Wednesday, November 2, 2016

Balozi Msechu azindua zoezi la kuchangia wahanga wa tetemeko la ardhi

Balozi wa Tanzania katika Nchi za Nordic na Baltic mwenye makazi yake Sweden,  Mhe. Dora Msechu wa pili kutoka kulia akikata utepe kuashiria uzinduzi wa zoezi la kuchangia wahanga wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera lilifanyika Stockholm, Sweden. Hafla hiyo iliandaliwa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Sweden kwa lengo la kuhamasisha Watanzania waishio Sweden kuchangia Wahanga wa Maafa ya tetemeko la ardhi Mkoani Kagera. Zoezi hili maalum la kuchangia maafa linaendelea mpaka tarehe 4 Novemba, 2016 na michango itakayopatikana itakabidhiwa kwa Mhe. Balozi Dora Msechu

Mhe. Balozi Dora Msechu akizungumza wakati wa hafla hiyo. Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania katika Mji wa Malmo ambaye aliwasilisha salaam za watanzania waishio Malmo

Sehemu ya wadau walioshiriki hafla hiyo

Mwanadiaspora Mbarouk Rashidi akikabidhi vifaa kwa Mhe.Balozi Dora Msechu

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro FC, Bw. Humphrey Kalanje akizungumza katika hafla hiyo

Tuesday, November 1, 2016

Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa akutana na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kutoka Liberia

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Celestine Mushy akizungumza na Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uratibu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Liberia, Bw. Theophilus Addey. Katika mazungumzo yao yalijikita katika kuelezea namna Serikali ya Tanzania inavyofanya kazi na Umoja wa Mataifa kupitia Mfumo wa One United Nations (One UN). Balozi Mushy alimweleza Bw. Addey kuwa Tanzania imekuwa nchi ya mfano wa kuigwa kutokana na mafanikio  makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mfumo huo tangu kuanzishwa kwake hapa nchini mwaka 2007. Bw. Addey ameambatana na ujumbe wa pamoja kutoa Serikali ya Liberia na Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Bw. Addey wafuatilia mazungumzo.
Sehemu ya Maafisa wa Mambo ya Nje nao wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mushy na Bw. Addey (hawapo pichani)
Sehemu nyingine ya Maafisa Mambo ya Nje.
Balozi Celestine Mushy akimwelezea Bw. Theophilus Addey kitabu kinachoelezea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini
Balozi Mushy akiwa katia picha ya pamoja na ujumbe wa pamoja kati ya Serikali ya Liberia na Ofisi ya Umoja wa Mataifa. 

NI MUHIMU ICC NA AFRIKA KUZUNGUMZA –TANZANIA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopokea na kujadili Ripoti ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) hapo jumatatu. Katika kuchangia Ripoti hiyo, Tanzania imesisitiza haja na umuhimu kwa ICC kukaa na kuzungumza na Nchi za Afrika ili kutafuta suluhu ya misuguano baina ya pande hizo mbili.

 ****************************************************************

Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muugano wa Tanzania imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) kukaa meza moja na nchi wanachama wa Mkataba wa Roma hususani zile za Afrika ili kutafuta suluhu ya changamoto na tofauti zilizopo kati ya mahakama hiyo na wanachama wake.
 
Tanzania imetoa wito huo siku ya jumatatu kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili Taarifa ya Utendaji ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.

Taarifa ICC imewasilishwa na Rais wa mahakama hiyo Jaji Slivia Fernandez de Gumendi katika kupindi ambacho Jumuiya ya Kimataifa imekumbwa na taharuki baada ya wanachama wawili wa Mkataba wa Roma, Afrika ya Kusini na Burundi kuwasilisha rasmi katika Umoja wa Mataifa kusudio la kujiondoa huku Gambia nayo ikitangaza kutaka kujitoa ingawa bado haijawasilisha rasmi nia yake hiyo.

Mwakilishi huyo wa Tanzania katika mchango wake amesema, uwepo au kuanzishwa kwa ICC kulitokana kwa kiasi kikubwa na uungwaji mkono kutoka Afrika. Akasema uungwaji mkono huo ulitokana hasa baada ya nchi hizo za Afrika kukatishwa tamaa na kuvunjika moyo baada ya kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

“Baada ya kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo, Mahakama hii, ilikuja kuwa chombo cha kutenda haki dhidi ya watu waliojihusisha na vitendo vya kikatili vikiwamo vya ukatili dhidi ya binadamu, uhalifu kivita na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Madhira yasiyoelezeka yaliyotokea Barani Afrika yakaifanya mahakama hii kuwa chombo cha matumaini dhidi ya wale ambao hawakuweza kuguswa au walikuwa juu ya sheria”. Akasema Balozi Manongi.

Tuesday, October 25, 2016

Wamisri watangaziwa fursa za Uwekezaji za hapa nchini


Mhe. Mohammed Haji  Hamza, Balozi wa Tanzania nchini Misri akiwakaribisha wageni waliohudhuria katika ufunguzi wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na misri lililofanyika  katika miji ya Cairo na Alexandria kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2016.
Kongamano hili lililowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili lilifunguliwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Mhe Balozi Amina Salim Ali. Kongamano hilo lilihudhuriwa na washiriki kutoka sekta mbalimbali zinahusika na uwekezaji, biashara, ujenzi, usafirishaji, elimu, afya, viwanda, uhandisi ,kilimo na utalii. Kongano hilo liligharmiwa na kuratibiwa  kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Jumuiya za Wafanyabiashara wa Misri na makampuni binafsi ya biashara ya Misri.
Katika kongamano hilo washiriki wa Tanzania pamoja na kutoa mada zilizohusu fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na hasa katika sekta ya viwanda na utalii pia walipata fursa ya kushiriki katika mazungumzo  ya ana kwa ana ya kibiashara.
Siku ya pili ya kongamano hili washiriki kutoka Tanzania walipata nafasi ya kutembelea sehemu mbalimbali za uzalishaji na huduma zikiwemo: kijiji cha teknolojia cha Cairo, viwanda vya utengezaji madawa, vifaa tiba na rangi za ujenzi mjini Cairo pamoja na viwanda vya nguo, vifaa vya ujezi na samani za chuma katika miji wa Tenth Ramadhani .  Siku ya tatu ya kongamano hilo baadhi ya washiriki kutoka Tanzania walitembelea vyuo vikuu vya Alexandria na chuo kikuu cha kiarabu cha sayansi, teknolojia na usafiri wa bahari mjini Alexandria na kuwa na mazungumzo ya ushirikiano na viongozi wa vyuo vikuu hivyo. Ujumbe wa Tanzania pia ulipata nafasi ya kutembelea kiwanda cha kutengenezea manukato kilichopo nje kidogo ya jiji la Akexandria.

Akiwa jijini Cairo, Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo alipata nafasi ya kukutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Rais na Mtendaji Mkuu wa  Afri exim bank na Katibu Mkuu wa Wakala wa Ushirikiano na Maendeleo wa Misri.. 

Vingozi mbalimbali walioshiriki kwenye ufunguzi wa konganano la kibiashara mjini Cairo siku ya  tarehe 17 Oktoba 2016 wakisimama wakati wa Nyimbo za Taifa za Tanzania na Misri zilipopigwa. Wa kwanza kutokea kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda wa Misri. Wa pili ni Katibu Mkuu wa Wakala wa Ushirikiano na Maendeleo wa Misri, watatu ni Mhe Balozi Amina Salim Ali, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Mohamed Haji Hamza , watano ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar na wa sita ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Biashara ya Misri. Waliosimama mbele ya meza kuu ni Mabalozi kutoka nchi za  SADC waliopo mjini Cairo.

Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Zanzibar akifuatilia neno la ukaribisho kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Mohammed Haji Hamza
Balozi Hamza akisalimiana na kubadilishana mawazo na washiriki mbalimbali wa kongamano la biashara jijini Cairo mara baada ya ufunguzi kukamilika.

Monday, October 24, 2016

Waziri Mahiga ahimiza umuhimu wa somo la Umoja wa Mataifa

WAZIRI MAHIGA AHIMIZA UMUHIMU WA SOMO LA UMOJA WA MATAIFA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine mahiga amependekeza ni vema somo la Umoja wa Mataifa likaingizwa katika mitaala ya masomo, ameeleza hayo alipokuwa akihutubia  katika kilele cha Maadhimisho ya 71 ya Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo Waziri Mahiga alisema “Maadhimisho haya ni muhimu  kwa historia ya nchi yetu kwakua yanawezesha vizazi vyetu kuelewa historia ya nchi yetu na Shirika la Umoja wa Mataifa tangu kupatikana kwa Uhuru hivyo ni vyema Walimu na Wadau wote katika Sekta ya Elimu wakatilia mkazo umuhimu wa somo la Umoja wa Mataifa katika shule zetu za Msingi na Sekondari.”

