Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini, Bw. Japhet Justine (kushoto).
Mazungumzo kati yao yalijikita katika kuangalia namna ya kushirikana ambapo Bw. Justine amemweleza Prof. Palamagamba John Kabudi kuwa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki hususan katika kuangalia fursa za masoko nje ya nchi kupitia Balozi za Tanzania. Masoko hayo yatakuza biashara ya bidhaa ghafi za Tanzania nje pamoja na kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa nchini.
Kwa upande wake, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi alimhakikishia ushirikiano Mkurugenzi huyo ili kuhakikisha mazao kutoka Tanzania yanapata soko nje ya nchi. Pia alimweleza kuwa, Wizara itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji kutoka nje kwa ajili ya kuja nchini kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwani kuimarika kwa sekta hiyo kutatoa fursa ya kuanzishwa kwa viwanda vya usindikaji mazao ndani ya nchi na kuzalisha ajira kwa vijana.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zilizopo jijini Dar es Salaam tarehe 03 Mei 2019 |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.