Monday, May 15, 2023

MWILI WA MEMBE WAWASILI RONDO, LINDI


Mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe umewasili kijijini kwake Rondo mkoani Lindi kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2023.

Mwili wa Marehemu Membe umewasili kijijini hapo majira ya saa  06.40 mchana na Helikopta ya Jeshi na kupokelewa na mamia ya waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Limdi, Mhe. Shaibu Ndemanga

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb.) aliongoza ujumbe uliosafiri na mwili wa marehemu Membe kutoka Jijini Dar es Salaam hadi Rondo mkoani Lindi. Mhe. Nape ni Mbunge wa Jimbo la Mtama ambalo awali liliongozwa na Marehemu Membe kwa miaka 15 mfululizo (2000-2015).

Mwili marehemu mara baada ya kuwasili nyumbani kwake ulipokelewa na wanafamilia kwa simanzi, huzuni pamoja na vilio.

Mwili huo utalala nyumbani kwake hadi kesho tarehe 16 Mei 2023 atakapopumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Marehemu Membe aliaga Dunia tarehe 12 Mei, 2023 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki, Jijini Dar es Salaam.
Helikopta ya Jeshi iliyobeba mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Marehemu Bernard Membe ikiwasili kijijini kwake Rondo

Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa umebebwa na wananchi ulipowasili kijijini kwake Rondo
Wananchi wa Rondo na kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwa wamejipanga kupokea mwili wa Marehemu Bernard Membe ulipowasili nyumbani kwake kijiji cha Rondo, Lindi. 

Sehemu ya waombolezaji wakiwa katika hali ya huzuni na majonzi kwenye msiba wa Marehemu Bernard Membe kijijini kwake Rondo, Lindi 

Sunday, May 14, 2023

RAIS SAMIA ASHIRIKI KUUAGA MWILI WA BERNARD MEMBE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameungana na waombelezaji mbalimbali kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 2007 hadi 2015, Ndugu Bernard Kamilius Membe katika viwanja kwa Karimjee jijini Dar Es Salaam tarehe 14 Mei, 2023.


Akitoa salamu za rambirambi, Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa kuondoka kwa Ndugu Membe kumeleta masikitiko kwake binafsi, familia yake, Serikali, wadau mbalimbali, familia ya marehemu, wana Lindi na wananchi kwa ujumla. 


“Msiba huu umewagusa watu wengi ndani na nje ya nchi, kutokana na uhodari wake katika masuala ya siasa na diplomasia, hivyo nguzo kuu imeondoka Mwenyezi Mungu awape wanafamilia subira katika kipindi hiki cha majonzi”


Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ambaye pia ni mwenyeji wa tukio hilo la kuaga mwili, katika salamu zake za pole alieleza kuwa Wizara imempoteza kiongozi mahiri na hodari ambaye alijenga misingi mizuri katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.

“Marehemu Membe pamoja na kusimamaia maslahi ya nchi alitumia umahiri wake kuwajenga watumishi wa Wizara ambao kwa sasa wengine wanahudumu katika nafasi za Balozi”.


Aidha, Ndugu Membe alikuwa mcheshi, mwenye upendo na hodari hivyo Wizara itaendelea kuyaenzi mafanikio yaliyofanywa naye wakati wa utumishi wake.


Tukio hilo la kuaga mwili wa Marehemu Bernard Membe lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ambao ni pamoja na: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa; Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma; Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu; Mawaziri, Manaibu Waziri, Wakuu wa Taasisi na Viongozi wengine wa Serikali, Taasisi binafsi na za dini na vyama vya siasa.


Wengine waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na: Mwakilishi wa kundi la wake wa Viongozi (Millenium group) Bi. Arafa Kikwete; Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe; Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Chongolo; Mkuu wa Mabalozi na Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih; Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Amos Makala; Mtendaji Mkuu wa Mahakama (kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania), Prof. Elisante Ole Gabriel; na Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Mussa Azan Zungu.

=============================================

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Kamilius Membe mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2023
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na waombolezaji wakati wa kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Kamilius Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2023

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe tarehe 14 Mei, 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji walioshiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa pole kwa Mjane wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe na familia yake  katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimpa pole Denis Membe mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei 2023.

