Thursday, November 16, 2023

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI KUHUSU USALAMA WA BAHARI YA HINDI

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.

 

Mkutano huo ambao umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Biashara za Kimataifa ya Mauritius kwa kushirikiana na Kamisheni ya Bahari ya Hindi, pamoja na mambo mengine ulipokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mikutano ya aina hiyo iliyofanyika mwaka 2018 na 2019 pamoja na kujadili hatua za kuchukua ili kuimarisha ulinzi na usalama wa bahari. 

 

Kadhalika, wakati wa Mkutano huo, Nchi mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa na kikanda na wadau wa maendeleo zilipitisha  Azimio la Pamoja  kuhusu umuhimu wa  ushirikiano  na nguvu ya pamoja katika kulinda watumiaji wa Bahari ya Hindi dhidi ya changamoto mbalimbali zinazotokana na matumizi ya bahari ikiwemo ongezeko la makosa yanayovuka mipaka, uharamia na uvuvi haramu.

 

Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Rosemary Jairo, Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Marday Venkatasamy na Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambao unawakilisha pia nchini Mauritius.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (wa pili kulia) akishiriki Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023. Mhe. Makame aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Marday Venkatasamy.  Mhe. Makame aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.

Waziri wa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Marday Venkatasamy, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Bi. Rosemary Jairo (wa pili kulia) na Afisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambao unawakilisha pia Mauritius, Bi. Gwantwa  Mwaisaka wakati wa  Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.

Mhe. Makame (wa nne kulia waliosimama) katika picha ya pamoja na Viongozi wengine walioshiriki Mkutano wa Tatu wa Mawaziri kuhusu Usalama na Ulinzi wa Bahari  Magharibi mwa Bahari ya Hindi uliofanyika Balaclava nchini Mauritius tarehe 16 Novemba 2023.



 

RAIS WA ROMANIA AWASILI NCHINI


Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis, amewasili nchini kwa ziara ya Kitaifa kuanzia leo tarehe 16 hadi 19 Novemba 2023 kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere amepokelewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)

Lengo la ziara hiyo ni pamoja na kushawishi uwekezaji zaidi na kuvutia watalii wengi kutoka nchini Romania.

Aidha katika mazungumzo rasmi yatakayofanyika tarehe 17 Novemba 2023 Rais huyo na mwenyeji wake watajadili namna bora ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati sekta za elimu, afya, kilimo nishati na madini.

Kabla ya kuondoka nchini tarehe 19 Novemba 2023 Rais wa Romania atapata fursa ya kwenda Zanzibar ambapo atazungumza na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kutembelea Mji Mkongwe ambao ni moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii duniani
Rais wa Romania Mheshimiwa Klaus Iohannis akiwapungia wananchi waliojitokeza kumlaki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.) alipompokea wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)

Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis kizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)  alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam

Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis kizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb.)  alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam
Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samuel Shelukindo alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam

Wednesday, November 15, 2023

RAIS WA ROMANIA KUFANYA ZIARA YA KITAIFA NCHINI



 

“TANZANIA NI SEHEMU SALAMA KWA BIASHARA NA UWEKEZAJI” WAZIRI MAKAMBA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), amezihakikishia sekta binafsi na za umma nchini Uholanzi kuwa Tanzania ni sehemu salama ya biashara na kuwekeza.

Hayo yameelezwa wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi lililofanyika jijini The Hague, Uholanzi tarehe 14 Novemba 2023.

Kongamano hilo lililotanguliwa na mkutano wa ndani kati ya sekta za umma na binafsi za nchi hizo, ambapo zilitumia fursa hiyo kujadili kwa kina fursa zilizopo Tanzania pamoja na taratibu nyingine zinazotakiwa kufuatwa na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mengine.

Kongamano hilo lililokuwa na kauli mbiu isemayo “Ushirikiano sawa kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu” liliandaliwa na kuratibiwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini The Hague, Uholanzi kwa kushirikiana na Baraza la Biashara kati ya Uholanzi na Afrika (NABC).

Akifungua kongamano hilo Waziri Makamba pia alieleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka azma ya kutekeleza kwa vitendo dira ya Serikali ya kufanikisha ushindani na uanzishaji wa viwanda kwa maendeleo ya Taifa.

