Tuesday, May 16, 2023

MCHANGO WA TANZANIA KATIKA MEDANI ZA KIKANDA NA KIMATAIFA UTUNZWE: DKT TAX


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali nchini kuendelea kutunza kumbukumbu za historia ya Tanzania na mchango wake katika medani za kikanda na kimataifa ili kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.


Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma tarehe 16 Mei 2023 wakati wa hafla fupi ya kikabidhi Machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi 18 zikiwemo za elimu.


Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, Tanzania ina historia kubwa na nzuri katika medani za kikanda na kimataifa ikiwemo mchango wake katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali kuunganisha nguvu ya kutunza kumbukumbu ya historia hiyo nzuri na kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.


Ameeleza kuwa, Wizara imeamua kuyakabidhi machapisho hayo kwa Taasisi hizo ili yasaidie kurithisha historia iliyomo kwa vizazi vijavyo, na kujenga hamasa ya uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


“Wizara inawakabidhi nyinyi machapisho haya kama wawakilishi wa wengi. Tunaamini kupitia Vyuo na Taasisi zenu machapisho haya yatawafikia na kusomwa na Watanzania wengi. Vilevile kupitia machapisho haya historia kuhusu mchango uliotolewa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla itatunzwa na kukumbukwa daima” amesisitiza Mhe. Dkt. Tax.


Pia ameziomba taasisi hizo kuwa chachu katika kueneza historia adhimu iliyomo kwenye chapisho hilo kwa kuhakikisha linasomwa. “Pamoja na kulitumia chapisho hili kama rejea, na kuhamasisha lisomwe, niwaombe wadau mbalimbali nchini kuona uwezekano wa kuandaa simulizi au filamu ya chapisho ili kuweza kuwafikia watu wengi hususan vijana” alisisitiza Mhe. Dkt. Tax.


Aidha, amefafanua kuwa, Chapisho hilo ambalo pamoja na mambo mengine linaeleza harakati za ukombozi katika nchi za Angola, Namibia, Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Msumbiji na mchango wan chi za Tanzania, Zambia, Botswana, Lesotho, Malawi na Swaziland, lilipewa jina la Hashim Mbita kutoka na mchango thabiti na uongozi mahiri wa Hayati Brigedia Generali Hashim Mbita  alioutoa akiwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Kupigania Uhuru Afrika kuanzia mwaka 1972 hadi 1994.


Mhe. Dkt. Tax pia ameshukuru na kupongeza  mchango uliotolewa na Viongozi mbalimbali wa Tanzania akiwemo  Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika kwani fikra na mtazamo wake kuhusu umuhimu wa uhuru kwa nchi za Afrika zilifanikisha nchi zote za Afrika kujikomboa dhidi ya ukoloni.


Pia Mhe. Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Kitanzania ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota kwa kuchapisha chapisho hilo kwa umahiri.


“Nawashukuru wadau wote waliofanikisha uchapishaji wa Chapisho la Hashim Mbita ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa  kuandaa Chapisho hilo lenye Volume 9 na kwa kutambua mchango wa Tanzania katika harakati za Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Pia kipekee  namshukuru Rais Mstaafu wa wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuniagiza nikiwa Katibu Mtendaji wa SADC na kunisisitiza kuhakikisha chapisho hili linakamilika baada mchakato wa awali kusimama ambapo mwaka 2014 kufuatia maagizo hayo, mchakato ulitekelezwa katika  awamu tatu na kukamilika mwaka 2020” alifafanua Dkt. Tax.


Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amesema kwamba, Wizara imepokea makasha 28 ya Chapisho la Hashim Mbita lenye Volume 9.


Pia aliongeza kusema Sektretarieti ya SADC inaendelea na mchakato wa kutafsiri Chapisho la Hashim Mbita kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kulisoma na kuijua historia ya nchi yao hususan mchango wa Tanznaia katika Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika.


Hafa hiyo ilihudhuriwa na viongozi na wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais, Bunge, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Maktaba ya Taifa, Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Mwalimu Nyerere. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Machapisho Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali za hapa nchini. Hafla hiyo ambayo ilizishirikisha Taasisi 18 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ilifanyika jijini Dodoma tarehe 16 Mei 2023

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali nchini. Katikati ni Mhe. Dkt. Tax na kulia ni Mhe. Vincent Mbogo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama

Sehemu nyingine ya washiriki

Wawakilishi wa Taasisi zilizoshiriki hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita wakifuatailia tukio. kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali.


Mhe. Dkt. Tax akimkabidhi Bw. Mbwana Msingwa kutoka Ofisi ya Rais Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita

Mhe. Dkt. Tax akiwakabidha Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita Wawakilishi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mabo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mbogo (kulia)

Makabidhiano yakiendelea kwa wawakilishi wa taasisi mbalimbali ikiwemo Maktaba ya Taifa.

Makabidhiano ya Machapisho ya Hashim Mbita yakiendelea

Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) naye akikabidhiwa amachapisho ya Hashim Mbita

 

BALOZI FATMA RAJAB APOKEA ZAWADI YA TENDE KUTOKA SAUDI ARABIA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea zawadi ya tende kutoka kwa wawakilishi wa Kituo cha Hisani cha Mfalme wa Saudi Arabia. Zawadi hiyo ya tende imetolewa na Serikali ya Saudi Arabia kupitia Kituo hicho na hafla ya makabidhiano imefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiangalia nyaraka alipopokea zawadi ya tende tani 25 zilizotolewa na Serikali ya Saudi Arabia kupitia Kituo cha Hisani cha Mfalme wa Saudi Arabia katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kulia) akizungumza na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Bw. Fahad Alharbi katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam alipofika kukabidhi zawadi ya tende zilizotolewa na Mfalme wa Saudi Arabia kupitia Kituo cha Hisani cha Mfalme wa Saudi Arabia

 Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Bw. Fahad Alharbi (kushoto) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kulia) katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam alipofika kukabidhi zawadi ya tende zilizotolewa na Mfalme wa Saudi Arabia kupitia Kituo cha Hisani cha Mfalme wa Saudi Arabia

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kulia) akiwa na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Bw. Fahad Alharbi wakionesha hundi yenye thamani ya Dola za Marekani 64,000 ambao ni msaada uliotolewa na Serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya kuimarisha huduma za TEHAMA katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (wa pili kulia) akiwa na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Bw. Fahad Alharbi (wa pili kushoto) wakiwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Leonce Bilauri na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Isaack Kalumuna.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amepokea zawadi ya tende zilizotolewa na Serikali ya Saudi Arabia katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Tende hizo, tani 25 zimetolewa na Mfalme wa Saudi Arabia, Mtukufu Salman bin Abdulaziz Al Saud kupitia Kituo cha Hisani cha Mfalme wa Saudi Arabia na kuwasilishwa nchini na wajumbe maalum wa Taasisi hiyo ya Mfalme Bw. Alrazani Abdulaziz Abdulahman na Alqunur Fahad Abdulahman.

Akipokea zawadi hiyo Balozi Fatma amemshukuru Mtukufu Mfalme Salman kwa kuendelea kutambua urafiki na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Saudia Arabia.

"Zawadi hii ya tende imetolewa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Watanzania wote, hii inaonesha uhusiano uliopo kati ya nchi zetu kupitia ujumbe mahsusi uliowasili nchini kwa ajili ya kuwasilisha tende hizi” alisema Balozi Fatma.

Vilevile, Balozi Fatma ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia unaendelezwa kwa vitendo ambapo Serikali ya Saudi Arabia imekuwa na ziara mbalimbali za wataalam nchini katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, afya ambapo wataalamu wa matibabu wamekuwa wakija kufanya huduma za pamoja za upasuaji nchini na katika sekta ya anga Saudi Arabia imeanzisha safari za ndege za moja kwa moja kuja nchini.

Naye Kaimu Balozi Bw. Fahad Alharbi alieleza kuwa Saudi Arabia inatambua umuhimu wa ushirikiano wake na Tanzania katika kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na akaahidi kuwa Ofisi ya Ubalozi itaendelea kuhakikisha inadumisha uhusiano huo.

