Thursday, May 26, 2016

Tanzania na China kuendelea kuimarisha ushirikiano

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akiwaonyesha waandishi wa habari  kitabu kinachoelezea Historia ya Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye Mkutano na vyombo vya habari  uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano ambao  Bi. Kasiga aliwaelezea mafanikio ya ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Aziz Mlima nchini China  ambapo  pamoja na kufadhili shughuli mbalimbali za kiuchumi, nchi hiyo pia imekubali kutoa ufadhili wa nafasi kumi za masomo ya kidiplomasia ambapo itatoa nafasi tano za  mafunzo ya muda mrefu na tano za muda mfupi kwa kila mwaka
Mkutano ukiendelea
==================================================================



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Kikazi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini China

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima alifanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia tarehe 15 – 19 Mei 2016 kufuatia mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na China katika nyanja za siasa, uchumi na utamaduni.

Akiwa nchini China, Dkt. Mlima pamoja na mambo mengine alipata fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Makampuni makubwa ya China ambayo baadhi yao yameshawekeza nchini na mengine yameonesha dhamira ya kuwekeza.

Wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Zhang Ming, masuala mbalimbali yalijitokeza ikiwa ni pamoja na China kusisitiza dhamira yake ya dhati ya kukuza ushirikiano na Tanzania katika nyanja ya uchumi kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu. China imeweka kipaumbele cha juu katika miradi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na eneo la viwanda pamoja na maboresho ya Reli ya TAZARA na ipo tayari kuanza upembuzi yakinifu wa Reli ya Kati. 

Kwa upande wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Kampuni ya China ya Merchant Holding International (CMHI) ambayo imeingia ubia na Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Oman kujenga bandari hiyo, wapo katika hatua nzuri ya kukamilisha mazungumzo ya ubia wao ili waanze awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ndani ya mwaka huu wa 2016.
Kwa suala la ujenzi wa eneo la viwanda, Serikali ya China imebainisha kuwa ikwishatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu wezeshi (barabara, nishati ya umeme, maji, TEHAMA).

Kuhusu Reli ya TAZARA, China imeahidi kuwa itaendelea kuipa kipaumbele cha juu reli hiyo kwa sababu inabeba historia ya mahusiano yake na Afrika. China imeridhishwa na mazungumzo ya wataalamu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kuahidi kufanyia kazi yaliyokubalika ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kupitia Itifaki ya 16 kwa ajili ya maboresho makubwa ya miundombinu ya TAZARA pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye mikutano itakayofuata kuangalia namna bora ya kuendesha reli hiyo kwa ushirikiano na Tanzania na Zambia. 

Mkutano na Mamlaka ya Tumbaku

Katibu Mkuu alikutana na Kamishna wa State Tobacco Monopology, Bw. Lin Chengxing ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia utekelezaji wa Mkataba wa Kuruhusu Tumbaku ya Tanzania kuingia soko la China uliosainiwa mwaka 2013 wakati Rais wa nchi hiyo, Mhe. Xi Jinping alipofanya ziara nchini. Bw. Lin alijulisha kwamba makampuni mawili ya China-Hunan Industries na Shandong Industries yamepewa jukumu la kuinunua tumbaku ya Tanzania kwa ajili ya kufanya majaribio. 

Hadi hivi sasa wameshanunua tani 1500 ambazo zinahifadhiwa kwa kati ya miezi 24 hadi 30 (fermentation) kabla ya kutumika kuzalisha sigara. Matarajio yao ni kwamba sigara zitakazozalishwa na tumbaku ya Tanzania itaingia soko la China mwaka ujao. Endapo soko la China litapendelea sigara hizo, mahitaji ya tumbaku ya Tanzania katika soko la China yataongezeka kwa kiasi kikubwa. 

Mkutano na Chuo Kikuu cha Mambo ya Nje

Dkt. Mlima alikutana na Rais wa Chuo Kikuu cha Mambo ya Nje cha China, Prof. Qin Yaqing ambapo walijadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya chuo hicho na Chuo cha Diplomasia cha hapa nchini. Katika majadiliano hayo,  walikubaliana kushirikiana katika tafiti na utoaji wa mihadhara.  Aidha, Chuo hicho kimeahidi kutoa nafasi za masomo tano za muda mfupi na tano za muda mrefu kila mwaka kwa Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje. Chuo hicho kilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China na baadaye kilianzisha programu mbalimbali na kuchukua wanafunzi kutoka nje ya nchi. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 26 Mei 2016.
 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Afrika
Tanzania inaungana na nchi nyingine za Bara la Afrika kusherehekea Siku ya Afrika inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Mei.
Sherehe hizo hufanyika kuadhimisha siku ya kuundwa  kwa Muungano wa Nchi za Afrika (OAU) Mwaka 1963 na baadaye Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2002 pamoja na maendeleo ya demokrasia, amani na utulivu wa kisiasa, uchumi na kijamii yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwa umoja huo.
Wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwa Umoja huo tarehe 25 Mei 2013 mjini Addis Ababa, Ethiopia Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika katika tamko lao waliahidi kumaliza kabisa vita ifikapo mwaka 2020 (Silencing the Guns by 2020).
Aidha, Umoja wa Afrika ulipitisha Agenda 2063 yenye kutaka Afrika yenye Amani, Maendeleo na utangamano (Afrika tunayoitaka ifikapo 2063 -Africa we want - 2063). Katika kutekeleza Agenda hiyo Umoja wa Afrika umeandaa mpamgo wa kwanza wa miaka kumi ya utekelezaji wa miradi ya kwanza muhimu iliyojikita kwenye sekta za nishati, usafirishaji, usafiri wa anga, sayansi na teknolojia pamoja na kukuza utangamano barani Afrika.
Kwa muktadha huo, Tanzania inatumia siku hii kuuhakikishia Umoja wa Afrika na Bara la Afrika kwa ujumla kuwa, itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu na kuendelea kushirikiana na nchi nyingine katika kutekeleza malengo yake makubwa hususan Dira ya Maendeleo ya Afrika hususani Agenda 2063 na mpango wake huo wa kumaliza vita Barani Afrika ifikapo mwaka 2020.
Itakumbukwa kwamba, Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa kupigania uhuru wa nchi za Afrika, hususan Kusini mwa Afrika pamoja na kuendelea kutatua migogoro iliyopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Darfur, Sudan na Burundi. Hivyo, kuadhimishwa kwa siku hii kunatoa fursa nzuri kama nchi kupitia upya nafasi yake katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 25 Mei, 2016.



Tuesday, May 24, 2016

Press Release

PRESS RELEASE

JOB OPPORTUNITY AT ITU HEADQUARTERS-GENEVA

The Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation has received vacancy announcement from the International Telecommunication Union (ITU) inviting qualified Tanzanians to apply for the post of Web Developer.
 
Application details can be found on ITU website: http://www.itu.int/employment/Recruitment/index.html Closing date for application is 20th June, 2016.

“The Ministry encourages qualified Tanzanians to apply”.


Issued by: The Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation, Dar es Salaam.

24th May, 2016

Waziri Mahiga akutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mipango wa Korea Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Mipango na Uratibu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea, Mhe. Balozi Paik Ji-ah. Mazungumzo yao yalijikita katika kukuza mahusiano baina ya Tanzania na Korea Kusini katika nyanja za   miundombinu, biashara na afya. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi Paik kwa ushirikiano wanaouendeleza katika kuisaidia Tanzania ikiwemo mchango wao kwenye ujenzi wa Daraja la Malagarasi huko Kigoma na miradi mingine ya barabara.Mhe. Balozi Ji-ah yupo nchini kwa ziara ya siku tatu.
Ujumbe ulioambatana na Mhe. Balozi Paik Ji-ah nao wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Dkt. Mahiga na Balozi  Ji-ah. Kulia ni Balozi wa Korea Kusini nchini, Mhe. Song Geum-young.
Balozi Ji-ah akiendelea kuelezea jambo huku Waziri Mahiga akimsikiliza kwa makini.
Balozi wa Korea Kusini nchini, Mhe. Song Geum-young (kulia) akichangia jambo katika mazungumzo kati ya Waziri Mahiga na Naibu Balozi Mhe. Paik Ji-ah kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi wa Korea Kusini
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) pamoja na Afisa Mambo Nje Bi. Bertha Makilagi nao wakifuatilia mazungumzo.
Mazungumzo yakiendelea.
Waziri Mahiga akiagana na mgeni wake Balozi Paik Ji-ah mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Dkt. Mahiga akiagana na Balozi Geum-young.
Dkt. Mahiga na wageni wake wakiwa katika picha ya pamoja.

Picha na Reginald Philip

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia akutana na Balozi wa China nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki akizungumza na Balozi wa China nchini Mhe. Lu Youqing, alipomtembelea leo katika ofisi za Wizara na kuzungumza naye juu ya kuendelea kuimrisha ushirikiano ili kukuza fursa za kiuchumi zilizopo hususan katika kuboresha miundombinu na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda sambamba na kuinua maisha ya wananchi
Maafisa kutoka Ubalozi wa China walioambatana na Mhe. Lu Youqing wakifuatilia mazungumzo
Mhe. Lu Youqing akijadili jambo na Balozi Kairuki mara baada ya mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea

Wanafunzi kutoka Chuo cha Kijeshi cha India watembelea Wizara ya Mambo ya Nje

      Afisa Mwandamizi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Luangisa akiongoea na wanafunzi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu wa Jeshi nchini India (hawapo pichani) ambao jana walitembelea katika Ofisi za Wizara Jijini Dare es Salaam  kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali kuhusu Sera ya Mambo ya Nje. Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Maji nchini India, Admiral D. M. Sudan.Wanajeshi hao watakuwa na ziara ya siku tano nchini Tanzania ambayo inatarajiwa kukamilika tarehe 26 Mei, 2016.
Sehemu ya wanajeshi wakifuatilia na kuchangia mazungumzo

 Sehemu nyingine ya wanajeshi hao wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na Bw. Luangisa

Monday, May 23, 2016

Utaratibu wa matumizi ya Wimbo na Bendera ya Afrika Mashariki

TAARIFA KWA UMMA


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kutoa utaratibu wa matumizi ya Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kama ilivyotangazwa hivi karibuni.

Utaratibu huo ni kwamba  Bendera ya Taifa itaanza kupeperushwa ikifuatiwa na Bendera ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki, vivyo hivyo Wimbo wa Taifa utaanza kupigwa ukifuatiwa na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilitatangaza kuhusu matumizi ya Bendera na Wimbo wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Wizara, Idara, Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na Taasisi Binafsi.

Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unapatikana katika tovuti ya Wizara ambayo ni www.foreign.go.tz.

Aidha, kwa mujibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  vipimo maalum vya kutengeneza Bendera hiyo ni kama vinavyoonekana hapa chini.






Imetolewa na,
 Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 23 Mei, 2016.

Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki