Sunday, May 12, 2019

Waziri Mkuu awapokea watalii kutoka China

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI















Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amepokea kundi la kwanza la Watalii 336 kati ya watalii 10,000 kutoka China watakaotembelea nchini mwaka huu 2019.



Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili ya watalii hao ambao watafanya ziara ya kitalii kwa siku nne, Mhe. Majaliwa amesema kuwa ziara hiyo ni fursa kubwa kwa Tanzania kutangaza vivutio vya utalii kwa raia hao wa China na duniani kwa ujumla.

Mhe. Waziri Mkuu ameeleza kuwa, Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikipokea watalii, hata hivyo kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na kuboreshwa kwa mbinu za kuvutia watalii kutoka nje pamoja na kuweka msisitizo kwenye diplomasia ya uchumi kupitia Balozi zetu nje, Tanzania imeanza kupokea watalii makundi kwa makundi kutoka duniani kote.

Akielezea vivutio vya utalii vilivyopo nchini, Mhe. Waziri Mkuu amesema kwamba Tanzania ni nchi pekee yenye vivutio vya utalii vya asili kama vile hifadhi za wanyama, fukwe za bahari, milima mirefu, vyakula na mavazi ya asili ambavyo havipatikani kokote duniani isipokuwa Tanzania.

“Wageni wetu mmefika kwenye nchi salama kabisa, nawaomba mwendelee kufurahia vivutio vilivyopo. Ni matumaini yangukuwa, mtapfika Ngorongoro kwenye bonde lililosheheni wanyama badala ya maji kama yalivyo mabonde mengi. Eneo hili ni maarufu kama Ngorongoro Crater huwezi kulipata kokote duniani isipokuwa Tanzania pekee," alisema Mhe. Majaliwa.

Kadhalika Mhe. Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuuelezea Mlima Kilimanjaro kwa Watalii hao ambao ni Mlima mrefu barani Afrika na kuwaeleza kuwa hakuna anayeweza kuuona, kuuzunguuka wala kuupanda Mlima huo bila kuja Tanzania. “ Mkiwa hapa kwetu mtauona mlima mrefu kuliko yote Afrika ambao unapatikana Tanzania tu, Mlima Kilimanjaro. Ukitaka kuuzunguka mlima huu lazima uje Tanzania, ukitaka kuuona vizuri njoo Tanzania na ukitaka kuupanda tembelea Tanzania” alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu.

Aidha, Mhe. Waziri Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wote waliofanikisha ziara ya watalii hao akiwemo Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na kuwaomba Watalii hao kuwa mabalozi wazuri wa vivutio vya utalii vya Tanzania wanaporudi nchini kwao.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, alisema kuwa ziara ya watalii hao imedhihirisha namna Wizara kupitia Balozi zake na kwa kushirikiana na wadau wengine inavyotekeleza Diplomasia ya Uchumi ambayo imejikita katika kuvutia watalii na wawekezaji pamoja na kukuza biashara nchini.

Vilevile aliongeza kuwa, Serikali kwa sasa ina mpango mkubwa wa kutangaza utalii kwenye nchi mbalimbali kupitia mpango uliopewa jina la “New Horizon, Tour Africa” na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hii ya watalii wanaoendelea kuja nchini makundi kwa makundi ili wanufaike na uwepo wao.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasilia na Utalii, Mhe. Hamis Kigwangala alieleza kwamba, sekta ya utalii nchini imepiga hatua kubwa katika kipindi kifupi cha Serikali ya Awamu ya Tano na kwamba ni ndoto yake kuendelea kukuza sekta hiyo muhimu kwa uchumi wan chi. “Hii ni hatua kubwa kwenye sekta ya utalii nchini kuona makundi ya watalii yakija nchini mfululizo. Tumeamua kuwekeza katika nchi tano za kipaumbele cha pili kwa maana ya China kama mdau wetu namba moja, Israel, Oman na nchi zingine za mashariki ya kati, Australia na Urusi, alifafanua Mhe. Kigwangala.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China, Bw. Liehui He ambayo ndiye mratibu mkuu wa ziara za watalii hao, alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi makubwa na kwamba kampuni yake itaendelea kushirikiana na Serikali kwenye sekta ya utalii kama walivyoahidi kwenye makubaliano waliyosaini kati yao na TTB.

Wakiwa nchini, Watalii hao watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Wanyama ya Manyara, Ngorongoro, Serengeti, Olduvai Gorge pamoja na kutembelea Maboma ya wamaasai. Aidha, sehemu ya watalii hao ambao ni wawekezaji 57 kutoka kampuni 26 za China wanatarajiwa kushiriki Kongamano la Uwekezaji litakalofanyika jijini Arusha tarehe 13 Mei 2019.

Kutokana na jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini China za kutangaza utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ilisaini makubaliano na Kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China kwa ajili ya kusafirisha watalii 10,000 kutoka China watakaotembelea nchini kwa kutumia ndege maalum ikiwemo Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL). Makubaliano hayo pia ni kwa kampuni hiyo kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kwenye soko la China.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Arusha
12 Mei 2019

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza kwenye hafla maalum ya kuwapokea watalii 336 kati ya watalii 10,000 watakaotembelea nchini mwaka huu wa 2019. Hafla hiyo ilifanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na Mawaziri na Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini na Sekta binafsi.Watalii hao watafanya ziara kwenye vivutio mbalimbali vya utalii kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 13 hadi 16 Mei, 2019
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati wa hafla ya kuwakaribisha nchini watalii kutoka China.
Sehemu ya Watalii hao wakifuatilia hotuba zilizotolewa
Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki akiwa kwenye hafla ya kuwakaribisha watalii kutoka China ambao ameongozana nao.


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Caesar Waitara pamoja na mdau kutoka Bodi ya Utalii wakiwa kwenye hafla hiyo. 






Mhe. Waziri Mkuu akisalimiana na Mkuu wa Msafara wa watalii kutoka China mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro katikati ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Touch Road na mratibu wa ziara ya watalii hao.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) akisalimiana na mmoja wa watalii kutoka China.
Mhe. Waziri Mkuu akimsikiliza Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi alipokuwa akimweleza jambo kabla ya kuwasili kwa watalii kutoka China. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mgwira.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.