TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Umoja wa Ulaya waazimia kuimarisha
Uhusiano
Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) wamekubaliana kuimarisha
uhusiano na ushirikiano kwa kufanya majadiliano ya mara kwa mara yatakayojengwa
katika misingi ya kuaminiana, usawa, uwazi na kuheshimiana ili kujenga uelewa
wa pamoja katika maeneo mbali mbali yenye changamoto kwa manufaa mapana ya watu wa pande zote mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo
kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Augustine Mahiga (Mb) na Mkurugenzi wa Idara ya Pembe ya Afrika na Afrika
Mashariki, Huduma za Nje katika Umoja wa Ulaya, Bw. Patrick Simonnet wakati wa
ziara yake iliyofanyika nchini kuanzia tarehe 17 hadi 20 Februari 2019.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri aliushukuru
Umoja wa Ulaya kwa misaada ambayo umekuwa ukiipatia Tanzania kwa ajili ya
utekelezji wa miradi mbalimbali ya maendelea katika sekta za kilimo, nishati na
ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege. “Umoja wa Ulaya ni mbia
muhimu wa Tanzania katika shuguli za maendeleo tokea mahusiano rasmi ya
kidiplomasia yalipoanzishwa mwaka 1975; baada ya kusainiwa kwa mkataba wa
kwanza wa Rome baina ya kundi la nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (ACP) na
nchi wanachaama wa Umoja wa Ulaya”; alisema Mhe. Mahiga.
Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa kuazimia
kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya pande mbili hizi katika maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara, uwekezaji, ushirikiano wa maendeleo na
usalama wa majini, hususan katika pwani ya Bahari ya Hindi.
Aidha, walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika
nyanja za kimataiafa ikiwa ni pamoja na kusaidia juhudi za kudumisha na
kuimarisha hali ya amani, usalama na utulivu katika eneo la Maziwa Makuu.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dodoma.
21 Februari
2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.