Tuesday, May 7, 2019

Balozi wa Tanzania nchini Oman auelezea Muungano kama kielelezo cha Umoja barani Afrika

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Intercontinental jijini Muscat hivi karibuni. Pamoja Mhe. Balozi Kilima aliuelezea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa ni kielelezo muhimu kinachoonesha kwa vitendo nia thabiti ya Serikali ya Tanzania kuimarisha umoja na mshikamano miungoni mwa nchi za Afrika na kwamba ndio iliyokuwa azma  ya waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati, Rais Abeid  Amani Karume.

Mhe. Balozi  Kilima alieleza kuwa katika miaka 55 ya Muungano, Tanzania imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta za uchumi, elimu, biashara, uwekezaji na huduma za jamii kama vile afya na upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Alieleza pia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi  wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inaendeleza  jitihada  za kujenga mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji, jitihasa hizi zinahusisha kujenga misingi ya utawala bora, kupambana na rushwa na ufisadi na kujenga utumishi wa umma wenye maadili na viwango.  Balozi Kilima alitumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyabiashara wenye nia kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji kwa kuwekeza na kuanza biashara Tanzania. Wakati wa hafla hiyo Ubalozi uligawa vipeperushi mbalimbali kwa wageni waalikwa kuhusu utalii, uwekezaji pamoja na taarifa mbalimbali kuhusu Tanzania.


Wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe. Balozi Kilima ambaye haonekani pichani

Balozi Kilima (mwenye shati la kitenge) akiwaongoza wageni waalikwa kuimba wimbo wa Taifa wa Tanzania wakati wa Maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Balozi Kilima kwa pamoja na Mhe. Dkt. Ahmed Mohamed Salim Al Futaisi, Waziri wa  Mawasiliano na Uchukuzi wa Oman wakikata keki kama ishara ya kuzitakia mema Tanzania na Oman.

Balozi Kilima kwa pamoja na Mke wake Mama Fatma Abdallah wakimpokea mgeni rasmi, Mhe. Dkt. Ahmed Mohamed Salim Al Futaisi, Waziri wa  Mawasiliano na Uchukuzi wa Oman kabla maadhimisho kuanza

Mhe. Balozi Kilima akimwongoza  Meja Jenerali Salim bin Musallam bin Ali Qatan, Commandant wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College) cha Oman kuchukua chakula kilichoandaliwa mahsusi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.