Tuesday, May 28, 2019

Makamu wa Rais ashiriki sherehe za uapisho za Rais wa Comoro



Dodoma, 28 Mei 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Makamu wa Rais ashiriki sherehe za uapisho za Rais wa Comoro

Kufuatia Mwaliko kutoka Serikali ya Comoro, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliongoza ujumbe wa Tanzania katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assouman zilizofanyika Moroni, terehe 26 Mei 2019.

Sherehe hizo zinafuatia ushindi alioupata Mhe. Azali katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 24 Machi  2019.

Mara baada ya Sherehe za Uapisho, Mhe. Makamu wa Rais alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mhe. Azali ambapo katika mazungumzo hayo, Mhe. Makamu wa Rais aliishukuru Serikali na Wananchi wa Comoro kwa mwaliko na mapokezi mazuri.

Aidha, aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumhakikishia kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wake, Mhe. Azali alielezea furaha yake kwa ujio wa Mhe. Makamu wa Rais na kueleza kwamba hiyo ni ishara ya udugu na uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Comoro.

Aidha, Mhe. Rais alieleza kwamba kutokana na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Serikali ya Tanzania, ipo haja kwa Tanzania kuendelea kuisadia Comoro katika sekta mbalimbali.

Mwisho, aliishukuru Tanzania kwa salamu za pole kufuatia nchi hiyo kukumbwa na kimbunga Kenneth tarehe 26 Aprili 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
                          
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Comoro,Mhe. Azali Assouman jijini Moroni, Comoro. Mhe. Makamu wa Rais alikwenda nchini humo kushiriki sherehe za uapisho za Rais huyo zilizofanyika tarehe 26 Mei 2019.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.