Wednesday, July 13, 2022

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA RAIS WA CARE INTERNATIONAL

Shirika lisilo la kiserikali la Care International limetakiwa kupanua huduma zake katika mikoa mingi zaidi badala ya mikoa tisa tu ambayo shirika hilo kwa sasa linatoa huduma zake hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, wakati wa mazungumzo yake na Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Bi. Michelle Nunn

Bi. Nunn ametaja baadhi ya shughuli ambazo shirika lake inazifanya hapa nchini kuwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira, afya, elimu, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kilimo, haki za kijamii na usawa wa kijinisa. Amesema utekelezaji wa shughuli hizo umezingatia kipaumbele cha mwanamke.

“Tunasaidia watoto wa maeneo ya vijijini kupata elimu bora, tunasaidia jamii kutumia aridhi yao vizuri ili izalishe chakula, wakati huo huo ikitunzwa vizuri na programu zetu za kutoa mikopo na kuwasaidia wanawake wa vijijini kujiwekea akiba kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kidigitali zimewawezesha wanawake wengi kumiliki rasilimali na kunyanyuka kiuchumi”, Alisema Bi. Nunn.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula alilishukuru shirika hilo kwa misaada inayotoa nchini na kueleza kuwa programu zao za misaada zinaenda sanjari na dira ya maendeleo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aliendelea kueleza kuwa changamoto kwa wanawake ni nyingi zikiwemo za afya ya uzazi na ugonjwa wa malaria ambao bado unakatisha maisha ya watu wengi katika nchi za Afrika, hivyo alishauri umuhimu wa “Care International” kuangalia kwa jicho la pekee eneo hilo.

Aidha, Balozi Mulamula alilipongeza shirika hilo kwa kujikita katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa na watu wengi hawalioni, ingawa madhara ya uharibifu wa mazingira yanamfikia kila mmoja wetu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo nchini Tanzania

Ujumbe ulioambatana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn ukifuatilia mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn huku maafisa walio chini yao wakifuatilia mazungumzo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (katikati) akifurahia jambo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Care International, Bi. Prudence Masako

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi walioambatana nao wakati walipofanya mazungumzo jijini Dar Es Salaam. 

Tuesday, July 12, 2022

KIWANDA CHA LABIOFAM KIBAHA KUPANULIWA

Serikali za Tanzania na Cuba zipo katika mchakato wa kupanua kiwanda cha Labiofam kilichopo Kibaha, Pwani cha kuzalisha viuadudu vya mazalia ya mbu ili kiwe na uwezo wa kuzalisha mbolea na dawa nyingine za kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo.

Hayo yamesemwa leo tarehe 12 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Magembe wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Serikali za Tanzania na Cuba cha kujadiliana kuhusu upanuzi wa kiwanda hicho kinachoendeshwa kwa ubia baina ya Serikali hizo mbili.

Dkt. Magembe ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania unaojadiliana na ujumbe wa Cuba, alisema kuwa ana matumaini makubwa katika kikao hicho cha siku mbili, wajumbe watafikia makubaliano yatakayokuwa na manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

 

“Kama unavyofahamu asilimia 70 hadi 80 ya Watanzania ni wakulima, hivyo, uwepo wa kiwanda hiki na uzalishaji wa mbolea na viuadudu ni fursa nzuri kwa wakulima wetu na nchi kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na wananchi kujipatia kipato kwa mazao watakayovuna”, Dkt. Magembe alisema.

 

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez alisema kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni ishara ya wazi ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Cuba na Tanzania.

Aidha, naye alielezea matumaini yake kuwa majadiliano hayo ya siku mbili yatakuwa na faida kubwa kwa maendeleo ya sekta ya kilimo ya Tanzania na azma ya Serikali ya kupamabana na ugonjwa wa malaria na hatimaye kuuangamiza kabisa.


Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya Serikali za Tanzania na Cuba cha kujadiliana kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM cha Kibaha. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Magembe ambaye ni Kiongozi wa timu ya majadiliano ya Tanzania. 


Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez akielezea matumaini yake kuwa kikao cha majadiliano kitakuwa na manufaa kwa pande zote mbili

Wataalamu wa Tanzania wanaoshiriki kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC),     Dkt. Nicolous Shombe akiongea jambo katika kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola akiongea jambo katika kikao hicho. Mwingine ni MKurugenzi wa Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme

Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera akiongea jambo katika kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM
Wajumbe wa Tanzania na Cuba wakiwa katika ufunguzi wa kikao cha majadiliano kati ya Tanzania na Cuba kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Cuba na Tanzania

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt Grace Magembe (katikati), Kiongozi wa ujumbe wa Cuba ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo, Bw. Orlando Diaz Rodriguez (kulia) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dkt. Nicolous Shombe wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Cuba unaofanya majadiliano kuhusu upanuzi wa kiwanda cha LABIOFAM

 

Monday, July 11, 2022

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ISRAEL ULIVYOADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

Wadau mbalimbali nchini Israel wamepongeza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuienzi Lugha ya Kiswahili.

Pongezi hizo zimetolewa na wadau hao wakati wa Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe katika Makazi ya Balozi wa Tanzania nchini humo tarehe 07Julai 2022

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Gabriel Kalua amesema kuwa ametumia maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kukukutana na kujadiliana na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kukuza na kuendeleza Lugha hiyo adhimu.

Aidha, Mhe. Balozi Kalua ambaye alijumuika na viongozi kutoka Serikali ya Israel, wadau mbalimbali wanaoshirikiana na Tanzania, Watanzania wanaoishi nchini humo na wageni mbalimbali, alitumia maadhimisho  hayo kugawa vitabu vya kujifunzia Kiswahili kikiwemo cha “Jifunze Kiswahili, Hazina ya Afrika: Kitabu cha Kwanza”, pamoja na kushiriki chakula cha Kitanzania na wadau hao.

Kadhalika, Mhe. Balozi Kalua alitoa hotuba yake kwa lugha ya Kiswahili ambayo ilitafsiriwa kwa Kiebrania.

Naye Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Bibi Amit Gil Bayaz ambaye ni miongoni mwa viongozi kutoka Serikali ya Israel walioshiriki aliipongeza Tanzania kwa maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yalihitishwa kwa Wadau mbalimbali  kushiriki chakula na vinywaji vya kitanzania  ambapo walieleza kufurahishwa na ukarimu wa watanzanaia na kufurahia vinywaji na chakula cha kitanzania kilichoandaliwa kwa ajili yao.

Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Gabriel Kalua akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi nchini humo tarehe 7 Julai 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali. Wengine katika picha ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ambaye ni Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Bibi Amit Gil Bayaz (wa pili kutoka kushoto), Rais wa Klabu ya Mabalozi waliopo Israel, Mhe. Balozi Yzihack Elden (kushoto) na Mwakilishi wa Balozi wa Heshima, Mhe. Chirich Nuriel Kasbian (wa pili kulia)


Mhe. Balozi Kalua akimkabidhi kitabu cha kujifunza Kiswahili, Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Bibi Amit Gil Bayaz.

Mhe. Balozi Kalua akimkabidhi kitabu cha kujifunza Kiswahili, Rais wa Klabu ya Mabalozi waliopo Israel, Mhe. Yitzhack Elden


Mhe. Balozi Kalua akiwa na wadau mbalimbali aliowakabidhi vitabu

Wawakilishi kutoka Jeshi la Israel walioshiriki maadhimisho ya siku ya Kiswahili wakiwa na Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Tanzania nchini, Israel, Brig. Jen. Mziray


Wadau mbalimbali wakionesha vitabu vya kujifunza Kiswahili walivyokabidhiwa

 

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA WANAFUNZI-DIASPORA WA MAREKANI.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani wanaofundisha na kusoma vyuo mbalimbali vya Marekani ambao wapo nchini kwa ziara ya kikazi hadi tarehe 17 Julai 2022.

