Friday, February 27, 2015

Rais Kikwete akutana na Watanzania waishio Zambia


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio Zambia (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Edgar Chagwa Lungu.
Sehemu ya Jumuiya ya Watanzania waishio Zambia wakimsikiliza Rais Kikwete (hayupo pichani) alipozungumza nao.

Mkuu wa Itifaki, Balozi Mohammed Juma Maharage (wa pili kushoto) akiwa na Balozi Samwel Shelukindo (wa pili kulia), Mshauri wa Rais Masuala ya Diplomasia pamoja na Bi. Zuhura Bundala (kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bi. Talha Mohammed (kusoto) Afisa Mambo ya Nje wakimsikiliza Mhe. Rais Kikwete (hayupo pichani alipozungumza na Diaspora ya Zambia
Sehemu nyingine ya Watanzania hao wakishangilia hotuba ya Mhe Rais
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akijibu moja ya maswali wakatiwa Mkutano wa Rais Kikwete na Watanzania waishio Zambia. Wengine ni Mama Salma Kikwete, Waziri wa Fedha, Mhe. Saaada Mkuya Salu na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Kandoro 


Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma naye akizungumza wakati wa mkutano huo
Rais Kikwete akiagana na Watanzania hao mara baada ya kuzungumza nao
Mama Salma Kikwete akipata picha na baadhi ya Watanzania waishio Zambia
==================================



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amewahimiza Watanzania wanaoishi nje ya nchi kujenga nyumbani, kuwa waadilifu na kuishi kwa  kufuata sheria za nchi walizopo.

Rais Kikwete alitoa rai hiyo wakati wa mkutano wake na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Zambia wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya nchini humo  hivi karibuni.

Mhe. Rais Kikwete ambaye alizungumzia masuala mbalimbali yanayoendelea nchini ikiwemo hali ya siasa, uchumi, elimu na miundombinu kwa Jumuiya hiyo alisema kuwa, imefika wakati sasa kwa Watanzania wanaoishi nje kuzisaidia jamii zao zilizobaki nchini hususan katika suala la elimu ili kuziinua.

 “Nawahimiza ndugu zangu jengeni nyumbani, heshima ya mwanadamu ni kupata mahali pa kukaa pia inapowezekana saidieni ndugu zenu hususan katika elimu ili nao waimarike”, alisisitiza Rais Kikwete.

Pia Mhe. Rais aliwaasa kuheshimu sheria za nchi walizopo kwa kuzingatia maadili na kusisitiza kuwa sheria haibadiliki iwe ni ndani ya nchi au nje hivyo ni wajibu wao  kuzifuata sheria zilizowekwa ili waishi kwa amani na kufanya shughuli zao.

Akizungumzia masuala ya uchumi nchini alisema kuwa hali ni nzuri  ambapo mfumuko wa bei unaendelea kupungua na pia hali ya chakula ni nzuri na kwamba Serikali inajaribu kutafuta masoko kwa chakula cha ziada.

“Hadi sasa kuna tani laki 6 za mchele na mahindi tani milioni 2.6 ambazo ni ziada. Hivyo kazi kubwa sasa ni kuangalia masoko na pia namna ya kuhifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye” alisema Rais Kikwete.

Kuhusu elimu, Mhe. Rais Kikwete alisema kuwa Serikali imefanikiwa kuwawezesha watoto wote wanaofaulu kwenda Sekondari pia wale wanaotakiwa kujiunga na darasa la kwanza wanajiunga. 

Alisema Serikali imejenga Sekondari za kutosha ambapo alitoa mfano wa Wilaya ya Kinondoni ya Jijini Dar es Salaam kuwa mwaka 2006 ilikuwa na Sekondari za Serikali 5 pekee lakini hadi kufikia mwaka 2014 kuna jumla ya Sekondari 49. Aidha, wanafunzi waliofaulu na kujiunga na Sekondari hizo Wilayani humo ni Milioni 1.9 kutoka laki 525 mwaka 2005.

“Tumepiga hatua kubwa sana katika suala la elimu, tumejenga Sekondari za kutosha na maabara na sasa tunajitahidi kutafuta vitabu na walimu wa masomo ya sayansi ili kukidhi haja ya masomo hayo nchini”, alifafanua Rais Kikwete.

Mhe. Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuipongeza Jumuiya hiyo yenye zaidi ya Watanzania mia tatu kwa kuanzisha chama na kuwataka wakitumie kama jukwaa la kuwaunganisha na kuwasiliana.  

Awali akijibu swali kuhusu  uraia pacha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe alisema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje imeendelea na jitihada za kutambua Watanzania wote walioko nje ya nchi (Diaspora) lakini pia suala hilo lilipelekwa na kujadiliwa na Tume ya Katiba.

“Kama Wizara tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha Watanzania wote walioko nje ya nchi wanatambulika lakini pia tumehakikisha Katiba inayopendekezwa ina kipengele kinachohusu diaspora. Kipengele hicho kinanaeleza kuwa Mtanzania aliyeko nje ya nchi (diaspora) anaweza kupata haki kadhaa sawa na raia kwa kupewa hadhi maalum”, alifafanua Waziri Membe.

Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini humo kwa mwaliko wa Rais wan chi hiyo Mhe. Edgar Chagwa Lungu alifuatana na Mama Salma Kikwete, Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Mamlaka mbalimbali.

_Mwisho_


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.