Friday, May 31, 2024

MAWAZIRI WA BIASHARA ,VIWANDA, FEDHA NA UWEKEZAJI WA EAC WAAZMIA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA

Picha ya pamoja kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Mawaziri wanaosimamia sekta ya Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kuboresha ya mazingira ya biashara katika Jumuiya, huku wakitilia mkazo katika kuondoa vikwazo visivyo vya kodi, kurahisisha uvushaji wa mizigo mipakani, na kuimarisha utendaji wa miundombinu ya kusaidia biashara ikiwemo Vituo vya kutoa Huduma Pamoja Mpakani (OSBP). 

Vilevile wamekubaliana mapendekezo ya viwango mbalimbali vya ushuru wa forodha vitakavyo tumika katika mwaka wa fedha 2024/25 ambavyo vitachochea ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama.

Azma hiyo imefikiwa leo tarehe 31 Mei 2024 kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Akizungumzia kuhusu azma hiyo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya kuwataka Watendaji na Viongozi walipo chini yao kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara katika Jumuiya.

Waziri Nchemba aliongeza kutaja maeneo yaliyofanyiwa maboresho katika mkutano huo kuwa ni pamoja makubaliano kuhusu viwango vya tozo za barabara kwa Nchi Wanachama kutoka Dola za Marekani 16 hadi 10. 

Eneo jingine ni makubaliano ya utekelezaji wa mkakati wa Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) hasa kwa upande wa Tanzania na Kenya, ambapo Tanzania ilishaanza utelezaji wake. 

Jamhuri ya Kenya imeahidi kuanza kupitisha bidhaa za Tanzania katika mfumo wa himaya moja ya forodha mara moja na kufikia mwenzi Julai 2024, na kuleta wafanyakazi wake wa mamlaka ya forodha kwa ajili ya kuwezesha ukaguzi kabla mzigo haujaanza kuondoka ili mzigo usisimame mpakani. Hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano, usumbufu na upotevu wa mapato kwa Serikali na wasafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzani na Kenya.

“Tanzania tumekuwa tukikabiliwa na tatizo la msongamano wa maroli katika mipaka yetu ikiwemo Namanga, Sirari, Holili na Hororo, hii imechangiwa na kuto kuwepo kwa maafisa wa KRA upande wa Tanzania ambao wangesaidia kufanyia kazi nyaraka za kupitisha mzigo mpakani kabla gari husika halijafika mpakani tofauti na ilivyo sasa, utelezaji wa ahadi hii itasaidia kutatua tatizo hili lililo tusumbua kwa muda mrefu” Alisema Nchemba. 

Katika hatua nyingine Waziri Nchemba kwenye mkutano huo amewa ongoza Mawaziri wenzake kuzindua mfumo mpya wa Kielektroniki wa masuala ya forodha unaolenga kuongeza ufanisi katika biashara kwa kuweka mazingira ya uwazi, uwajibikaji na hatimaye kuongeza mapato kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya.

Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na mkutano ngazi ya Wataalam uliofanyika tarehe 27 hadi 29 Mei 2024 na ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 30 Mei 2024. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifuatilia mkutano

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umejumuisha Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania, Mhe. Shariff Ali Shariff, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji- Zanzibar, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud S. Kigahe.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akichangia jambo kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato wakishirikishana jambo kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Mawaziri Sekta ya Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji wa Afrika Mashariki wakishuhudia uzinduzi wa mfumo mpya wa Kielektroniki wa masuala ya forodha unaolenga kuongeza ufanisi na mapato kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud S. Kigahe wakifuatilia Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamin Mwesiga wakifuatilia Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Shariff Ali Shariff (kushoto) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.

TANZANIA KUJIIMARISHA KATIKA UKANDA WA IORA


Tanzania imeweka nia ya dhati ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) kupitia uanachama wake kwenye Jumuiya hiyo. 


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dodoma na kuhitimishwa leo tarehe Mei 31, 2024.


Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao huku ujumbe wa Tanzania ukishiriki kutokea jijini Dodoma, Balozi Mussa amesema zipo fursa nyingi katika Jumuiya hiyo ambazo Tanzania ikijipanga itanufaika nazo ikiwemo utunzaji wa mazingira na rasilimali za bahari, ulinzi na usalama baharini, namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uvuvi na utalii na kwamba wakati umefika sasa wa kuhakikisha wananchi wa Tanzania wananufaika kupitia jumuiya hiyo.


Aidha, kupitia mkutano huo Balozi Mussa amewasisitiza wajumbe wa mkutano waliotoka katika Taasisi, Wizara na Idara za Serikali kuendelea kuhakikisha maazimio mbalimbali yanayofikiwa kupitia Jumuiya hiyo yanatekelezwa kikamilifu ili kulinufaisha taifa kiuchumi na kijamii kwa ujumla.


“Ninawahimiza tuendelee kushirikiana ili taarifa za utekelezaji wa maazimio ya mkutano huu yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka na kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kuratibu shughuli za kikanda na kimataifa kwa tija na maslahi mapana ya Nchi’’ alisema Balozi Mussa.


Kadhalika wakati wa Mkutano huo, Tanzania iliwasilisha pendekezo la Mradi kuhusu Ushirikishwaji wa Jamii za Pwani katika Utunzaji wa Rasilimali za Bahari za ukanda wa Pwani ambalo linalenga pamoja na mambo mengine kuzijengea uwezo jamii za Pwani kutunza rasilimali za bahari na kuibua fursa za kiuchumi zitakazowanufaisha na kuinua kipato cha wananchi wa ukanda wa Pwani.


Akiwasilisha pendekezo hilo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt. Saida Fundi amesema Chuo hicho kilikuja na wazo la kuandaa mradi huo baada ya kuona upo umuhimu mkubwa wa kuziwezesha jamii zilizopo kwenye mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi kunufaika na rasilimali zitokanazo na bahari.


Amesema pendekezo la mradi huo ambalo litahusisha Warsha itakayofanyika hapa nchini mwezi Oktoba 2024 na kuzihusisha nchi wanachama na wadau mbalimbali lina malengo mahsusi ikiwemo kuimarisha mtandao wa watumiaji wa rasilimali za bahari katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na kuzijengea uwezo jamii za ukanda wa Pwani ili kunufaika na fursa mbalimbali.


========================

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akichangia katika Mkutano  wa 26 wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dodoma na kuhimishwa leo tarehe 31 Mei, 2024.

Balozi Mussa akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bi. Talha Waziri wakati wa mkutano wa 26 wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea jijini Dodoma na kuhitimishwa leo 31 Mei, 2024

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania.



Mkutano ukiendelea.



UBALOZI WA TANZANIA NAMIBIA WARATIBU JUKWAA LA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi akizungumza



 

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar Bi. Fatma Mabrouk Khamis akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

 

Balozi wa Tanzania nchini Nambia Mheshimiwa Ceasar Waitara akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

 

Washiriki wa jukwaa hilo wakifuatilia akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

Washiriki wa jukwaa hilo wakifuatilia akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

Washiriki wa jukwaa hilo wakifuatilia akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

Washiriki wa jukwaa hilo wakifuatilia akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

Washiriki wa jukwaa hilo wakifuatilia akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

Washiriki wa jukwaa hilo wakifuatilia akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024

meza kuu katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa jukwaa hilo





Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia umeratibu na kushiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Windhoek tarehe 30 Mei 2024.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi,ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Jukwaa hilo. 

Jukwaa hilo limejumuisha Sekta za Kilimo, Mifugo, Utalii, Biashara na Uwekezaji.





Thursday, May 30, 2024

MAKATIBU WAKUU SEKTA YA UVUVI NA UKUZAJI VIUMBE MAJI WA EAC WAKUTANA ARUSHA


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Arusha. 

Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika leo tarehe 30 Mei 2024 jijini Arusha.

Mkutano huo ulio ongozwa na Mwenyekiti wake Bi. Daisy Olyel Aciro ambaye pia ni Kamishna wa Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uganda, umepokea na kujadili taarifa ya kikao cha Wataalam kilichofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Mei 2024, ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Sekta hiyo utakaofanyika terehe 31 Mei 2024 jijini Arusha. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo Bi. Aciro ameeleza kuwa rasilimali za samaki na viumbe maji vimeendelea kuwa tegemeo kubwa la kiuchumi na chakula kwa wananchi wengi katika ukanda Afrika Mashariki, hivyo juhudi kubwa zinahitajika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kustawi. 

Aliongeza kusema Baraza hilo kupitia Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo kuweka mifumo ya usimazi endelevu wa rasilimali samaki na viumbe maji, mifumo ya uhifadhi na ufuatiliaji ili kuongeza tija zaidi. 

Vilevile Bi. Aciro ametoa wito kwa LVFO kuendelea kutumia fursa na nafasi iliyonayo kutafuta rasilimali fedha kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuweza kutekeleza miradi mipya inayoibuliwa kwa manufaa ya Jumuiya. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, amehimiza kuhusu umuhimu wa Jumuiya na wadau kuendelea kuunganisha nguvu na kushirikiana katika kuendeleza rasilimali samaki na viumbe maji kufuatia mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa Jumuiya. 

Katika Mkutano huo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka.