Alisema kuwa kituo cha hisani cha Mfalme Salman ambacho kimekuja na ujumbe wa Mfalme huyo kukabidhi salamu pamoja na tende, kimekuwa kikitoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo usaidizi wa chakula, dawa na malazi kwa jamii zilizopatwa na majanga.

“Katika nyakati tofauti kituo hicho kimewezesha ziara za madaktari kutoka nchini Saudia Arabia ambao huweka kambi za huduma za matibabu ya upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo” alisema Bw. Fahad.

Pia akaeleza kuwa huduma hiyo ya madakatari itaendelea kutolewa na kwamba hivi karibuni madaktari wengine wanatarajia kuja nchini kuendelea kutoa huduma ya matibabu katika hospitali mbalimbali.

Wakati huohuo Serikali ya Saudi Arabia imekabidhi msaada wa kifedha wenye thamani ya Dola 66, 532 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 159 kwa lengo la kuimarisha huduma za TEHAMA katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Tanzania na Saudi Arabia zinashirikiana katika sekta za uvuvi, kilimo, mifugo, ujenzi wa miundombinu na masuala ya anga na utalii.

SERIKALI YA TANZANIA IMEJIPANGA KUENDELEA KUNUFAIKA NA FURSA ZA MTANGAMANO WA KIKANDA

Serikali ya Tanzania imejipanga kuendelea kunufaika na fursa zinazotokana na Mtangamano wa Kikanda ili kuwawezesha watanzania kufaidika na uanachama wa Tanzania katika Jumuiya mbalimbali za kikanda.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika   Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakati wa ufunguzi wa semina kuhusu “Nafasi ya Tanzania katika Mtangamano wa Kikanda” iliyotolewa na Wizara jijini Dodoma kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kukuza uelewa kuhusu masuala ya mtangamano wa kikanda.

Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, mtangamano wa kikanda ni dhana muhimu katika kukuza uchumi, kuimarisha uhusiano wa kisiasa, amani na usalama katika mataifa  na kwamba Kamati hiyo ni miongoni mwa wadau muhimu wanaotakiwa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu mtangamano wa kikanda ili kushirikiana na Wizara kueleza fursa na faida zake kwa wananchi.

Ameongeza kusema kwamba kwa Tanzania mtangamano wa kikanda ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hivyo uelewa wa pamoja kuhusu dhana hii hususan fursa, faida na changamoto na namna ya kuzitatua unahitajika ili kufikia malengo kusudiwa.

Vilevile ameeleza kuwa, Tanzania inao mchango mkubwa katika Mtangamano wa kikanda na inategemewa ambapo pia imeendelea kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na uanachama wake katika Jumuiya za Kikanda hususan, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ikiwemo ajira, biashara, teknolojia, elimu na uwekezaji.

Mhe. Dkt. Tax pia alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kila Jumuiya kwa kusisitiza kuwa kila Jumuiya ina umuhimu na mchango mkubwa kwa Tanzania kulingana na lengo la kuanzishwa kwake.

“Naomba niweke hoja hii sawa. Kumekuwa na ulinganifu wa utendaji wa Jumuiya hizi ambapo baadhi ya watu wanaona jumuiya moja ni bora kuliko nyingine pasipo kujua kwamba kila moja ina umuhimu wake kulingana na lengo la kuanzishwa,” amesema Dkt. Tax.

Akitoa mfano amesema SADC ilianzishwa kwa lengo la kupigania ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Hivyo kwa kiasi kikubwa Jumuiya  hii imejikita kwenye masuala ya amani, ulinzi na usalama na kwamba ni kutokana na lengo hilo nchi za kusini zilikombolewa katika ukoloni lakini pia nchi wanachama kama Madagascar na Lesotho zilizokuwa na migogoro zimerejea katika hali ya amani na utulivu.

Kuhusu EAC amesema lengo la kuanzishwa kwake lilikuwa ni kuimarisha uchumi na biashara, hivyo kila jumuiya ni muhimu kulingana na majukumu yake.