Ziara hiyo iliyoratibiwa na Mtanzania-Diaspora, Bi Zawadi Sakapala ambaye ni mmiliki wa kituo cha “Community Centre” kilichopo Kijichi jijini Dar Es Salaam inalenga pamoja na mambo mngine, kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujifunza masuala ya utamaduni wa Tanzania na kubadilishana ujuzi na uzoefu katika masomo ya sayansi, ufundi, ufundishaji na Usimamizi wa watoto wadogo (daycare).

Katika kikao hicho, Bi Zawadi alimfahamisha Mhe. Balozi Mulamula kuwa kituo chake kimekuwa kikishirikiana na vyuo vikuu mbalimbali nchini Marekani kuratibu ziara za walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani kutembelea nchi za Afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika sekta ya elimu.

Hivyo, ili kuimarisha sekta ya elimu katika nchi za Afrika, kikao hicho kiliazimia kuongeza jitihada za kuhamasisha Waafrika wengi zaidi kujiunga na vyuo vya Marekani, kuunganisha vyuo vya Afrika na Marekani, wanafunzi-Watanzania wanaopata fursa ya kusoma Marekani, watumike kufundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni moja ya njia ya kueneza lugha hiyo duniani pamoja na kwahimiza watu wenye asili ya Afrika kutumia elimu, ujuzi na maarifa waliyopata wakiwa ughaibuni kuinua jamii za nchi za Afrika.

Wakati huo huo, Balozi Mulamula amekutana na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (UNDP) ambao upo nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wadau wa siasa ili kubainisha maeneo ambayo, shirika hilo linaweza kusaidia katika uendeshaji wa uchaguzi mkuu ujao.

Ujumbe huo unaongozwa na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa, Bw. Akinyemi Adegbola umefanikiwa kufanya vikao na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wawakilishi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia, umepokea maoni ya wadau hao ya maoneo yanayohitaji msaada na umeahidi utayafanyia kazi kikamilifu. Maeneo hayo ni pamoja na uelimishaji wa wapiga kura, msaada wa kiufundi katika upigaji na uandikishwaji wa wapiga kura na teknolojia ya mawasiliano wakati zoezi la uchaguzi.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula aliueleza ujumbe huo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kipindi kifupi cha uongozi wake ameonesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya kisiasa nchini, kwa kuhamasisha majadiliano ya kisiasa, ushirikishwaji wa wadau wote, umoja na mshikamano wa kitaifa. Hivyo, aliuhakikishia ujumbe huo kuwa uchaguzi ujao utaendelea kuwa huru, haki na amani kama ilivyo desturi ya Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani (hawapo pichani) wanaosoma na kufundisha vyuo mbalimbali vya Marekani ambao wapo nchini kwa ziara maalum hadi tarehe 17 Julai 2022.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mmoja wa mwanafunzi anayesoma katika vyuo vikuu vya Marekani kuhusu mikakati ya kusaidia vijana wa Afrika kupata elimu bora itakayoweza kukabili mazingira ya dunia ya sasa.

Mhitimu wa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Howard cha nchini Marekani ambaye pia ni Kiongozi wa Taasisi ya 3GC Inc. akieleza shughuli za taasisi hiyo zinazolenga kuwasaidia vijana wa Afrika 
Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani wanaosoma na kufundisha vyuo mbalimbali vya Marekani


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimvisha scurf ya bendera ya Tanzania, mmiliki wa kituo cha “Community Centre” kilichopo Kijichi jijini Dar Es Salaam, Bi. Zawadi Sakapala

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na walimu na wanafunzi wenye asili ya Afrika na Marekani wanaosoma na kufundisha vyuo mbalimbali vya Marekani



BALOZI MULAMULA AKUTANA NA  AFISA UCHAGUZI MKUU WA UN


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa, Bw. Akinyemi Adegbola yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam

Baadhi ya ujumbe uliongozana na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa, Bw. Akinyemi Adegbola kwenye mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Afisa huyo.

Ujumbe wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ukifuatilia mazungumzo yake na Afisa Uchaguzi Mkuu katika Idara ya Siasa na Masuala ya Amani ya Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiagana na ujumbe wa UNDP ambao upo nchini kwa ajili ya kuzungumza na wadau wa siasa kuhusu uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa UNDP ambao upo nchini kwa ajili ya kuzungumza na wadau wa siasa kuhusu uchaguzi.


BALOZI MULAMULA AKUTANA NA MWAKILISHI MKAZI WA UN WOMEN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa  UN Women, Bi.  Hodan Addou kwenye Hoteli ya Seana jinini Dar Es Salaam.


BALOZI MULAMULA AKUTANA NA  BALOZI MTEULE LT. JEN. MATHEW EDWARD MKINGULE 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi Mteule Lt. Jen. Mathew Edward Mkingule yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi Mteule Lt. Jen. Mathew Edward Mkingule baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam


 

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

Saturday, July 9, 2022

WAZIRI MULAMULA: WAFANYABIASHARA CHANGAMKIENI FURSA ZA MASOKO KATIKA JUMUIYA ZA KIKANDA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa rai kwa Wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za masoko zinazopatikana katika Jumuiya za Kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na fursa zitokanazao na Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA)

Waziri Mulamula ametoa rai hiyo wakati akizungumza na wafanyanyabisha kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba “Bukoba Expo" yaliyofanyika katika Viwanja ya CCM mjini Bukoba. Maonesho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu isemayo “Biashara, viwanda na utalii ni fursa ya uwekezaji Mkoani Kagera”.

Akizungumza na wafanyabiashara wakati wa akifunga maonesho hayo Waziri Mulamula alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inayo dhamira ya dhati ya kukuza uchumi wa nchi kupitia biashara na uwekezaji kwa kudumisha ushirikiano na nchi jirani na kutafuta fursa za masoko kwa bidhaa zinazozalishwa nchini. Aliongeza kusema wakati Serikali inafanya hayo ni vyema sekta binafsi ikaunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kuchangamkia fursa za masoko zinazopatikana katika Jumuiya za Kikanda ili kujiongezea tija zaidi katika shughuli zao. 

"Mtakumbuka kuwa Tanzania pamoja na kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia ni mwanachama wa SADC na hivi karibuni tumeridhia mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (Africa Continental Free Trade Area-AfCFTA). Eneo Huru la Biashara la Afrika ni soko kubwa kuliko masoko yote yaliyoanzishwa ulimwenguni kwa kuwa na uwingi wa nchi wanachama zinazofikia 55. Soko hili linakadiriwa kuwa na idadi ya watu wapatao Bilioni 1.3 na Pato ghafi la Taifa (GDP) lenye jumla ya Dola za Marekani trilioni 3.4 na fursa za uchumi unaokua kwa kasi". Alieza Waziri Mulamula

Akizungumzia kuhusu maonesho hayo Waziri Mulamula ameleeza kuwa ubunifu wa waandaji umeakisi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Mkoa wa Kagera na wananchi wake wanapata maendeleo kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, biashara na uwekezaji kwa kutumia fursa zilizopo katika Mkoa huo na nafasi ya Kijiografia ya Mkoa kwa kupakana na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

Kwa upande wake mratibu na mwandaaji wa Maonesho ya Bukoba Bw. William Rutta ameeleza kuwa maonesho hayo ambayo yamewavutia washiriki zaidi ya 350 wakiwemo wajasiliamari, wafanyabiashara, Taasisi za serikali na washiriki kutoka nchi za Burundi, Uganda, na Congo yametembelewa na wateja zaidi ya 10,000.

Aidha Bw. Rutta amebainisha malengo ya amonesho hayo kuwa ni pamoja na kuweka mwendelezo wa wiki ya uwekezaji ya Kagera ya mwaka 2019, kuunganisha wafanyabiashara na wananchi wote kushiriki katika shughuli za kuzalisha, mali, kuendeleza utalii na kubadilishana teknolojia ya uzalishaji na kuhamasisha utalii kwa kuandaa safari katika mbuga za wanyama asili za Burigi, Ibanda kyerwa, Runanyika Karagawe, Hifadhi ya Rubondo, Seregeti na vivutio vya asili kama fukwe za ziwa Victoria. Lengo lingine ni uboreshaji wa mazingira kwa kuhamasishwa upandaji miti aina ya palm tree katika mji wa Bukoba.

Waziri Mulamula kwenye maadhimisho ya kilele cha maonesho hayo pamoja na wajumbe wengine aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali, Charles Mbuge, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Moses Machali na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera Bi. Costansia Guhiye.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na mmoja wa washiriki wa Maonesho ya Bukoba 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (aliyevalia kilemba) na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Charles Mbuge akiwa katika picha ya pamoja Waandaaji wa Maonesho ya Kagera na Washiriki wa maonesho hayo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Moses Machali alipowasili kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba yaliyofanyika katika viwanja vya CCM Bukoba mjini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi cheti cha kufanyavizuri mmoja wa washiriki wa Maonesho Bukoba kutoka nchini Burundi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza hadhira iliyojitokeza kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha na mmoja wa washiriki wa Bukoba Expo mzalishaji wa bidhaa za mafuta ya asili ya ngozi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akipokelewa katika viwanja vya CCM mjini Bukoba alipowasili kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba “Bukoba Expo”.
Meza kuu wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea kwenye madhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwasili kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba “Bukoba Expo” yaliyofanyika katika viwanja vya CCM Bukoba mjini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na mmoja wa washiriki wa Maonesho ya Bukoba
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiangalia bidhaa za mmoja wa washiriki wa Bukoba Expo 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Mati Super Brands Ltd Bw. Living Munishi kwenye maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifurahia jambo baada zoezi la upandaji mti kwenye madhimisho ya kilele cha Maonesho ya Bukoba

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA NSSF ZAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI NJE YA NCHI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Bw. Masha Mshomba tarehe 8 Julai 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Viongozi hao wamejadili juu ya umuhimu wa kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara na mfuko huo wa NSSF.  


Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamezungumzia kuhusu uwekezaji kwenye viwanja vya Serikali nje ya nchi ili kuona namna ambavyo Wizara na NSSF wanaweza kushirikiana katika miradi ya ujenzi wa ofisi na vitega uchumi.


Aidha, Balozi Sokoine akaeleza kuwa Serikali ina miliki viwanja zaidi ya 40 kwenye maeneo ya uwakilishi nje ya nchi, hivyo akatoa rai kwa taasisi hiyo kushirikiana na Wizara katika kuviendeleza kwa kujenga majengo ya Ofisi za Balozi pamoja na vitega uchumi ili kuipunguzia Serikali gharama ya kupanga lakini zaidi  kupata faida kutokana na vitega uchumi hivyo.


Naye Bw. Mshomba aliafiki wazo hilo la uwekezaji na kueleza kuwa  NSSF imeshakuwa na mipango ya miradi ya uwekezaji nje ya nchi hivyo, wazo hilo limekuja wakati mwafaka na kwamba NSSF inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kufungua mipaka hususan katika sekta ya biashara na uwekezaji.


Aidha, Kikao hicho kiliridhia kuundwa kwa timu ya Wataalamu kutoka katika pande zote mbili ili kuruhusu kufanyika kwa tathmini ya kina juu ya uwekezaji huo na faida zake ili kuweza kuwa na miradi ya pamoja na Wizara wenye tija kwa Taifa.


======================================


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Joseph Sokoine (kulia) amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Bw. Masha Mshomba tarehe 8 Julai 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF, Bw. Masha Mshomba (wa pili kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi Joseph Sokoine (hayupo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
 Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Utawala - NSSF, Bw. Gabriel Silayo na wa tatu kutoka kulia ni Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma - NSSF, Bi. Lulu Mengele.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango, Bw. Justin Kisoka akifafanua juu ya uwekezaji wa miradi ya pamoja na namna Wizara na NSSF zinavyoweza kushirikiana katika kutathmini uwekezaji kwenye maeneo ya miradi.

Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana na kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara hiyo wakifuatilia mazungumzo.

Picha ya pamoja