Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa wa Tanzania mara baada ya kuhutubia kikao hicho cha Baraza la Haki za Bianadamu kinachofanyika Geneva, Uswisi.
=====================================================
Waziri wa
Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano
itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu na
ustawi wa jamii kama kipaumbele chake na itaendelea kushirikiana na
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhakikisha haki za binadamu nchini na duniani kote zinadumishwa.
Prof.
Kabudi amesema hayo jana alipohutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu
la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi. Prof. Kabudi
amesema Serikali ya Tanzania imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha haki
za binadamu, utawala bora na utii wa sheria nchini na kuondoa ukatili dhidi ya
wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Serikali
imelenga kuimarisha haki za binadamu, utawala bora, utii wa sheria na kuondoa
ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, kwa sasa tunatekeleza
mpango mkakati wa kitaifa wa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa
mwaka 2017/18 - 2021/22, lengo likiwa ni kulinda na kudumisha haki za wanawake,
watoto na watu wenye ulemavu,” alisema Prof. Kabudi.
Amesema
Serikali pia inazingatia suala la kuwapatia haki kwa haraka wananchi wasio na
uwezo kwa kutolea maamuzi kwa haraka mashauri yanayowahusu watu wasio na uwezo
na kuwapatia msaada wa kisheria kupitia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa
Kisheria ya mwaka 2017 ili wananchi hao waweze kupata haki zao kwa
wakati.
Aidha,
Prof. Kabudi amelihakikishia Baraza hilo kuwa Serikali inatambua kazi kubwa
inayofanywa na vyombo vya habari nchini na imeendelea kuhakikisha uhuru wa
vyombo hivyo unalindwa huku jumla ya vituo vya redio 152, televisheni 34,
magazeti 172 nchini kote yamesajiliwa na kuongeza kuwa Serikali
itaendelea kuweka mazingira stahiki yatakayowezesha vyombo vya habari kufanya
kazi zao kwa uhuru.
Ameongeza
kuwa Serikali imedhamiria kuleta ustawi wa jamii kwa kutekeleza mipango
mbalimbali ya maendeleo ikiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025
na kunadi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya
kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote.
“Tanzania
imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji
zinawafikia wananchi wote na kuongeza kuwa Serikali inatumia zaidi ya Shilingi
Bilioni 23 kwa mwezi kutoa elimu pasipo malipo na hivyo kuongeza udahili wa
watoto wanaojiunga darasa la kwanza kwa asilimia 35.2 na asilimia 20.1 kwa
wanaojiunga na kidato cha kwanza,” alisema.
Prof.
Kabudi pia amesema Serikali imedhamiria kufikisha huduma za afya karibu na
watanzania wote ambapo imeongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31
mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 269 mwaka 2017/2018 na kuongeza kuwa
Serikali inatekeleza mikakati ya kujenga vituo vya afya ambapo hadi sasa
imejenga vituo 304, na nyumba za watumishi wa afya 578 zimejengwa nchini kote.
Baraza la
Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye
jukumu la kukuza na kulinda haki za binadamu duniani kote na kushughulikia
uvunjwaji wa haki za binadamu unaotokea katika nchi wanachama wa umoja huo na
kushauri hatua za kuchukuliwa ili kuboresha haki za binadamu duniani.
Baraza hilo
pamoja na mambo mengine linatarajia kupokea taarifa mbalimbali kuhusu haki za
binadamu duniani na kutoa nafasi kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa kutoa maelezo yao kuhusu utekelezaji wa wajibu wao wa kulinda na kukuza
haki za biandamu katika nchi zao.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.