kutekeleza mpango wake wa kutangaza amani Duniani na kusaidia jamii.

Mhe. Naibu Waziri alimshukuru kwa kuja kumsalimia na kumpongeza kwa ushindi alioupata ambao unaitangaza Tanzania nje ya mipaka ya nchi.

Alimtaka ajivunie ushindi huo aliopata na kuwa mfano mzuri kwa wasichana wengine katika masomo na kuhudumia jamii inayomzunguka. Alimuahidi ushirikiano wa Wizara katika masuala ambayo ameazimia kuyafanya kwa ajili ya Jamii na kuitangaza Tanzania.
Mrembo Bi. Queen Elizabeth Manule ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Kwanza (Public Sector Accounting and Finance) katika Chuo cha Uhasibu (TIA).
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Dkt.Susan Kolimba akisalimiana na Bi. Queen Elizabeth Manule walipokutana kwa mazungumzo Wizarani jijini Dodoma

Naibu Waziri Mhe. Dkt.Susan Kolimba akimsiliza Mrembo Bi. Queen Elizabeth Manule wapokutana kwa mzungumzo Wizarani jijini Dodoma.


Wednesday, April 25, 2018

Ufunguzi rasmi wa maonesho ya kipekee ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya


Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Mwangi Kiunjuri akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo imeambatana na maonesho ya huduma, vivutio vya utalii na bidhaa za viwanda vya Tanzania yanayofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 28 Aprili 2018 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (KICC) Jijini Nairobi, Kenya.


Mhe. Waziri Kiunjuri akihutubia wageni waalikwa (hawapo pichani) katika hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo itaenda sambamba na Maonesho ya bidhaa za viwanda, Kongamano la biashara na Maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanzania. Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya tarehe 25 Aprili 2018.

Mhe. Wanjuri katika hotuba yake amesisitiza umuhimu wa kilimo cha kisasa ili kupata mazao yatakayokidhi vigezo vya ubora na kuingia katika ushindani wa biashara kimataifa utakaopelekea maendeleo ya uchumi hususan uchumi wa viwanda.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hassan Khamis Hafidh akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambapo alieleza kuwa tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya marais wa Tanzania na Kenya walipokutana katika Mkutano wa 19 wa Kawaida wa Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Pindi Chana akiwakaribisha wageni waalikwa katika hafla ya ufunguzi rasmi wa wiki ya Tanzania nchini Kenya.
Katika ufunguzi huo Mhe. Chana alieleza  umuhimu wa maonesho hayo ni pamoja na kuzitangaza huduma na bidhaa za viwanda  vya Tanzania ili ziweze kupenyeza katika soko la Kenya. Maonesho hayo yametoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania kukutana na kufanya mazungumzo ya biashara na wafanyabishara kutoka katika kampuni za Kenya.

Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Katibu wa kamati ya maandalizi ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya, Balozi Anisa Mbega  na mjumbe kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Francis Mossongo wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Sehemu ya wafanyabiashara kutoka Tanzania wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa hafla hiyo. 
Sehemu nyingine ya wafanyabiashara wakifuatilia hafla ya ufunguzi huo.



Sehemu ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa  nchini Kenya wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Sehemu nyingine ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa  nchini Kenya wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakifuatilia hafla hiyo.
 =======================================================================
Wakati huo huo Mhe. Waziri Kiunjuri alitumia fursa hiyo kukabidhi vyeti kwa washiriki pamoja na kutembelea mabanda ya maonesho.

Mhe. Waziri Kiunjuri akikabidhi cheti cha ushiriki kwa mwakilishi wa kampuni ya Lake Group, Bw. Peter Sifa

Mhe. Waziri wa Kiunjuri akimkabidhi cheti cha ushiriki mwakilishi kutoka Kampuni ya vinywaji (Tanzania Distillers Ltd)
Mhe. Waziri Kiunjuri akikabidhi cheti cha ushiri kwa mmoja wa wafanyabiashara kutoka Zanzibar, Bw. Nassoro Omar wa Kampuni ya ZANOP.
Mhe. Kiunjuri akimkabidhi cheti mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maonesho na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE),  Bw. Edwin Rutageruka.

Mhe. Waziri Kiunjuri akimkabidhi cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na mwenyekiti mwenza wa kamati ya maandalizi ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya, Bw. Godfrey Simbeye kwa kufanikisha zoezi la uratibu wa wiki hiyo.

Mhe. Waziri Kiunjuri akipokea maelezo kwa mmoja wa washiriki wa maonesho ya bidhaa kutoka Tanzania, Bw. Amir Esmail kutoka kampuni ya kahawa ya AMIMZA.

Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Tanzania, India apandishwa cheo

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka H. Luvanda akimvalisha cheo cha Brigedia Jenerali A.S Mwami ambaye ni Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Tanzania nchini India.Brigedia Jenerali A.S Mwami ni miongoni mwa Maafisa Wakuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania ambao Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliwapandisha vyeo tarehe 12 Aprili, 2018. Awali Brigedia Jenerali Mwami alikuwa na cheo cha Kanali. Hafla hiyo fupi imefanyika katika Ubalozi wa Tanzania nchini India na  kuhudhuriwa na watumishi wa ubalozi huo.
Brigedia Jenerali Mwami akiwa kwenye picha ya pamoja na familia yake.
Balozi Baraka Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Brigedia Jenerali A.S Mwami
Balozi Luvanda pamoja na Brigedia Jenerali A.S Mwami wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini India.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA BENKI YA AfDB NCHINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina atafanya ziara ya siku nne (4) nchini kuanzia tarehe 25 hadi 28 Aprili, 2018 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Lengo la ziara ya Dkt. Adesina nchini ni kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miradi ya miundombinu nchini.
Akiwa nchini, Mhe. Dkt. Adesina ataonana kwa mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuzindua Barabara kutoka Dodoma kwenda Babati hafla itakayofanyika katika eneo la Mradi wa Barabara wa Mayamaya-Mela-Bonga Wilayani Kondoa.
Aidha, Dkt. Adesina atatembelea Mtambo wa Kusafirisha Umeme wa Iringa kwenda Shinyanga pamoja na Kituo Kidogo cha Umeme cha Zuzu cha Mkoani Dodoma.
Dkt. Adesina ambaye ameambatana na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anatarajiwa kushiriki Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Mkoani Dodoma tarehe 26 Aprili, 2018.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza kwa kupokea misaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF). Aidha, tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa nchini mwaka 1971, Tanzania imenufaika kwa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3.5 huku miradi ya maendeleo ya miundombinu ikipewa kipaumbele.
Aidha, hadi kufikia mwezi Novemba 2017 Benki ya Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitekeleza miradi 25 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.9. Kati ya miradi hiyo, 22 ni ya Sekta ya Umma yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 huku miradi mitatu (3) ikiwa chini ya Sekta Binafsi kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 187.0.
Kati ya miradi yote, miradi ya maendeleo ya miundombinu inachukua asilimia 73 ambapo kati yake miradi ya Barabara ni asilimia 51, Maji na Usafi wa Mazingira asilimia 12 na Nishati asilimia 10. Asilimia 27 zilizosalia zinasaidia miradi ya sekta binafsi hususan katika kilimo na ustawi wa jamii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Aprili, 2018
-Mwisho-
 

Monday, April 23, 2018

Naibu Waziri akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Bunge la Afrika

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Rais wa Bunge la Afrika Mhe.Roger Nkodo Dang Wizarani Mjini Dodoma.

Mhe. Dang amekuja nchini kwa lengo la kuishukuru Serikali kwa ushirikiano iliompa katika kipindi chote ambacho amelitumikia hilo.

Mhe.Dang anakaribia kumaliza muda wake wa kipindi cha miaka miwili wa kutumikia nafasi hiyo.  
Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akimsikiliza  Rais wa Bunge la Afrika Mhe.Roger Nkodo Dang


Saturday, April 21, 2018

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Balozi wa China nchini wazungumzia maandalizi ya Mkutano wa FOCAC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano wa Afrika na China (FOCAC) utakaofanyika mwezi Septemba, 2018 nchini China. Mkutano huo ambao utajadili masuala mbalimbali kwa maendeleo ya Bara la Afrika utatanguliwa na vikao vya maafisa waandamizi na vile vya mawaziri. Kikao kati ya Prof. Mkenda na Balozi Wang Ke kimefanyika Wizarani tarehe 21 Aprili, 2018
Maafisa kutoka Ubalozi wa China nchini wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Wang Ke (hawapo pichani)
Prof. Mkenda akimsikiliza Balozi Wang Ke alipokuwa akimweleza kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Mkutano wa FOCAC utakaofanyika mwezi Septemba, 2018 nchini China
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nao wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Wang Ke (hawapo pichani). Kulia ni Bi. Berha Makilagi na Bw. Halmesh Lunyumbu.
Mkutano ukiendelea
Picha ya pamoja

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA WAZIRI WA SHERIA WA ISRAEL NCHINI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Taarifa kuhusu ziara ya Waziri wa Sheria wa Israel nchini

Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 22 hadi 24 Aprili, 2018. 

Akiwa nchini, Mhe. Waziri Shaked ambaye anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara na wawakilishi wa makampuni kutoka Israel atashiriki Kongamano la Tano la Biashara kati ya Tanzania na Israel litakalofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 23 na 24 Aprili, 2018.

Kongamano hilo ambalo linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Israel, litahusisha Sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambazo ni pamoja na Kilimo, Viwanda, Afya, Nishati na Utalii. Aidha, kupitia Kongamano hilo wafanyabiashara katika sekta hizo watabadilishana mawazo baina yao pamoja na watendaji wa Serikali ili kufikia malengo waliyopanga.

Kongamano hilo linaratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT).

Pamoja na kushiriki katika Kongamano hilo, Mhe. Waziri Shaked ameomba miadi ya kukutana na Viongozi mbalimbali Serikalini akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Aderladus Kilangi.

Kabla ya kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Shaked atakutana na vyombo vya habari tarehe 24 Aprili, 2018 kwa ajili kueleza mafanikio ya ziara yake nchini. Mhe. Shaked na ujumbe wake wataondoka nchini siku hiyohiyo kurejea Israel.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 21 Aprili, 2018
-Mwisho-