Friday, September 25, 2020
Wednesday, September 23, 2020
SERIKALI YAELEZA SABABU ZA VYOMBO VYA HABARI VYA KIMATAIFA KUSAJILIWA
Serikali imefafanua hatua yake ya kuvitaka vyombo
vya habari vya Kimataifa vinavyotaka kuvitumia vyombo vya habari vya
Tanzania kurusha matangazo yake yana lengo la kutambua vyombo hivyo
vinashirikiana vyombo gani vya hapa nchini na sio kuvizuia kutangaza na
kuendesha vipindi vyake hapa nchini kama inavyoripotiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Dkt. David Concar na kufafanua kuwa mpaka sasa vyombo vyote vya habari vya Kimataifa zimekwishatekeleza matakwa hayo ya kisheria na kupata leseni ya kutangaza na kuendesha vipindi vyao.
"Leo nimekutana na Balozi mteule wa Uingereza
hapa nchini Dkt. David Concar na kumueleza lengo la kusajili vyombo vya Habari vya
kimataifa lilikuwa ni kutaka kujua ni chombo gani cha kimataifa kinashirikiana
na chombo gana hapa nchini lakini pia ilikuwa ni matakwa ya kisheria," Amesema Prof. Kabudi
Kuhusu suala la mabadiliko ya sheria za asasi za kiraia (NGOs) na vyama vya siasa Prof. kabudi amefafanua kuwa lengo lake lilikuwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika fedha zinazoingia kwa asasi hizo pamoja na matumizi yake na kuwa linaendana na sheria na taratibu za kimataifa za kuzuia utakatishaji wa fedha na kuhakikisha makundi yenye nia ovu na misimamo mikali inayokwenda kinyume na tunu za demokrasia hayatumii njia hizo kupenyeza fedha zao.
Balozi mteule wa Uingereza Dkt. David Concar amesema mazungumzo yao mbali
na kulenga masuala ya kidiplomasia na maendeleo pia yalilenga kuangalia namna
ya kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya NGOs na vyombo vya habari vya
kimataifa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni uminywaji wa haki ya uhuru wa vyombo
vya habari.
Katika tukio jingine pia Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark hapa nchini Balozi Mette Norgaard ambapo mbali na suala la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 28 hapa nchini,wamejadili pia masuala yanayohusu mashirikiano katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
akimkabidhi Balozi mteule wa Uingereza nchini, Dkt. David Concar nakala za sheria
ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
akimuonesha Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini, Dkt. David Concar namna
magazeti yanavyo ripoti habari za uchaguzi mkuu bila upendeleo
Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet akiongea na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette
Norgaard Dissing-Spandet akimueleza jambo wakati walipokutana kwa mazungumzo jijini
Dar es Salaam
Monday, September 21, 2020
TANZANIA IMETAJWA KAMA NCHI YA KIELELEZO CHA AMANI NA DEMOKRASIA KATIKA BARA LA AFRIKA
Norway
yaitaja Tanzania kama kielelezo cha amani na demokrasia katika chaguzi Barani Afrika
kutokana na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu unavyofanyika kwa
amani,utulivu na usawa kwa wagombea wa vyama vyote huku wananchi wakijitokeza
kwa wingi kusikiliza sera za wagombea.
Balozi wa Norway nchini Tanzania Balozi Elisabeth Jacobsen ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na kuongeza kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu yamefanyika kwa kufuata taratibu za kisheria huku tume ya Taifa ya Uchaguzi ikishughulikia baadhi ya malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya vyama vya siasa na wadau mbalimbali jambo ambalo linaifanya Tanzania kuwa kinara wa demokrasia katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Pamoja na masuala ya kisiasa Balozi huyo amesema katika mazungumzo yao wamegusia pia masuala ya ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi hususani katika suala la elimu,afya,nishati na uwekezaji pamoja na biashara baina ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amemuomba Balozi huyo wa Norway kuendelea kushirikiana na Tanzania na kumshukuru kwa Nchi hiyo kukubali kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 7 kwa ajili ya mradi wa TASAF jambo litakalosaidia kupunguza umasikini kwa watanzania hususani katika kipindi hiki ambapo nchi nyingi zimeathiriwa na janga la Corona.
Mbali na Balozi huyo wa Norway pia Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden hapa nchini Balozi Anders Sjöberg ambapo amezungumzia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi,haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari na kuvipongeza vyombo vya habari hapa nchini kwa kuandika habari za wagombea wa vyama vyote bila ya ubaguzi na ameonesha kufurahishwa kwake na mwitikio wa wananchi katika mikutano ya kampeni na kuomba maamuzi ya wananchi katika sanduku la kura yaheshimiwe.
Kuhusu suala la haki za binadamu prof. Kabudi amesema taswira inayotolewa kuhusu suala hilo haiakisi hali halisi iliyopo nchini na kwamba Tanzania inaheshimu na kulinda misingi ya haki za binadamu kiasi cha suala hilo kuingizwa katika ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ili kikiingia madarakani kitekeleze na kulinda misingi hiyo.
Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Uswis hapa Nchini Mhe. Didier Chassot.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi
akimuonesha Balozi Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen moja ya kipengele cha
sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi wakati alipokuwa akimkabidhi nakala ya
nyaraka hizo |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi
akikagua nakala za hati za utambulisho za Balozi mteule wa Uswisi hapa nchini
Mhe. Didier Chassot |
Friday, September 18, 2020
TANZANIA YAKABIDHIWA HATI MILIKI YA ARDHI NA SERIKALI YA INDIA
Naibu Afisa Mkuu wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Miji ya India, Bw. Satish Kumar Singh akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda hati miliki ya ardhi ya jengo la Ubalozi, jijini New Delhi tarehe 17 Septemba 2020.
TANZANIA YAKABIDHIWA HATI MILIKI YA ARDHI MJINI NEW
DELHI.
Ubalozi
wa Tanzania nchini India umekabidhiwa rasmi na Serikali ya India Hati Miliki ya
Ardhi yenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 2120.60 ambapo ndipo lilipo jengo
la Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini New Delhi.
Akipokea
hati hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Ofisi za
Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya India tarehe 17 Septemba 2020, Balozi
wa Tanzania nchini humo, Mhe. Baraka H. Luvanda ameishukuru Serikali ya India
kwa hatua hiyo ambayo inathibitisha uhusiano mzuri uliojengeka kati ya nchi
hizi mbili.
Kwa
upande wake, Naibu Afisa Mkuu wa Ardhi wa Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji
ya India, Bw. Satish Kumar Singh amesifu uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo
kati ya India na Tanzania na kueleza kuwa, hiyo ndiyo sababu India imeona
fahari kubwa kuipa Tanzania umiliki wa eneo katika sehemu mahsusi ya Jumuiya ya
Kidiplomasia (Diplomatic Enclave).
Ni
sera na mkakati wa Serikali ya Tanzania ya kuhakikisha kuwa, Balozi zote
zilizopo katika maeneo ya kimkakati zinakuwa na majengo na nyumba za watumishi
ili kuipunguzia Serikali gharama kubwa za kupanga majengo na nyumba hizo. Katika
hafla hiyo Balozi Luvanda aliambatana na maofisa ubalozi, Bibi Natihaika Msuya
na Dkt. Kheri Goloka.
Thursday, September 17, 2020
Wednesday, September 16, 2020
MAADHIMISHO YA TISA YA SIKU YA MARA YAFIKIA TAMATI WILAYANI BUTIAMA
Maadhimisho ya Tisa (9) ya Siku ya Mara (Mara Day) yaliyofanyika katika uwanja wa Maria Nyerere uliopo wilayani Butiama Mkoa wa Mara yamehitimishwa tarehe 15 Septemba, 2020. Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka, kwa mzunguko kati ya Tanzania na Kenya kwa lengo la kuhamasisha utunzaji na Ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa jamii inayolizunguka bonde hilo. Madhimisho ya Mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu "Ikolojia ya Mara iliyotunzwa - Ustawi wetu"
Kwa kutambua umuhimu na changamoto za Ikolojia ya Bonde la Mto Mara, Baraza la Kisekta la 10 la Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria, lililofanyika Kigali, Rwanda mnamo Mei 4, 2012, liliazimia na kutangaza kuwa kila tarehe 15 Septemba kuwa "Siku ya Mara", kwa kuzingatia pia katika msimu huo kuna uhamaji mkubwa wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Serengeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Pori la Akiba la Kitaifa la Maasai-Mara katika Jamhuri ya Kenya.
Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na nchi hizi mbili Tanzania na Kenya maadhimisho ya 9 ya Mto Mara ya mwaka huu , yalipaswa kufanyika nchini Kenya, lakini kutokana na changamoto ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) pande zote mbili zimekubaliana kufanya maadhimisho ya siku hiyo nchini mwao.
Madhimisho ya mwaka huu yalienda sambamba na shughuli mbalimbali kama vile, semina ya masuala ya udongo na kilimo kwa wakazi wa mkoa wa Mara waliohudhuria katika uwanja wa Maria Nyerere, Butiama, maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiliamali, maonesho ya mashamba darasa na kazi za sanaa na ubunifu.
Akizungumza katika sherehe za maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima ambaye pia alikuwa mgeni mashuhuri katika sehehe hizo amesema serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Mara katika Ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa jamii ya pande zote mbili (Tanzania na Kenya) zinazolizunguka Bonde hilo. Sambamba na hilo Mhe. Malima amewahimiza wananchi kuendelea kutunza Ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kushauriwa na Wataamu katika kundesha shughuli zao za kila siku kwenye mzingira yanayozunguka Bonde hilo.
Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Judith Ngoda akizungumza na wananchi kwenye sherehe za madadhimisho hayo amepongeza utayari na ushiriki wa hali ya juu wa wananchi katika kulitunza Bonde la Mto Mara na kuongeza kuwa juhudi, nguvu na umoja unaoonyeshwa na Serikali za nchi zote mbili za Tanzania na Kenya unadhihirisha ushirikiano na mshikamano uliopo katika kuhakikisha ustawi wa uchumi kwa jamii inayozunguka Bonde la Mto Mara unakuwa endelevu kupitia mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima na Mgeni Rasmi wa sherehe za maadhimisho ya 9 ya Siku ya Mara akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Maria Nyerere, wilayani Butiama, Mkoa wa Mara
Tuesday, September 15, 2020
NCHI 15 ZARUHUSIWA KULETA WAANGALIZI WA UCHAGUZI MKUU 2020
Nchi 15 kupitia Balozi zao hapa nchini zimeruhusiwa kuleta waangalizi wa Kimataifa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Octoba, 2020 baada ya Balozi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti na kuongeza kuwa uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza umekuwa tofauti na miaka iliyopita kwa kuwa unafanyika kwa kugharamiwa na fedha za ndani badala ya wahisani jambo ambalo baadhi ya watu walianza kuhofia kutokuwepo kwa waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi.
"Huu ni uchaguzi mkuu ambao kwa mara ya kwanza kwa asilimia 100 tunaugharamia sisi wenyewe kama Serikali ya Tanzania, utaratibu wa uchaguzi chini ya sheria ya uchaguzi na chini ya utaratibu wa Kimataifa huwa tunakuwa na waangalizi wa uchaguzi na mwaka huu nchi hizo 15 kupitia balozi zao zimepata kibali mara baada ya kufuata taratibu za kuomba kuleta waangalizi wa uchaguzi mkuu," Amesema Prof. Kabudi
Mbali na Balozi wa Umoja wa Ulaya pia Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Balozi Roberto Mengoni na baadae Balozi wa Poland Balozi Krzysztof Buzalski ambapo amewakabidhi vitabu vya sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu namna uchaguzi unavyoendeshwa hapa nchini hasusani baada ya uwepo wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani juu ya kuenguliwa kwa wagombea wao.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Balozi Manfred Fanti amesema Nchi za Umoja huo zimekuwa zikifuatilia kwa karibu mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea hapa nchini ambapo mpaka sasa wanaridhishwa na kampeni zinavyofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na zoezi la uangalizi wa uchaguzi huo.
Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni amesema amevutiwa na namna vyombo vya habari vimekuwa vikitoa nafasi kwa wagombea wote kwa uhuru na bila ya ubaguzi na kupongeza namna Watanzania wanavyojitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea mbali na tishio la corona na kwamba ana imani kuwa Kiongozi atakayechaguliwa atakuwa ametokana na utashi wa wananchi.
Mbali na masuala ya uchaguzi mkuu, Waziri Kabudi na Mabalozi hao wamejadili pia masuala ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia,maendeleo ya kiuchumi,biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu,afya,maji na miundombinu.
Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti akimuelezea
jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba John Kabudi walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Prof. Kabudi akimkabidhi Balozi wa Italia nchini
Balozi Roberto Mengoni vitabu vya sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi na
miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Prof. Palamagamba John Kabudi akimfafanulia jambo Balozi wa Poland hapa nchini,
Balozi Krzysztof
Monday, September 14, 2020
UMOJA WA ULAYA KUTOA BILIONI 70 KUSAIDIA MAPAMBANO YA COVID 19 -TANZANIA
Balozi wa
Tanzania nchini Ubelgiji na mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya Mhe.
Jestas Abuok Nyamanga pichani kulia akisisitiza vipaumbele vya Tanzania na zile
za nchi za OACPS kwa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel
kushoto. Kulia mwa Balozi ni afisa Mwandamizi wa ubalozi Dkt Geofrey Kabakaki
na Kushoto mwa Rais Michel ni Afisa wa EU anayeshughulikia masuala ya Tanzania
kutoka makao makuu ya Umoja huo Bibi Christina Barrios.
Mhe. Balozi
Jestas Nyamanga kuliaa akiwasilisha hati za utambulisho kwa Mkuu wa Itifaki wa
Ofisi ya Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya
Thursday, September 10, 2020
Nchi za Ulaya Zahimizwa Kuondoa Vizuizi vya Kusafiri
Mhe.Balozi
Nyamanga kwa nafasi yake ya Mwenyeki wa Mabalozi wa OACPS akimtambulisha Waziri
wa Ushirikiano wa Ujerumani Mhe. Dkt. Muller na timu yake katika Ukumbi wa OACPS. |
Mhe. Balozi Nyamanga akimsindikiza Mgeni wake Mhe.
Dkt.Muller nje ya ukumbi wa mkutano baada ya mkutano wa mashauriano kukamilika.
|
Tuesday, September 8, 2020
MAREKANI YAWATAKA WATANZANIA KUSHIRIKI UCHAGUZI, KUMCHAGUA KIONGOZI BORA
Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo.
Dkt. Wright amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam ambapo wamejadili masuala ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Marekani pamoja na kugusia harakati za kampeni za uchaguzi mkuu unaoendelea hapa Nchini.
Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amemhakikishia Balozi wa Marekani Dkt. Wright kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza hususani katika sekta za utalii,kilimo,na biashara na kumhakikishia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru,haki na wa amani.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika sekta ya utalii serikali ya awamu ya tano imedhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na kupambana na ujangili jambo ambalo limeiwezesha serikali kuanzisha hifadhi za Taifa mpya nane ikiwa ni pamoja na kuimarisha hatua za usalama kwa watalii baada ya janga la corona kumalizika nchini.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Donald Wright amemhakikishia Waziri kabudi kuwa atahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika sekta za kilimo, biashara, huduma za afya na viwanda pamoja na kuhamasisha watalii kutoka marekani kuja nchini.
"Natumia fursa hii kuwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo," Amesema Dkt. Wright.
Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright akimuelezea
jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba John Kabudi walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Prof. Kabudi akimkabidhi Balozi wa Marekani hapa nchini
Mhe. Dkt. Donald Wright moja ya nakala ya kitabu kinachoelezea masuala ya
uchaguzi mkuu nchini Tanzania
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright. Kulia mwa Waziri ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Monday, September 7, 2020
BALOZI IBUGE AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke ofisini kwake jijini Dodoma.
Katika kikao hicho Katibu Mkuu, Balozi Ibuge na Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine wameongelea juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi za uwakilishi wa kudumu kwa Bara la Afrika..
katika Kikao hicho Balozi Ibuge amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo. Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini na Azimio la Sirte la mwaka 1999.
Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezzaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12. tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.
Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka.
Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.
Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufakisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.
Viongozi hao pia wamejadiliana na kubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.
PROF. KABUDI AMUAGA BALOZI WA IRAN NCHINI TANZANIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amemuaga Balozi wa Iran nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini.
Akiongea
katika hafla ya kumuaga balozi wa Iran iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Prof.
Kabudi amempongeza Balozi Farhang kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha
uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi yake na Tanzania.
Pamoja
na mambo mengine, Prof. Kabudi amemuahidi Balozi Farhang kuwa Tanzania
itaendelea kushirikiana na Iran katika sekta za elimu, afya na utalii kwa
maslahi mapana ya nchi zote mbili.
"Kwa
niaba ya Serikali ya Tanzania nakuahidi ushirikiano kutoka kwetu, nakutakia
kila la kheri katika maisha yako nje ya Tanzania na ni imani yangu kuwa utakuwa
balozi mzuri wa Tanzania duniani," Amesema Prof. Kabudi
Kwa
upande wake Balozi Farhang ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa
ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.
Balozi
Farhang ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya Iran na
Tanzania na amepongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea
kuzichukua katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.
Balozi wa Iran Mhe. Mousa Ahmed Farhang akiongea na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi
wakati alipokuwa anamuaga baada ya kumaliza
muda wa uwakilishi nchini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Iran aliyemaliza muda
wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro,
Balozi wa Iran aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Mousa Ahmed
Farhang
Saturday, September 5, 2020
PROF. KABUDI, BALOZI IBUGE WASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO KUFUTIA KIFO CHA RAIS WA ZAMANI WA INDIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wamesaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa India nchini kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa Taifa hilo Shri Pranab Mukherjee kilichotokea tarehe 31 Agosti 2020.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa India nchini Tanzani. Pembeni yake kulia ni Balozi wa India nchini Mhe. Shri Sanjiv Kohli