Thursday, March 3, 2016

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI WANACHAMA WA EAC



Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ally Mohamed Shein akisalimiana na Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe Waziri wa Katiba na Sheria mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Rais Mhe. Dkt. Ally Mohamed Shein akivipongeza vikundi vya wacheza ngoma vilivyokuja kumpokea uwanjani hapo.

Kikundi cha ngoma cha wanawake kikimpokea kwa shangwe Rais wa Zanzibar.

 Mhe. Yoweri Kaguta Museveni Rais wa Uganda mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe  wa pili kulia aliongoza mapokezi ya kiongozi huyo.

Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame akisalimiana na viongozi wa jeshi ambao walikuja kumpokea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, kushoto kwake ni Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Charles Kitwanga akiwa ameambatana naye mara baada ya kumpokea.


Kaimu Mkuu wa Itifaki Bw. James Bwana akitoa maelezo kwa Mhe. Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ambaye alimpokea Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyata ambaye aliwasili kwa ajili ya kushiriki mkutano huo.

Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyata akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya  Mhe. John Haule mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.

Mhe. Rais Uhuru Kenyata akisalimia vikundi vya ngoma havipo pichani vilivyokuwa vikitoa burudani uwanjani hapo.

Wakuu wa Nchi wanachama wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika Mkutano  wa 17 ambapo katika Mkutano huo Sudan ya kusini nayo imepata usajili wa uanachama katika umoja huo baada ya maombi yake kujadiliwa na kukubaliwa.


Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo akihutubia katika Mkutano, ambapo ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki Mkutano huo tangu ashinde uchaguzi na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu Mkuu mteule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw, Liberat Mphumukeko kutoka nchini Burundi akiapa katika mkutano huo wa wakuu wa nchi mara baada ya uteuzi wake.

Bw. Liberat Mphumukeko akipewa pongezi na Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa nchini Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga mara baada ya kukamilisha taratibu za kiapo.

Waheshimiwa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wameshika Hati ya kimataifa ya kusafiria ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambapo uzinduzi wa hati hiyo ulifanyika katika mkutano huo.
Kijana Simon Moleli kutoka shule ya Sekondari ya Mzumbe ambaye alikuwa mshindi wa kwanza katika mashindano ya uandishi wa insha ya Afrika Mashariki mara baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi na fedha vikiwa ni tuzo kwa ushindi alioupata.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Balozi Innocent Shio wa pili kutoka kushoto akifatilia mkutano.

Wah. Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Wah. Mawaziri wa Jumuiya hiyo.


==============================================================================================


Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki umefanyika Jijini Arusha ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji na muandaaji wa Mkutano huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa Victoria katika Hoteli ya Ngurudoto, tarehe 2 Februari 2016. 


Burundi pia ilishiriki mkutano huo ambapo Mhe. Rais Pierre Nkurunziza aliwakilishwa na Makamu wa pili wa Rais Mhe. Joseph Butole. Sudan Kusini nayo ilialikwa na ikashiriki katika mkutano huo ambapo Makamu wa Rais Mhe. James Wani Igga alimwakilisha Rais wa Taifa hilo. Aidha mkutano ulihudhuriwa na waalikwa kutoka katika mataifa na jumuiya mbalimbali duniani. 

Muongozo wa maadili ya biashara  "Code of conduct for business in EAC" pia ulisainiwa na wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo, lengo likiwa kuziinua nchi hizo katika hali duni ya umasikini na kuwekeza katika biashara zenye manufaa makubwa kwa mataifa hayo na kuhakikisha kila taifa halikiuki taratibu zilizowekwa.

Pia Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeombwa kuendelea kuongoza umoja huo kwa mwaka mmoja zaidi. Wakuu hao wa nchi walimuomba Mhe Rais Magufuli kusimamia jumuiya hiyo kwa kutumia kauli mbiu yake ya "hapa kazi tu" kwa vitendo na si kwa maneno. Rais Magufuli alikubali ombi hilo na kuahidi kutowaangusha katika utendaji kazi na kwamba ataanza na kuangalia utendaji wa ofisi ya Jumuiya hiyo akisisitiza asiyeweza kuendana na kasi yake basi hafai kuwepo katika taasisi hiyo.

Mhe. Rais Magufuli alieleza pia kwa upande wa usuluhishi wa mgogoro wa Burundi Mhe. Yoweri Museveni alifanyie kazi suala hilo ili kuepuka madhara yatokanayo na migogoro. Wakati huo huo, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin W. Mkapa amechaguliwa kuwa msuluhishi katika mgogoro wa Burundi,  hivyo ataenda kuongeza nguvu kwa Mhe. Yoweri Museveni na akawasihi wanajumuiya kuwapa ushirikiano wasuluhishi hao.


Sambamba na hayo suala la kuanzisha na kukuza viwanda ndani ya jumuiya nalo lilionekana kuwa jambo la msingi kwa mataifa yote ili kuweza kuzalisha bidhaa zenye ubora na zitakazowezesha kukua kwa uchumi, pamoja na lugha ya Kiswahili kutumiwa na wanachama wote ili kurahisisha mawasiliano katika shughuli za kiuchumi.


Mwisho wakuu hao wa nchi walimpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kushinda katika uchaguzi na kupata nafasi ya kuwa Rais na pia walimpa pongezi kwa kuweza kuandaa Mkutano uliofanyika katika hali ya amani na utulivu na kuwezesha kufanikisha mambo muhimu yaliyoweza kutekelezwa katika mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.