Saturday, March 9, 2019

Serikali ya awamu ya tano haichukii wawekezaji, Dkt. Magufuli

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya awamu ya tano haichukii wawekezaji, Dkt. Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema Serikali ya awamu ya tano anayoiongoza inathamini wawekezaji, tofauti na dhana ya baadhi ya watu kuwa wawekezaji katika awamu ya tano wanaonekana kuwa ni maadui.

Mhe. Rais Magufuli alisema hayo wakati wa sherehe ya kufungua mwaka 2019 ya wanadiplomasia (sherry party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar Es Salaam tarehe 08 Machi 2019, na kuhudhuriwa na Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yaliyopo hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli alisema uamuzi aliochukua hivi karibuni wa kuunda Wizara maalum ya uwekezaji ni ishara ya wazi kuwa Serikali ya awamu ya tano inathamini wawekezaji, na kuwasihi wanadiplomasia kuitumia wizara hiyo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ameifanyia mabadiliko.

Rais Magufuli alisema, Serikali yake imeshaanza mpango kabambe wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutoa wito kwa wale wenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini, waende mamlaka husika ili wahudumiwe.  “Mwenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini, aende Wizara ya Uwekezaji au Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akikwamishwa huko aje kwangu ili nimkwamue huyo aliyekwamisha”, Rais Magufuli alisema.

Wanadiplomasia walioshiriki hafla hiyo, walisisitizwa kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, madini na viwanda vya nguo. “Serikali inahimiza uwekezaji katika sekta zinazotumia malighafi zinazopatikana nchini na zitakazotoa ajira za kutosha kwa vijana wa kitanzania kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi”.  Rais Magufuli alisema.

Kuhusu utalii, Rais Magufuli alieleza kuwa, Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, zikiwemo fukwe, uoto wa asili, malikale, mbuga za Wanyama na kwamba Serikali imejipanga kutangaza vivutio hivyo, hususan, vile vinavyopatikana kanda ya kusini. Mhe.  Rais aliitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa uamuzi wake wa kuanzisha channel maalum ya kutangaza vivutio vya utalii.

Kwa upande wa sekta ya madini, Serikali imejipanga kudhibiti wizi, biashara ya magendo, kuanzisha masoko ya kuuza madini na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata madini, ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi.

Aidha, Rais Magufuli alitumia hafla hiyo kuwaeleza wanadiplomasia, mafanikio ya Serikali ya mwaka 2018, mafanikio hayo ni Pamoja na Serikali kuendelea kulinda na kudumisha amani ya nchi; kukuza uchumi wa nchi ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2018, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tano barani Afrika, uchumi wake umekua kwa kasi ikizidiwa na Ethiopia pekee.

Tanzania pia iliweza kudhibiti mfumuko wa bei na iliongoza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 1.18.

Mafanikio mengine ni Pamoja na ujenzi wa Miundombinu ikiwemo: ujenzi unaondelea wa reli ya kiwango cha Kimataifa kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma; ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa Mega Watts 2100 katika Mto Rufiji; ujenzi na upanuzi wa barabara mbalimbali nchini; ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria; upanuzi wa bandari za Dar Es Salaam, Mtwara na Tanga na kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa Terminal 3 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Serikali pia imepiga hatua katika kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika sekta ya afya, elimu na maji. Kwa upande wa afya, bajeti ya sekta hiyo imeongezeka kutoka bilioni 31 hadi kufikia bilioni 270 ambapo ujenzi wa vituo vya afya 305 umekamilika na ujenzi wa hospitali 67 za Wilaya unaendelea, ukilenga kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kuhusu elimu, Serikali imeendelea na mpango wake wa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Aidha, Miundombinu ya maji imeimarishwa ambapo upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini umefikia asilimia 80 na asilimia 65 kwa maneo ya vijijini.
Rais Magufuli alieleza kuwa mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya tano inaendelea kuyapata yanatokana na Ushirikiano na mchango mkubwa kutoka kwa wanadiplomasia, na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kudumisha Ushirikiano huo.

Alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa, watumishi wengi wa Serikali walishahamia Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma na kuelezea matumaini yake kuwa, baadhi ya Balozi zitakuwa zimeshaanza mchakato wa kuhamia Dodoma, ukizingatia kuwa Serikali imetoa viwanja bure kwa ofisi zote za balozi.  
  
