Friday, September 27, 2013

Waziri Membe ashiriki Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Kamalesh Sharma  mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola uliofanyika tarehe 26 Septemba, 2013 Mjini New York sambamba na Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kujadili masuala muhimu kuhusu jumuiya hiyo.

Mhe. Membe na Mhe. Sharma wakifurahia jambo.

Mhe. Membe akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Peter Kalaghe wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Afisa Mwandamizi katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo .

Mhe. Membe akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Mhe. G.L. Peiris kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaoandaliwa na nchi hiyo na kufanyika mwezi Novemba, 2013

 Mhe. Peiris akimpatia maelekezo Afisa wake huku Mhe. Membe akisikiliza.


Mhe. Membe akiteta jambo na Balozi Adonia Ayebare ambaye ni mmoja wa Wajumbe wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola

Mhe. Membe akiongozana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Mhe. Hannah Tetteh mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola.
 
----------------------------------------

 MKUTANO WA 12 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JUMUIYA YA MADOLAWAFANYIKA MJINI NEW YORK.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameshiriki Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Mjini New York sambamba na Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadili masuala mbalimbali muhimu kuhusu Jumuiya hiyo.

Wakati wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Kamalesh Sharma alitoa taarifa kwa Mawaziri kuhusu kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa miaka minne  kuanzia mwaka 2013/2016 ulioandaliwa na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo ili kuiwezesha kukidhi mahitaji ya nchi wananchama. Mpango Mkakati huo umezingatia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nchi wanachama zinafuata utawala wa sheria, zinaimarisha demokrasia, zinaheshimu haki za binadamu pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia.

Katika maelezo yake, Mhe. Sharma alisema kuwa, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola inaendeleza jitihada zake kuzisaidia nchi wanachama kuimarisha demokrasia na maendeleo endelevu ambapo pamoja na mambo mengine waangalizi katika chaguzi mbalimbali zinazofanyika katika nchi wanachama wamekuwa wakipelekwa ikiwa ni pamoja chaguzi zilizofanyika hivi karibuni katika nchi na Ghana, Maldives na Sri Lanka.

Aidha, Mawaziri hao walipata fursa pia ya kupitia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Jopo la Watu Mashuhuri wa Jumuiya hiyo (EPG) kuhusu mageuzi katika Jumuiya hiyo. Vile vile ilielezwa kuwa, Katika kutekeleza mapendekezo hayo, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola imeanzisha mipango mbalimbali  ikiwa ni pamoja na kuunda Kikundi cha Wataalam kwa ajili ya kutafuta fedha  ili kuiwezesha Sekretarieti kuzisaidia nchi wanachama zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na zile zinazoendelea.

Katika hatua nyingine, Mawaziri  hao  walipokea  taarifa kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (CHOGM) unaotarajiwa kufanyika mjini Colombo, nchini Sri Lanka mwezi Novemba, 2013.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo wa CHOGM ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Mhe. G.L. Peiris alisema kuwa, nchi yake imekamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mkutano huo na kuwahakikishia Mawaziri hao kuwa hali nchini kwake ni ya amani na usalama tofauti na taarifa zinazotolewa na baadhi ya nchi kuwa hali si shwari nchini humo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama 54 wa Jumuiya ya Madola ambayo Kiongozi wake Mkuu ni Malkia Elizabeth II wa Uingereza.

-Mwisho-
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.