Thursday, September 24, 2015

Tanzania yapongezwa kwa uongozi bora wa Kikundi Kazi cha Mawaziri Jumuiya ya Madola

Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola ukiendelea pembezoni mwa Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani.

Sekretarieti ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola wamesifu kazi iliyofanywa na Tanzania kama Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya hiyo ya kusimamia na kuimarisha misingi imara ya jumuiya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. 

Hayo yamesemwa na Dkt. Josephine Ojiambo Makamu Katibu Mkuu wa Sekretarieti hiyo, kwenye taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi za Jumuiya kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Septemba 24, pembezoni mwa Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa uongozi wa Mhe. Bernard Membe (Mb.), ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania umeibua mbinu za kisasa za kutatua matatizo ya nchi wanachama zilizokuwa na changamoto ya kuheshimu misingi na taratibu za Jumuiya ya Madola. 

Waziri Membe ambaye anamaliza muda wake wa uongozi kwenye kikundi kazi hicho mwaka huu, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri aliokuwa anaupata kutoka kwa Sekretarieti inayoongozwa na Kamalesh Sharma, ambao ndio waratibu wa shuguli za Kikundi Kazi cha Mawaziri. Vilevile ushirikiano aliopewa na Makamu Mwenyekiti wa Kikundi hicho Mhe. Murray McCully, Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand pamoja na wajumbe wengine wa Kikundi hicho maalum kimewezesha kazi za kuratibu kazi za Jumuiya hiyo kuwa na mafanikio makubwa. 

Masuala mengine yaliyojadiliwa kwenye mkutano wa Mawaziri ni utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo kuhusu uimarishwaji wa mifumo ya tehama na  nyenzo mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwenye nchi wanachama uliofanyika mwaka 2013  Jijini Colombo, nchini Sri Lanka. 

Kwenye mkutano huo pia Mhe. George William Vella, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malta alitoa taarifa fupi kuhusu maandalizi ya Mkutano wa mwaka huu wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Novemba 2015, nchini Malta. 

(Pichani juu na chini) Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akifuatilia Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.