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania

09 Machi 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini katika Sherehe za kufungua Mwaka 2019 (sherry party) zilizofanyika Ikulu, Dar Es Salaam jana. Sherehe hizo zimehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiendelea kuzungumza wakati wa sherehe hizo.
Mabalozi wakimpongeza Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli 
Rais Magufuli akiendelea kuzungumza na wanadiplomasia

Kiongozi wa Mabalozi ambaye ni Balozi wa Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed naye akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa.
Sehemu ya Mabalozi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (kulia)
Mshereheshaji kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Bertha Makilagi akisherehesha kwenye Shughuli hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa Namibia, Mhe.Theresa Samaria mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa Oman hapa nchini, Mhe. Ali A. Al Mahruqi mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Sarah Cooke mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na Balozi wa India hapa nchini, Mhe. Sandeep Arya mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) akisalimiana na Balozi wa Ufaranza nchini, Mhe. Frederic Clavier mara baada ya kumalizika kwa sherehe za mwaka 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaoziwakilisha nchni zao hapa nchini, mara baada ya kumalizika kwa Sherehe za kufungua Mwaka 2019 (Diplomatic Sherry Party).




Friday, March 8, 2019

Sakata la Chuo cha Diplomasia lahamia Takukuru

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji K. Mnyepe (kulia) akikabidhi ripoti za ukaguzi za Chuo cha Diplomasia, kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (PCCB), Bw. Diwani Athumani kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu wa fedha uliofanywa na baadhi ya viongozi wa chuo hicho. Makabidhiano hayo yalifanyika leo kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar Es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Diplomasia, Balozi Ombeni Sefue akishuhudia makabidhiano ya ripoti za ukaguzi ambazo zimeainisha ubadhilifu wa fedha katika Chuo cha Diplomasia.
Balozi Sefue (kushoto), Dkt. Mnyepe na Bw. Diwani wakibadilishana mawazo kuhusu utendaji kazi wa Chuo cha Diplomasia. 
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Diwani Athumani akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Diplomasia, Balozi Ombeni Sefue.




Thursday, March 7, 2019

Prof. Kabudi akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Mhe. Dkt. Richard Sezibera. Katika mazungumzo yao, Mhe. Sezibera alimpongeza Mhe. Kabudi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Ernest Mangu na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Wilbroad Kayombo. Mhe. Sezibera yupo nchini kwa ajili ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame. 
Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Eugene Kayihura (kulia) na Afisa Ubalozi wa Rwanda wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Dkt. Sezibera (hawapo pichani). 
Mhe. Prof. Kabudi akimwelezea jambo Mhe. Dkt. Sezibera wakati wa mazungumzo hayo.
Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Ernest Mangu pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Bw. Wilbroad Kayombo wakiwa kwenye Mazungumzo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Mhe. Dkt. Richard Sezibera (wapili kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Ernest Mangu (wa kwanza kulia) na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Eugene Kayihura (wa kwanza kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.




ZIARA YA KIKAZI YA RAIS KAGAME WA RWANDA NCHINI TANZANIA


Rais Kagame awasili nchini kwa ziara ya kikazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (kulia) akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ziara ya siku mbili. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi akitembea na Rais Kagame kuelekea katika chumba cha wageni maalum.
Rais Kagame akiwapungia mkono wananchi waliofika uwanja wa ndege kwa ajili ya kumpokea.
Prof. Kabudi na Rais Kagame wakiingia kwenye gari kwa ajili ya kuelekea Ikulu jijini Dar Es Salaam.




Wednesday, March 6, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa kuhusu ziara ya Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda

Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, atawasili nchini tarehe 7 Machi 2019 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Ziara hiyo inafanyika kufuatia mwaliko wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Ziara hii itatoa fursa kwa viongozi hao wawili kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Aidha, Viongozi hao wanatarajia kuzungumzia masuala mbalimbali ya mtangamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mhe. Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa Tisa Alasiri tarehe 7 Machi 2019 na kupokelewa na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Rais Kagame anatarajia kuondoka nchini tarehe 8 Machi, 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
6 Machi 2019


Tuesday, March 5, 2019

RAIS DKT. MAGUFULI AWAAPISHA MAWAZIRI WAWILI, BALOZI MMOJA PAMOJA NA KUSHUHUDIA UAPISHWAJI WA MAOFISA WATANO WA JESHI LA POLISI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi Yahya Simba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi katika picha ya pamoja na Makamishna watano kutoka jeshi la Polisi, Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Palamagamba Kabudi, pamoja na Balozi Yahya Simba mara baada ya hafla ya Uapisho Ikulu jijini Dar es Salaam.

Thursday, February 28, 2019

Watumishi wa Mambo ya Nje wahimizwa kuzingatia sheria za utumishi wa umma


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akizungumza kwenye kikao cha pili na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hawapo pichani) Pamoja na mambo mengine amewataka Watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo. Kikao hicho kilifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano  wa Wizara uliopo Chuo Kikuu cha Dodoma hivi karibuni
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bibi Savera Kazaura akizungumza wakati wa kikao hicho
Sehemu ya Watumishi wa Wizara wakiwemo Wakuu wa Idara 
Balozi Mteule, Dkt. Mpoki Ulusubisya akitoa mada kuhusu afya kwa Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hawapo pichani) wakati wa kikao kati yao na Katibu Mkuu wa Wizara. Pamoja na mambo mengine aliwashauri Watumishi kuwa na utratibu wa kupima afya zao mara kwa mara.
Sehemu ya Watumishi wa Wizara wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo wakifuatilia mada
Sehemu ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara

Sehemu nyingine ya Wakuu wa Idara na Vitengo

Wakuu wa Vitengo akifuatilia mkutano

Wakurugenzi wakiwa kwenye mkutano

Mkutano ukiendelea

Sehemu ya Watumishi wakifuatilia mkutano

Watumishi wakiwa kwenye mkutano

Mkutano ukiendelea

Sehemu nyingine ya Watumishi wakati wa mkutano

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye mkutano na Katibu Mkuu.






Prof. Kabudi akutana na viongozi mbalimbali wakati wa kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la UN

Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wa tatu kushoto) akizungumza na Kamishna wa Haki za Biandamu, Bi. Michelle Bachelet (mwenye miwani kulia) kuhusu masuala ya haki za binadamu. Wakati wa mazungumzo yao, Bi. Bachelet aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupambana na rushwa, kupigia hatua za maendeleo ya kiuchumi, kuendelea kuwahifadhii wakimbizi na ushiriki katika ulinzi wa amani barani Afrika. Kwa upande wake, Prof. Kabudi alisema Tanzania itaendeea kulinda Haki za Binadamu kwa wananchi wote na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Kamishna huyo.
Mhe. Prof. Kabudi na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na Bi. Michelet.
Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Hassan Shire, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Defenddeffenders mara baada ya mazungumzo kati yao. Pamoja na mambo mengine mazungumzo yao yalijikita kwenye masuala yanayohusu haki za binadamu ambapo, Mhe. Prof. Kabudi aliishauri taasisi hiyo ambayo inajishughulisha na masuala ya haki za binadamu  kujikita katika kufanya tafiti ili kuandaa taarifa za uhakika kuhusu nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinavyotekeleza haki za binadamu. 
Mhe. Prof. Kabudi ( wa tatu kushoto) na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na Bw. Shire (wa nne kulia) na mjumbe aliyeongozana naye Bw. Nicolas Agostini (wa pili kulia) 

Rais Magufuli akutana na Makamu Rais Mtendaji wa JICA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA), Bw. Kazuhiko Koshikawa (wa tatu Kushoto) na ujumbe wake walipokutana  Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Damas Ndumbaro (Mb).
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimpa zawadi ya picha ya kuchora ya wanyama wakuu watano (Big Five)  Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA), Bw. Kazuhiko Koshikawa alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019.
Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro (Mb).
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimpa zawadi ya kinyago cha UJAMAA  Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA), Bw. Kazuhiko Koshikawa alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam leo Februari 28, 2019.
Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb)
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja na  Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA), Bw. Kazuhiko Koshikawa (wa tatu Kushoto) na ujumbe wake baada ya kukukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Februari 28, 2019. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb).
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiagana na Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa (wa tatu Kushoto) na ujumbe wake baada ya kukukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Februari 28, 2019. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb).


Wednesday, February 27, 2019

Serikali ya Awamu ya Tano kuendelea kulinda na kutetea Haki za Binadamu-Prof. Kabudi aliambia Baraza la Haki za Binadamu la UN


Waziri wa katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi
Mhe. Prof. Kabudi alipata fursa pia ya kuzungumza na Kundi la Mabalozi kutoka nchi za Afrika waliopo Geneva kama anavyoonekana pichani
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wa nne kulia) akiwa katika picha  ya pamoja na baadhi ya maafisa wa Tanzania mara baada ya kuhutubia kikao hicho cha Baraza la Haki za Bianadamu kinachofanyika Geneva, Uswisi.

=====================================================


Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu na ustawi wa jamii kama kipaumbele chake na  itaendelea kushirikiana na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhakikisha haki za binadamu nchini na duniani kote zinadumishwa.

Prof. Kabudi amesema hayo jana alipohutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi. Prof. Kabudi amesema Serikali ya Tanzania imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha haki za binadamu, utawala bora na utii wa sheria nchini na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu. 


Serikali imelenga kuimarisha haki za binadamu, utawala bora, utii wa sheria na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, kwa sasa tunatekeleza mpango mkakati wa kitaifa wa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18 - 2021/22, lengo likiwa ni kulinda na kudumisha haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu,” alisema Prof. Kabudi.

Amesema Serikali pia inazingatia suala la kuwapatia haki kwa haraka wananchi wasio na uwezo kwa kutolea maamuzi kwa haraka mashauri yanayowahusu watu wasio na uwezo na kuwapatia msaada wa kisheria kupitia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ili wananchi hao waweze kupata haki zao kwa wakati. 

