Thursday, February 26, 2015

Tanzania na Zambia zadhamiria kufufua Reli ya TAZARA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Zambia kwa ajili ya mazungumzo rasmi na Mwenyeji wake Rais Edgar Lungu ( mwenye suti ya kijivu aliyesimama mbele ya Rais Kikwete)
Rais Lungu akimkaribisha Rais Kikwete (hayupo pichani kuzungumza)
Mhe. Rais Kikwete akizungumza wakati wa mazungumzo rasmi na Rais Lungu na Ujumbe wake katika Ikulu ya Zambia. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Mebe na kulia ni Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya Salu na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma.
Mazungumzo yakiendelea
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania wakati wa mazungumzo rasmi akiwemo Mhe. Charles Tizeba (wa kwanza  kulia), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Abbas Kandoro (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Zuhura Bundala (wa tatu kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Talha Mohammed (wa kwanza kushoto), Afisa Mambo ya Nje.

Picha ya Pamoja
Mhe. Rais Lungu akiwa amefuatana na Mhe. Membe.
==============================================



Tanzania na Zambia kufufua Reli ya TAZARA

Tanzania na Zambia zimekubaliana kushirikiana na kuimarisha sekta ya miundombinu hususan kufufua Reli inayounganisha nchi hizi mbili (TAZARA) ili kukuza biashara na uwekezaji.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete nchini Zambia.

Akizungumza wakati wa mkutano rasmi kati yake na mwenyeji wake, Mhe. Edgar Lungu, Rais wa Zambia, Rais Kikwete alisema kuwa umefika wakati sasa  wa kuifufuA Reli ya TAZARA ambayo ni kiungo muhimu na alama kubwa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Mhe. Rais Kikwete alifafanua kuwa umuhimu wa reli hiyo ni wa kihistoria ambao unahusisha nchi tatu za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China ambao kwa kiasi kikubwa walichangia ujenzi wa reli hiyo.

“Upo umuhimu mkubwa wa kuifufua Reli ya TAZARA ili ifanye kazi kama awali kwani ni alama na kiungo muhimu cha ushirikiano wetu sisi Tanzania na Zambia”, alisema Rais Kikwete.

Aidha, aliongeza kuwa Tanzania na Zambia zimekubaliana kuwekeza zaidi katika reli hiyo ikiwemo kuboresha uendeshaji na ukarabati ili kuirejesha katika hali yake ya awali na hatimaye kukuza biashara na uwekezaji. Alifafanua kwamba hapo awali reli hiyo iliweza kusafirisha tani zaidi ya milioni 2 za bidhaa kwa mwaka wakati sasa reli hiyo inasafirisha  tani laki 2 kwa safari inayotumia hadi siku 12 kutoka Dar es Salaam hadi New Kapiri Mposhi wakati malori yanatumia siku tano pekee.

“TAZARA inapita katika kipindi kigumu sasa, hivyo tumezungumza namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo uendeshaji na ukarabati ili irejee katika hali yake ya awali”, alisisitiza Rais Kikwete.

Katika  hatua nyingine Mhe. Rais Kikwete alimpongeza Rais Lungu kwa kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Rais wa Zambia na pia alitoa salamu za pole kwa Rais huyo na Wazambia wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati Michael Satta.

Kwa upande wake, Rais Lungu alisema kuwa Tanzania na Zambia zinajivunia mafanikio ya ushirikiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambayo yamejikita katika sekta za Kilimo, Usafirishaji, Nishati na Mawasiliano.

Pia, alisema kwamba nchi yake ipo tayari kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo ambao unaanzia ngazi ya serikali, kanda, Bara  na Kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuitumia Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1992 kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa na nchi hizi mbili. Aidha, alikubaliana na hoja ya kuifufua reli ya TAZARA kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini humo kwa mwaliko wa Rais Lungu alifuatana na Mama Salma Kikwete, Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Mamlaka mbalimbali.

_Mwisho_


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.