Wednesday, March 9, 2016

Tanzania isiogope kujifunza kutoka katika nchi zilizoendelea, Dkt. Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema kuwa nchi yake ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam, nchi ambayo kwa kipindi kifupi imeweza kujikwamua kutoka katika dimbwi la umasikini na kuwa nchi ya uchumi wa kati. Rais Magufuli alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam leo akiwa na Mgeni wake, Mhe. Troung Tan Sang, Rais wa Vietnam mbele ya waandishi wa habari. 

“Vietnam ilipata uhuru mwaka 1945 na baadaye ikakumbwa na vita vya muda mrefu ambapo utulivu kamili katika nchi hiyo ulipatikana kuanzia mwaka 1976. Kuanzia kipindi hicho, Vietnam imeweza kupiga hatua kutoka nchi masikini yenye kipato cha Dola za Marekani 100 kwa mtu mmoja na kufikia nchi yenye uchumi wa kati wa pato la Dola 2000 kwa mtu mmoja kwa mwaka”. Rais Magufuli alisema.

Mhe. Dkt. Magufuli alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Vietnam ni mzuri na unazidi kuimarishwa na ziara za viongozi wa ngazi ya juu baina ya nchi hizi mbili. Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alifanya ziara nchini Vietnam mwaka 2004 na baadaye Rais wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Kikwete mwaka 2014.  Aidha, Rais Magufuli amealikwa kufanya ziara nchini Vietnam mwaka 2017.

Rais Magufuli aliendelea kueleza kuwa Vietnam ni maarufu kwa kuuza korosho duniani wakati mbegu za zao hilo ilizichukua Tanzania. Vietnam pia inavuna mpunga misimu mitatu kwa mwaka wakati Tanzania inavuna kwa msimu mmoja tu. Mbali na hayo, Vietnam ni maarufu kwa uuzaji wa samaki duniani lakini Tanzania yenye maziwa 21, bahari na mito haina hata kiwanda cha kusindika samaki. “Hivi ni vitu ambayo Tanzania inatakiwa kujifunza kutoka Vietnam” Rais Magufuli alisisitiza.

Alieleza kuwa katika mazungumzo na Mgeni wake walisisitiza umuhimu wa kukuza biashara kati ya Tanzania na Vietnam kutoka kiwango cha sasa cha Dola za Marekani milioni 300 na kufikia Dola bilioni moja kwa mwaka.

Kwa upande wake, Rais wa Vietnam alielezea furaha yake ya kuwa Rais wa kwanza wa Vietnam kufanya ziara katika nchi nzuri ya Tanzania. Alisema licha ya umbali uliopo kati ya Tanzania na Vietnam lakini Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kabisa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vietnam. Rais Tang aliipongeza Tanzania kwa ukuaji imara wa uchumi na kwamba wamekubaliana na mwenyeji wake kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ili kuimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo, uvuvi, biashara, mawasiliano kwa faida ya wananchi wa pande zote.

Kwa upande wa masuala ya kimataifa wamekubaliana suala la amani lipewe kipaumbele na umuhimu wa kuzingatia sheria za kimataifa katika kushughulikia migogoro duniani.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (Kushoto) akimkaribisha Mgeni wake, Rais Truong Tan Sang wa Vietnam ambaye yupo nchini kwa Ziara ya Kitaifa ya siku tatu.
Rais Truong pamoja na Mkewe, Bi. Mai Thi wakipokea maua wakati walipowasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli (kulia) pamoja na Mgeni wake, Rais wa Vietnam wakitembea pamoja.
Viongozi Wakuu wa Serikali wakishuhudia mapokezi ya Rais wa Vietnam yakiendelea katika viwanja vya Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Mgeni wake, Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tan Sang wakiwa kwenye jukwaa tayari kwa ajili ya kupigiwa Wimbo wa Taifa uliyoambatana na Mizinga 21, kisha kukagua Gwaride la Heshima
Kikosi cha bendi cha Polisi kikipiga nyimbo za Mataifa yote mawili wakati wa mapokezi ya Rais wa Vietnam (hayupo pichani)
Rais Truong Tan Sang akikagua gwaride la heshima

Rais Magufuli pamoja na Mgeni wake, Mhe. Truong Tan Sang wakisalimiana na wananchi waliojitokeza katika mapokezi hayo 
Waandishi wa Habari nao wakiwa kazini kwa kuchukua matukio muhimu wakati wa mapokezi ya Rais Truong Tan Sang (hayupo pichani). Kiongozi huyo ameambatana na waandishi 22 wa habari.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tan Sang
Rais wa Tanzania (kulia) na Rais wa Vietnam na wake zao wakiwa katika moja ya vyumba vya kupokelea wageni mashuhuri, Ikulu Dar es salaam.
Rais Magufuli (kulia) akifanya mazungumzo na mgeni wake, Mhe. Tan Sang. Katikati yao ni Mkalimani wa Rais Tan Sang 
Rais Dkt. Magufuli akiongea na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa ziara hiyo.
Rais Tan Sang naye akiongea na waandishi wa habari kuhusu ziara hiyo ambapo ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ambaye pia alikuwa muendeshaji mkutano wa waandishi wa habari Bw. Gerson Msigwa akipitia ratiba. Wanaomwangalia kutoka kushoto ni Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Vietnam Bw. Le Hai Binh na mwenyeji wake Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania Bi. Mindi Kasiga 
Kaimu Mkuu wa Itifaki Bw. James Bwana akipokea maagizo kutoka kwa Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli
Rais Magufuli (kulia) akimsikiliza Rais Truong Tan Sang alipokuwa akimweleza jambo kabla ya mazungumzo yao na vyombo vya habari
Viongozi mbalimbali wa Tanzania na Vietnam pamoja na waandishi wa habari wakiwasikiliza kwa makini Marais wa Tanzania na Vietnam (hawapo pichani)

Picha na Reginald Philip.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.