Pia amesema anaishukuru kamati hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Wizara kwenye masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo katika masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.

Akiwasilisha mada hiyo, Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Bw. Charles Mtakwa amesema zipo faida nyingi kwa Tanzania kuwa mwanachama katika EAC na SADC ikiwemo ajira, biashara, elimu, teknolojia na uendelezaji miundombinu ya kikanda.

“Mtangamano wa Kikanda ni dhana muhimu kwa Tanzania na hususan katika kukuza uchumi kupitia biashara, uwekezaji lakini pia kuboresha ufanisi wa soko la bidhaa mbalimbali kwani ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea kukuza biashara miongoni mwake ambayo bado ipo katika kiwango cha chini cha asilimia 13 ukilinganisha na nchi za Bara la Asia asilimia 61 na Amerika asilimia 47” amesema Bw. Mtakwa.

Amesema kupitia Mtangangamano wa kikanda nchi wanachama huweza kufanya maamuzi ya pamoja ya kisera na kuchochea  mageuzi ikiwemo yale ya kiuchumi. Pia kupitia mtangamano wa kikanda nchi wanachama hushirikiana kuchangia gharama za miradi mikubwa na miundombinu kama miradi ya umeme na miradi ya barabara na reli.

Ameeleza kuwa, Mtangamano wa Kikanda ambao unalenga katika kuziwezesha nchi wanachama kushirikiana katika masuala mbalimbali  unazo hatua tano ambazo ni biashara huria; muungano wa forodha;soko la pamoja;muungano wa kifedha na muungano wa kisiasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa anaipongeza na kuishukuru Wizara kwa kuendelea kutoa semina kuhusu mada mbalimbali za umuhimu na kwamba Kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri unaohitajika kwa Wizara.

Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati hiyo wameishauri Wizara kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kutangaza fursa zinazopatikana katika mtangamano wa kikanda na kuendelea kusimamia makubaliano na mikataba iliyokwisha sainiwa katika kanda hizo ili itekelezwe kama ilivyopangwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akifungua semina kuhusu Nafasi ya Tanzania katika Mtangamano wa Kikanda iliyoandaliwa na Wizara kwa Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama 9NUU) iliyofanyika Dodoma hivi katibuni

Semina ikiendelea

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akizungumza wakati wa semina iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu Mtangamano wa Kikanda.

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakifuatilia semina kuhusu Mtangamano wa Kikanda
Semina ikiendelea
Washiriki wakifuatilia semina
katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akichangia jambo wakati wa semina kuhusu Mtangamano wa Kikanda. Kushito kwake ni Naibu katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. Haji Janabi

Mkutano ukiendelea















Monday, May 15, 2023

MWILI WA MEMBE WAWASILI RONDO, LINDI


Mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe umewasili kijijini kwake Rondo mkoani Lindi kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2023.

Mwili wa Marehemu Membe umewasili kijijini hapo majira ya saa  06.40 mchana na Helikopta ya Jeshi na kupokelewa na mamia ya waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Limdi, Mhe. Shaibu Ndemanga

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb.) aliongoza ujumbe uliosafiri na mwili wa marehemu Membe kutoka Jijini Dar es Salaam hadi Rondo mkoani Lindi. Mhe. Nape ni Mbunge wa Jimbo la Mtama ambalo awali liliongozwa na Marehemu Membe kwa miaka 15 mfululizo (2000-2015).

Mwili marehemu mara baada ya kuwasili nyumbani kwake ulipokelewa na wanafamilia kwa simanzi, huzuni pamoja na vilio.

Mwili huo utalala nyumbani kwake hadi kesho tarehe 16 Mei 2023 atakapopumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Marehemu Membe aliaga Dunia tarehe 12 Mei, 2023 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki, Jijini Dar es Salaam.
Helikopta ya Jeshi iliyobeba mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Marehemu Bernard Membe ikiwasili kijijini kwake Rondo

Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa umebebwa na wananchi ulipowasili kijijini kwake Rondo
Wananchi wa Rondo na kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwa wamejipanga kupokea mwili wa Marehemu Bernard Membe ulipowasili nyumbani kwake kijiji cha Rondo, Lindi. 