Katika hatua nyingine Uganda imekabidhi Uenyekiti wa Baraza hilo kwa Jamhuri ya Burundi ambayo itashika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja. 
Picha ya pamoja
Kamishna wa Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uganda Bi. Daisy Olyel Aciro akikabidhi Uenyekiti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mazingira, Kilimo na Mifugo Bw. Emmanuel Niyungeko wa Burundi kwenye Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Arusha

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka akifuatilia Mkutano

BALOZI MUSSA AONGOZA MKUTANO WA ISHIRINI NA SITA WA KAMATI YA MAKATIBU WAKUU WA IORA



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Ishirini na Sita (26) wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) unaofanyika tarehe 30 na 31 Mei, 2024 kwa njia ya mtandao huku ujumbe wa Tanzania ukiwa jijini Dodoma.

Pamoja na masuala mengine mkutano huo umejadili juu ya maboresho ya taasisi na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa taasisi hizo kikanda pamoja na taarifa ya fedha na utawala.

Akichangia katika mkutano huo, Balozi Mussa ameipongeza Sekretarieti ya IORA kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za kikanda na kimataifa kwa maslahi mapana ya ukanda huo wa IORA.

Aidha, ameziomba nchi wanachama kuendelea kushirikiana ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotishia usalama katika shughuli za majini na bahari kwa ujumla ikiwemo uharamia, usafirishaji haramu wa bidhaa na dawa za kulevya pamoja na uharibifu wa mazingira.

Kadhalika amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kushirikiana katika kutekeleza maeneo makuu manne ya kipaumbele katika IORA ambayo yatasaidia kukabiliana na changamoto ya utafutaji na uokozi pale ajali za majini zinapotokea. 

Maeneo hayo ni pamoja na Utafutaji na Uokoaji, Kukabiliana na Uhalifu wa Majini, Kubadilishana Taarifa na kuimarisha Ulinzi na Usalama katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Kadhalika, Balozi Mussa ametoa rai kwa Sekretarieti ya IORA kuendelea kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kutoka nchi wanachama pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa michango kwa wakati itakayowezesha utekelezaji wa majukumu ya IORA kwa tija kwa maslahi ya nchi wanachama.
======================================

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akiongoza Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Ishirini na Sita (26) wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) unaofanyika tarehe 30 na 31 Mei, 2024 kwa njia ya mtandao ambapo ujumbe wa Tanzania umeshiriki mkutano huo kutokea Mji wa Serikali-Mtumba, Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akifatilia mkutano huo.

Ujumbe wa Tanzania ukifatilia mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia mkutano.

Picha ya pamoja.

Mkutano ukiendelea.

Wednesday, May 29, 2024

MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA UVUVI NA UKUZAJI VIUMBE MAJI LA EAC WAFANYIKA ARUSHA


Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe maji katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Amos Madalla akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Wataalam unaoendelea jijini Arusha 

Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji katika Ziwa Victoria la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea jijini Arusha katika ngazi ya Wataalam ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Sekta hiyo wanaotarajiwa kukutana tarehe 31 Mei 2024. 

Mkutano huo wa siku tano terehe 27-31 Mei 2024, unalenga kufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo, maamuzi na makubaliano yaliyofikiwa kwenye musuala mbalimbali katika mikutano iliyopita ya Baraza hilo, ikiwemo masuala ya kiutawala, utekelezaji wa programu na miradi ya Jumuiya inayoratibiwa na kutekelezwa na Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ambayo inasimamiwa na Baraza hilo. 

Tathimini na majadiliano yakayofanyika katika mkutano huo pamoja na masuala mengine ni mahsusi katika kukuza sekta ya uvuvi na ustawi wa viumbe maji ikiwemo kuendeleza ufugaji samaki endelevu katika Bonde la Ziwa Victoria na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kupambana na magojwa yanayoathiri ustawi wa samaki na viumbe maji.

Mbali na hayo mkutano huo umepoke taarifa ya maandalizi ya mkutano wa kikanda wa wadau wa tasnia ya ukuzaji viumbemaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa Agosti, 2024 Jijini Mwanza. 

Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya EAC yenye Makao Makuu yake mjini Jinja, Uganda chini ya usimamizi wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji inajukumu la kuratibu na kusimamia uendelezaji wa rasilimali za uvuvi na ukuzaji viumbe maji katika Jumuiya. 

Miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Taasisi hiyo ni pamoja uendeshaji wa boti katika ziwa Victoria zinazosaidia shughuli za doria na utafiti wa masuala mbalimbali ya samaki na viumbemaji na mradi wa UE-EAC TRUE-FISH unaolenga kukuza ufugaji samaki endelevu katika bonde hilo.

Mradi mwingine ni wa ECOFISH ambao umejikita katika kuendeleza matumizi bora na usimamizi endelevu wa rasilimali samaki na viumbemaji kwa kuweka sera na mifumo inayohimiza ufanisi ikiwemo matumizi ya mbinu bora za uvuvi.

Mkutano huo Ngazi ya Wataalam umehudhuriwa na nchi ya Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda ambao ndio nchi wanachama za Taasisi hiyo.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo Ngazi ya Wataalam unajumuisha wataalam kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), na unaongozwa na Dkt. Nazael Amos Madalla ambaye ni Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mkutano ukiendelea

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Dorah Neema akichangia jambo kwenye Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Wataalam unaoendelea jijini Arusha
Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji na Masuala ya Jamii Bw. Aime Nkurunziza na mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji EAC akiongoza mkutano wa Baraza hilo katika ngazi ya Wataalamu uliofanyika jijini Arusha

TAARIFA KWA UMMA



 

Tuesday, May 28, 2024

BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeridhia na kupitisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Shillingi Bilioni 241 kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Jijini Dodoma leo Mei 28, 2024

 

Awali akiwasilisha bungeni hotuba yake, Waziri Mhe. January Makamba  amelieleza Bunge kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Wizara imejipanga kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa nguvu mpya  ili kuchochea Uwekezaji, Utalii, na Biashara pamoja na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa maendeleo ya Nchi.

 

Kadhalika amesema, Wizara itaendelea kukuza ushirikiano wa uwili wa kimkakati pamoja na kuhakikisha ushiriki wenye tija wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi mapana ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisasa na kujenga uhusiano wa karibu na nchi washirika.

 

Amesema kipaumbele kingine kwa Wizara ni kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuimarisha utawala bora na rasilimaliwatu pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, makazi ya watumishi na vitega uchumi katika Balozi za Tanzania na makao makuu.

 

Mhe. Makamba amelifahamisha Bunge kuwa, Wizara imekamilisha rasimu ya awali ya Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ambao umeainisha maeneo saba ya kipaumbele ambayo Wizara itayatilia mkazo katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ikiwemo Kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje; na Kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi. 

 

Maeneo mengine ni kuvutia watalii kuja Tanzania; Kutafuta misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje; Kutafuta fursa za ajira na masomo kwa Watanzania nje ya nchi; Kujenga taswira nzuri ya nchi yetu kimataifa na Kujenga uwezo wa kitaasisi wa Wizara, na Wizara na Taasisi nyingine kusimamia vizuri utekelezaji wa Mkakati wa Diplomasia ya Uchumi.

 

Kuhusu Diaspora, Mhe. Makamba amesema Wizara inatambua mchango wao katika maendeleo ya nchi na kwamba Serikali imejumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na Sera Mpya ya Ardhi ya 2024 na kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania ili kuwapa haki na upendeleo mahsusi.

 

Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, mwezi ujao, Serikali itawasilisha katika Bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria utakaokuwa na marekebisho madogo ya Sheria za Uhamiaji Sura ya 54 na Sheria ya Ardhi Sura  ya 113 nia ikiwa ni kukamilisha utoaji wa  Hadhi Maalum kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania.

 

Katika medani za kimataifa na kikanda Mhe. Makamba amelijulisha Bunge kuwa, sauti ya Tanzania imeendelea kusikika na kukubalika ambapo kuanzia mwezi Agosti, 2024 Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nafasi ambayo itaiwezesha Tanzania kuratibu na kuongoza majadiliano na maamuzi yote yanayohusu masuala ya siasa, ulinzi na usalama. 

 

Aidha, nafasi hii itaimarisha ushawishi wake katika ukanda wa SADC katika masuala haya hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa Waasisi wa SADC walioshiriki kwa hali na mali katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

 

Aidha, Mhe. Makamba ametumia jukwaa hilo kuwahimiza watanzania wenye sifa, wakiwemo Wabunge kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi za kikanda na kimataifa huku akimpongeza Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile (Mb.) kwa kujitokeza kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani – Kanda ya Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwasilisha Bungeni  jijini Dodoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Bajeti hiyo ya Wizara ambayo imeainisha vipaumbele mbalimbali imewasilishwa tarehe 28 Mei 2024
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza wakati Wizara ilipowasilisha Bungeni  jijini Dodoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akizungumza wakati Wizara ilipowasilisha Bungeni  jijini Dodoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025
Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi pamoja na  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharik, Balozi Said Shaib Mussa wakati wa uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara Bungeni jijini Dodoma
Viongozi wa Wizara wakifuatilia  Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwasilishwa. Kulia ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa anayeshughulikia Siasa, na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Abdallah Hamid 
Mkuu wa Itifaki, Balozi Yusuph Mndolwa (kushoto) akiwa Bungeni na wageni wengine waalikwa walioshiriki uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara Bungeni jijini Dodoma
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim akiwa Bungeni kwa ajili ya kushiriki uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Sehemu ya Menejimenti na Watumishi wa Wizara wakifuatilia uwasilishaji wa Bajeti
Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirikia waliopo nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara

Sehemu nyingine ya wageni waalikwa kutoka Balozi na Mashirika ya kimataifa hapa nchini
 Sehemu nyingine ya wageni waalikwa
   
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja