Monday, November 20, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Shelisheli awasilisha Hati za Utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini Shelisheli mwenye makazi yake nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Mhe. Danny Faure. Makabidhiano hayo yalifanyika tarehe 14 Novemba 2017, katika Ikulu ya nchi hiyo.
Mhe. Balozi Chana  akizungumza na Mhe. Rais Faure ambapo Serikali ya Jamhuri ya Shelisheli imemuhakikishia kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mhe. Balozi Chana akiwasili katika Ikulu ya Jamhuri ya Shelisheli.

Sunday, November 19, 2017

UFAFANUZI KUHUSU UINGIZWAJI WA MIFUGO NCHINI TANZANIA


TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU UINGIZWAJI WA MIFUGO NCHINI TANZANIA

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari na kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuishutumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia hatua ya kukamata na kupiga mnada mifugo iliyoingizwa nchini bila kufuata sheria. Aidha, taarifa hizo zinajenga sintofahamu kuhusiana na suala la vifaranga vya kuku vilivyoteketezwa kufuatia kuingizwa nchini bila kufuata sheria. Baadhi ya taarifa hizo zimeenda mbali zaidi na kudai kuwa hatua hizi zinaweza kudhoofisha mahusiano yetu na nchi jirani. 

Kadhalika, kufuatia suala hilo la kupigwa mnada kwa ng’ombe walioingia nchini kinyume cha sheria, na wenye ng’ombe hao kukaidi kuondoa mifugo yao hata baada ya kupewa muda kufanya hivyo, na kufuatia kuteketezwa kwa vifaranga vilivyoingia nchini kinyume cha sheria na kanuni, Serikali ya Kenya ilimwita Balozi wetu aliyeko Nairobi kutaka maelezo. Balozi wetu alisikiliza maelezo ya Serikali ya Kenya na akatumia fursa hiyo kuelezea masuala haya kwa Serikali ya Kenya. Vile vile Serikali imepokea barua kutoka Serikali ya Kenya kuhusu masuala haya, na Serikali itaijibu barua hiyo kutoa ufafanuzi.

Serikali inapenda kuufahamisha umma kwa ujumla kuwa uingizwaji wa mifugo na bidhaa zake nchini Tanzania huongozwa na sheria za nchi, makubaliano ya kikanda na kimataifa.


Sheria na taratibu hizi ni pamoja na:
(i)    Sheria ya Magonjwa ya Wanyama (Animal Disease Act) Na. 17 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2007 na 2010, ambazo zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji wa mifugo na mazao yake katika maeneo ya mpakani, bandarini na viwanja vya ndege;
(ii)   Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama (Grazing-land and Animal Feed Resources Act) Na. 13 ya mwaka 2010 ambayo inasimamia nyanda za malisho na ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo;
(iii)   Zuio (quarantine)  la uingizaji ndege na mazao yake nchini la mwaka 2006, kutokana na uwepo wa ugonjwa hatari wa Homa ya Mafua Makali ya Ndege katika nchi mbalimbali duniani. Ugonjwa huo umejitokeza kwenye nchi jirani ya Uganda mwanzoni mwa mwaka 2017 na hivyo kuiweka nchi yetu katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu iwapo zuio hili litakiukwa. Zuio hilo halijaondolewa hadi leo.
(iv)  Ukweli kwamba katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mifugo na bidhaa za mifugo zinavuka mipaka kwa utaratibu maalum kupitia kwenye vituo vya mipakani ambapo maofisa mifugo kutoka pande zote za mipaka hufanya shughuli ya udhibiti.
Utekelezaji wa sheria na makubaliano haya hufanyika bila ubaguzi wa uraia wa mwingizaji wa mifugo au nchi inakotoka mifugo hiyo. Nchi zote duniani, zikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zinadhibiti uingizwaji wa mifugo na mimea katika nchi zao. Udhibiti huu hufanyika katika viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mipakani. Kwa mfano, katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani cha Namanga, wapo maofisa wa mifugo na kilimo kutoka Kenya na Tanzania wanaodhibiti uingizwaji wa mifugo na mimea kwenye nchi zao.

Katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hii, ilibainika kuwa idadi kubwa ya mifugo kutoka nchi za jirani imeingizwa nchini pasipo kufuata sheria na taratibu zilizopo. Serikali iliagiza mifugo hiyo irudishwe kwenye nchi ilikotoka kwani ilikuwa inahatarisha mazingira na kuongeza uwezekano wa kusambaa magonjwa ya mifugo. Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa wamiliki wa mifugo hiyo kuiondoa nchini. Tahadhari ilitolewa kwamba muda uliotengwa ukifikia ukomo, mifugo hiyo itakamatwa na kushugulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Pamoja na agizo hilo, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilituma Waraka wa Kidiplomasia  kwa Serikali za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, ikizihimiza kuwataka raia wao walioingiza mifugo nchini isivyo halali waiondoe. Wamiliki wengi walitii agizo hilo la Serikali ya Tanzania na kuondoa mifugo yao nchini.