Sehemu ya waombolezaji wakiwa katika hali ya huzuni na majonzi kwenye msiba wa Marehemu Bernard Membe kijijini kwake Rondo, Lindi 

Sunday, May 14, 2023

RAIS SAMIA ASHIRIKI KUUAGA MWILI WA BERNARD MEMBE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameungana na waombelezaji mbalimbali kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 2007 hadi 2015, Ndugu Bernard Kamilius Membe katika viwanja kwa Karimjee jijini Dar Es Salaam tarehe 14 Mei, 2023.


Akitoa salamu za rambirambi, Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa kuondoka kwa Ndugu Membe kumeleta masikitiko kwake binafsi, familia yake, Serikali, wadau mbalimbali, familia ya marehemu, wana Lindi na wananchi kwa ujumla. 


“Msiba huu umewagusa watu wengi ndani na nje ya nchi, kutokana na uhodari wake katika masuala ya siasa na diplomasia, hivyo nguzo kuu imeondoka Mwenyezi Mungu awape wanafamilia subira katika kipindi hiki cha majonzi”


Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ambaye pia ni mwenyeji wa tukio hilo la kuaga mwili, katika salamu zake za pole alieleza kuwa Wizara imempoteza kiongozi mahiri na hodari ambaye alijenga misingi mizuri katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.

“Marehemu Membe pamoja na kusimamaia maslahi ya nchi alitumia umahiri wake kuwajenga watumishi wa Wizara ambao kwa sasa wengine wanahudumu katika nafasi za Balozi”.


Aidha, Ndugu Membe alikuwa mcheshi, mwenye upendo na hodari hivyo Wizara itaendelea kuyaenzi mafanikio yaliyofanywa naye wakati wa utumishi wake.


Tukio hilo la kuaga mwili wa Marehemu Bernard Membe lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ambao ni pamoja na: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa; Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma; Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu; Mawaziri, Manaibu Waziri, Wakuu wa Taasisi na Viongozi wengine wa Serikali, Taasisi binafsi na za dini na vyama vya siasa.


Wengine waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na: Mwakilishi wa kundi la wake wa Viongozi (Millenium group) Bi. Arafa Kikwete; Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe; Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Chongolo; Mkuu wa Mabalozi na Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih; Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Amos Makala; Mtendaji Mkuu wa Mahakama (kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania), Prof. Elisante Ole Gabriel; na Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Mussa Azan Zungu.

=============================================

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Kamilius Membe mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2023
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na waombolezaji wakati wa kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Kamilius Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2023

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe tarehe 14 Mei, 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa salamu za rambirambi kwa waombolezaji walioshiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa pole kwa Mjane wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe na familia yake  katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimpa pole Denis Membe mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei 2023.

Pichani, sehemu ya Waombolezaji walioshiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,, Marehemu Bernard Membe. 

Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe likiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

VIONGOZI MBALIMBALI WAMUAGA MHE. MEMBE KARIMJEE

Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umeungana na waombolezaji wengine kumuaga  aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Mhe. Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.  

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa (Mb.) akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  (Mb.) akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassoro Mbarouk  akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga  akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Majeshi  mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Ethiopia nchini  Mhe. Yonas Yosef akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  (Mb.) akisalimiana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (2021- 2022) wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam. kulia ni Mkuu wa Majeshi Msataafu Jenerali Davis Mwamunyange.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax  (Mb.) akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Joseph Sinde Warioba wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam. Kushoto ni naibu Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azan Zungu.

Baadhi ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam.

Saturday, May 13, 2023

SALAAM ZA RAMBIRAMBI

 

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea kwa mshtuko, taarifa za kifo cha Mhe. Bernard Kamillius Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (2007-2015).

Kama Mawaziri wa Mambo ya Nje aliyehudumu Kwa kipindi Kirefu, atakumbukwa kwa mchango wake katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa. 
Wizara inatoa pole za dhati kwa familia na watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza Mwanadiplomasia mahiri. 
"Tunaiombea Roho yake ipumzike Kwa Amani"