Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha haki
za binadamu zinalindwa na kutekelezwa kwa mujibu wa mikataba ambayo Tanzania ni
mwanachama.
Kauli hiyo imetolewa na
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi wakati akifungua Kikao cha 77 cha Kawaida cha Tume ya Afrika ya Haki za
Binadamu na Watu kilichofanyika jijini Arusha tarehe 20 Oktoba 2023.
Mhe. Dkt. Mwinyi ambaye
alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwenye ufunguzi wa kikao hicho amesema
kuwa jitihada za Serikali za kulinda na kuimarisha haki za binadamu zimewezesha
kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya upatikanaji wa haki mbalimbali zikiwemo
haki ya usawa mbele ya sheria, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, haki ya
kumiliki mali, na uhuru wa vyombo vya habari.
“Kwa taarifa ni kwamba
kutokana na uhuru huo wa vyombo vya habari, hivi sasa Tanzania ina vyombo vya
habari vingi ikiwemo Radio 210,Televisheni 56, Magazeti 288 pamoja na mitandao
mbalimbali ya kijamii. Pia tumefikia hatua kubwa ya kuimarika kwa uhuru wa
kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia
usawa wa kijinsia,” amesema Mhe. Rais Dkt. Mwinyi.
Kadhalika ameongeza kusema,
Tanzania na Afrika kwa ujumla inaheshimu haki za binadamu na watu kwa
kuzingatia utamaduni, maadili na tunu kama waafrika ambapo katika kutekeleza
jukumu hili Serikali ya Tanzania inasimamia haki za binadamu kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kanuni na taratibu zilizopo.
“Katika Katiba yetu, haki
za binadamu zimeainishwa kuanzia Ibara ya 12 hadi 24 lakini pia Katiba yetu
kuanzia Ibara ya 25 hadi 30 imeanisha wajibu wa kila raia” amesisitiza Mhe.
Rais Dkt. Mwinyi.
Pia ameeleza kuwa katika
kuhakikisha haki za binadamu na watu zinalindwa na kutetewa kikamilifu hapa
nchini, Serikali ilianzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni
Taasisi ya Kitaifa yenye jukumu la kulinda, kutetea na kuhifadhi haki hizo.
Akizungumzia hali ya
ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika amesema bado jitihada za pamoja
zinahitajika ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazorejesha nyuma jitihada
hizo ikiwemo mapinduzi ya Serikali zilizo madarakani, vita vya wenyewe kwa wenyewe,
mila na desturi zisizofaa, ukatili wa kijinsia, athari hasi za utandawazi na
uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao.
Mhe. Rais Dkt. Mwinyi
alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha washiriki kutenga muda wao na kutembelea vivutio
vya utalii vinavyopatikana kote nchini pamoja na Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu
ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuheshimu haki za binadamu na kuitaja amani iliyopo kama alama na kielelezo cha
ulinzi wa haki hizo za binadamu.
“Nchi hii inaheshimu haki
za binadamu na amani inatawala. Tanzania ina utamaduni wa kutatua changamoto
zao kwa njia ya amani na katika hili tunapaswa kujifunza” alisisitiza Mhe.
Lumbu.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali
Suleiman amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Uongozi wa Mhe.
Dkt. Mwinyi imeendelea kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwa kuboresha
mazingira na huduma za kijamii ikiwemo afya, maji, miundombinu na elimu.
Awali akimkaribisha Mhe.
Dkt. Mwinyi kuzungumza, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi
Chana amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kikao hicho muhimu kufanyika nchini na kwamba
kikao hicho pamoja na mambo mengine kitajadili namna bora ya kuendelea
kusimamia masuala ya haki za binadamu na watu barani Afrika.
Pia Mhe. Dkt. Chana
amesema kikao hicho ambacho kilitanguliwa na vikao viwili vya Asasi za kiraia
na Taasisi za Haki za Bianadamu, kimehudhuriwa na takribani wadau 1,000 kutoka
Serikalini, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Asasi za Kiraia,
waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
|
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akifungua rasmi Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha tarehe 20 Oktoba 2023. Mhe. ais Dkt. Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi huo. Kikao hicho kitafanyika kuanzia tarehe 20 Oktoba 2023 hadi 09 Novemba 2023
|
|
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 20 Oktoba 2023 hadi 09 Novemba 2023.
|
|
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe.
Haroun Ali Suleiman akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
|
|
Mwenyekiti
wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
|
|
Sehemu ya Viongozi na wageni waalikwa wakishiriki Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
|
|
Sehemu nyingine ya washiriki
|