Vilevile ameeleza umuhimu na mchango wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa Tanzania na  kwa nchi wanachama wengine wa Umoja huo ni pamoja na kutengeneza agenda ya kimataifa ya maendeleo; kuleta amani hususan baada ya vita ya kwanza na  ya pili ya Dunia; vilevile Shirika hilo limekuwa likiendelea kuhakikisha amani na Ulinzi inapatikana katika mataifa yenye migogoro ambapo Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekuwa zikishiriki katika masuala ya ulinzi wa amani katika baadhi ya mataifa kama Lebanon, Sudan Kusini (Dafur) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Pamoja na hayo ameeleza kuwa kupitia shirika la umoja wa Mataifa Tanzania imefanikiwa kuwa na  wawakilishi wa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa ambao pamoja na shughuli nyingine za mashirika hayo yamekuwa yakifadhili na kushiriki katika shughuli za maendeleo ambapo wastani wa bilioni za fedha za miradi ya maendeleo zimekuwa zikitolewa kwaajili ya miradi ya maendeleo. Vilevile Mahakama ya Umoja wa mataifa ya mauaji ya kimbari iliamuriwa kujengwa nchini Tanzania ambapo makao makuu yake yapo Jijini Arusha licha ya kumalizika kwa kesi majengo pamoja na nyaraka zote zilizokuwa zikitumika zimeendelea kubaki nchini kama kumbukumbu za marejeo.

Naye Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez alieleza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs), umuhimu wa kutunza amani na kuheshimu haki za binadamu sambamba na usawa wa jinsia.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa yanayowakilisha nchi zao hapa nchini. Wengine ni wadau wa maendeleo kutoka Sekta binafsi na taasisi za Serikali. 


Mfalme wa Morocco aendelea na ziara nchini

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 



Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
             11466 DAR  ES SALAAM, 
                                    Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MFALME WA MOROCCO AENDELEA NA ZIARA NCHINI

Mfalme wa Morocco, Mtukufu Mohammed VI aliyewasili jana kwa ziara ya kitaifa, ameendelea na ziara yake nchini ambapo leo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika kuboresha mahusiano ya Tanzania na Morocco katika maeneo mbalimbali ya Kidiplomasia, Siasa, Uchumi, Ulinzi na Ustawi wa Jamii.

Akielezea mahusiano ya Tanzania na Morocco, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alisema kuwa ziara hii ni matokeo ya  Mhe. Rais kuridhia ujio huo wa Mfalme wa Morocco na ujio wake umekuwa ni maalum sana kwa kuwa unakumbushia historia iliyowekwa na mgeni wa kwanza kutoka Morocco, Bw. Iban Batutu aliyetembelea Tanzania eneo la Kilwa Mwaka 1631.

Baada ya mazungumzo,  Mhe. Rais Magufuli na Mgeni wake, Mtukufu Mfalme wa Morocco walishuhudia uwekaji saini wa Mikataba 22 ambayo inalenga kuendeleza sekta mbalimbali kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco.

Baadhi ya Mikataba hiyo ni Makubaliano baina ya Benki ya Kilimo ya Tanzania na Benki ya Kilimo ya Morocco  ili kuwawezesha wakulima wetu kusindika mazao yao na kuyasafarisha nje yakiwa yamekamilika, Makubaliano baina ya Kampuni ya Mbolea ya Morocco na ya Tanzania ambapo kwa pamoja zitabadilishana uzoefu na utaalamu kwa lengo la kuiwezesha kampuni ya Tanzania kuzalisha mbolea ya kutosha kulingana na mahitaji, Makubaliano katika Sekta ya Anga ambapo katika siku za usoni Shirika la Ndege la Morocco litaanzisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Rabat hadi Dar es Salaam.

 Makubaliano mengine ni pamoja na kusaidia wakulima wadogo wadogo, kuendeleza Sekta ya Utalii ya Tanzania hususan katika fukwe za Zanzibar na hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro, makubaliano  baina ya Shirika la reli la Tanzania na lile la Morocco ambapo watashirikiana  kuboresha usafiri  wa reli kwa madhumuni ya kupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kuendeleza reli ya Mtwara-Mchuchuma/Liganga.

Viongozi hao pia walishuhudia uwekaji saini ya Mkataba baina ya Kampuni ya chai ya Tanzania na ile ya Morocco kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kutengeneza chai yenye ubora wa hali ya juu ili iweze kupata soko nchini Morocco na nchi nyingine.

Aidha, akiongea katika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Bw. Salahddine Mezouar amesema wakati sasa umefika nchi hizi kupeleka mbele mahusiano yao na hii ndio sababu kubwa iliyopelekea nchi hizi mbili kukubaliana kusaini jumla ya mikataba 22, amesema nchi ya Morocco imefurahishwa na utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuri.

Mtukufu Mfalme atahitimisha ratiba yake kwa siku ya leo kwa kushiriki dhifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli  Ikulu, Dar es Salaam.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 24 Septemba 2016

Rais Magufuli ampokea Mfalme Mohammed VI wa Morocco Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Mfalme Mohammed VI wa Morocco wakipungia mikono wananchi waliojitokeza kwenye mapokezi ya Mfalme huyo Ikulu Jijini Dar es Salaam
Mfalme Mohammed VI wa Morocco akisalimia wananchi waliojitokeza kumpokea Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mfalme Mohammed VI wa Morocco mara baada ya Mfalme huyo kuwasilia Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mfalme Mohammed VI wa Morocco wakiwa katika Mazungumzo, Ikulu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza katika hafla ya kutoa taarifa ya mazungumzo maalum, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika hafla ya kutoa taarifa ya mazungumzo maalum, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Tanzania yaungana na Nchi zingine Duniani kuadhimisha kilele cha Siku ya Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na watendaji wa mashirika mbalimbali ya Kimataifa yaliyopo Nchini kwenye maadhimisho ya kilele cha Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika katika viwanja vya Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa amesimama sehemu maalumu wakati wimbo wa taifa ukipigwa
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akikagua gwaride maalum katika maadhimisho  ya kilele ya Siku ya Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria maadhimisho ya Kilele ya Umoja wa Mataifa
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akihutubia kwenye maadhimisho ya kilele ya Siku ya Umoja wa Mataifa 
Baadhi ya wanafunzi wenyemahitaji maalum wakiwa wameshikilia mabango ya malengo 17 ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa

Sunday, October 23, 2016

Rais Magufuli ampokea Mfalme Mohamed VI wa Morocco

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Mfalme H.M Mohammed VI wa Morocco wakati wimbo wa Taifa ukipigwa mara baada ya Mfalme huyo kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mfalme Mohamme VI wa Morocco
Mfalme Mohamed VI akipungia wananchi waliojitokeza kumpokea uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Friday, October 21, 2016

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza awasilisha Hati za Utambulisho kwa Malkia Elizabeth II

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro akisalimiana na Malkia Elizabeth II wa Uingereza mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya nchi hiyo ya Buckingham kwa ajili ya kuwasilisha Hati za Utambulisho. Kulia ni mwenza wa Dkt. Migiro, Prof. Cleophas Migiro.
Mhe. Balozi Dkt. Migiro akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Malkia Elizabeth II wa Uingereza huku mwenza wake Prof. Migiro akishuhudia
Malkia Elizabeth II akisalimiana na Prof. Cleophas Migiro
Malkia Elizabeth II akizungumza na Mhe. Balozi Migiro 

Waziri Mahiga akutana na Balozi wa Iran Nchini aliyemaliza muda wake

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Iran Nchini aliyemaliza  Muda wake Mhe.Mehdi Aghajafari. Balozi Mhe. Mehdi Aghajafari wiki ijayo anatarajia kuondoka Nchini kurejea Iran. 
Kutoka Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Abdalah Kilima, maafisa kutoka Wizarani Bi. Zainab Angovi, Bw. Gerald Mbwafu na Kisa Doris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Balozi wa Iran Nchini aliyemaliza muda wake Mhe.Mehdi Aghajafari wakionesha zawadi ya picha iliyokabidhiwa Mhe. Balozi


Wakati huo huo Waziri Mahiga amekutana na kuongea na Balozi wa Kuwait Nchini Mhe. Jasem Al-Najem  

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Agustine Mahiga akimsikiliza Balozi wa Kuwait Nchini Mhe. Jasem Al-Najem wakati wakifanya mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam


Waziri Mhe. Mahiga akielezea jambo wakati akifanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait Nchini Mhe. Jasem Al-Najem. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya kati Balozi Abdallah Kilima akifuatilia mazungumzo.

Tanzania na Uswisi zasaini Mkataba wa Makubaliano kuhusu ushirikiano wa kisheria kwenye masuala ya Jinai

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) kwa pamoja na Mhe. Florence Tinguely Mattli, Balozi wa Uswisi hapa nchini wakisaini Mkataba wa Makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uswisi kuhusu Ushirikiano wa Kisheria kwenye masuala ya Jinai. Mkataba huu utasaidia kuzijengea uwezo mamlaka zinazohusika na masuala ya Jinai na pia kubadilishana taarifa kuhusu masuala hayo.
Mhe. Mahiga na Mhe. Mattli wakiendelea na zoezi la kusaini huku Maafisa kutoka Wizarani na Ubalozini wakishuhudia. Kulia aliyesimama ni Bw. John Pangipita, Afisa Mambo ya Nje na Bi. Sheila Ally.
Tukio hilo pia lilishuhudiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Baraka Luvanda (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, Balozi Joseph Sokoine (wa pili kutoka kushoto), Katibu wa Waziri, Bw. Gerald Mbwafu na Bw. Pangipita (wa pili kutoka kulia)
Dkt. Mahiga pamoja na Balozi Mattli wakibadilishana Mkataba mara baada ya kumaliza kuweka saini.

Thursday, October 20, 2016

Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco kufanya ziara ya siku tatu nchini

Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongea na Wahandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ziara rasmi ya siku tatu ya Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco nchini. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara Jijini Dar es Salaam.  Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco anatarajiwa kuanza ziara hiyo tarehe 23 hadi 25 Oktoba, 2016.
Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga