Wednesday, April 23, 2014

Mhe. Naibu Waziri azindua Kambi ya Airtel Rising Stars International Soccer

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa Kambi Maalum ya Kimataifa ya Mafunzo ya Mpira wa Miguu kwa vijana wa kike na kiume wenye umri chini ya miaka 17 kutoka nchi 12 za Afrika ikiwemo Tanzania. Uzinduzi huo ulifanyika Viwanja vya Azam vilivyopo Chamazi jijini Dar es Salaam tarehe 23 Aprili, 2014. Kambi hiyo inadhaminiwa kwa ushirikiano kati ya kati ya Kampuni ya Simu ya Airtel-Tanzania na Klabu ya Mpira wa Miguu ya Manchester United ya Uingereza.
Baadhi ya vijana hao wakimsikiliza kwa makini Mhe. Naibu Waziri (hayupo pichani).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Airtel-Tanzania, Bw. Sunil Colaso ambao ni wadhamini wa kambi hiyo kwa kushirikiana na Manchester United akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Mhe. Mahadhi akimsikiliza Bw. Colaso, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel-Tamnzania (hayupo pichani wakati wa uzinduzi huo.
Mmoja wa Walimu kutoka Manchester United Bw. Neil Scott akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

Katibu wa Naibu Waziri, Bw. Adam Isara akiwa na mmoja wa wadau wa michezo wakati wa uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Ayoub Nyenzi akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Bw. Sunil Colaso kwa pamoja na Walimu wa Vijana hao chini ya miaka 17 wakimsikiliza Bw. Nyenzi (hayupo pichani) kutoka TFF alipokuwa akizungumza. Kulia ni Bw. Andrew Stokes na katikati ni Bw. Neil Scott.
Wanamichezo na wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri.
Mshereheshaji Bw. Ephraim Kibonde akiendelea na kazi
Mhe. Maalim akipongezwa na Bw. Colaso baada ya kutoa hotuba.
Mhe. Maalim akielekea kuzindua rasmi kambi hiyo kwa kupiga mpira.
Mmoja wa vijana hao ambaye ni mlinda mlango akiwa tayari kudaka mpira kutoka kwa Naibu Waziri.

Mhe. Naibu Waziri akijiandaa kupiga mpira kuashiria kuzindua kambi hiyo ya vijana.
Mhe. Maalim akimsikiliza Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi Juliana Yasoda ambaye pia alishiriki uzinduzi huo.

Mhe. Naibu Waziri akizungumza na Waandishi wa Habari
Vijana hao wakiwa kwenye mazoezi
Mhe. Naibu Waziri katika picha ya pamoja na viongozi walioambatana na wanamichezo.
Mhe. Maalim katika picha ya pamoja  na wanamichezo.
Picha na Reginald Philip




Naibu Waziri wa Mambo ya Nje azindua Airtel Rising Stars International Soccer

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) amezindua rasmi Kambi Maalum ya Kimataifa ya Mafunzo ya Mpira wa Miguu kwa vijana wa kike na wa kiume wenye umri chini ya miaka 17 kutoka nchi 12 za Afrika ikiwemo Tanzania.

Uzinduzi wa Kambi hiyo umefanyika katika Viwanja vya Azam vilivyopo Chamazi Jijiji Dar es Salaam tarehe 23 Aprili, 2014 na inadhaminiwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Simu ya Airtel-Tanzania na Klabu ya Mpira wa Miguu ya Manchester United ya Uingereza. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhe. Dkt. Maalim amesema kuwa, kambi hiyo inalenga kuwapatia mafunzo maalum vijana hao wadogo ili kuwawezesha kuwa wachezaji mahiri katika mchezo huo ambao unapendwa na watu wengi duniani ikiwemo Tanzania.

“Mimi binafsi kama ilivyo kwa mamilioni ya Watanzania, mpira wa miguu una nafasi maalum katika mioyo yetu na tunazitambua na kuzipongeza jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Simu ya Airtel kwa ushirikiano na Manchester United katika kusaidia maendeleo ya mchezo huo hapa Tanzania na sehemu nyingine za Bara la Afrika. Asanteni sana Airtel na Manchester United” alishukuru Mhe. Maalim.

Mhe. Maalim alieleza kuwa, mafunzo hayo ambayo yatasimamiwa na Waalimu kutoka Shule za Mpira wa Miguu za Timu kubwa ya Manchester United, yanalenga kuwaandaa vijana hao wadogo na kukuza vipaji vyao katika mafanikio ya mpira wa miguu Afrika kwani watu wanahitaji kuona mapinduzi katika mchezo huo na kuondokana na matokeo mabaya katika mashindano ya kimataifa.

“Ushiriki wa watoto wetu kwenye mafunzo haya ambayo yatajikita katika kuwajengea uwezo kiakili, kimwili na kisaikolojia, yatawasaidia kuwa na umoja, yatawapa kujiaamini na hatimaye kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na afya njema na pia kuwa wachezaji wa kulipwa Barani Afrika na duniani hapo baadaye”, alisema Mhe. Maalim.

Mhe. Maalim aliongeza kuwa, anaona fahari kubwa kama mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwepo kwenye uzinduzi huo ikiwa ni katika kuhamasisha Diplomasia ya Michezo ambayo kwa sasa ni muhimu katika kukuza urafiki, undugu, ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya mtu mmoja mmoja kwa maana ya wachezaji na pia kwa nchi na nchi kama ilivyo kwa vijana hao ambao wametoka mataifa ya nje 11.

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sasa inahamasisha Diplomasia ya Michezo ikiwa ni njia mojawapo za kuimarisha mahusiano na mataifa mengine kupitia michezo. Wizara inaunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Wizara yenye dhamana ya michezo na Taasisi nyingine zote za michezo na kitendo cha mimi kuwepo hapa leo ni katika kuongeza nguvu kwenye jitihada hizo ili nchi yetu iendelee kimichezo,” alisisitiza Mhe. Maalim.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Airtel-Tanzania, Bw. Sunil Colaso aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya kuwekeza kwenye michezo.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Ayoub Nyenzi ambaye alimwakilisha Rais wa Shirikisho hilo,  alimshukuru Naibu Waziri kwa kuzindua Kambi hiyo ambayo ni ya pili kwa Tanzania baada ya ile ya mwaka 2011. Aidha, aliwaasa vijana hao kuzingatia mafunzo watakayopewa kwani ndio msingi wa maisha yao hapo baadaye.

Kwa upande wao Walimu wa vijana hao kutoka Manchester United Bw. Andrew Stokes na Bw. Neil Scott walisema kwao ni upendeleo wa pekee kufundisha vijana hao na kwamba Manchester United imedhamiria kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kuendeleza michezo.

Kambi hiyo ambayo ipo kwa siku tano itahusisha vijana 74 kutoka mataifa 12 ya Afrika ikiwemo Tanzania. Jina la nchi na idadi ya vijana kwenye mabano ni kama ifuatavyo; Tanzania (19), Niger (17), Chad (4), Kenya (4), Malawi (4), Shelisheli (2) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (6). Nchi nyingine ni Burkina Faso (4), Congo Brazaville (2), Gabon (4), Madagascar (2) na Siera Leone (6).

-Mwisho-














No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.