Tuesday, April 16, 2024

NJE SPORT YAIZIBUA BILA HURUMA MAMLAKA YA AFYA YA MIMEA NA VIUATILIFU

Timu ya Nje – Sport wanaume imeizibua bila huruma magoli 2 kwa buyu Timu ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika mchezo uliofanyika kwenye  viwanja vya Shule ya sekondari ya Iliboru jijini Arusha leo Aprili 16, 2024.

Magoli hayo yamepachikwa wavuni na washambuliaji hatari wa timu hiyo, Bw. Mikidadi Magola, Goli la kwanza na goli la pili likiwekwa kimyani kwa ustadi mkubwa na Bw. Mukrimu Mustafa. 

Kocha wa timu hiyo, Bw. Shabani Maganga aliwapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo yake pamoja na kucheza vizuri na kuifanya timu yake kubeba alama tatu muhimu katika mzunguko wa kwanza

Katika mchezo mwingine timu ya Wanawake ya mpira wa pete ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports) imepokea kichapo cha magoli 52 kwa 7 kutoka  timu ya Ikulu. 

Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Bi. Pili Sukwa ameeleza kuwa licha ya kichapo hicho, Timu yake imeendelea kuimarika na ameahidi kufanya vizuri katika michezo inayofuata.

 Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameungana na mamia ya watumishi wenzao kushiriki michezo ya Mei mosi ambapo maadhimisho ya kitaifa yamepangwa kufanyika Mkoani Arusha.

Timu ya mpira wa Miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla kuingia uwanjani kucheza dhidi ya Timu ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA)

Timu ya Mpira wa Miguu ikifanya mazoezi ya kupasha viungo.



Mechi kati ya Nje na Hazina FC ikiendelea katika uwanja wa Ujenzi mjini Morogoro

Mshambuliaji machachari wa Nje Sports Bw. Mukrimu Mustafa akipongezwa na kocha wa Nje FC katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Ilboru mjini Arusha


Kepteni wa Nje FC akipatiwa matibabu mara baada ya kuchezewa rafu na mchezaji wa timu pinzani.

Wachezaji wa Nje FC wakiburudika mara baada ya kupata ushindi wa 2 - 0.

Timu ya mpira wa pete ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Ikulu muda mfupi kabla kuingia uwanjani kucheza mchezo wa raundi ya kwanza.

Timu ya mpira wa pete ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakipasha viungo muda mfupi kabla kuingia uwanjani kucheza dhidi ya Timu ya Ikulu


Juu na chini Mchezo ukiendelea.




 

WAZIRI MAKAMBA AWASILI UTURUKI KUELEKEA ZIARA YA KITAIFA YA MHE. RAIS SAMIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amewasili Ankara, Uturuki leo tarehe 16 Aprili 2024 na kukutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mhe. Hakan Fidan.


Pamoja na mambo mengine viongozi hao wamejadili kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan itakayofanyika nchini humo kuanzia tarehe 17 hadi 21 Aprili 2024.


Wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia ambayo inafanyika kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayyip ErdoÄŸan viongozi hao watashuhudia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano nane (8) katika sekta za Elimu, Utalii, Utunzaji Nyaraka na ushirikiano katika masuala ya Diaspora. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe.  Hakan Fidan baada ya kuwasili nchini Uturuki kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini humo
Mhe. Makamba akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Hakan Fidan


Mhe. Waziri Makamba na Mhe. Waziri Fidan wakiwa na ujumbe walioongozana nao wakati wa mazungumzo yao. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Bakari. Wa pili kulia ni Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Mehmet Gulluoglu







 

BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC LAPOKEA MAPENDEKEZO YA KATIBU MKUU MTEULE WA JUMUIYA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki

Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) leo tarehe 16 Aprili, 2024 limepokea mapendekezo ya uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo katika Kikao chake cha 52 cha Dharura kilichofanyika kwa njia ya mtandao.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa kufuatia mabadiliko ya nafasi hiyo yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto ambapo amemteua Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Dkt. Peter Mutuku Mathuki kuwa Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Urusi.

Hivyo, Mhe. Ruto amempendekeza Bi. Veronica Mueni Nduva kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya mara baada ya kuthibitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katibu Mkuu wa Jumuiya huteuliwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa Mkuu wa Nchi husika kulingana na utaratibu wa mzunguko ambao unatoa kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu katika nafasi hiyo.

Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Peter Mathuki aliteuliwa na Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Februari, 2021. Hivyo, kulingana na muda wa kuhudumu Jamhuri ya Kenya imebakiwa na miaka miwili kukamilisha kipindi chake cha miaka matano (5).

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri umeamua kuwa, katika kipindi cha mpito majukumu ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Ssemiwemba kulingana na kifungu 63 (3) cha Mkataba wa Uanzishawaji wa Jumuiyya hiyo.
Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki uliofanyika terehe 16 Aprili 2024 ukiendelea kwa njia ya mtandao
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi wakifuatilia Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki
Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki uliofanyika terehe 16 Aprili 2024 ukiendelea kwa njia ya mtandao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akifuatilia jambo wakati wa Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki

Friday, April 5, 2024

SERIKALI YA UINGEREZA YATANGAZA MIKAKATI MIPYA YA USHIRIKIANO NA TANZANIA KATIKA KUBORESHA UWEKEZAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza jijini Dodoma


Serikali ya Uingereza imetangaza mipango na mikakati mipya ya ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kuzimarisha ushirikiano katika Sekta za Afya, Uwekezaji na Biashara na kusaidia miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Mipango hiyo imetangazwa leo tarehe 05 Aprili 2024 jijini Dodoma na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika, Mhe. Andrew Mitchell wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi Ndogo za Ubalozi wa Uingereza jijini hapa.

Akitangaza mipango hiyo, Mhe. Mitchell amesema Serikali ya Uingereza imechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 18.9 kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Afya kwa Wote unaotekelezwa nchini ili kuimarisha mifumo ya afya, kuimarisha ustahimilivu wa huduma za afya, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika, Uingereza imetoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye masuala ya maboresho ya Afya ya Uzazi ikiwemo kuboresha huduma za uzazi wa mpango kwa lengo la kuwafikia takribani watu 900,000.

Katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan kwenye kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, Serikali hiyo imeahidi kuendelea kusaidia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ambao hutoa ruzuku kwa asilimia 15 kwa kaya maskini zaidi katika mikoa yote ya Tanzania ili kuimarisha uchumi, upatikanaji wa chakula na kuboresha mazingira kwa kaya hizo.

Kadhalika Serikali hiyo imepongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada hizo imeahidi kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 6.9 hadi mwaka 2026 ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi na kukuza teknolojia safi ya kupikia kwa utunzaji mazingira.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kwa kutangaza mipango na ufadhili kwa miradi mbalimbali ya manufaa kwa wananchi wa Tanzania.

Pia ameipongeza nchi hiyo kwa kufungua Ofisi Ndogo za Ubalozi jijini Dodoma ikiwa ni mwitikio wa wito wa Serikali ya Tanzania wa kuhamishia Makao Makuu yake jijini humo. 

Amesema mbali na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama Reli ya Kisasa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa jijini Dodoma, Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha jiji hilo ili kuwa na hadhi stahiki ya makao makuu ya nchi.

Wakati huohuo, Tanzania na Uingereza zimesaini Hati ya Makubaliano kuhusu Ushirikiano unaozingatia Maslahi ya Pande Zote Mbili. Hati hii pamoja na mambo mengine inalenga kuongeza ushirikiano katika maeneo ya uwekezaji kutoka Uingereza; Kuongeza biashara baina ya Tanzania na Uingereza; Kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kuisaidia sekta ya madini nchini.

Kwa upande wa Tanzania Hati hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida huku Uingereza ikiwakilishwa na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar. Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika, Mhe. Andrew Mitchell.

Mhe. Mitchell ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amekutana pia kwa mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell wakishuhudia zoezi la upandishwaji wa bendera za mataifa hayo mawili kwenye hafla ya ufunguziwa Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza jijini Dodoma
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America Balozi Swahiba Mndeme akifuatalia hafla ya ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi ya Uingereza jijini Dodoma
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell yaliyofanyika jijini Dodoma. 
Mazungumzo yakiendelea
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concar wakibadilisha Hati ya Makubaliano kuhusu Ushirikiano unaozingatia Maslahi ya Pande zote Mbili waliyoisaini jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell yaliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell yaliyofanyika jijini Dodoma

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell (katika) na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda yaliyofanyika jijini Dodoma.

WAZIRI WA DERMARK AKUTANA NA DR. NCHEMBA, DR. JAFO NA PROF. MKUMBO


Kampuni za Denmark zimealikwa kuja kuwekeza nchini katika sekta za uchukuzi, nishati, madini, mazingira na uchumi wa buluu ambazo ni moja ya sekta za kipaumbele za Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mwaliko huo umetolewa wakati wa mikutano baina ya Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Masuala ya Hali ya Hewa wa Denmark, Mhe. Dan Jorgensen na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo iliyofanyika jijini Dodoma leo Aprili 5, 2024.

Waziri Nchemba alisema Serikali inajenga miundombinu ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) ambapo Serikali ya Denmark imesaidia kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutupora ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 90. Alisema Serikali inakaribisha wawekezaji kuendesha reli hiyo ambapo itakapokamilika itaunganisha Tanzania na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda.

 

Dkt. Nchemba pia alizitaka kampuni za Denmark kuchangamkia fursa za ujenzi wa barabara ya mwendo kasi (express way) ya kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo kuu nchini.

Kwa upande wake, Dkt. Jafo alisisitiza umuhimu wa Denmark kushirikiana na Tanzania katika programu za utunzaji wa mazingira ikiwemo uwekezaji katika sekta ya nishati jadidifu. Aliiomba Denmark kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Misaada inayohitajika, alisema kuwa ni pamoja na kujenga uwezo wa watumishi, misaada ya kiufundi na rasilimali mbalimbali zikiwemo fedha.

Prof. Mkumbo, kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa kampuni za Denmark kuja kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani (processing industries) hususan katika madini hadimu nchini. Alisema fursa katika sekta hiyo ni kubwa kwa kuwa Tanzania ina takribani aina 10 za madini hayo. 

Aliiomba Denmark kuunga mkono jitihada za Serikali za kuchochea sekta binafsi nchini ambayo mchango wake bado uko chini, licha ya umuhimu wake katika kuongeza ajira na kuondoa umasikini nchini. “Tunaomba kuungwa mkono katika misaada ya kiufundi, elimu ya ufundi, urasimishaji wa sekta binafsi, kuchochea uhai wa sekta binafsi ili tuweze kujenga uwezo wa watu wetu hasa vijana kuwa na mbinu za kujiajiri wenyewe”, Prof. Mkumbo alisema.

Waheshimiwa Mawaziri walihitimisha mazungumzo yao kwa kuishukuru Denmark kwa misaada inayoipatia Tanzania katika sekta mbalimbali. Ulitolewa mfano wa msaada wa Krone bilioni 1.95 uliotolewa na Denmark kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2021.

Kwa upande wake, Mhe. Jorgensen alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za mwanzo kabisa barani Afrika kuanza ushirikiano wa kidiplomasia na Denmark katika miaka ya 1960. Hivyo, ameahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa kuzingatia vipaumbele vitakavyobainishwa na pande zote mbili.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) akizungumza na Waziri wa Maendeleo na Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgensen (hayupo pichani) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 5 Aprili, 2024. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.

Dkt. Mwigulu akimuaga Mhe. Dan Jørgensen.

Picha ya pamoja

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) akizungumza na  Waziri wa Maendeleo na Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgensen (hayupo pichani) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 5 Aprili, 2024. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Tausi Kida.

Waziri wa Maendeleo na Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgensen akizungumza na Mhe. Prof. Mkumbo jijini Dodoma tarehe 5 Aprili, 2024. 

Picha ya pamoja.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira ), Mhe. Dkt. Selemani Jafo (wa pili kushoto) akizungumza na Waziri wa Maendeleo na Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgensen (hayupo pichani) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 5 Aprili, 2024. Wa pili kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Denmark mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu.

Waziri wa Maendeleo na Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgensen (wa tatu kulia) akizungumza na Mhe. Dkt. Jafo (hayupo pichani) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 5 Aprili, 2024.

Picha ya pamoja.

Wednesday, April 3, 2024

WAZIRI WA DENMARK ATEMBELEA KIWANDA CHA CHEMI AND COTEX

Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen akisikiliza maelezo alipowasili katika Kiwanda cha Chemi and Cotex cha jijini Dar es salaam na kujionea jinsi Wafanyakazi wenye ujuzi wa kiwanda hicho wanavyotekeleza shughuli zao za kila siku kiwandani hapo.

Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen akielekea ndani ya Kiwanda  Chemi and Cotex cha jijini Dar es salaam alipotembelea kiwanda hicho kujionea jinsi Wafanyakazi wenye ujuzi wa kiwanda hicho wanavyotekeleza shughuli zao za kila siku kiwandani hapo.

Wafanyakazi wa Kiwanda cha Chemi and Cotex cha jijini Dar es salaam wakiendelea na kazi wakati Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen alipotembelea  kiwanda hicho



kiwandani humo




Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mhe. Dan Jorgensen ametembelea Mhe. Dan Jorgensen ametemebelea Kiwanda cha Chemi and Cotex cha  jijini Dar es salaam na kujionea jinsi Wafanyakazi wenye ujuzi wa kiwanda hicho wanavyotekeleza shughuli zao za kila siku kiwandani hapo.


Kiwanda cha Chemi and cotex kimeajiri wanawake na vijana zaidi ya 200 ambao ni wanufaika wa mafunzo ya ufundi  na hivyo kuwapatia ujuzi wanawake na vijana wa Kitanzania ikiwa ni sehemu ya kuongeza ajira na kuboresha
hali za maisha yao.

Mhe. Jorgensen ametembelea sehemu zinazozalisha bidhaa mbalimbali za Kiwanda hicho na kuelezea kuridhishwa kwake na ujuzi walionao watumishi wa Kiwanda hicho