|
Dodoma, 20 Mei 2019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Uholanzi zazindua Mradi wa Kukua na Kuku
Ubalozi
wa Tanzania nchini Uholanzi kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Uholanzi na Africa (Netherlands – Africa
Business Council - NABC) hivi
karibuni waliongoza ujumbe wa Makampuni 7 kutoka Uholanzi yaliyobobea katika Sekta
ya Ufugaji wa Kuku kwenda Mkoani Kilimanjaro kuzindua Mradi maalum wa ufugaji
utakaoendeshwa na Makampuni hayo nchini Tanzania maarufu kama “Kukua Na Kuku (Growing with Chicken)
Impact Cluster”.
Mradi
wa “Kukua Na Kuku” ni matokeo ya makubaliano ya kuanzisha
ubia kati ya Tanzania na Uholanzi yanayolenga kuboresha Sekta ya Ufugaji Kuku nchini
Tanzania na kuifanya kuwa endelevu kwa kutumia teknolojia ya kisasa kutoka
Uholanzi. Makampuni hayo yatatoa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo wafugaji
wazawa kwa kuboresha usimamizi wa kilimo cha ufugaji, afya ya wanyama,
upatikanaji wa chakula (lishe) bora kwa ajili ya mifugo, vifaa muhimu vya
kufugia, na hata utafutaji masoko.
Uzinduzi
huo ulifanyika kwenye Chuo cha Kilimo na Ufugaji wa Mifugo Kilacha, Mkoani
Kilimanjaro kwa kusaini Makubaliano ya Ushirikiano, na ukawa ndio mwanzo wa
ushirikiano wa miaka 3 kati ya makampuni hayo 7, Serikali ya Uholanzi na wadau
wazawa wa Tanzania. Chuo cha Kilimo na Ufugaji wa Mifugo cha Kilacha kinasimamiwa
na Kituo cha Uzalishaji na Mafunzo kinamilikiwa na Kanisa Katoliki Mkoani humo.
Mgeni
rasmi wakati wa sherehe za uzinduzi huo alikuwa Mhe. Anna Mgwira, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Balozi wa Tanzania
nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju,
Kaimu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi
Lianne Houben, na Mkurugenzi wa Biashara na Kilimo wa NABC, Bw. Mackenzie Masaki.
Makampuni
hayo kutoka Uholanzi ni pamoja na: Aeres
University of Applied Sciences; Ebit+/I Grow Chicken; GD Animal Health; Impex;
Hendrix Genetics; Koudijs de Heus; na Vencomatic Group.
|
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki
|
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Dkt. Anna Mngwira ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kukua na Kuku akitoa neno katika sherehe za uzinduzi wa Mradi huo. Kushoto kwake ni Padri Paul
Huria, Msaidizi wa Meneja Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji na Mafunzo, Kilacha
akimsikiliza kwa makini. |
|
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene
Kasyanju (pichani juu) na Kaimu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Bibi Lianne
Houben (pichani chini) wakitoa hotuba fupi wakati wa Uzinduzi wa
Mradi wa Kukua Na Kuku huko Kilacha, Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
|
|
Kutoka kulia ni Padri Landelimi
Makiluli, Meneja Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji na Mafunzo, Kilacha; Padri
(Monsignor) Paul Huria, Msaidizi wa Meneja Mkuu wa Kituo; Mhe. Dkt. Anna
Mgwira, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro; Bibi Lianne Houben, Kaimu Balozi wa
Uholanzi nchini Tanzania; na mwishoni kushoto ni Mhe. Irene Kasyanju, Balozi wa
Tanzania nchini Uholanzi wakijiandaa na uzinduzi wa Mradi wa Kukua na Kuku
|
|
Wawakilishi wa Taasisi zenye ubia katika Mradi wa Kukua na Kuku wakiongozwa na Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro wakiweka saini Makubaliano ya Ushirikiano tayari kuanza
utekelezaji wa Mradi huo huko Kilacha, Mkoani Kilimanjaro |
|
Picha ya pamoja baada ya kusainiwa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Uholanzi, Makampuni tajwa 7 yakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara na Kilimo kutoka NABC, Bw. Mackenzie Masaki (wa pili kutoka kushoto). Wa kwanza kushoto ni Bibi Theo Mutabingwa, Afisa Kilimo katika Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania.
|
Balozi Irene Kasyanju akibadilishana mawazo na wawakilishi wa Kampuni ya Hendrix Genetics, Bw. Peter Arts (kushoto); na Ebit+/I Grow Chicken, Bw. Eric Mooiweer (kulia) mara baada ya uzinduzi wa Mradi wa Kukua na Kuku utakaoendeshwa na Makampuni tajwa 7 kutoka Uholanzi
|
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.