Kongamano likiendelea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akihutubia katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi lililofanyika jijini The Hague, Uholanzi. Kongamano hilo limeratibiwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Biashara kati ya Uholanzi na Afrika (NABC)

Picha ya pamoja meza kuu na wawakilishi kutoka sekta za umma za Tanzania na Uholanzi walioshiriki katika kongamano hilo.

Mjumbe wa kongamano kutoka Uholanzi akiwasilisha hoja zake kwa Waziri Makamba ili ziweze kufafanuliwa wakati wa kongamano hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akisalimiana na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchini Uholanzi waliposhiriki katika kongamano.

Mheshimiwa Waziri Makamba akishuhudia zoezi la kubadilishana Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzani (TIC), Bw. Gilead Teri na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Biashara kati ya Uholanzi na Afrika, Bi. Rosmarijn Fens wakati wa kongamano hilo jijini The Hague, Uholanzi.


Tuesday, November 14, 2023

MCHAKATO HADHI MAALUM KWA DIASPORA KUKAMILIKA MWAKA 2024



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi katika kikao kilichofanyika jijini The Hague, Uholanzi ambapo amewasisitiza Watanzania hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Taifa lao.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kukamilisha utaratibu wa kuwapatia Hadhi Maalum Watanzania waishio nje ya nchi, yaani diaspora ifikapo mwaka 2024.

Hayo yamesemwa katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi kwa heshima ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 13 - 15 Novemba 2023.

Akifafanua masuala mbalimbali yaliyowasilishwa kupitia risala ya Watanzania iliyosomwa na Mwakilishi wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Uholanzi, Bi. Sylvana Lubuva, Mhe. Makamba alisema utekelezaji wa Hadhi Maalumu unategemea kufanyika kwa mapitio ya baadhi ya sheria za nchi kama ile ya ardhi na uhamiaji ili kurahisisha utekelezaji wenye tija kwa walengwa, yaani diaspora na kwamba mchakato huo unatajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele kwenye Hadhi Maalum ni haki ya kurithi au kurithishwa mali kwa diaspora wa Kitanzania aishiye nje ya nchi. Ili kutekeleza hili kuna maeneo ya sheria yetu lazima yabadilishwe ili watoto wenu wanaoishi huku nje waweze kurithi au kumiliki ardhi” alisema Waziri Makamba.

Sambamba na hilo, ni utaratibu wa kulipa visa pindi diaspora wa Tanzania wanaporudi nyumbani. “Kwenye Hadhi Maalum, mtaruhusiwa kuja nyumbani na kukaa kwa muda mnaotaka bila malipo ya visa. Lakini kwanza ni lazima sheria yetu ya uhamiaji ipitiwe na kurekebishwa, ili kuruhusu kurudi nyumbani bila kulipishwa visa” alisisitiza Waziri Makamba.

Baadhi ya masuala mengine yatakayowanufaisha watumiaji wa Hadhi Maalum ni fursa na motisha mbalimbali za kuwekeza nchini Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC). 

Kadhalika, Mheshimiwa Makamba alisisitiza umuhimu wa kujisajili kwenye mfumo wa Diaspora Digital Hub ambapo alisema licha ya kusaidia kuwatambua Watanzania waishio nje ya nchi, pia inarahisisha kwa kiasi kikubwa kuwarejesha nchini pindi majanga makubwa yanapotokea maeneo mbalimbali duniani. 

“Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi imara wa Mama Samia Suluhu Hassan, imeelekeza kuokoa Mtanzania au Watanzania popote pale walipo pindi majanga yanapowakuta. Imefanya hivyo kuwaokoa Watanzania waliokua masomoni Ukraine, imewarejesha nyumbani Watanzania waliokuwa Sudan na hivi karibuni Israeli” Mhe. Makamba aliongeza.

Mazoezi haya ya kuwarejesha Watanzania nyumbani hufanyika chini ya uratibu wa Ofisi za Ubalozi zilizopo nchi husika au nchi jirani na hivyo huratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mhe. Makamba yupo nchini Uholanzi kwa ziara ya kikazi ambapo siku ya pili ya ziara hiyo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka katika ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, jumla ya watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi nchini Uholanzi na maeneo ya karibu.
Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akisalimiana na baadhi ya watanzania wanaoishi nchini Uholanzi 
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Carilone Chipeta akifafanua jambo wakati wa mkutano wa Mheshimiwa Waziri na Diaspora uliofanyika jijini The Hague, Uholanzi.
Sehemu ya Watendaji wa  Wizara wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi
Sehemu ya Watumishi wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa Waziri Makamba na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi
Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Ramadhan Mzuzuri akifafanua masuala mbalimbali yanayohusu Diaspora katika mkutano wa Mheshiwa Waziri na Diaspora uliofanyika jijini The Hague, Uholanzi.
Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe aliofuatana nao katika ziara hiyo, watumishi wa ubalozi na watanzania wanaoishi nchini Uholanzi baada ya kumalizika kwa 
Sehemu ya Watumishi wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa Waziri Makamba na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi

Monday, November 13, 2023

WAZIRI MAKAMBA AWASILI UHOLANZI KWA ZIARA YA KIKAZI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akielezea juu ya ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi litakalofanyika tarehe 14 na 15 Novemba 2023 jijini The Hague, Uholanzi. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida na kushoto ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano waTanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Chipeta.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.) amewasili Jijini The Hague, Uholanzi kwa ziara ya kikazi ya siku tatu (3) kuanzia tarehe 13 - 15 Novemba 2023. 

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Makamba ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji Kati ya Tanzania na Uholanzi litakalofanyika tarehe 14 na 15 Jijini The Hague.

Aidha, pembezoni mwa kongamano hilo, Mhe. Waziri Makamba atapata nafasi ya kukutana na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Mhe. Kanke Bruins Slot. Kadhalika, Mhe. Makamba anatarajiwa pia kukutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi (Tanzania Diaspora).

Waziri Makamba ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi. Wengine wanaoshiriki kwenye ujumbe wa Mhe. Waziri ni Mabalozi na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pamoja na Wakuu wa Mashirika mbalimbali Serikalini yanayotafuta ubia na mashirika ya Uholanzi. 

Aidha ujumbe wa Waziri Makamba umehusisha wafanyabiashara 16 kutoka sekta binafsi za Tanzania ambao wanashiriki kwenye kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Balozi John Ulanga akifafanua masuala mbalimbali yatakayojiri wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (kushoto) na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya mifugo), Dkt. Daniel Mushin a wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.
Viongozi Waandamizi kutoka sekta ya umma na binafsi walioambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) nchini Uholanzi wakifatilia ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika kikao cha ndani cha maandalizi.
Viongozi Waandamizi kutoka sekta ya umma na binafsi walioambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) nchini Uholanzi wakifatilia ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika kikao cha ndani cha maandalizi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akimsikiliza Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Chipeta mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Amsterdam, Uholanzi tarehe 13 Novemba 2023
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akielezea juu ya ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi litakalofanyika tarehe 14 na 15 Novemba 2023 jijini The Hague, Uholanzi. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida na kushoto ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano waTanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Chipeta

Sunday, November 12, 2023

TANZANIA NA FINLAND KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO KUMUENZI HAYATI AHTISAARI


Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na Finland ili kuenzi misingi mizuri ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili iliyowekwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati Martti Ahtisaari.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipozungumza katika hafla ya kumbumbuku ya kumuenzi Hayati Ahtisaari  iliyofanyika jijini Helsinki Finland tarehe 11 Novemba 2023.


Amesema Hayati Ahtisaari ambaye dunia inamtambua kwa mchango wake mkubwa katika kutetea amani, Tanzania itaendelea kumuenzi na kutambua mchango wake mkubwa alioutoa katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania tangu akiwa Balozi wa Finland nchini Tanzania mwaka 1973 hadi 1976 na alipokuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1994 hadi 2000.

Amesema kupitia misingi hiyo,   Finland imekuwa mshirika mzuri wa Tanzania katika kutekeleza agenda mbamlimbali  za maendeleo na kwamba mchango wa nchi hiyo  kwenye sekta mbalimbali za maendeleo utaendelea kubaki kama alama ya kukumbukwa tangu Tanzania ilipotoka na ilipo sasa.


“Ninayo furaha kusema kwamba, Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili na watu wake unaimarika siku hata siku” alisisitiza Mhe. Balozi Mbarouk.



Vilevile amesema kuwa, mtazamo wa Tanzania na Filand katika agenda  mbalimbali za kimataifa unafanana, hivyo Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo kuhakikisha agenda hizo  ikiwemo kuleta maendeleo ya kiuchumi duniani, ulinzi wa amani na mapambano dhidi ya umaskini zinatekelezwa ili kuifanya dunia mahali salama pa kila mmoja kuishi.


Kadhalika Mhe. Balozi Mbarouk amepongeza kuwepo kwa Mfuko wa Amani wa Martti Ahtisaari (CMI) ambao una jukumu kubwa la kuendelea kuenzi urithi mwema aliouacha Hayati Ahtisaari ambaye anatambulika kama mtetezi bingwa wa Amani duniani.



Mhe. Balozi Mbarouk alitoa hotuba hiyo kwa  niaba ya Rais Mstaafu,  Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya kitaifa ya Hayati Ahtisaari yaliyofanyika jijini Helsiknki tarehe 10 Novemba 2023. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akihutubia wakati wa hafla maalum ya kumbukumbu kumuenzi aliyekuwa Rais Mstaafu wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari iliyofanyika jijini Helsinki, Finland tarehe 11 Novemba 2023. Mhe. Balozi Mbarouk alitoa hotuba hiyo kwa niaba ya Rais Mstaafu, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwenye mazishi ya Hayati Ahtisaari yaliyofanyika jijini hapo tarehe 10 Novemba 2023

Mhe. Balozi Mbarouk akiendelea na hotuba yake, ambapo pamoja na mambo mengine alisema Tanzania itaimarisha ushirikiano na Finland kumuenzi Hayati Ahtisaari


Mhe. Balozi Mbarouk akihutubia


 

Saturday, November 11, 2023

KIKWETE AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MAZISHI YA RAIS WA ZAMANI WA FINLAND


Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya Mazishi ya Kitaifa ya Rais wa Zamani wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari iliyofanyika Helsinki tarehe 10 Novemba 2023. 

Wakati wa kutoa salamu za pole, Rais Kikwete alisema kuwa Rais Samia anatoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Findland, Mhe. Sauli Niinistö, Familia ya Marehemu na watu wote wa Finland kufuatia kifo cha kiongozi huyo mashuhuri duniani.

Rais Kikwete aliungana na viongozi mbalimbali walioshiriki mazishi hayo wakimwemo Rais wa Kosovo, Mhe. Vyosa Osmani na Rais wa Namibia, Mhe. Hage Geingob na kummwagia sifa Hayati Martti Ahtisaari kwamba alikuwa kiongozi mwenye maono na mpenda amani duniani.

Hayati Martti Ahtisaari aliwahi kuwa Balozi wa Finland nchini Tanzania kuanzia mwaka 1973 hadi 1976 na alikuwa Rais wa Finland kuanzia mwaka 1994 hadi 2000. Katika vipindi vyote hivyo, Hayati Martti Ahtisaari aliimarisha uhusiano wa Tanzania na Finland katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania mwaka 1997 wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa inaongozwa na Hayati Benjamin Mkapa.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete akimpa pole Mjane wa Rais wa Zamani wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete akiwa katika mazungumzo na Rais wa Finland, Mhe. Sauli Niinistö wakati wa hafla alyoiandaa kwa viongozi na wageni walioshiriki Mazishi ya Kitaifa ya Rais wa zamani wa nchi hyo, Hayati Martti Ahtisaari yaliyofanyika tarehe 10 Novemba 2023.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete (kulia) akiwa na viongozi na waombolezaji wengine katika hafla ya mazishi ya kitaifa ya Rais wa Zamani wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari iliyofanyika Helsinki tarehe 10 Novemba 2023. Rais Kikwete alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi hayo.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete (kulia) akiwa na viongozi na waombolezaji wengine katika hafla ya mazishi ya kitaifa ya Rais wa Zamani wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari iliyofanyika Helsinki tarehe 10 Novemba 2023. Rais Kikwete alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi hayo
Hafla ya Mazishi ya Kitaifa ya Rais wa Zamani wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari ikiendelea Helsinki tarehe 10 Novemba 2023