Aidha, Prof. Kabudi amelihakikishia Baraza hilo kuwa Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari nchini na imeendelea kuhakikisha uhuru wa vyombo hivyo unalindwa huku jumla ya vituo vya redio 152, televisheni 34, magazeti 172  nchini kote yamesajiliwa na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira stahiki yatakayowezesha vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru.

Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuleta ustawi wa jamii kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na kunadi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote. 

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote na kuongeza kuwa Serikali inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 23 kwa mwezi kutoa elimu pasipo malipo na hivyo kuongeza udahili wa watoto wanaojiunga darasa la kwanza kwa asilimia 35.2 na asilimia 20.1 kwa wanaojiunga na kidato cha kwanza,” alisema. 

Prof. Kabudi pia amesema Serikali imedhamiria kufikisha huduma za afya karibu na watanzania wote ambapo imeongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 269 mwaka 2017/2018 na kuongeza kuwa Serikali inatekeleza mikakati ya kujenga vituo vya afya ambapo hadi sasa imejenga vituo 304, na nyumba za watumishi wa afya 578 zimejengwa nchini kote.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kukuza na kulinda haki za binadamu duniani kote na kushughulikia uvunjwaji wa haki za binadamu unaotokea katika nchi wanachama wa umoja huo na kushauri hatua za kuchukuliwa ili kuboresha haki za binadamu duniani. 

Baraza hilo pamoja na mambo mengine linatarajia kupokea taarifa mbalimbali kuhusu haki za binadamu duniani na kutoa nafasi kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa maelezo yao kuhusu utekelezaji wa wajibu wao wa kulinda na kukuza haki za biandamu katika nchi zao.


Tuesday, February 26, 2019

Finland yaipongeza Tanzania vita dhidi ya Rushwa.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Finland yaipongeza Tanzania vita dhidi ya Rushwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Timo Soini.amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli za kupambana na rushwa na kusimamia uwajibikaji.

Pongezi hizo alizitoa wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye yupo nchini Finland kwa ziara ya kikazi ya siku mbili tarehe 25 na 26 Februari 2019.

Kwenye mazungumzo yao, Mawaziri hao wamesisitiza umuhimu wa Tanzania na Finland kuboresha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, uwekezaji, mafunzo ya ufundi, ajira kupitia sekta ya misitu, ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa kwa kuzingatia usawa, pamoja na kuwajengea uwezo wanawake na watoto.

Aidha, Mhe. Soini  alitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi na mchango mkubwa katika usuluhishi wa migogoro inayozikabili baadhi ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu. Hivyo, walikubaliana kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama ikiwa ni pamoja na biashara ya madawa ya kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, na matishio ya ugaidi.

Kabla ya mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Sampo Suihko, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha OMNIA Espoo ambaye alieleza utayari wa Taasisi yake wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa kutoa mafunzo ya elimu ya ufundi yanayoendana na soko la ajira.

Mhe. Mahiga pia alifanya mazungumzo na Mhe. Matti Ahtisaari, Rais Mstaafu wa Finland na Mwanzilishi wa Taasisi ya Utatuzi wa Migogoro. Mhe. Ahtisaari aliipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya katika utatuzi wa migogoro kwenye nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na kusihi kuendeleza jitihada hizo kwa ustawi wa Dunia nzima.

Vilevile, Dkt. Mahiga alifanya mazungumzo na Bw. Jukka Kallio, Makamu wa Rais wa Helsinki. Katika mazungumzo hayo, uongozi wa Bandari ya Vuosaari umeahidi kushirikiana na uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania katika kuboresha mifumo ya kidigitali (Digitalization) itakayoongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Katika kuhamasisha uwekezaji wa viwanda nchini, Mhe. Waziri Mahiga alifanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara (Business Finland) na Makampuni makubwa ya kibiashara nchini humo. Wafanyabiasha hao walipongeza jitihada zinazoendelea kufanyika nchini Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na  waliahidi kuwekeza na kushawishi makampuni mengine kuona umuhimu wa kuwekeza nchini Tanzania.

Mhe. Waziri anahitimisha ziara hiyo kwa kufanya mazungumzo na Bi. Anne-Mari Virolainen, Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland; Bw. Mauri Pekkarinen, Naibu Spika wa Bunge la Finland, Bw. Juhan Damski, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi  ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya nchini Finland na baadaye kuzungumza na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Finland.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
26 Februari 2019

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Timo Soini (kulia) akimkaribisha ofisini kwake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga. Dkt. Mahiga yupo nchini Finland kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Waziri Mahiga na ujumbe wake (kushoto) ukiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland na ujumbe wake.