Friday, March 31, 2017

WAZIRI MAHIGA AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA MHE. RAIS MAGUFULI KWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Augustine  Mahiga akiwakilisha Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Magufuli kwa Bi Maria Luiza Ribeiro - Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani jana

Mhe. Mahiga akitoa maelezo kuhusu ujumbe aliouwasilisha  kutoka kwa Rais Magufuli.
(Kushoto kwa Mhe. Mahiga ni  Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, kulia ni Mhe. Balozi Modest Mero - Mwakilishi wa Kudumu  wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa  na mwisho ni Lt Col George Itang'are - Mwambata Jeshi.
Mhe Mahiga akisindikizwa na Bi  Ribeiro baada ya kumaliza mazungumzo.

Mhe. Mahiga akizungumza na Mabalozi wa nchi za SADC wanaochangia majeshi ya Ulinzi wa Amani - FIB - MONUSCO - DRC.

Mhe. Dkt Augustine Mahiga amewasilisha kwenye Umoja wa Mataifa ujumbe maalumu wa Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaoeleza msimamo wa Wakuu wa Nchi na Serikali ya Nchi za SADC kuhusu kuongezewa muda wa jukumu wa kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO – Force Intervention Brigade - FIB) nchini DRC kinachotarajiwa kumaliza muda wake wa jukumu ifikapo tarehe 31 Machi 2017.

Waziri Mahiga aliwasilisha ujumbe huo kwa Mhe. Maria Luiza Ribeiro, Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chef de Cabinet) kwa niaba ya Mhe. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa safarini nje ya Marekani kikazi.

Akiwasilisha ujumbe huo, Mhe. Mahiga alieleza kuwa, moja ya maazimio ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2017 nchini Swaziland ni pamoja na Jumuiya ya SADC kufikisha ujumbe kwenye Umoja wa Mataifa wakuunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Mataifa (Baraza la Usalama) kukiongezea muda kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa kinachotarajia kumaliza muda wake wa jukumu kwa mujibu wa Mkataba tarehe ifikapo 31 Machi 2017.

Mhe. Mahiga alimueleza Bibi Maria kuwa, Jumuiya ya SADC inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa jitihada za kuleta amani nchini DRC na kwamba, Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC wana matumaini kuwa kuongezewa muda kwa kikosi hicho kutazingatia mahitaji ya changamoto za usalama zilizopo nchini DRC na hivyo kukiwezesha kikosi hicho kukabiliana na changamoto hizo.
Mhe.Mahiga alitumia nafasi hiyo kueleza hali iliyopo kwa sasa ya ulinzi na usalama katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo aligusia na kuomba Umoja wa Mataifa kuongeza jitihada za kupatia ufumbuzi wa matatizo yaliyopo nchini DRC na Burundi.

Waziri Mahiga alifanya mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mabalozi wa Nchi zinazochangia vikosi vya Ulinzi na Usalama MONUSCO – FIB nchini DRC, Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa ambaye ni Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa (Pen-holder) wa DRC na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa.
Mhe. Mahiga   alitarajiwa kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe30 Machi  2017.







Thursday, March 30, 2017

Waziri Mkuu wa Ethiopia kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo pichani) juu ya ziara ya siku mbili ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini. Waziri Mkuu huyo atawasili nchini tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Akiwa nchini atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli pamoja na  kutembelea Bandarini. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Balozi Naimi Aziz (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo (kulia).
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya Dkt. Kolimba (hayupo pichani)
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Aziz naye akielezea jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 


Taarifa kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia nchini



Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 31 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Ziara ya Mhe. Dessalegn inakuja kufuatia mkutano kati yake na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu.

 Mhe. Dessalegn anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na atapokelewa na Mhe. Rais Magufuli. 

Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Jioni ya siku hiyo, Mhe. Dessalegn na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.

Tarehe 01 Aprili, 2017 Mhe. Dessalegn ataendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.
Mahusiano ya Tanzania‎ na Ethiopia

Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri. Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi, Kenya. 

Aidha, kumekuwa na ziara za viongozi wa ngazi mbalimbali wa nchi hizi mbili ili kukuza na kudumisha mahusiano. Ziara hizo ni pamoja na ile ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa nchini Ethiopia mwaka 2005. Wakati wa ziara hii Mhe. Mkapa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia wakati huo, Hayati Meles Zenawi walisaini Mkataba wa Jumla wa Ushirikiano. 

Vile vile, mwaka 2015 Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba. Pia, Mhe. Dessalegn alishiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi Novemba, 2015 Jijini Dar es Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
30 Machi, 2017


 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje apokea Nakala za Utambulisho za Mabalozi Wateule kutoka Ethiopia na Vietnam nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Vietnam nchini,  Mhe. Nguyen Kim Doanh. Tukio hilo limefanyika Wizarani tarehe 30 Machi, 2017.
Dkt. Kolimba akizungumza na Balozi Mteule wa Vietnam, Mhe. Nguyen Kim Doanh mara baada ya  kupokea nakala zake za hati za utambulisho
Balozi Mteule Mhe. Nguyen Kim Doanh naye akizungumza.
Dkt. Kolimba na Balozi Mteule Mhe. Nguyen Kim Doanh wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Magabilo Murobi na Afisa kutoka Ubalozi wa Vietnam nchini
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ethiopia nchini, Mhe. Dina Mufti Sid.Tukio hilo lilifanyika Wizarani tarehe 30 Machi, 2017.
Dkt. Kolimba akizungumza na Balozi Mteule wa Ethiopia nchini, Mhe. Dina Mufti Sid.
Picha ya pamoja.

SADC yahamasisha raia wa nchi wanachama kujisajili katika masuala ya ulinzi wa amani Barani Afrika

Mratibu wa Mafunzo kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Bi. Eliet Magogo akiwasilisha mada katika warsha ya kuhamasisha raia kujiunga katika jeshi la ulinzi wa amani la jumuiya hiyo iliyofanyika leo katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Watumishi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. Katikati ni Mkuu wa Kitengo kinachoshughulikia raia katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Bw. Ernest Kantchentche na kushoto ni Bi. Caroline Chipeta, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Sehemu ya Maafisa waliohudhuria warsha hiyo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kutoka kulia ni Bi. Felista Rugambwa, Bw. Deogratius Dotto na Bw. Abdallah Mrisho.
Sehemu nyingine ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa.
Warsha ikiendelea
Picha ya pamoja.

Friday, March 24, 2017

Balozi Kairuki awasilisha Hati za Utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mberwa Kairuki akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping wakati wa hafla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho iliyofanyika  Ikulu kwenye Ukumbi wa Great hall of the people siku ya Ijumaa tarehe 17 Machi 2017.
Balozi Kairuki (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa China, Mhe. Xi Jinping
Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Mbelwa Kairuki amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping tarehe 17 Machi 2017. 

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ikulu ya China (Great Hall of the People) ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi na maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China. 

Katika mazungumzo mafupi baada ya kuwasilisha hati, China na Tanzania zimekubaliana kukuza zaidi mahusiano ya kiuchumi kupitia mpango maalum wa China wa kuhamishia viwanda vyake nje ya China (Production Capacity Cooperation Programme) pamoja na programu ya kukuza ushirikiano wa biashara na ujenzi wa miundombinu ijulikanayo kama Maritime Silk Road initiative. 

Aidha, Tanzania imeihakikishia China kuendelea kuunga mkono sera yake ya ONE CHINA POLICY sambamba na kuunga mkono mtazamo wa China kuhusu mgogoro wa Bahari ya Kusini mwa China.

Thursday, March 23, 2017

Katibu Mkuu Mambo ya Nje apokea vifaa vya kuendesha mikutano kwa njia ya Video


Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (Kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kuendeshea Mikutano kwa njia ya Video Wizarani Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Machi, 2017. Makabidhiano yanakamilisha sehemu ya vifaa vilivyotolewa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Awa Dabo ambavyo vilikabidhiwa tarehe 2 Februari, 2017 ili kuiwezesha Wizara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi.
Katibu Mkuu akimpongeza Balozi Mushy kwa jitihada zake za kuimarisha mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo sambamba na kuhakikisha shughuli za kiutendaji za Wizara zinaenda na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Katibu Mkuu na Balozi Mushy wakipokea maelezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eric Kombe kuhusu namna vifaa hivyo vinavyoweza kurahisisha Mawasiliano.

Mhe. Rais Magufuli apokea Hati za Utambulisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Hungary nchini, Mhe. Laszlo Eduard Mathe mwenye makazi yake Nairobi, Kenya. Hafla hiyo fupi imefanyika tarehe 23 Machi, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Mathe akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Aziz Mlima huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa kwanza kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Mary Matari wakishuhudia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Guinea nchini, Mhe. Sidibe Fatoumata KABA mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia. Hafla hiyo fupi imefanyika tarehe 23 Machi, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.
Mhe. Sidibe Fatoumata KABA (katikati) akiwa ameongozana na Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Balozi Grace Martin (kushoto) na Mnikulu, Bw. Ngusa Samike.
Mhe. Rais Magufuli akimtambulisha Balozi Kaba kwa Waziri Mahiga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Belarus nchini, Mhe. Dmitry Kuptel mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia. Hafla hiyo fupi imefanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 23 Machi, 2017.
Mhe. Dmitry Kuptel akisikiliza wimbo wa taifa lake kutoka Bendi ya Polisi kabla ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Mhe. Rais Magufuli
Mhe. Dmitry Kuptel akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Botswana nchini, Mhe. Lebonaamang Thanda Mokalake mwenye makazi yake Lusaka, Zambia. Hafla hiyo fupi imefanyika Ikulu, Dar es Salaam tarehe 23 Machi, 2017
Balozi Mokalake akisikiliza wimbo wa taifa lake kutoka Bendi ya Polisi kabla ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Mhe. Rais. Kulia ni Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Balozi Grace Martin na kushoto ni Mnikulu, Bw. Ngusa Samike
Mhe. Rais Magufuli akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi Mokalake, Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ikulu na Maafisa kutoka Ubalozi wa Botswana.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho  kutoka kwa Balozi Mteule wa Niger nchini, Mhe. Adam Maiga ZAKAKARIAOU mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia.
Balozi ZAKAKARIAOU akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akipokea Hati za Utambulisho  kutoka kwa Balozi  wa Mauritius nchini, Mhe. Jean Pierre Jhumun mwenye makazi yake Maputo, Msumbiji.
Bendi ya Polisi ikipiga wimbo wa taifa wa Mauritius kwa heshima ya Mhe. Balozi Jean Pierre Jhumun.

Wednesday, March 22, 2017

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho za Mabalozi Wateule

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Mauritius nchini, Mhe. Jean Pierre Jhumun mwenye makazi yake Maputo, Msumbiji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Nepal nchini, Mhe. Amrit Rai mwenye makazi yake Pretoria, Afrika Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ecuador nchini, Mhe. Benys Toscano Amores mwenye makazi yake Addis Ababa, Ethiopia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Congo Brazaville nchini, Mhe. Guy Nestor Itoua mwenye makazi yake Kigali, Rwanda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa New Zealand nchini, Mhe. Michael Gerrard Burrel mwenye makazi yake Pretoria, Afrika Kusini.