Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amepokea ujumbe
maalum kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry uliowasilishwa
kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia
masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.
Akizungumza mara baada ya
kupokea ujumbe huo leo tarehe 26 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Tax
ameishukuru Serikali ya Misri kwa kuendelea kuthamini ushirikiano wa kihistoria
uliopo baina yake na Tanzania hususan kwenye sekta ambazo zinagusa maisha ya
wananchi moja kwa moja kama afya, elimu, maji, nishati na ujenzi wa
miundombinu.
Amesema, ni kutokana na kuthamini
mchango unaotolewa na Misri kwenye sekta mbalimbali za maendeleo nchini Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alifanya ziara nchini humo mwezi Novemba 2021 na maeneo mbalimbali ya
ushirikiano yalijadiliwa na kukubalika.
“Ninayo furaha kukukaribisha
nchini Mhe. Waziri. Nakiri kupokea ujumbe huu muhimu kutoka kwa Waziri
mwenzangu. Nitaupitia na kuufanyia kazi na kuwasilisha kwenu mrejesho haraka
iwezekanavyo”, amesema Mhe. Dkt. Tax.
Naye, Mhe. Issa amempongeza
Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa katika wadhifa huo mpya na kumweleza utayari wa
Serikali ya Misri katika kushirikiana naye.
Kadhalika amesema, Serikali ya Misri itaendelea kushirikiana na
Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza na kukamilisha
miradi yote ya pamoja ambayo nchi hizo zimekubaliana ukiwemo Mradi wa Bwawa la
Kufua Umeme la Julius Nyerere.
“Mradi wa Kufua Umeme wa
Julius Nyerere ni kwa ajili ya
Watanzania. Mradi huu ni mkubwa na wa kwanza kwa Misri kuutekekeleza hapa
nchini. Hivyo tutajitahidi kama Serikali kushirikiana na Tanzania ili
kuhakikisha mradi wote unakamilika na kukabidhiwa”, alisisitiza Mhe. Issa.
Pia Mhe. Issa alitumia nafasi hiyo kuikaribisha
Tanzania kushirki kwenye Mkutano wa 27 wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya
Tabianchi (COP27) utakaofanyika mwezi Novemba 2022 katika Mji wa Sharm El
Sheikh, nchini humo.
Kwa upande wake, Waziri wa
Nishati, Mhe. January Makamba ambaye alishiriki mazungumzo hayo amesema, Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere ni
alama ya ushirkiano kati ya Tanzania na Misri na kwamba Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wote unaohitajika kwa
Serikali ya Misri na Timu ya Wataalam wa Mradi huo ili kuufanikisha.
|
Waziri wa Mambo ya Nje
na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea
ujumbe maalum kutoka
kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Sameh Hassan Shoukry
uliowasilishwa kwake
na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri
anayeshughulikia
masuala ya Afrika wa nchi hiyo, Mhe. Sherif Issa.Mhe. Dkt. Tax amepokea
ujumbe huo leo tarehe 26 Oktoba, 2022 akiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara
zilizopo jijini Dar es Salaam
|
|
Mhe. Dkt. Tax akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia
masuala ya Afrika, Mhe. Sherif Issa | | |
|
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ambaye alishiriki mazungumzo hayo naye akichangia jambo
|
|
Mazungumzo yakiendelea
|
|
Mhe. Dkt. Tax na mgeni wake wakimsikiliza Balozi wa Misri hapa nchini Mhe. Mohammed Gaber Abulwafa wakati akifafanua jambo
|
|
Mhe. Makamba akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Maharage Chande pamoja na wadau wengine wakaishiriki mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Issa (hawapo pichani)
|
|
Picha ya pamoja
|