Wednesday, March 27, 2019

Waziri Mkuu atembelea Mji wa Serikali uliopo Mtumba, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza alipotembelea Jengo  la  Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki linalojengwa kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Mkuu alizipongeza baadhi ya Wizara kwa kukamilisha majengo ya Ofisi zao na kuzitaka Wizara  zote kuhakikisha zinakamilisha hatua za mwisho za ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kusawazisha maeneo na kuweka miundombinu muhimu kama maji na umeme kabla ya tarehe 15 Aprili 2015. Aidha, aliziagiza Taasisi kama TANESCO, TARULA na DUWASA kukamilisha kuweka huduma hizo muhimu  za umeme, maji na barabara kwenye mji huo. Tayari Wizara 20 zimekamilisha majengo ya ofisi zao kwa zaidi ya asilimia 98. Wengine katika picha ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega (kulia) na  Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kutaribu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma,  Bw. Meshack Bandawe (katikati). Ziara hiyo imefanyika tarehe 27 Machi 2019
Baadhi ya mafundi wanaoendea na ujenzi wa jengo la ofisi za Wizara Mtumba wakiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Deus Kaganda wakati wa ziara ya Waziri Mkuu kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba
Mhe. Waziri Mkuu akikagua moja ya chumba cha ofisi katika jengo la Wizara lililopo Mtumba 
Mhe. Waziri Mkuu akitoa maelekezo kwa Kaimu Katibu Mkuu, Balozi Mbega alipotembelea jengo la Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Mtumba jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine ameitaka Wizara kuharakisha usawazishaji wa eneo la nje (landscaping) la jengo hilo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Petrobas Katambi. Kushoto ni Meneja wa Mradi wa ujenzi wa ofisi za Wizara,  Mhandisi Elikyus Msigwa.
Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kutaribu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma,  Bw.  Bandawe (mwenye kipaza sauti) akitoa taarifa fupi kwa Mhe. Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa ofisi mbalimbali za Wizara
Mhe. Waziri Mkuu akitoa maelekezo kuhusu kukamilisha ujenzi wa ofisi za Wizara kwenye mji wa Serikali uliopo Mtumba. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama 
Sehemu ya Watumishi wa Umma walioshiriki ziara ya Waziri Mkuu kwenye Mji wa Serikali
Watumishi wakimsikiliza Mhe. Waziri Mkuu (hayupo pichani)
Mhe. Kassim Majaliwa akimpongeza Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kutaribu mpango wa Serikali kuhamia Dodoma,  Bw. Meshack Bandawe kwa kuratibu mpango huo kikamilifu.









Fursa za mafunzo nchini Thailand


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO KWA WATANZANIA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mrefu katika fani mbalimbali kutoka Serikali ya Thailand.

Kozi hizo zitakazotolewa kwenye Vyuo mbalimbali nchini humo, zitajikita katika fani za Filosofia ya Uchumi Timilifu; Mabadaliko ya Tabianchi, Usalama wa Chakula; Afya ya Jamii na Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Wizara inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi hizo za mafunzo zilizotangazwa na Serikali ya Thailand kwa mwaka 2019.

Mwisho wa kuomba nafasi hizo ni tarehe 31 Machi 2019. Kwa maelezo zaidi kuhusu kozi hizo na namna ya kuomba, tafadhali tembelea tovuti  ifuatayo: http://www.tica.thaigov.net


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
27 Machi 2019

Nchi za SADC zimeahidi kushikamana na Saharawi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Pretoria Afrika Kusini tarehe 25 na 26 Machi 2019. Mkutano huo ni maalum kwa ajili ya kuonesha mshikamano na nchi ya Saharawi, ambapo washiriki walielezea dhamira yao ya kusimama pamoja na Saharawi.

Dkt. Damas Ndumbaro akisalimiana na Rais wa Saharawi, Mhe. Brahim Ghali katika ukumbi wa mikutano jijini Pretoria.

Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC na wawakilishi wa Wakuu Nchi na Marafiki wa Sharawi walioshiriki mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja.