Pichani, sehemu ya Waombolezaji walioshiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,, Marehemu Bernard Membe. 

Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe likiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

VIONGOZI MBALIMBALI WAMUAGA MHE. MEMBE KARIMJEE

Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umeungana na waombolezaji wengine kumuaga  aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Mhe. Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.  

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa (Mb.) akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  (Mb.) akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassoro Mbarouk  akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga  akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Majeshi  mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Ethiopia nchini  Mhe. Yonas Yosef akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  (Mb.) akisalimiana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (2021- 2022) wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam. kulia ni Mkuu wa Majeshi Msataafu Jenerali Davis Mwamunyange.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  (Mb.) akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Joseph Sinde Warioba wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam. Kushoto ni naibu Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azan Zungu.

Baadhi ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Saturday, May 13, 2023

SALAAM ZA RAMBIRAMBI

 

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea kwa mshtuko, taarifa za kifo cha Mhe. Bernard Kamillius Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (2007-2015).

Kama Mawaziri wa Mambo ya Nje aliyehudumu Kwa kipindi Kirefu, atakumbukwa kwa mchango wake katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa. 
Wizara inatoa pole za dhati kwa familia na watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza Mwanadiplomasia mahiri. 
"Tunaiombea Roho yake ipumzike Kwa Amani"

Friday, May 12, 2023

BALOZI SHELUKINDO AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MABALOZI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana na kuzungumza na mabalozi wa China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan kwa nyakati tofauti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao.

Mabalozi waliokutana na Balozi Shelukindo ni Balozi wa China, Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Kenya, Mhe. Isaac Njenga, Balozi wa Denmark, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet, Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali.

Dkt. Shelukindo amekutana na mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili na kuahidi kuongeza ushirikiano katika sekta za elimu, michezo, biashara na uwekezaji.

“Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan ambapo uhusiano huo umesaidia kuwa na misingi imara ya ushirikiano kwa maslahi mapana ya Taifa letu na nchi zao,” alisema Dkt. Shelukindo

“Vilevile nimepata fursa ya kukutana na balozi wa Sudan na amenijulisha juu ya uwezekano wa mapigano yanayoendelea nchini humo kufikia mwisho kwa njia ya makubaliano. Na amenihakikishia kuwa wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini Sudan watapokelewa na kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika.

Amesema tarehe 11 Mei, 2023 pande zinazopigana nchini humo zilisaini mkataba wa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano,” alisema Dkt. Shelukindo 

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Sudan nchini, Mhe. Mustafa Ali amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumalizika kwa mapigano yanayoendelea nchini humo kwa njia ya makubaliano ya amani. 

“Naomba nikuhakikishie kuwa Serikali ya Sudan itawapokea wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini kwetu na kupata fursa ya kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika,” alisema Mhe. Mustafa Ali

Naye Balozi wa China nchini, Mhe. ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendeleza harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati.

Kwa nyakati tofauti mabalozi hao  wameishukuru Tanzania kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiupata wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuahidi kuwa nchi zao zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwa maslahi ya pande zote.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Isaac Njenga 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Shwahiba Mndeme pamoja na Afisa wa Idara hiyo, Bi. Kisa Mwaseba. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



TANZANIA, UINGEREZA KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Uingereza katika sekta za biashara pamoja na uwekezaji.

Dhamira hiyo imeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) aliposhiriki hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023. 

 Dkt. Tax alisema kuwa Tanzania na Uingereza zinafurahia uhusiano mzuri wa kihistoria na kirafiki uliodumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa kupitia uhusiano huo, Tanzania na Uingereza zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu katika sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote. 

“Uingereza ni miongoni mwa washirika wa kibiashara wa Tanzania wa siku nyingi na imesalia kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na uwekezaji mkubwa wa Kigeni hapa nchini katika sekta mbalimbali. Tanzania inaahidi kuendelea kushirikiana na utawala wa Mtukufu Mfalme Charles III katika nyanja mbalimbali,” alisema Waziri Tax

Alisema Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi. 

“ Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi, Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Uingereza kwa manufaa mapana ya nchi na watu wake,” aliongeza Dkt. Tax. 

Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Waingereza na wageni mbalimbali walioshiriki hafla hiyo kuwa, Tanzania ina mazingira salama ya uwekezaji na biashara kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja na sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar alisema Uingereza na Tanzania zimeendelea kuwa na urafiki imara kwa muda mrefu kutokana na heshima, dhamira ya kukuza maendeleo na kuthaminiana kwa wananchi wa pande zote mbili.

“Uingereza imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta ya biashara na uwekezaji ambapo wafanyabiashara wengi kutoka Uingereza wamewekeza nchini Tanzania, tutaendelea kuwaeleza kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na biashara ili wawekeze kwa wingi” alisema Balozi Concar.   

Balozi Concar aliongeza kuwa Ushirikiano wa Uingereza na Tanzania umekuwa ukistawishwa na juhudi za maendeleo katika sekta mbalimbali hususan za fedha zikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

“Uingereza na Tanzania hivi karibuni zitasaini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya afya hususan Utafiti wa matibabu lengo likiwa ni kuimarisha sekta ya afya. Uingereza na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa lengo la kuendeleza malengo ya pamoja kwa maslahi ya pande zote mbili,” aliongeza Balozi Concar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023

Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akiwakaribisha wageni mbalimbali walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023

Sehemu ya wageni walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023

Sehemu ya wageni walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023


Thursday, May 11, 2023

TANZANIA YAMTEUA DKT. TULIA KUGOMBEA URAIS UMOJA WA MABUNGE DUNIANI

 




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (Hawapo pichani), wakati alipokuwa akiwaomba kumnadi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson ambaye anagombea nafasi ya Urais katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Mhe. Tax amezungumza na Mabalozi hao Jijini Dar es Salaam.

Mbunge wa Singida Magharibi ambaye pia ni mbunge wa Bunge la IPU, Mhe. Elibariki Kingu akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini Jijini Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wakati alipokuwa akiwaomba kumnadi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson ambaye anagombea nafasi ya Urais katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU)


Sehemu ya Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa akizungumza nao Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini

FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO NCHINI JAPAN


 

Wednesday, May 10, 2023

TANZANIA, UGANDA ZAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara ili kuendeleza na kuboresha ushirikiano kati ya mataifa hayo kwenye nyanja mbalimbali.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa majadiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano wao, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha michakato ya kuendeleza miundombinu ili kukamilisha barabara zinazounganisha Uganda na Tanzania, usafiri katika ziwa Victoria ambao pia utaunganisha reli ya kisasa ya SGR kwenda Uganda. 

“Tumewekeana muda ili tuweze kukamilisha baadhi ya masuala kwa haraka lakini pia kuona jinsi gani pale panapo hitaji kila nchi itoe rasilimali iweze kujipanga na kuhakikisha rasilimali hizo zinapatikana kwa wakati,” alisema Dkt. Tax.

Katika mkutano huo viongozi hao wamekubaliana pia kukamilisha ujenzi wa kituo cha uokoaji Jijini Mwanza kitakachoshughulikia maafa yanayoweza kutokea katika ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga amesema mkutano huo umewawezesha kukamilisha baadhi ya mambo yaliyokuwa mezani na kujipa muda hadi mwishoni mwa mwezi Julai 2023 kukamilisha machache yaliyosalia.

Amesema wataendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili waweze kutatua vikwazo vilivyopo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha. 

“Tuendelee kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja ili tuweze kutatua vikwazo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha,” alisema Mhe. Kadaga

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga (aliyevaa barakoa) katika mkutano wao uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga akiongoza ujumbe wa Uganda katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Ujumbe wa Uganga ukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga



Tuesday, May 9, 2023

NAIBU WAZIRI MKUU WA KWANZA WA UGANDA AWASILI NCHINI KIKAZI

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Mhe. Kadaga anatarajia kuwa na mkutano wa majadiliano baina yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) tarehe 10 May, 2023, katika Ofisi Ndogo ya Wizara, Jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kuwasili nchini, Mhe. Kadaga alipokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yatahusu kuimarisha ushirikino kati ya Tanzania na Uganda, pamoja na ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Rebecca Kadaga akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz (katikati) pamoja Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye (kulia) baada ya kuwasili amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere