Thursday, November 18, 2021

WAZIRI MULAMULA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA IRELAND

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Mhe. Mary O'Neil walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Mhe. Mary O'Neil akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 


Na Waandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano ya muda mrefu yaliyopo baina ya Tanzania na Ireland.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Mulamula ameiomba Serikali ya Ireland kusaidia harakati za Tanzania za kushawishi na kuvutia uwekezaji na biashara nchini ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Mhe. Waziri pia ameomba Ireand kuendelea kusaidia eneo la kuwawezesha na kuwajengea uwezo vikundi vya kijamii vya wanawake nchini ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za ufadhili wa masomo kwa wananchi wa Tanzania.

“Tanzania na Ireland tumekuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu sasa, mmekuwa mkitusaidia katika maeneo mbalimbali, niombe muelekeze nguvu zenu katika kusaidia vikundi vya kijamii vya wanawake nchini ili kuwasaidia hasa katika kuwajengea uwezo ili nao washiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu,” amesema Waziri Mulamula.

Naye balozi wa Ireland nchini Mhe. O’Neil ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuongeza kuwa kuna muwekezaji kutoka nchini humo ambaye ameonesha utayari wa kuwekeza katika eneo la ubanguaji wa Korosho mjini  Mtwara.

Balozi O’Neil pia amesema nchi yake kupitia taasisi ya utawala wa sheria inashirikiana na Mahakama ya Tanzania kuangalia namna ya kupunguza unyayasaji wa kijinsia katika jamii mbalimbali nchini na wanatarajia kushiriki kikamilifu katika siku 16 za kupinga ukatili huo zinazotarajiwa kufayika nchini.

“Taasisi ya ‘Irish rule of law’ kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania hasa katika eneo la unyanyasaji wa kijinsia zinaangalia kwa pamoja juu ya namna ya kupunguza vitendo hicyo nchini na tutashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku 16 za kupinga vitendo hivyo,” amesema Balozi O’Neil 

 

BALOZI MBENNAH ATETA NA MAKAMU RAIS WA JAMHURI YA MAURITIUS

BALOZI MBENNAH ATETA NA MAKAMU RAIS WA JAMHURI YA MAURITIUS

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Prof. Emmanuel Mbennah amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu Rais wa Jamhuri ya Mauritius Mhe. Eddy Boissezon, GOSK.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wameonesha kuridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo na kuahidi kuendelea ushirikiana katika sekta za uchumi, biashara  utalii na uwekezaji.

Makamu huyo wa Rais pia ameiipongeza Tanzania kwa ushindi wa Bw. Abdulrazak Gurnah katika Tuzo ya Amani ya Fasihi.

Oktoba 7, 2021 Mwandishi wa riwaya nchini Tanzania Abdulrazak Gurnah alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kuhusu fasihi 2021.


Makamu Rais wa Jamhuri ya Mauritius Mhe. Eddy Boissezon, GOSK akiteta na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Prof. Emmanuel Mbennah  


Makamu Rais wa Jamhuri ya Mauritius Mhe. Eddy Boissezon, GOSK akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Prof. Emmanuel Mbennah  




Wednesday, November 17, 2021

TANZANIA, KOREA KASKAZINI ZAAHIDI KUIMARISHA DIPLOMASIA

Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) zimekubaliana kuimarisha misingi ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Balozi wa Korea Kaskazini mhe. Kim Yong Su walipokutana leo kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri Mulamula amesema Tanzania na Korea Kaskazini zitaendelea kushikiana katika kuimarisha zaidi misingi ya uhusiano baina ya nchi hizo kwa kuzingatia Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

“Nimemhakikishia Balozi wa Korea Kaskazini kuwa sisi misingi yetu ya Sera ya Mambo ya Nje (Tanzania) haijabadilika iko vilevile, na tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu, amesema Waziri Mulamula.

Kwa upande wake Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini, Mhe. Kim Yong Su amesema kuwa Korea na Tanzani ni marafiki wa muda mrefu na kwa mkutano wetu tumejadili namna ya kuboresha uhusiano wetu wa kidiplomasia.

Balozi Kim Yong Su amesema kuwa pamoja na mambo mengine wamekubaliana kuboresha uhusiano wa kidiploasia kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Ushirikiano wa Korea Kusini na Tanzania ni mzuri na imara ………. naahidi kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi, ulinzi na kilimo hii ikiwa ni jitihada za kuimarisha ushirikiano wetu kwa maslahi ya mataifa yetu,” amesema Balozi Su.

Balozi Su ameongeza kuwa Korea Kaskazini inapongeza jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Tanzania katika kuhakikisha inasonga mbele kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi pamoja na kuimarisha/kuboresha diplomasia na mataifa mengine duniani.

“Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazaochukua katika kuimarisha uchumi wa Tanzania na wananchi wake pamoja na kidiplomasia,” ameongeza Balozi Su.

Tanzania na Korea Kaskazini zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia Aprili, 1992, ambapo nchi hizi zimekuwa zikishirikiana kidiplomasia katika sekta ya elimu, afya, sayansi na utamaduni pamoja na utalii.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Heshima wa Kazakhstan nchini Tanzania Bw. Ameir Nahdi ambapo viongozi hao wajejadili masuala mbalimbali ikiwemo za biashara na uwekezaji katika sekta za mafuta na gesi, kilimo pamoja na uchimbaji na uchakataji wa madini na utalii.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Balozi wa Korea Kaskazini nchini Mhe. Kim Yong Su katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini Mhe. Kim Yong Su akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini Mhe. Kim Yong Su ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Korea Kaskazini hapa nchini Mhe. Kim Yong Su mara baada ya kumaliza mkutano wao leo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mwakilishi wa Heshima wa Kazakhstan nchini Tanzania Bw. Ameir Nahdi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Mwakilishi wa Heshima wa Kazakhstan nchini Tanzania Bw. Ameir Nahdi akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam



Tuesday, November 16, 2021

MAJALIWA AFUNGUA KONGAMANO LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UINGEREZA

 

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza kufungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati wa Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Mjumbe maalum wa Waziri Mkuu wa uingereza anayeshughulikia masuala ya biashara kwa Tanzania Bw. Lord Walney ambaye yuko nchini kuhudhuria Kongamano hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Dotto James katika Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipofungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza wakifuatilia kongamano hilo jijini Dar es Salaam.



Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amefungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza lililowakutanisha wafanyabiashara zaidi ya 300 kutoka Tanzania na Uingereza jijini Dar es Salaam.

Mhe. Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa Uingereza kuja kwa wingi nchini kuwekeza na kufanya biashara kwani Serikali ya Tanzania iko tayari kuwapokea wakati wowote.

‘‘Kwanza niishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuonesha  nia na utayari wa kuwekeza nchini, nichukue fursa hii kuwakaribisha sana na kuwaahidi kuwa Tanzania iko tayari kuwapokea wakati wowote, na niwaombe muendelee kuja kwa wingi kuwekeza,’’ amesema Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa pia ametoa shukurani kwa Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya biashara kwa Tanzania Bw. Lord Walney kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania. Bw. Walney pia yuko nchini kuhudhuria Kongamano hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uingereza.

Amesema ni matumaini yake kuwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uingereza wataendelea kuimarisha mahusiano yao ambayo yatakuza uchumi wa Tanzania na kutoa  ustawi kwa wale watakaoshiriki katika mnyororo wa uwekezaji kati ya nchi hizo.

Amesema Tanzania imeboresha mazingira yake ya uwekezaji ili kuvutia zaidi wawekezaji na kuongeza kuwa Tanzania iko tayari kuvutia uwekezaji katika maeneo ya kilimo, utengenezaji dawa, uvuvi, gesi na mafuta, alizeti, kuchakata mazao ya kilimo na mengineyo na hivyo kutengeneza ajira kwa vijana na kuongeza mapato ya serikali.

Amesema Tanzania inahitaji mitaji na teknolojia kutoka Uingereza ili kuboresha na kuutumia ukanda wa mwambao wa bahari ya Hindi kutoka Tanga hadi Mtwara na hivyo kukuza uchumi wa  nchi na kuitaka Sekta binafsi kutumia vizuri kikao hicho kwa kuzungumzia maeneo wanayoweza kufanya biashara na wawaalike kuja nchini kuwekeza na wawe sehemu ya uwekezaji huo ili kuwahakikishia usalama wa uwekezaji wao.

Katika Kongamano hilo kumefanyika mijadala kati ya Serikali ya Tanzanaia na Serikali ya Uingereza, wafanyabiashara na wafanyabiashara na Serikali na wafanyabiashara ili kupata uelewa wa pamoja wa jinsi mambo yalivyo na hivyo kuvutia uwekezaji na kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili kwa  manufaa ya pande mbili.

Awali kizungumza katika Kongamano hilo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesema kufanyika kwa kongamano hilo ni utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo kwa kuvutia uwekezaji na kukuza biashara nchini na kuongeza uwepo wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza kunaonesha uhusiano mkubwa uliopo baina ya Tanzania na Uingereza na kuna haja ya kuendelea  kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo.

Kongamano hilo lina lengo la kuhamasisha Wafanyabiashara wa Uingereza kuja kwa wingi kuwekeza nchini na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao kwa wingi zaidi nchini Uingereza. Kongamano hilo pia limelenga kubadilishana uzoefu kwa wafanyabiashara wa nchi hizo ikiwa ni  pamoja na kujadili fursa na Changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Biashara na Uwekezaji katika pande zote mbili na namna bora ya kuzitumia fursa hizo.

 


 


 

 

 

 

Monday, November 15, 2021

WAZIRI MULAMULA AAGANA NA BALOZI WA KOREA KUSINI

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Tae-ick Cho wakati alipokwenda kumuaga Mhe. Waziri katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Tae-ick Cho katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Tae-ick Cho akimkabidhi zawadi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alipofika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kumuaga
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha ya jahazi Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Tae-ick Cho katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Tae-ick Cho katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caesar Waitara.

 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kumuaga Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Tae-ick Cho katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

  “Katika kipindi chake cha uwakilishi ameiwakilisha vyema nchi yake na kufurahishwa na namna ushirikiano baina ya Tanzania na Korea ya Kusini ulivyoimarika hasa katika miradi ya maendeleo ya kimkakati na nimemuomba aendelee kuwa Balozi mzuri wa Tanzania huko aendako,” amesema Balozi Mulamula.


Nae Balozi wa Korea ya Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini, Mhe. Tae-ick Cho ameipongeza Tanzania kwa hatau mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi, kijamii  na kisiasa ambazo imekuwa ikizichukua chini ya Uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan.

 

 



BALOZI MULAMULA AMPOKEA MJUMBE MAALUM WA WAZIRI MKUU WA UINGEREZA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshugulikia masuala ya biashara Tanzania Bw. Lord Walney walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshugulikia masuala ya biashara Tanzania Bw. Lord Walney akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati wa mazungumzo yao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) katika kikao na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshugulikia masuala ya biashara Tanzania Bw. Lord Walney kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshugulikia masuala ya biashara Tanzania Bw. Lord Walney, katika picha ya pamoja na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. David Concar (mwenye suti ya bluu), kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amempokea na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshugulikia masuala ya biashara Tanzania Bw. Lord Walney katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.


Bw. Walney yupo nchini kwa ziara maalum yenye lengo la kujitambulisha rasmi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushiriki Kongamano la Biashara baina ya Tanzania na Uingereza litakalofanyika Jijini Dar es Salaam Tarehe 16 Novemba 2021.


Viongozi hao wamejadili fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na namna ya kuangalia njia za kuvutia wawekezaji kutoka Uingereza kuja kuwekeza nchini na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao nchini Uingereza.


Akiongelea ujio wa Bw. Walney nchini, Waziri Mulamula amesema kuwa pamoja na kwamba Tanzania na Uingereza zimekuwa na mahusiano ya muda mrefu katika eneo la biashara lakini biashara ambapo wafanyabiashara wa Uingereza wamekuwa wakiuza zaidi kuliko watanzania na kuongeza kuwa, kongamano hilo litawakutanisha wafanyabiashara wa Uingereza na Tanzania kwa lengo la kuhamasisha Waingereza kuja kuwekeza zaidi nchini na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao zaidi Uingereza.

 
“Kongamano hilo litawakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Uingereza kwa lengo la kuhamasisha Waingereza kuja kuwekeza zaidi nchini na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao Uingereza,” amesema Balozi Mulamula.


Waziri Mulamula ameongeza kuwa Kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Uingereza litafunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam.


Kwa upande wake, Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshugulikia masuala ya biashara Tanzania Bw. Lord Walney amesema kongamano hilo litatoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili kukutana na kujadiliana juu ya fursa zilizopo katika nchini hizi na namna ya kuzitumia kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Naamini kuwa kongamano hilo litakuwa nafasi muafaka kwa wafanyabiashara wa Uingereza na Tanzania kukutana na kujadili fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zinazopatika kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi zetu,” amesema Bw. Walney.


Kongamano hilo pia linatarajiwa kuhusisha wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 300 kutoka Tanzania na Uingereza.