Tuesday, March 26, 2019

Balozi wa Tanzania nchini Sudan akutana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika

Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Mhe. Silima Kombo Haji,  amekutana na kufanya  mazungumzo rasmi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika (International University of Africa - IUA), Profesa Kamal Muhammed Ubeid, mjini Khartoum, Sudan. Katika mazungumzo baina yao, Prof. Ubeid alimhakikishia Balozi Silima kuwa, chuo hicho kitaendeleza ushirikiano  na Tanzania kwa kuendelea kutoa ufadhili wa elimu ya juu kwa wanafunzi wengi zaidi wa Kitanzania kadri hali itakavyoruhusu.
Takribani wanafunzi wa Kitanzania wapatao 517 wanaosoma katika vyuo mbalimbali nchini Sudan ambapo 490 kati yao wanasoma katika chuo hicho kilichopo Khartoum katika fani mbalimbali zikiwemo uhandisi wa mafuta na gesi, uchumi, udaktari na dawa na maabara, sheria, lugha na fani nyinginezo. 


Balozi Silima mara baada ya mazungumzo na Profesa Ubeid.

Mtanzania ateuliwa kuongoza Taasisi ya Kimataifa nchini China

Balozi Ali Mchumo

=============================================================
Balozi Mstaafu, Mhe. Ali Mchumo (Pichani) kutoka Tanzania ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya International Network for Bamboo and Rattan (INBAR) yenye makao yake makuu mjini Beijing, China. Taarifa ya uteuzi wake imetangazwa tarehe 25 Machi 2019 katika tovuti ya taasisi ya INBAR. Taasisi ya INBAR ilianzishwa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kukuza matumizi ya mianzi (Bamboo) kama njia endelevu ya utunzaji wa mazingira . Taasisi hiyo inaundwa na nchi wanachama 45 na ina ofisi zake za kanda nchini  Ethiopia, Ghana na Equador. Tanzania ni mojawapo ya nchi mwanachama mwanzilishi wa taasisi hiyo na imenufaika na uwepo wa taasisi hiyo kupitia miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na INBAR pamoja na mafunzo kwa wataalam wa zao la mianzi. 


Mawaziri wa Afrika wakutana Morocco

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Mhe. Nasser Bourita,  baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa mkutano.

Dkt. Mnyepe amemwakilisha Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika kuhusu maamuzi ya Umoja wa Afrika (AU) kuunga mkono jitihada za usuluhishi wa mgogoro wa eneo la Sahara Magharibi kati ya Morocco na Saharawi uliofanyika jijini Marrakech, Morocco tarehe 25 Machi, 2019.
Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe akifuatilia mazungumzo na michango ya wajumbe kutoka nchi mbalimbali wakati wa mkutano huo.
Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe wa tatu kutoka kushoto, mstari wa nyuma, akiwa katika picha ya pamoja ya Mawaziri na Wawakilishi wa Mawaziri walioshiriki mkutano huo.


Monday, March 25, 2019

Nafasi za ajira katika Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NAFASI ZA AJIRA KATIKA JUMUIYA YA NCHI ZA UKANDA WA MAZIWA MAKUU (ICGLR)

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahimiza Watanzania wenye sifa kuomba nafasi za ajira katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) yenye makao makuu Bujumbura, Burundi; Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia (Regional Training Facility on SGBV) kilichopo Kampala, Uganda na Kituo cha Demokrasia na Utawala Bora cha Levy Mwanawasa (Levy Mwanawsa Regional Centre for Democracy and Good Governance) kilichopo Lusaka, Zambia. Ajira hizo ni kama ifuatavyo:-

SEKRETARIETI YA MAZIWA MAKUU

  1. Mkurugenzi wa Utawala na Fedha (Director, Administration and Finance);
  2. Mkurugenzi wa Nyaraka na Mikutano (Director, Documentation and Conferences);
  3. Mkurugenzi wa Mawasiliano (Director, Communications);
  4. Mshauri wa Masuala ya Sheria (Legal Adviser).

