Friday, January 25, 2019

Naibu Waziri awasilisha taarifa ya Wizara ya utekelezaji wa majukumu kwa Kamati ya Bunge ya Nje, Ulinzi na Usalama



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Kipindi cha Julai hadi Desemba, 2018 mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) (hawapo pichani) kilichofanyika kwenye Ofisi za Bunge, Dodoma tarehe 25 Januari, 2019. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Mhe. Mussa Azan Zungu akizungumza wakati wa kikao kati ya Wajumbe wa Kamati ya NUU na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kulia ni Katibu wa Kamati
Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Salum Mwinyi Rehani akichangia jambo wakati wa kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kushoto ni Mhe. Ruth Mollel, Mjumbe wa Kamati hiyo.
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Fakharia Shomar Khamis nae akichangia hoja wakati wa kikao kati ya Kamati ya NUU na Wizara
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi kutoka Wizarani wakifuatilia kikao


Wakurugenzi kutoka Wizarani wakisoma nyaraka mbalimbali wakati wa kikao

Juu na chini ni Wakurugenzi kutoka Wizarani
Wajumbe wa Kamati ya NUU wakifuatilia kikao
Kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Prosper Mbena akichangia jambo wakati wa kikao
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Janeth Masaburi nae akichangia jambo
Mhe. Mboni Mhita ambaye ni Mjumbe wa Kamati akitoa ushauri kwa Wizara kuhusu kuboresha masuala mbalimbali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi


Mjumbe wa Kamati ya NUU, Mhe. Shamsi Vuai Nahodha nae akizungumza
Wajumbe wa Kamati wakifuatilia kikao
Watumishi kutoka Wizarani wakifuatilia kukao

Thursday, January 24, 2019

Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya heshima nchini India

Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan akitunukiwa Tuzo ya Juu (Pravasi Bharatiya Samman Award ) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind tarehe 23 Januari, 2019. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu wa Mauritius, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh nchini humo.
Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind akihutubia katika hafla ya kuhitimisha Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India [15thPravasi Bharatiya Divas 2019] uliofanyika tarehe 23 Januari, 2019 katika mji wa Varanasi, Uttar Pradesh nchini India 
Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkubwa wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh, India
Picha ya pamoja



Mama Shamim Khan katika picha ya pamoja na Afisa Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Dkt. Kheri Goloka baada ya kupokea Tuzo tarehe 23 Januari, 2019.
=======================================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Yah: Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya juu ya heshima na Mhe. Ram Nath Kovind, Rais wa India

Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima (Pravasi Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India (15th Pravasi Bharatiya Divas 2019) uliofanyika kwenye mji wa Varanasi, Uttar Pradesh tarehe 23 Januari, 2019.

Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi  uliwahusisha viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya India akiwemo Waziri Mkuu wa Mauritania, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Sushma Swaraj, Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje ya India, Mhe. Gen [Dr.) V. K. Singh na Waziri Kiongozi wa Jimbo la Utter Pradesh, Mhe. Yogi Adityanath.

Mama Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii hususan katika masuala ya akina mama na kudumisha amani na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini. 

Wakati akimtunuku tuzo hiyo, Rais Kovind alieleza kutambua mchango mkubwa wa Mama Shamim Khan katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na Serikali ya Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zao. Aidha, alimpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Kwa upande wake, Mama Shamim Khan alimshukuru sana Rais Kovind na kueleza kufarijika kwake kwa kutunukiwa Tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwake. Aidha, Mama Shamim Khan alipongeza juhudi za Serikali ya India kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na India na amemuomba Mhe. Rais Kovind kuendelea kusaidia juhudi za Serikali ya Mhe.Rais Dkt. John P. Magufuli katika kuwaletea maendeleo watanzania.

Tuzo hiyo hutolewa kwa raia wenye asili ya India ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mama Shamim Khan bali kwa Tanzania kwa ujumla.  Mama Shamim Khan aliongozana na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dkt. Kheri Goloka kwenye hafla hiyo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
24 Januari 2019





Wednesday, January 23, 2019

Balozi wa Tanzania, Ujerumani awasilisha hati za utambulisho nchini Bulgaria

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye anawakilisha pia nchini Bulgaria , Mhe. Dkt. Abdallah Posi akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Bulgaria, Mhe. Rumen Radev. Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya nchi hiyo hivi karibuni.
Mhe. Balozi Dkt. Posi akizungumza na Mhe. Rais Radev mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho
Mhe. Balozi Dkt. Posi akiagana na Mhe. Rais Radev mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho


Mhe. Balozi Dkt. Posi akiwa mbele ya gwaride la heshima alipowasili Ikulu ya Bulgaria kwa ajili ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa nchi hiyo.

Thursday, January 17, 2019

Tanzania kushiriki Maonesho ya Biashara ya Dunia ya EXPO 2020


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania kushiriki Maonesho ya Biashara ya Dunia ya EXPO 2020

Tanzania itashiriki Maonesho ya Dunia ya Biashara (Expo 2020 yatakayofanyika Dubai kuanzia mwezi Oktoba 2020 na kumalizika mwezi April 2021.

Uwekaji saini wa Mkataba wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho hayo ulifanywa tarehe 16 Januari 2019 na Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk.

Kwa upande wa UAE, mkataba huo uliwekwa saini na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali.

Baada ya uwekaji saini wa Mkataba huo, Mhe. Balozi Mbarouk alieleza kuwa Serikali inayapa umuhimu mkubwa maonesho hayo kwa kuwa ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kwenye sekta za uwekezaji, biashara, viwanda, utalii na mila na utamaduni.

Aidha, Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020 alieleza kuwa amefurahishwa na hatua ya Tanzania kusaini Mkataba huo ambapo itatoa fursa kwa nchi kujiandaa mapema na taratibu nyingine za ushiriki.

Baada ya uwekaji saini wa Mkataba huo,` kitakachofuata ni utayarishaji wa simulizi ya maudhui ya maonesho (pitch story) ambayo inatakiwa kuthibitishwa na Kamati ya Kitaifa ya Tanzania ya DUBAI Expo 2020. Simulizi ya maudhui hayo yatahusu vipaumbele vya Tanzania kama vile maendeleo ya viwanda, miundombinu, masuala ya biashara na uwekezaji, utalii, kilimo, elimu, afya, sanaa na utamaduni.  Simulizi ya maudhui pia itatumika katika kusanifu muonekana wa banda la maonesho la Tanzania.

Tanzania inakuwa miongozi mwa nchi washiriki zipatazo 100 ambazo tayari zimesaini Mkataba wa Ushiriki tangu Dubai ilipochaguliwa kuwa mwenyeji wa maonensho hayo.

Wengine walioshuhudia uwekaji saini wa Mkataba huo ni Bw. Ali Jabir Mwadini, Kansela Mkuu, Ubalozi Mdogo wa Tanzania, Dubai; Bi Samira Ahmed Diria, Afisa Ubalozi; na kwa upande wa DUBAI EXPO 2020 ni  Bi Manuela Garcia Pascual, Mkurugenzi wa Washiriki wa Kimataifa na Bi. Esther Omondi, Meneja wa Nchi/Afisa dawati la Tanzania.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
17 Januari 2019

Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakiweka saini Mkataba wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Dunia (Dubai Expo 2020. Uwekaji saini huo ulifanyika Dubai tarehe 16 Januari 2019.  
Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakionesha Mkataba mara baada ya zoezi la kuweka saini kukamilika.
Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wao.

Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakibadilishana mawazo mara baada ya zoezi la kuweka saini kukamilika.

Wednesday, January 16, 2019

DKT. NDUMBARO ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO UBALOZI WA NIGERIA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) akisaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Nigeria hapa nchini kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa sita wa nchi hiyo Mhe. Alhaji Shehu Shagari kilichotokea tarehe 28 Desemba 2019. Dkt. Ndumbaro alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Dkt.Sahabi Isa Gada. Tukio hilo limefanyika jijini Dar Es Salaam katika Ubalozi wa Nigeria hapa nchini.  
Balozi Gada akimwelezea jambo Dkt. Ndumbaro wakati wa mazungumzo.
Sehemy ya Maafisa wa Ubalozi wa Nigeria nchini wakisikiliza kwa makini mazungumzo kati Dkt. Ndumbaro na Balozi Gada (hawapa pichani).
Dkt. Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Gada na maafisa wa Ubalozi huo.
Dkt. Ndumbaro akiagana na Balozi Dkt. Gada. 





Balozi wa Italia atembelea Wizara ya Mambo ya Nje


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni. Wawili hao walijadiliana umuhimu wa kuibua maeneo mapya ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Italia hussusan katika sekta ya biashara na uwekezaji.  Dkt. Mahiga alitumia fursa hiyo pia kueleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Balozi Mengoni akimwelezea jambo Dkt. Mahiga


Katibu wa Mhe. Waziri, Bw. Magabilo Murobi pamoja na Bi Happyness Lwangisa wakifuatilia na kunukuu mambo muhimu ya mazungumzo hayo.

Dkt. Mahiga akagua ujenzi wa ofisi ya Wizara Ihumwa, Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akiweka saini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye eneo linalojengwa jengo la ofisi ya Wizara Ihumwa, Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara Ihumwa Dodoma. Mhe. Waziri alielezwa kuwa ujenzi huo unaenda katika kasi inayoridhisha ambapo wakandarasi wapo mbele ya mpangoa kazi.

Waziri Mahiga na Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Hamid Mbegu wakioneshana alama za mipaka ya kiwanja cha Wizara.

Waziri Mahiga akiendelea na ukaguzi wa jengo la ofisi ya Wizara.
Waziri Mahiga akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Hamid Mbegu 

Watanzania 70 wahitimu Chuo Kikuu cha Galgotias nchini India


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watanzania 70 wahitimu Chuo Kikuu cha Galgotias nchini India

Watanzania zaidi ya 70 wakiwemo wawili wa shahada ya uzamivu wamehitumu masomo yao katika Chuo Kikuu cha Galgotias nchini India katika fani mbalimbali tarehe 14 Januari 2019.

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya nne ya chuo hicho aliwatunuku vyeti wanafunzi hao na wengine kutoka nchi mbalimbali duniani na kuwasihi  kutumia ujuzi walioupata kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi walizotoka.

‘Ulimwengu unasubiri uongozi mpya na mawazo mapya na kanuni na miiko madhubuti kutoka kwenu. Hivyo, kifanyeni chuo kijivune kupitia kwenu kwa kutoa michango yenye tija katika mataifa na jamii zenu, hususan kwa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na uadilifu mkubwa katika kutimiza majukumu yenu', Balozi Luvanda alisema.

Balozi Luvanda alisema kuwa wanafunzi hao wanahitimu huku dunia ikishuhudia mapinduzi ya teknolojia mbalimbali zikiwemo za kidigitali, teknolojia ya matumizi ya sarafu za kidigitali (block chain), matumizi ya kiwango kikubwa cha data katika kufanya maamuzi (big data revolution), usalama wa mitandao (cybersecurity) na matumzi ya teknolojia katika kutekeleza kazi ambazo awali zilikuwa zinafanywa na mwanadamu (artificial intelligence). Alielezea matumaini yake kuwa chuo hicho kitakuwa kimewandaa vyema wahitimu hao  kukabiliana na changamoto za mapinduzi ya teknolojia katika kutekeleza majukumu yao.

Mhe. Balozi alihitimisha hotuba yake kwa kuwasihi wahitimu hao kuwa, kutunukiwa vyeti sio mwisho wa kujifunza. Wanatakiwa waendelee kusoma vitabu kwa kuwa kusoma vitabu ni sawa na kuufanyia matengenzo ubungo. ‘Akili ya mwanadamu ni kama bustani, bustani isipomwagiwa maji na kupaliliwa itaota magugu na kufa kabisa.   Mhe. Balozi alimaliza.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
16 Januari 2019

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Chuo Kikuu Galgotias kutunukuu vyeti kwa wahitimu wa chuo.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akitoa heshima katika picha ya Mahatma Gandhi kwa kuweka shada la maua.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akitoa hotuba katika mahafali ya nne ya Chuo Kikuu cha Galgotias

Umati wa wahitimu wa chuo kikuu cha Galgotias
wakisikiliza kwa makini hotuba ya Balozi Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akipokea memento kutoka kwa mwanzilishi na mkuu wa chuo kikuu cha  Galgotias, Bw. Suneel Galgotia.






Tuesday, January 15, 2019

Dkt. Ndumbaro akutana na Mwakilishi wa UNHCR

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.), amekuatana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la kutetea wakimbizi la Umoja wa Mataifa Tanzania UNHCR, Chansa Kapaya.

Katika mazungumzo yao Bi. Chansa alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa mara ya kwanza pamoja na Kumpongeza Dkt. Ndumbaro kwa Kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwa upande wake Dkt. Ndumbaro alimshukuru kwa kuja ofisini kwake na kumwahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha wakati wote wautendaji wa majukumu yake akiwa hapa nchini. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.  
Mazungumzo yakiendelea.
Dkt. Ndumbaro akimkaribisha Bi. Shansa ofisini kwake walipokutana kabla ya kuanza kwa mazungumzo yao. 




Waziri Mahiga akutana kwa Mazungumzo na Balozi wa Misri.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Misri hapa nchini Mhe. Mohamed Gaber Abouelwafa. Katika mazungumzo yao Balozi Abouelwafa alimweleza Dkt. Mahiga kuwa wanafurahishwa na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Misri, ambapo kwa sasa Misri wanatekeleza mradi mkubwa wa Bwawa la kuzalisha Umeme Nchini, vilevile Misri itaendelea kuboresha miundombinu ya uzalishaji wa maji kwa kuchimba visima vingine vya maji Nchini.
Pamoja na Mambo mengine Dkt. Mahiga alimweleza Balozi Abouelwafa kuwa Tanzania itaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha  katika utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Aidha, Dkt. Mahiga alimweleza Balozi kuwa Tanzania inatambua mchango wa Misri kwenye sekta mbalimbali zikiwemo Afya, Elimu na Biashara. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, zilizopo jijini Dar Es Salaam 
Katibu wa Waziri Bw. Magabilo Murobi (wa kwanza kushoto), pamoja na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Afrika Bw. Wilbroad Kayombo wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Abouelwafa (hawapo pichani).
Mazungumzo yakiendelea kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Abouelwafa
Maafisa kutoka Ubalozi wa Misri nchini Tanzania wa kwanza kushoto ni Bw. Ahmed Elghoul na Bi. Nevine Elsaeed nao wakifuatilia kwa makini mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati ya Dkt. Mahiga na Balozi Abouelwafa (hawapo pichani).



Monday, January 14, 2019

Dkt. Ndumbaro awaaga Watanzania wanaokwenda Japan kujifunza masuala ya Uongozi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan, Mhe. Shinichi Goto aliyeambatana na washiriki kutoka Tanzania wanao kwenda Nchini Japan kwa ajili ya kupata mafunzo ya Uongozi katika sekta mbalimbali. Mafunzo hayo yatadumu kwa muda wa siku 50. Aidha, Dkt. Ndumbaro amemshukuru Balozi Goto kwa kuendelea kuiwakilisha vyema nchi ya Japan hapa nchini ambapo aliahidi kuwa Japan itaendelea kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali.
 Dkt. Ndumbaro amewaasa Washiriki wanaokwenda katika mafunzo hayo kuitumia fursa hiyo vyema kwa kujifunza mambo mampya kutoka Taifa hilo. 


Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. Caesar Waitara (hayupo pichani) yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  jijini Dar Es Salaam.
Mazungumzo yakiendelea 
Dkt. Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Goto
Dkt. Ndumbaro pamoja na Balozi Goto wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki kutoka Tanzania wanao kwenda nchini Japani.