Friday, September 13, 2013

Naibu Waziri awatembelea Watanzania wanaojishughulisha na biashara mjini Lusaka



Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushurikiano wa Kimataifa akizungumza na mmoja wa wajasiriamali wa kitanzania wanaofanya shughuli zao katika soko la Comesa lililopo mjini Lusaka, Zambia alipofanya ziara ya kuwatembelea Watanzania wanaojishughulisha katika eneo hilo, tarehe 12 Septemba 2013.


 
Mhe. Naibu Waziri akikagua shughuli za wajasiriamali Watanzania katika soko la Comesa. Kulia kwa  Naibu Waziri ni Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia na kushoto ni Bw. Mboweto, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Comesa ambaye ni Mtanzania.
 
Naibu Waziri azungumza na Wajasiriamali wa Kitanzania, Lusaka
Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewatembelea Wajasiriamali ambao ni Raia wa Tanzania wanaoishi na kufanya shughuli zao nchini Zambia katika maeneo ya Viwanja vya COMESA. Katika ziara hiyo iliyofana, Mhe. Naibu Waziri aliambatana na Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia pamoja na Maofisa wengine wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Baada ya kutembelea mabanda mbalimbali na kukagua shughuli zinazofanywa na Watanzania hao, Mhe. Naibu Waziri alipata fursa ya kubadilishana nao mawazo. Watanzania hao walielezea furaha yao kwa kutembelewa na kiongozi wa Serikali ya Tanzania na kubainisha kufarijika kwao kwa namna Serikali yao inavyowajali. Waliomba juhudi zifanyike kupanua barabara katika eneo la Tunduma ili kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo. Aidha, waliomba mashauriano yafanyike ili kituo cha mpaka cha Tunduma/Nakonde kifanye kazi kwa masaa 24. Walisema hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano, kuongeza kasi ya biashara, kupunguza vitendo vya jinai na kuiongezea mapato Serikali.

Kwa upande wake, Mhe. Naibu Waziri aliwapongeza Watanzania hao kwa kuamua kufanya shughuli zinazoweza kuwapatia kipato cha halali na kujenga taifa lao. Aliwataka wahakikishe kwamba wote wanaishi kisheria na kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka za Zambia ili kuepusha  usumbufu kwao na kwa Serikali. Aidha, aliwataka wasijihusishe  na vitendo vyovyote vya jinai ili kuepusha kuchafua sifa nzuri za taifa la Tanzania.

Mhe. Naibu Waziri yupo nchini Zambia akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa kimataifa kuhusu Mkataba unaolenga Kutokomeza matumizi ya Mabomu ya kusambaa (Convention on Cluster Munitions). Kabla ya kutembelea wajasiriamali, Mhe. Naibu Waziri alikutana na kuzungumza na Watanzania wa rika na kada mbalimbali wanaoishi nchini Zambia, mazungumzo ambayo yalifanyika katika Ubalozi wa Tanzania, Lusaka
 
 
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.