KITUO CHA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA CHA LEVY MWANAWASA

  1. Mkurugenzi wa Kanda (Regional Director);
  2. Mkuu wa Utafiti (Head, Research);
  3. Mkuu wa Jukwaa na Uchunguzi (Head, Fora and Observatories).

KITUO CHA KIKANDA CHA KUPAMBANA NA UKATILI NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA
  1. Mratibu wa Mafunzo (Training Coordinator) na
  2. Mratibu wa masuala ya TEHAMA, Utafiti na Elimu (IT, Research and Knowledge Coordinator).
Waombaji wa nafasi hizo wanapaswa kuwasilisha barua za maombi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kabla ya tarehe 4 Aprili 2019 ili yaweze kuwasilishwa kwenye Sekretarieti ya ICGLR kwa wakati.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
25 Machi 2019


Sunday, March 24, 2019

Prof. Kabudi afungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi amelitaka Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kubuni mikakati na mbinu mpya za utekelezaji na namna ya kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza na kuhimiza Wafanyakazi kujituma na kuondokana na uzembe katika utumishi wa Umma.

Profesa Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Dodoma wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Dkt John Pombe Magufuli kuiongoza Wizara hiyo na kuongeza kuwa, ni wajibu wa Baraza hilo kubuni mbinu na mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza  pamoja na kuhimiza ushirikishwaji wa watumishi badala ya kusubiri mtu mwingine kuzitatua changamoto hizo.

“Sote tunatambua kuwa ushirikishwaji wa watumishi kwenye mipango ya Taasisi na Wizara ni jukumu la kisheria na kwa miaka yote Serikali imekuwa ikisisitiza taasisi kujenga na kutekeleza utaratibu wa kuwashirikisha watumishi kwa kuwa kunaongeza umiliki wa mipango iliyowekwa” 

Aidha, Waziri Profesa Palamagamba John Kabudi amelisisitiza Baraza hilo kupitia upya vipaumbele vilivyowekwa na jinsi gani ya kuvitekeleza, akitolea mfano namna ya kutekeleza kipaumbele cha diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje, watalii na kutafuta fursa mbalimbali ikiwemo masoko ya bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.

Pia kwa mwaka huu wa 2019 amelitaka Baraza hilo la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujiandaa mapema na kuwashirikisha wote wanaohusika katika na mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika  (SADC) kwa kuwa mwezi Agosti  2019 Tanzania itachukua nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

“ Hili ni tukio kubwa ambalo ni lazima tujipange vizuri, mara baada ya kazi ya kuandaa bajeti ya wizara ya 2019/2020 lazima tuanze kazi ya kujiandaa kwa mkutano wa SADC mara moja”

Profesa Palamagamba John Kabudi amelitaka pia Baraza la wafanyakazi la wizara hiyo kutathmini kwa kina shughuli zitakazotekelezwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha na kuyapitia kwa umakini maeneo yote yaliyopewa kipaumbele na serikali na kubaini mipango na mikakati mizuri katika kutekeleza vipaumbele hivyo.

Imetolewa na: 
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, Tarehe 24 Machi 2019

=======================================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi rasmi wa  Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dodoma, tarehe 24 Machi 2019. Prof. Kabudi aliwataka wajumbe wa Baraza hilo ambao ni wawakilishi wa watumishi wote wa Wizara kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa kuzingatia vipaumbele vya Wizara ikiwemo Diplomasia ya Uchumi ili kukuza uwekezaji na biashara pamoja na kuvutia utalii  kwa maslahi mapana ya Taifa
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakimsikiliza Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani)


Sehemu nyingine ya wajumbe wa Baraza wakati wa mkutano wao wa mwaka

Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ambao ni wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wakifuatilia mkutano

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ukiendelea na wajumbe wakifuatilia


Wajumbe wa Baraza
Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja  na wajumbe wa meza kuu mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, kushoto kwake ni Katibu wa  Baraza, Bw. Magabilo Murobi. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bibi Savera Kazaura na kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara , Bw. Hassan Mnondwa

Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa TUGHE wa Wizara

Picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza

Rais Nyusi aishukuru Tanzania kwa misaada ya dawa na chakula



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi na Wananchi wake  wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Wananchi wa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kutoa misaada ya Madawa, Magodoro na vyakula kwa watu wa Msumbiji walioathirika na kimbunga.

Kimbunga kilichopita katikati ya Jamhuri ya Msumbiji  kilicho anza tarehe 14 Machi 2019,  kimesababisha madhara makubwa katika mji wa Beira ambao ni wa tatu kwa ukubwa na wa pili kibiashara baada ya Maputo.

Upepo uliambatana na mvua uling'oa miti, mapaa ya nyumba za mabati na vigae na kuvunja madirisha ya vioo bila huruma katika mji huo.

Kufuatia janga hilo ambalo limezikumba pia nchi za Malawi na Zimbabwe, Rais Magufuli alitangaza kutoa msaada wa haraka ambapo ndege kubwa za JWTZ zilipeleka misaada hiyo kama inavyoonekana katika picha. 

Mjini wa Beira na wilaya  za jirani ziko kwenye uwanda wa tambarale. Mji huo pia una mito miwili mikubwa inayoingia katika bahari ya Hindi na hiyo ndiyo sababu ya mara kwa mara unakabiliwa na mafuriko.

Tanzania inaomba Mungu mvua zipungue kwa majirani hao ili waweze kuidhibiti hali hii ya mafuriko inayoendelea sasa baada ya Kimbunga kupita.

Mji wa Beira umeharibika vibaya ambapo asilimia 97 ya majengo, miundombinu, na mali za wananchi zimeathiriwa na kimbunga hicho.

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Rajab Luhwavi ambaye alipokea shukrani hizo kwa niaba ya Serikali ameihakikishia Msumbiji kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo  kwa hali na mali. 

Aidha, Mhe. Balozi ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wadau wengine kwa kufanikisha msaada huo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, 
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Dodoma, Tarehe 24 Machi 2019

==============================================================================

....Picha zinazoonesha madhara yaliyotokana na Kimbunga...









Saturday, March 23, 2019

Waziri wa Mambo ya Nje azungumza na Watumishi wa Wizara

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mahsariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe mara baada ya kuwasili kwenye eneo la Ukumbi wa Mikutano la Informatics lililopo Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya kukutana kwa mara ya kwanza na Watumishi wa Wizara tarehe 23 Machi 2019
Mhe. Prof. Kabudi akizungumza na Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) alipokutana nao kwa mara ya kwanza  baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nafasi hiyo tarehe 3 Machi 2019. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Prof. Kabudi aliwataka Watumishi wa Wizara kubadilika na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu miongozo na maelekezo mbalimbali pamoja na kuwa wazalendo na kufanya kazi zao kwa kushirikiana na  kwa weledi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.


Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakimsikiliza Mhe. Prof. Kabudi ambaye haonekani pichani alipozungumza nao


Sehemu nyingine ya Watumishi wakifurahia jambo wakati wakimsikiliza Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani)


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye mkutano wao na Mhe. Waziri


Mkutano ukiendelea huku Watumishi wa Wizara wakifuatilia

Sehemu nyingine ya Watumishi


Mhe. Prof. Kabudi alitumia fursa ya mkutano wake na Watumishi wa Wizara kugawa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 kwa Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara na kuwaagiza kuitekeleza kwani ni miongoni mwa miongozo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Pichani Mhe. Waziri akimkabidhi Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Mohammed Hamza Ilani hiyo
Mhe. Waziri akimkabidhi Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama Ilani ya Chama cha Mapinduzi
Mhe. Prof. Kabudi akimkabidhi Ilani ya Chama cha Mapinduzi Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. Joachim Otaru
Mhe. Prof. Kabudi akimkabidhi Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Wilbroad Kayombo
Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Watumishi na kuahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Waziri
Mhe. Waziri (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa meza kuu. Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizzi wa Rasilimali Watu, Bibi Savera Kazaura na kulia ni Bw. Hassan Mnondwa, Mwenyekiti wa TUGHE Wizarani .

Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo