TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Ufaransa ushirikiano wazidi kuimarika
Tanzania na Ufaransa zimeahidi kuimarisha ushirikiano wa
kimaendeleo; kuongeza uwekezaji na biashara; na kutafuta ufumbuzi wa migogoro
inayozikabili nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Ukanda wa Bahari ya Hindi na
changamoto nyingine za kiusalama katika maeneo hayo.
Ahadi hiyo ilitolewa na Mawaziri wa
Mambo ya Nje wa nchi hizo jijini Paris leo walipokutana kwa ajili ya
mazungumzo. Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki yupo nchini Ufaransa kwa ziara ya kikazi siku siku mbili 21
na 22 Februari 2019 kufuatia mwaliko wa Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa
Ufaransa, Mhe. Jean- Yves Le Drian ambaye ameahidi pia kufanya ziara ya kikazi
nchini Tanzania hivi karibuni.
Kabla ya mazungumzo hayo, Mheshimiwa
Balozi Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na kundi la Maseneta wa Ufaransa
ambao ni marafiki wa Tanzania wakiongozwa na Seneta Ronan Dantec ambaye ni
Mwenyekiti wa Maseneta hao. Maseneta hao walipendekeza kuanzishwa kwa
ushirikiano dada kati ya jiji la Paris na Dodoma. Ushirikiano huo ujikite zaidi
katika matumizi bora ya ardhi, mipango miji na kutekeleza miradi mbalimbali ya
kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile, Maseneta hao wameelezea
dhamira yao ya kutaka kushirikiana na
Serikali ya Tanzania kuibua vipaji vya mchezo wa mpira wa miguu katika shule
mbalimbali nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Mahiga alifanya
mazungumzo na Bibi Marie Audouard, Naibu Mshauri wa Rais Emmanuel Macron wa
Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Afrika. Katika mazungumzo yao, Bibi Audouard
aliainisha maeneo ya kipaumbele ya Mhe. Rais Emmanuel Macron katika mahusiano
yake na nchi za Afrika. Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuimarisha zaidi
mahusiano na nchi zinazoongea lugha ya kiingereza na kireno; kuendelea
kushirikiana katika usuluhishi wa migogoro ya kikanda na kimataifa; kuhamasisha
sekta binafsi ya Ufaransa kwenda kuwekeza Afrika; na kubadilishana uzoefu katika nyanja za
utamaduni hasa kwa vijana.
Viongozi wengine aliofanya nao
mazungumzo Mhe. Waziri ni pamoja na Bibi Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa
UNESCO; na Bw. Bertrand Walckenaer, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Katika mazungumzo na Mkurugenzi wa
UNESCO, Waziri Mahiga alilishukuru Shirika hilo kwa kuwa mshirika wa Tanzania
kwa miaka mingi kwenye masuala ya elimu, sayansi na utamaduni na kuahidi kuwa
Tanzania itaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu elimu,
sayansi na utamaduni.
Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
AFD, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa, kutokana na ushirikiano mzuri uliopo
wameongeza mara mbili kiwango cha fedha za maendeleo nchini Tanzania ambazo
zitatumika kufadhili miradi katika sekta za uchukuzi, nishati, maji safi na
taka, kilimo, afya na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Waziri anahitimisha ziara
yake leo kwa kukutana na Jumuiya ya Wawekezaji na wafanyabiashara wa Ufaransa
(MEDEF) na Bi. Luise Mushikiwabo, Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya nchi
zinazozungumza Kifaransa (IOF).
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dodoma.
22 Februari
2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.