Monday, July 28, 2014

Watanzania waishio Comoro waandaa futari kwa kushirikiana na Ubalozi

Baadhi ya Watanzania wanaoishi Visiwani Comoro wakiwa katika picha ya pamoja na Bw. Ali Mwadini (wa pili kutoka kushoto), Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania, Comoro ambaye alimwakilisha Mhe. Balozi Chabaka Kilumanga wakati wa  futari ya pamoja iliyoandaliwa na Watanzania hao kwa kushirikiana na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Moroni. 
Jumuiya ya Watanzania waishio Comoro wakipata futari ya pamoja.


 WATANZANIA WANAOISHI VISIWANI COMORO WAANDAA FUTARI YA PAMOJA KWA KUSHIRIKIANA NA UBALOZI

Jamii ya Watanzania wanaoishi Visiwani Comoro wameandaa futari ya pamoja, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Moroni. Lengo la futari hiyo lilikuwa ni kuwakutanisha Watanzania wanaoishi Comoro, hususan katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili wajumuike pamoja. 

Wakizunguza wakati wa hafla hiyo, Watanzania hao walielezea kufurahishwa na kufarijika kwao kutokana na kitendo cha Serikali ya Tanzania kufungua Ubalozi nchini Comoro. Walieleza pia utayari wao wa kushirikiana na Ubalozi ili kuhamasisha maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

Akizungumza katika halfa hiyo kwa niaba ya Mhe. Balozi Chabaka Kilumanga, Bw. Ali Mwadini wa Ubalozi wa Tanzania Moroni, aliwashukuru Watanzania hao kwa kupata wazo zuri la kuandaa futari na kuushirikisha Ubalozi.

Aidha, aliwasihi waendelee na umoja huo kwa kusaidiana na kuwa raia wema kwa kutii sheria za nchi wanapoishi. Aliwakumbusha pia kufika Ubalozini na kujisajili kwa wale ambao bado walikuwa hawajafanya hivyo. Vile vile, aliwahimiza kushiriki katika Kongamano la Watanzania Wanaoishi Ughaibuni linalotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 na 15 Agosti 2014.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.