Hata hivyo, wapo wamiliki wachache kutoka nchi za jirani waliokaidi agizo hilo na hivyo ng’ombe wapatao 1113 walikamatwa katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro na kupigwa mnada baada ya wamiliki wake kushindwa kujitokeza. Katika mkoa huo wa Kilimanjaro wapo ng’ombe 74 ambao wamiliki wake walijitokeza, wakalipa faini kwa amri ya mahakama na kuondoka na ng’ombe wao. Katika Mkoa wa Kigoma ng’ombe 324 ambao wamiliki wake hawajajitokeza wamekamatwa na hatua stahiki zinachukuliwa. Aidha, katika mkoa huo wa Kigoma ng’ombe 728 walikamatwa na wamiliki wao walijitokeza na kulipa faini kutokana na maamuzi ya Mahakama. Katika mkoa wa Kagera jumla ng’ombe 1,536 ambao wamiliki wake bado hawajulikani wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama na sheria itachukua mkondo wake.

Kwa takwimu hizi ni wazi kwamba zoezi hili halijalenga nchi yeyote, kwa sababu sio nchi moja tu imeathirika. Zoezi hili limelenga kutekeleza sheria na kanuni za nchi yetu ili kulinda mazingira na kupunguza uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa ya mifugo. Hili suala halipaswi kusababisha mgogoro wa kidiplomasia na nchi yeyote, labda tu mtu aamue kwa makusudi yasiyo mema kupotosha na kuchochea mgogoro.

Aidha, tarehe 24 Oktoba, 2017 jumla ya vifaranga vya kuku wa mayai 6,400 vilikamatwa katika Mkoa wa Arusha kwa kuingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni. Vifaranga hivyo vilikuwa kwenye maboksi 60 vikiwa kwenye gari lenye namba za usajili T 285 BAY. Mmiliki wa vifaranga hivi alidai kwamba ameviingiza nchini kutokea Kenya. Vifaranga hivi viliteketezwa kutokana na msafirishaji wa vifaranga hivi kutokuwa na kibali cha aina yoyote kutoka mamlaka husika ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo hapa nchini ambayo ni Idara ya Huduma za Afya Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Pia, mmiliki huyu alishindwa hata kuonesha kibali cha Serikali ya Kenya kumruhusu kusafirisha vifaranga hivyo kutoka Kenya kuvileta Tanzania pamoja na kwamba mmiliki huyu alidai kwamba vifaranga hivyo amevitoa Kenya. Ni muhimu ikafahamika kwamba nchi zote duniani, ikiwemo Kenya, hufuata miongozo ya WTO na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kwa kutoa vibali (export permit) kwa mtu yeyote anayetaka kusafirisha mifugo nje ya nchi. Kosa jingine kubwa ni kwamba vifaranga hivi havikupitishiwa kwenye vituo rasmi vya Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake mipakani (zoosanitary border posts) kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.

Pamoja na yote haya, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania alimpigia simu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (Director of Veterinary Services) wa Kenya kutaka kujua kama Mamlaka za Kenya zina habari kuhusu vifaranga waliokamatwa na kama Kenya itakubali kuruhusu vifaranga hivyo virudishwe Kenya. Mkurugenzi huyu wa Kenya alisema hana taarifa kuhusu vifaranga hivyo na kwamba Kenya haiko tayari kuruhusu vifaranga hivyo kurudishwa nchini mwao kwa sababu havina nyaraka kulingana na miongozo ya kimataifa.

Ni vizuri umma ukajua kwamba hii si mara ya kwanza kwa Serikali kuteketeza vifaranga vilivyoingizwa nchini bila kufuata sheria kanuni na taratibu. Vipo vifaranga vingi tu vimeteketezwa kwa namna hiyo hiyo baada ya kukamatwa kwenye viwanja vyetu vya ndege na sehemu nyingine. Kadhalika vifaranga ambavyo vimekuwa vikiteketezwa havitokei nchi moja tu. Vifaranga vyote vinavyoingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni zinazotulinda dhidi ya uwezekano wa magonjwa vinateketezwa mara moja bila kujali vinatoka nchi gani. Hatua hizi tumekuwa tukizitekeleza tangu tuweke zuio mwaka 2006, na hazijaathiri kwa namna yeyote ile mahusiano yetu na nchi yeyote. Hatua yeyote ya kujaribu kufanya jambo hili kuwa ni la mgogoro wa kidiplomasia dhidi ya nchi yeyote ile ni hatua isiyo sahihi.

Serikali inawaasa wananchi na raia wa kigeni wazingatie sheria, kanuni na taratibu pale wanapotaka kuingiza nchini  au kusafirisha nje ya nchi mifugo na mazao yake. Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu za nchi, kikanda na kimataifa zinazohusu utoaji na uingizaji wa mifugo na mazao yake nchini. Tunapenda kuuhakikishia umma kwamba, usimamizi wa sheria hizi hauwezi na hautakiwi kwa namna yoyote ile kuathiri mahusiano yetu na nchi nyingine kwa sababu nchi zote duniani zinasimamia sheria kama hizi.
Mojawapo ya misingi ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kujenga na kuimarisha mahusiano na nchi nyingine pamoja na kudumisha ujirani mwema. Hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa inalinda mahusiano mazuri yaliyojengwa kwa muda mrefu kati yake na nchi nyingine duniani. Kadhalika, Serikali itaendelea kutumia fursa mbali mbali, kama vile vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikao vya pande mbili kati yetu na jirani zetu, na pia vikao vya ujirani mwema mipakani, kutatua changamoto zozote za kimahusiano zitakazo jitokeza kwa nia ya kuendelea kuimarisha ujirani mwema.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

19 Novemba, 2017

Tuesday, November 14, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Korea awasilisha hati za utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Matilda Masuka (kushoto) akitoa salam ya heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Moon Jae-in wakati wa hafla ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Taifa hilo.

Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Matilda Masuka (kushoto) akiwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Moon Jae-in

Balozi Mhe.Masuka na Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe.Moon Jae-in wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya zoezi la kuwasilisha hati za utambulisho

Monday, November 13, 2017

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje afanya mazungumzo na Balozi China nchini


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa China nchini Mhe. WANG Ke wakifuarahia jambo walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Mjini Dodoma.Naibu Waziri amemuhakikishia Mhe.Balozi WANG Ke kuwa Wizara na Serikali wataendelea kudumisha uhusiano wa kahistoria uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China. Pia Mhe. Dkt. Kolimba alitumia fursa hiyo  kuishukuru Serikali ya China kwa kufadhili miradi mbalimbali hapa nchini
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa China nchini Mhe. WANG Ke wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa nchi wa Falme za Kiarabu nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Umoja wa nchi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mhe. Balozi Abdulla Ibrahim Alsuwaidi walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalikita katika kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kudumisha na kukuza uhusiano baina ya pande mbili. (Tanzania na Umoja wa Nchi wa Falme za Kiarabu)  
Waziri Mhe.Balozi Dkt.Mahiga na Mhe. Balozi Alsuwaidi wakifurahia jambo wakati walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazunguzo
Waziri Mhe. Mahiga akimsikiliza Balozi wa Nchi wa Falme za Kiarabu nchini Mhe.Abdulla Ibrahim Alsuwaidi walipokutana kwa Mazungumzo Jijini Dar es Salaam

2018 SADC SECONDARY SCHOOL ESSAY COMPETITION





N:B All applicants are requested to send their applications to the following address:
    
         Permanent Secretary
         Ministry of Education,  Science and Technology
         Block 10,
         College of Business Studies and Law,
         University of Dodoma,
         P.O.Box 10
         DODOMA



















Friday, November 10, 2017

Kaimu Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa akutana na Ujumbe wa EU nchini

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Jestas Nyamanga akizungumza na Kaimu Kiongozi  wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Bw. Charlie Stuart alipofika Wizarani tarehe 10 Novemba, 2017 kwa ajaili ya kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu Umoja huo na masuala mengine ya Kimataifa.
Sehemu ya Ujumbe uliofuatana na Bw. Stuart wakifuatilia mazungumzo
Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka EU na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki


Thursday, November 9, 2017

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Pro.Adolf Mkenda akiwa katika mzungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) inchini Bibi Abla Beuhammouche,Wizarani Jijini Dar es Salaam. Pamoja na masuala mengine mazungumzo hayo yalijikita katika kujadili njia bora zaidi za kutekeleza miradi ya kilimo na uhifadhi wa mazingira. IFAD inatekeleza miradi ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa wananchi na uhifadhi wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda akimsiliza Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini Tanzania  Bibi Abla Beuhammouche walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda na Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini Tanzania  Bibi Abla Beuhammouche wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Mhe. Balozi wa China Nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akiwa katika mkutano na Balozi wa China Nchini Mhe. Wang Ke alipomtembelea Wizarani, tarehe 09 Novemba,2017.
 Katibu Mkuu Prof. Mkenda ( katikati), kushoto kwake ni Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke, wakiendelea na mazungumzo, wanaofutilia mazungumzo hayo ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia(wa kwanza kulia) Bi. Justa Nyange na anayefuata ni Afisa katika Idara hiyo Bw. Harmesh Lunyumbu.

Katibu Mkuu Prof. Mkenda akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa China Nchini Mhe. Wang Ke, baada ya mkutano

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Finland nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Adolf Mkenda akimkaribisha Wizarani Balozi wa Finland nchini, Mhe. Pekka Hukka alipofika kwa ajili ya kujitambulisha kwake kama Katibu Mkuu mpya na kuzungumzia jinsi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Finland. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 09 Novemba,  2017.
Prof. Mkenda akimweleza jambo Balozi Hukka wakati wa mazungumzo yao. Pamoja na mambo mengine wlizungumzia kuimarisha ushirikiano katika masuala ya elimu, biashara na uwekezaji ambapo Prof. Mkenda alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi Hukka kwa msaada unaotolewa na Serikali yake kwa Taasisi ya Uongozi.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvatory Mbilinyi kwa pamoja na Bi. Tunsume Mwangolombe wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Hukka (hawapo pichani)
Mazungumzo yakiendelea

Wednesday, November 8, 2017

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Mjumbe Maalum kutoka Norway

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Mjumbe Maalum kutoka Serikali ya Norway kwa Serikali ya Tanzania, Balozi Arild Oyen ambaye alifika Wizarani kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum. Pamoja na mambo mengine walizungumzia namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Norway hususan katika sekta za Nishati, Elimu na Utamaduni. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 08 Novemba, 2017.
Ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Oyen (hawapo pichani). Kutoka kushoto ni Bw. Jestas Nyamanga, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Salvatory Mbilinyi, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika na Bi. Ramla Hamis, Afisa Mambo ya  Nje.
Mazungumzo yakiendelea. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanne Marie Kaarstad.
Prof. Mkenda na Balozi Oyen wakimsikiliza Balozi Kaarstad mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao
Prof. Mkenda akiagana na Balozi Oyen

Katibu Mkuu Prof. Mkenda afanya Mazungumzo na Balozi wa Japan Nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akiwa katika mkutano na Balozi wa Japan nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida alipomtembelea Wizarani leo tarehe 08 Novemba,2017. Katika Mkutano huu walizungumzia masuala mbalimbali yanoyohusu uhusiano kati ya Tanzania na Japan hasa katika eneo la uwekezaji.

 Prof.Mkenda akipokea zawadi ya Kalenda ya Mwaka 2018 kutoka kwa Mheshimiwa Balozi Yoshida, kalenda hiyo ni maalum yenye picha  zinazoelezea utamaduni wa Japan.

Katibu Mkuu Prof. Mkenda na Mhe. Balozi Yoshida pamoja na maafisa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Japan wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya Mkutano.

Waziri Mahiga amkaribisha rasmi Wizarani Katibu Mkuu mpya Prof.Mkenda

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) wakati wa kikao rasmi cha kumkaribisha Katibu Mkuu mpya wa Wizara Prof. Adolf Mkenda (kulia). Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu, Bw. Hamid Mbegu.
Sehemu ya Wakurugenzi na Watumishi wa Wizara wakimsikiliza Waziri Mahiga (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya Wakuu wa Idara na Vitengo wakifuatilia kikao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiwasalimia Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) mara baada ya kukaribishwa rasmi Wizarani.
Watumishi wa Wizara wakimsikiliza Katibu Mkuu (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Wizara

Watumishi wengine wa Wizara

Tuesday, November 7, 2017

Waziri Mahiga akutana na Kamishna wa Umoja wa Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongea na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Neven Mimica alipomtembelea katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 6 Novemba, 2017. Bw. Mimica alikuwepo nchini kwa ziara ya siku sita (6) ambapo aliwasili nchini tarehe 1 Novemba 2017 na kukamilisha ziara hiyo kwa kukutana na Waziri Mahiga.
Mkuu wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Roeland van de Geer pamoja na afisa wa Ubalozi huo wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.
Afisa Mambo ya Nje, Bw. Salvatory Mbilinyi na Afisa aliyeambatana na kamishna wakifuatilia mazungumzo.

Picha ya pamoja.
Mazungumzo yakiendelea.

Friday, November 3, 2017

Msichana wa Kitanzania kuiwakilisha nchi Mkutano wa Dunia wa Vijana

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Deusdedit Kaganda akimkabidhi Bendera ya Taifa, Bi Hilda Jacob Mwakatumbula ambaye amechaguliwa na Kamati ya Kimataifa ya Vijana kuiwakilisha Tanzania kwenye Mkutano wa Dunia wa Vijana utakaofanyika Belize, Amerika ya Kati kuanzia tarehe 6 hadi 9 Novemba, 2017. Bi. Mwakatumbula ambaye anachukua Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Waseda nchini Japan amepata ufadhili wa kushiriki Mkutano huo kutoka Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez (kushoto). Akimkabidhi Bendera hiyo, Bw. Kaganda alimwomba Bi. Mwakatumbula kuwa Balozi mzuri wa Vijana wa Kitanzania kwenye mkutano huo hususan katika kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo.
Picha ya pamoja