Monday, August 13, 2018

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC wafunguliwa mjini Windhoek, Namibia

Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) umefunguliwa rasmi katika Hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia tarehe 13 Agosti 2018.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ambaye ameambatana na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania ambao ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda; Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayesimamia masuala ya Ujenzi) Mhandisi Joseph Myamhanga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa; Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu na Naibu Katibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Paul Mhede.

Mkutano huu ni sehemu ya mikutano ya awali ya maandalizi ya mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 na 18 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia.  Mikutano mingine ya awali ni mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC uliofanyika tarehe 9 na 11 Agosti 2018 na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa , Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Kanda kwa kipindi cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018. 

Mkutano  wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utapokea, kujadili na kutolea maamuzi ya mapendekezo mbalimbali yanayotokana na mikutano ya kisekta na kamati za jumuiya kwa kipindi cha mwaka 2017/18. Pamoja na mambo mengine mkutano huu;

Utafanya uteuzi wa Mwenyekiti wa SADC na inatarajiwa kuwa Jamhuri ya  Namibia ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa  Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha 2018/2019. Nafasi ya Makamu mwenyekiti itajazwa pia na nchi itakayoteuliwa ambayo itajulikana tarehe 17Agosti 2018.

Uteuzi wa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Inatarajiwa kuwa Jamhuri ya Zambia, ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha 2018/2019. Hivi sasa Tanzania ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwenye Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security).


Mambo mengine yanayotarajiwa kujitokeza na kujadiliwa katika mkutano huu ni pamoja na;  masuala ya fedha; Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Viwanda wa SADC  (Report on the operationazaition) na Maendeleo ya Viwanda;  Kutia saini itifaki mbalimbali ikiwa ni pamoja na itifaki ya Kulinda Hakimiliki ya Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea ya mwaka 2017. Pia Mkutano huu utatoka na tamko la nchi wanachama wa SADC la kutokomeza malaria katika ukanda wa SADC ifikapo mwaka 2030. 



==========================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika unaofanyika tarehe 13 na 14 Agosti 2018 katika hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia .

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena L. Tax (mstari wa mbele kati) akiwa katika picha ya pamoja na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika mara baada ya hafla ya ufunguzi wa mkutano huo mjini Windhoek, Namibia.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, Dkt. Stergomena L. Tax akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa Mawaziri wa SADC.

Katika hotuba yake aliwasilisha taarifa fupi ya mwaka ya utekelezaji ya Jumuiya hiyo pamoja na kuishukuru Serikali ya Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda) kwa uongozi na usimamizi mzuri katika kipindi chote cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018.

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mhe Dkt. Lindiwe Sisulu (kushoto) akikabidhi nafasi ya uenyekiti kwa mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwa. 

Mwenyekiti mpya wa Mawaziri wa SADC, Mhe. Nandi-Ndaitwa akihutubia mara baada ya  kupokea nafasi hiyo.
Katika hotuba yake alisistiza umuhimu wa kuwawezesha vijina kwa kuwa ndio nguzo kuu katika kuinua uchumi wa taifa lolote duniani sambamba na uwekezaji katika viwanda. Pamoja na hayo akaeleza malengo makuu ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuondoa umasikini na kuinua uchumi ndani ya kanda. 

Mkutano ukiendelea, walioketi nyuma ya Mhe. Waziri Mahiga kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Viwanda na Mawasiliano (anayeshughulikia masuala ya ujenzi) Mhandisi Joseph Nyamhanga.

Mkutano ukiendelea, Kutoka Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Mhede.

Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester Ambokile na wajumbe wengine wa Serikali ya Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa mkutano.

Sehemu nyingine ya wajumbe kutoka Serikali ya Tanzania wakifuatilia mkutano. 

Balozi wa Namibia nchini Tanzania pamoja na wajumbe wengine wa mkutano huo wakifuatilia hafla ya ufunguzi.

Saturday, August 11, 2018

Katibu Mkuu Mambo ya Nje atembelea Chuo Kikuu cha Tiba cha Namibia

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kulia) akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Namibia. Prof. Kenneth Kamwi Matengu (kushoto) alipomtembelea chuoni hapo mjini Windhoek, Namibia  tarehe  10 Agosti 2018. Wanaofatilia mazungumzo wa pili kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini Balozi Mhe.Sylivester Ambokile  na wa Pili kushoto ni Mkurugenzi msaidizi katika chuo hicho Bw. Evaristus Evaristus

Katika mazungumzo yao wawili hao wamejadili juu ya kuongeza maeneo ya ushirikiano na  kuanzishwa kwa programu za kujenga uwezo na kupeana uzoefu. Chuo Kikuu cha Namibia kinashirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na sasa  chuo hicho kina mpango wa kuanzisha mazungumzo ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Muhimbili. 

Mazungumzo yakiendelea, kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. James Lugaganya, Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria.

Picha ya pamoja.
==================================

Baada ya mazungumzo Katibu Mkuu, Prof. Adolf Mkenda alitumia fursa hiyo kutembelea Chuo Kikuu cha Tiba cha Namibia ambacho ni Tawi la Chuo kikuu cha Namibia kilichopo mjini Windhoek, Namibia. 

Prof. Kenneth Matengu (wa kwanza kulia) akimwongoza Prof. Mkenda na ujumbe wake kutembelea chuo hicho.
Wa kwanza kushoto ni Mhadhiri katika chuo hicho akifafanua taratibu za masomo ya nadharia na vitendo zinavyoendeshwa katika chuo hicho.



Wakitembelea Maabara za kufundishia.

Wakitembelea vyumba vya semina kwa wanafunzi.
Baadhi ya majengo ya ofisi na madarasa katika Chuo kikuu cha Tiba cha Namibia.

Wizara ya Mambo ya Nje yahamasisha uwekezaji katika sekta ya Kilimo na Mifugo


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amefanya mazungumzo na kampuni ya Burmeister & Partiners  (PTY) LTD ya nchini Namibia tarehe 10 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia.

Akiongea na uongozi wa kampuni hiyo Prof. Mkenda alieleza Tanzania ina eneo kubwa la ardhi yenye rutuba  ambayo haitumiki na rasilimali watu ya kutosha hivyo ni fursa kwa mwekezaji mwenye nia thabiti kuwekeza nchini.

“Lengo la Serikali ni kupata mwekezaji aliye makini kama wewe nimeona una mradi mkubwa wa shamba la mifugo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya machinjio nina imani ukija kuwekeza Tanzania hautajutia kabisa kwakuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika miradi itaongeza thamani ya mazao na bidhaa zitakazozalishwa na kuwezesha kupatikana kwa soko la kimataifa” alisema Prof. Mkenda

Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Mhandisi Hendrik Boshoff alieleza  kampuni imekuwa ikifanya kazi katika mataifa mbalimbali ambapo kampuni hiyo imefungua kampuni ya maziwa nchini Rwanda ambayo inauza na kusafirisha mataifa mengine pia imewekeza nchini Angola katika miradi ya uvuvi na imekuwa ikifanya vizuri katika biashara zake zote.

Pia alisema kampuni imebobea katika miradi ya ujenzi, nishati, miradi ya maji, usafiri, usanifu majengo, ujenzi wa majengo, miradi ya machinjio, mashamba ya mifugo na pia ipo katika mpango wa kuanzisha miradi ya viwanda vya dawa za binadamu ambapo utekelezaji wake utaanza mara baada ya kukamilisha mazungumzo na wataalamu kutoka nchini Cuba.

Prof. Mkenda alieleza miradi yote kutoka katika kampuni hiyo inatija kubwa kwa maendeleo ya taifa la Tanzania hivyo akaikaribisha kampuni hiyo kuja mapema nchini ili kuweza kujionea rasilimali zilizopo na kuainisha miradi watakayoweza kuanza nayo. Vilevile akaeleza  kampuni hiyo ina nafasi ya kutumia fursa za mji wa Dodoma katika uwekezaji kufuatia kuhama kwa mji wa Serikali kutoka Dar es Salaam.

Kampuni ya Burmeisters & Partiners (PTY) LTD ilianza kufanya kazi zake nchini Namibia mwaka 1984 na baadae kuwa miongoni mwa kampuni kubwa zilizowekeza nchini humo. Pia ni kampuni  hiyo inatoa huduma za  kihandisi na huduma za usimamizi wa miradi katika taaluma mbalimbali.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda(kulia) akizungumza na mwakilishi wa kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) LTD alipowatembela katika ofisi za kampuni hiyo iliyopo Windhoek, Namibia tarehe 10 Agosti 2018. Kulia kwa Katibu Mkuu ni  wajumbe walioambatana naye katika ziara hiyo, Mratibu wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Tanzania, Bi. Magreth Ndaba, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika Mashariki , Bw. James Lugaganya na Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Sylivester Ambokile.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Burmeister & Partners (PYT) LTD, Mhandisi Hendrik Boshoff akielezea usanifu wa miradi mbalimbali unaofanywa na kampuni ya Burmeister & patners (PTY) LTD.

Sehemu ya ofisi iliyosanifiwa na kampuni hiyo.

Mazungumzo yakiendelea.

Mwakilishi kutoka kampuni hiyo akiwasilisha miradi mbalimbali iliyosanifiwa na kampuni ya Burmeister & Partners (PTY) LTD

Prof. Mkenda akifafanua tunu na rasilimali zilizopo nchini ambazo ni fursa kwa uwekezaji.

Friday, August 10, 2018

Tanzania na Namibia kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Elimu ya juu.

Serikali ya Tanzania imeonesha nia ya wazi ya kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu na Serikali ya Namibia ambapo ushirikiano huo utawezesha walimu na wanafunzi kuwa na progamu za kubadilishana kwa lengo la kupeana uzoefu na kujengeana uwezo.

Hayo yamesemwa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf F. Mkenda katika chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia  Mjini Windhoek, Namibia tarehe 09 Agosti 2018.

Katika ziara hiyo Prof. Mkenda aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake mjini Pretoria nchini Afrika Kusini, Mhe. Balozi Sylivester Ambokile, Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria na Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. James Lugaganya.

Lengo la ziara hiyo ni kujadili namna ya kuongeza ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu kwenye masuala ya utafiti na ugunduzi katika taaluma za teknolojia zinazotolewa na vyuo vitakavyoingia makubaliano ya ushirikiano.

“Nimekuja tushirikishane mikakati mbalimbali tunayoweza kujiwekea ili kuvifanya vyuo vyetu viwe bora ndani ya kanda na Afrika kwa ujumla pia tujadili mbinu mpya za kielimu ambazo Tanzania na Namibia  zinaweza zikashirikiana,”alisema Prof. Mkenda

Pia akaeleza nchi nyingi za Afrika zinapata changamoto ya uwezo mdogo na uhaba wa rasilimali fedha katika kuhakikisha upatikanaji wa malazi kwa wanafunzi, upatikanaji wa elimu kwa vitendo na kwamba ni vema Tanzania na Namibia zikatumia fursa za ushirikiano wa elimu zinazosainiwa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Namibia  cha Sayansi na Teknolojia, Dkt. Tjama Tjivikua alieleza kuwa hadi sasa chuo kimefanikiwa kuanzisha ushirikiano na taasisi, makampuni na viwanda mbalimbali nchini humo na hata nje ya nchi ili kuwawezesha wahitimu katika chuo hicho kupata nafasi ya elimu kwa vitendo.

“Jitihada hizi zimeshaanza kuleta matunda kwa kuwa kwa sasa wahitimu wa chuo hiki wamefanikiwa kupata ajira katika taasisi hizo na wengine walifanikiwa kupata ajira kabla ya kuhitimu muda wa mafunzo” alisema Dkt. Tjivikua

Vilevile chuo kinashirikiana na wadau mbalimbali ambapo alieleza Tanzania ni mmoja wa wadau kupitia chuo cha Sayansi ya Kilimo Sokoine(SUA) na chuo kikuu cha Ardhi, wadau wengine ni pamoja na Afrika Kusini,  Cameroon, Kenya, Botwana, Uswiss, na mashirika mengine ya kimataifa.

Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Sylivester Ambokile naye alisema kwa kuwa jumuiya ya wanamibia imezungukwa na jamii inayozungumza Kiswahili hivyo ni vema ushirikiano uliopo ukazidi kuimarishwa kwa kuingiza lugha ya Kiswahili katika idara za lugha za kigeni kwenye vyuo vikuu nchini Namibia.

“Katika hafla ya utambulisho wangu kwa Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Hage Geingob niliwasilisha wazo la Kiswahili kuingizwa katika Idara za Lugha ya kigeni na lilipokelewa vizuri, hivyo kwa sasa ofisi za ubalozi zinafanya jitihada za kukumbushia katika sekta husika ili utekelezaji wake ukamilike mapema”. alisema Mhe. Balozi Ambokile

Nchini Namibia elimu ya juu imeanza mwaka 1979/1980 kutokana na kuchelewa huko kuliifanya Namibia kuhitaji Walimu wa taaluma mbalimbali kutoka mataifa mengine. Tanzania ni miongoni mwa nchi yenye walimu wengi katika vyuo vikuu ya Namibia. Pamoja na kuwepo kwa ushirikiano huo Chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992 kimekuwa kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) katika kupata wataalamu wazuri wa masuala ya mifugo ambao wamekuwa wakirejea baada ya masomo na kulitumikia taifa kwa tija.

====================================================

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akijadili jambo na Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Namibia, Dkt. Tjama Tjivikua mara baada ya kuwasili chuoni hapo kwa mazungumzo rasmi ya kikazi yaliyofanyika tarehe 09 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia. Pembeni ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester Ambokile.
Katibu Mkuu, Prof. Mkenda akitembelea maeneo ya chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia ili kuweza kujionea uendeshaji wa vipindi vya masomo na mpangilio wa majengo kwa ajili ya madarasa na malazi ya wanafunzi.
Katibu Mkuu, Prof. Mkenda na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na uongozi wa chuo, wa kwanza kulia ni Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria, kulia kwa Prof. Mkenda ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Ambokile na pembeni yake ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. James Lugaganya.



Mazungumzo yakiendelea.

Kaimu Balozi wa Kuwait nchini Tanzania awasilisha ujumbe Wizarani

Bw. Suleiman Saleh Kaimu Mkurugenzi Idara Mashariki ya Kati, akisalimiana na Bw. Nasser Bader Al Ramzi Kaimu Balozi wa Kuwait nchini Tanzania walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Bw. Nasser ameeleza kuwa Ubalozi unaandaa uataraibu wa kutembelea na kukagua maendelea ya miradi mbalimbali inayofadhiliwa Kuwait nchini Tanzania. Kaimu Mkurugenzi amemuhakikishia kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla watampa ushirikiano wa hali ya juu wakati wote wa utelezaji wa majukumu yake nchi.

Aidha Bw.Nasser amewasilisha ujumbe maalumu kutoka nchini Kuwait kwa Serikali ya Tanzania 

Bw. Suleiman Saleh Kaimu Mkurugenzi Idara Mashariki ya Kati (katika) akimsikiliza Bw. Nasser Bader Al Ramzi Kaimu Balozi wa Kuwait nchini Tanzania  (kulia) walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Bw. Hangi Mgaka Afisa Mambo ya Nje akifuatilia  mazungumzo

Bw. Suleiman Saleh Kaimu Mkurugenzi Idara Mashariki ya Kati akipokea ujumbe maalum kutoka kwa Bw. Nasser Kaimu Balozi wa Kuwait nchini Tanzania kushoto ni Bw. Hangi Mgaka Afisa Mambo ya Nje

Balozi wa Saudi Arabia akutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Wizara

Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kushoto), akisalimiana na Mhe. Mohamed Ben Mansour Al Malek Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania (kulia) walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam. Mazungumzo baina ya Viongozi wa Wizara na Balozi Mohamed yalijikita katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Mataifa haya mawili (Tanzania na Saudi Arabia).

Aidha viongozi hao wamekubaliana kukamilisha maandalizi ya kongamano la biashara litakalo husisha wafanyabiashara na wadau wengine kutoka Saudi Arabia na Tanzania. Balozi Mohamed amebainisha kuwa ujumbe kutoka Saudi Arabia utakuwa na wafanyabiashara zaidi ya 40 wakiongozwa na Waziri wa Biashara wa Saudi Arabia.

 Aidha Balozi Mohamed ameonesha nia yakuanzisha  majadiliano kati ya Tanzania na Saudi Arabia ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Saudi Arabia kwa lengo la kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili.
Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Mohamed Ben Mansour Al Malek Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Bw. Suleiman Saleh, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati (wa kwanza kulia) na Bw. Hangi Mgaka Afisa Mambo ya Nje (wa kwanza kushoto)

Bw. Suleiman Saleh, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati, akisalimiana na Mhe. Balozi Mohamed Ben Mansour Al Malek Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akisalimiana Balozi Mohamed Ben Mansour Al Malek Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (wa pili kushoto) akiwa katika mazungumzo na Ben Mansour Al Malek Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania (wa pili kulia) 

Thursday, August 9, 2018

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (The 38th Ordinary of the SADC Summit of Heads of State and Government) utafanyika tarehe 17-18 Agosti, 2018.

Mkutano huu utatanguliwa na mikutano ifuatayo;

(i)            Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda kwa kipindi cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018. Mkutano huu utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).

(ii)           Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Agosti 2018 pamoja; na

(iii)         Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 11Agosti 2018.

Prof Adolf Mkenda, Katibu Mkuu, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anaonagoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Makatibu Wakuu akisaidiana  na Eng. Joseph Nyamhanga, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ( Ujenzi), Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango. Mhe Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ataongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utapokea, kujadili na kutolea maamuzi ya mapendekezo mbalimbali yanayotokana na mikutano ya kisekta na kamati za jumuiya kwa kipindi cha mwaka 2017/18. Pamoja na mambo mengine mkutano huu;

1.    Utafanya uteuzi wa Mwenyekiti wa SADC na inatarajiwa kuwa Jamhuri ya  Namibia ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa  Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha 2018/2019. Nafasi ya Makamu mwenyekiti itajazwa pia na nchi itakayoteuliwa itajulikana tarehe 17Agosti 2018


2.    Uteuzi wa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Inatarajiwa kuwa Jamhuri ya Zambia, ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha 2018/2019. Hivi sasa Tanzania ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwenye Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security)

3.    Maeneo mengine yanayotarajiwa kujitokeza na kujadiliwa katika mkutano huu ni haya yafuatayo

(i)            masuala ya fedha;
(ii)           Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Viwanda wa SADC ( Report on the operaionazaition Maendeleo ya viwanda;
(iii)         Kutia saini itifaki mbalimbali ikiwa ni pamoja na tifaki ya Kulinda Hakimiliki ya Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea ya mwaka 2017.

(iv)         Pia Mkutano huu utatoka na Tamko la nchi wanachama wa SADC la kutokomeza malaria katika ukanda wa SADC ifikapo mwaka 2030. 
=======================================================


Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), Dkt. Stergomena L. Tax  (kushoto) akishuhudia makabidhiano ya uongozi katika nafasi ya Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa SADC baina ya mwenyekiti anayemaliza muda wake, Bw. K E Mahoai Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Mwenyekiti mpya, Balozi Selma Ashipala-Musavya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Namibia.
Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC uliofanyika katika Hoteli ya Safari Mjini Windhoek, Namibia tarehe 09 Agosti 2018. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu(kushoto)  na Mkurugenzi wa Idara ya ushirikiano wa Kikanda (kulia), Balozi Innocent Shiyo wakifuatilia majadiliano wakati wa mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa SADC,Balozi Selma Ashipala-Musavyi akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano huo ambapo aliwashukuru wajumbe kwa kuwa na imani naye na kumpa jukumu hilo na pia alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha anashirikiana na wanachama kusimamia suala la ulinzi na usalama linapatikana ndani ya jumuiya ili kuruhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Bw. K E Mahoai akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa mkutano mara baada ya kukabidhi nafasi ya uenyekiti ambapo aliwashukuru wajumbe kwa ushirikiano alioupata wakati wa uongozi huo kwa taifa lake. 

Wajumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia majadiliano katika mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC.

Picha ya pamoja Katibu Mkuu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena L. Tax (wa nne kutoka kushoto) na Makatibu Wakuu wa Jumuiya hiyo Mjini Windhoek, Namibia.
  

Rais Dkt. Magufuli afanya mazungumzo na Rais Museveni Ikulu jijini Dar es Salaam


Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) mara baada ya mazungumzo na Mhe. Yoweri Museveni Rais wa Jamhuri ya Uganda yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Rais Museveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mashariki amefanya ziara ya siku moja ya kikazi nchini.

Rais Museveni akizungumza na wanahabari mara baada ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dkt. Magufuli, alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu masuala yanayojiri kwenye mkutano wa BRICS uliofanyika Afrika Kusini.

Katika mkutano huo  ambao Afrika Mashariki ilishiriki kama kanda, Rais Museveni alitumia nafasi hiyo kuzishawishi nchi wanachama wa BRICS kuja kuwekeza Afrika Mashariki katika sekta za miundombinu ya uchukuzi na viwanda.

Aidha, Rais Museveni amempongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kufufua Shirika la ndege la Tanzani ambalo litaleta mchango mkubwa katika kukuza utalii nchini. 

Mhe. Yoweri Museveni Rais wa Uganda akizumgumza na wanahabari mara baada ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam
Mhe. Yoweri Museveni Rais wa Uganda akisalimiana na baadhi ya watendaji wa Serikali waliojitokeza kumlaki wakati akiwasili uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam



Mhe. Yoweri Museveni Rais wa Uganda  akiwa na mwenyeji wake Rais Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, akiwasalimia wananchi waliojitokeza kumpokea uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam

Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akijadili jambo na Mhe. Amelia Kyambade Waziri wa Biashara, Viwanda, na Ushirika wa Uganda  

Balozi Ramadhani Mwinyi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia mkutano uliokuwa ukiendelea

Baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Serikali wakimuaga Rais Museveni wakati anaondoka uwanja wa ndege wa jijini Dar es Salaam kurejea nchini kwake

Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifurahi pamoja na wananchi waliojitokeza kumuaga Rais Museveni wa Uganda uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam

Tuesday, August 7, 2018

TAARIFA KUHUSU: ZIARA YA RAIS WA UGANDA NCHINI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU ZIARA YA RAIS WA UGANDA NCHINI


Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni atafanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini tarehe 09 Agosti 2018.

Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na ujirani mwema uliopo kati ya Tanzania na Uganda.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Museveni atapokelewa na mwenyeji wake Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa nchini, Mheshimiwa Rais Museveni atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Mheshimiwa Rais Magufuli yatakayofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yatafuatiwa na Chakula cha Mchana kilichoandaliwa na Mheshimiwa Rais Magufuli kwa heshima ya Mheshimiwa Rais Museveni.

Mheshimiwa Rais Museveni na Ujumbe wake wataondoka nchini siku hiyo hiyo kurejea Uganda.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
07 Agosti 2018