Monday, February 8, 2016

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi Wateule wa Congo na Namibia nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hapa nchini, Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba. Hafla hiyo fupi ilifanyika Wizarani tarehe 08 Februari, 2016
Mhe. Dkt. Mahiga akizungumza na Balozi Mutamba mara baada ya kupokea nakala zake za hati za hati za utambulisho. Pamoja na mambo mengine walizungumzia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania  na DRC.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Medard Ngaiza akiwa na Afisa kutoka Idara hiyo, Bi. Elizabeth Rwitunga wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Mahiga na Balozi Mutamba (hawapo pichani)
Kaimu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. James Bwana (kulia) akiwa pamoja na Msaidizi wa Waziri Mahiga, Bw. Adolf Mchemwa (kushoto) na Afisa Habari, Rose Mbilinyi wakifuatilia mazungumzo kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Mutamba ambao hawapo pichani.
Mazungumzo yakiendelea.

 ....Waziri Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Namibia nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria. Hafla hiyo fupi ilifanyika Wizarani tarehe 08 Februari, 2016
Mhe. Dkt. Mahiga akimsikiliza Balozi Samaria walipozungumza kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia.
Dkt. Mahiga akiagana naMhe. Balozi Samaria mara baada ya kupokea Nakala za Hati za Utambulisho.

============================================

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi Wateule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Jamhuri ya Namibia leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

Wakati wa mazungumzo na Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba, Balozi Mteule wa DRC hapa nchini, Mhe. Waziri alimweleza kuwa katika mambo yanayoleta ukaribu na ushirikiano kati ya Tanzanzia na Jamhuri ya kIdemokrasia ya Kongo ni Lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa ikitumika na nchi zote mbili.

Aidha, Mambo mengine ambayo aliyataja kuwa yanaziunganisha nchi hizi mbili ni shughuli za kibiashara baina ya wananchi wa DRC na Tanzania na Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa ikitumika na wafanyabiashara wa DRC na Serikali yao kupitisha bidhaa.
Hivyo. Mhe. Waziri alitaja mambo hayo kuwa yataimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na DRC ambao ulianza muda mrefu uliopita.

Sambamba na hilo Mhe. Mahiga alisisitiza umuhimu wa Serikali ya DRC kuimarisha amani na utulivu Kaskazini mwa Jimbo Kivu ili wananchi wa jimbo hilo waishi maisha ya kawaida na kuweza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakati wa mazungumzo na Mhe. Theresia Samaria, Balozi mpya wa Namibia hapa nchini, Mhe. Waziri alieleza namna Tanzania ilivyoshiriki katika shughuli za ukombozi Kusini mwa Bara la Afrika  ambapo pamoja na mambo mengine Tanzania ilisaidia Namibia kufungua kambi kwa ajili ya mafunzo ya wapigania uhuru eneo la Kongwa Mkoani Dodoma na kurusha vipindi vyake kupitia Radio Tanzania. 

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mahiga aliwahakikishia Mabalozi hao wapya kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ili waweze kutekeleza  majukumu yao kwa wepesi na ufanisi kwa maslahi ya wananchi wa pande zote. Balozi Mahiga pia aliwahakikishia Mabalozi hao kuwa Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hizo zitaimarishwa na vikao vyake kuitishwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Mwisho, Mhe. Mahiga alimpongeza Balozi Mteule wa DRC kutokana na nchi yake kutwaa Ubingwa wa Kombe la CHAN kwa mwaka 2016.

-Mwisho-




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.