Saturday, August 31, 2024

RAIS DKT. MWINYI AWASILI INDONESIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasili jijini Bali,Indonesia leo tarehe 31 Agosti 2024 kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Pili la Indonesia na Afrika unaofanyika jijini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.

Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Mwinyi ambaye ameambatana na mwenza wake Mhe. Mama Mariam Mwinyi pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali alipokelewa na Naibu Waziri  wa Biashara wa Indonesia Mhe, Jerry Sambuaga. 

Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika ambao utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Bandung Spirit for Africa's Agenda 2063,” unalenga kuangazia kanuni za pamoja ambazo zimeweka msingi imara wa kuwa na uhusiano jumuishi, usawa na endelevu kati ya Indonesia na Afrika. 

Maeneo muhimu ya ushirikiano yanayotarajiwa kujadiliwa katika Jukwaa hilo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo na usalama wa chakula, nishati, uchumi wa buluu, madini, afya na ushirikiano wa maendeleo.

Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mhe. Rais Mwinyi atafanya ziara ya kikazi nchini Indonesia kuanzia tarehe 04 hadi 06 Septemba 2024. 

 


Sunday, August 25, 2024

Ujumbe wa Tanzania washiriki Mazoezi ya ‘Walk the Talk’


Brazzaville, Congo 

25 Agosti 2024

 

Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, wameungana na mgombea wa Tanzania kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Faustine Ndugulile (MB), katika mazoezi ya ‘Walk the Talk’.

 

Tukio hili la mazoezi ya ‘Walk the Talk’ lililofanyika Jijini Brazzaville, na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali waliowasili; lina lenga kuimarisha afya pamoja na kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza. 

 

Wakiwa kwenye mazoezi hayo, Waziri Mhagama na Waziri Kombo walipata fursa ya kusalimiana na mawaziri wenzao  na kuwaomba kuunga mkono mgombea wa Tanzania Dkt. Ndugulile katika juhudi zake za kuwania nafasi hii muhimu, huku wakisisitiza umuhimu wa kuwa na maisha yenye afya na kufuata mifumo bora ya kuzuia magonjwa.

 

Wakati wa tukio hilo, viongozi hawa wa Tanzania walikuwa sehemu ya ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioandamana na Dkt. Ndugulile kwa ajili ya kumnadi na kumpigia kura katika uchaguzi wa Mkutano wa 74 wa WHO Kanda ya Afrika.

 

Ushiriki wa Tanzania kwenye mazoezi haya ni sehemu ya maandalizi na mkakati wa kuhakikisha kuwa Dkt. Ndugulile anapata uungwaji mkono kutoka kwenye nchi wanachama wa WHO, na pia kuonesha dhamira ya Tanzania katika kukuza afya ya jamii. 

 

Pamoja na Mawaziri hawa wawili, ujumbe wa Tanzania kwenye mazoezi hayo umejumuisha pia wabunge mahiri kwenye masuala ya chaguzi za kimataifa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni  Mwenyekiti wa Bunge Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Elibariki Emmanuel Kingu. Wengine ni Mhe. Neema Kichiki Lugangira, Mhe. Shamsia Azizi Mtamba, na Mhe. George Ranwell Mwenisongole.

 

Kauli Mbiu ya Dkt. Ndugulile kwenye kinyang’anyiro hiki ni “Pamoja, Tujenge Afya Bora Barani Afrika” yaani “Building a Healthier Africa Together” 



 


 

WAZIRI CHUMI ASHIRIKI MKUTANO MAALUM WA AFYA WA TICAD 9








Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi tarehe 24 Agosti 2024, ameshiriki mkutano Maalum wa afya pembezoni ya Mkutano wa Tisa wa TICAD ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo. Mkutano huo uliongozwa na mada ya Ushirikiano Mpya kwa Usawa wa Afya Barani Afrika: Kuharakisha Ufikaji wa Huduma za Afya kwa Wote kwa Ubunifu kuelekea 2030.” Mkutano huo uliandaliwa na Muungano wa Chanjo (GAVI) na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ulilenga kuangazia umuhimu wa ushirikiano na ubunifu katika kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote barani Afrika. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bunge la Japani Mhe. Fukazawa Yoichi. Kwa kushiriki katika mkutano huo Tanzania ilipata fursa ya kujionea namna bora ya kutoa huduma za afya kwa watu wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizo bila ya kikwazo cha kukosa hela.

WAZIRI CHUMI ASHIRIKI UZINDUZI WA LOGO YA SUMMIT YA TICAD9 2025 JAPAN

 





Tarehe 24 Agosti,2024, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa logo ya Mkutano wa Tisa wa TICAD wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika 2025 nchini Japan. 

Uzinduzi wa Logo hiyo ya Summit ya #TICAD9 umefanyika jijini Tokyo wakati wa Mkutano wa TICAD ngazi ya Mawaziri, ambao unafanya maandalizi ya Summit hiyo inayotarajiwa kufanyika tarehe 20 - 22 Agosti 2025, jijini Yokohama, Japan. Uzinduzi huo ullihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za nchini
Japan ambao pia, walionesha huduma mbalimbali wanazozitoa katika nchi za Afrika. 

Katika tukio hilo, Mhe. Naibu Waziri Chumi akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda walipata nafasi ya kusalimiana na wadau wa taasisi na kampuni za Japan zenye ubia na Tanzania.

Saturday, August 24, 2024

TANZANIA YAZISIHI NCHI ZA AFRIKA KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOZIKABILI NCHI ZAO

 

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akichangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.

 


Waziri Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Yoko Kamikawa akifungua  Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifatilia ufunguzi wa  Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo


 

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 wakifuatilia mkutano huo

  

 

Washiriki wa Mkutano wa Tisa wa TICAD 2024 katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Mkutano huo

  

 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo na changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo. Pia imemewahimiza wadau wote wa maendeleo kutoka nchini Japan kuendelea  kufanya biashara na kuwekeza zaidi barani Afrika ili kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya binadamu katika bara hilo ikiwa ni katika juhudi za kuendeleza amani na utulivu kikanda na kimataifa.

 

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi alipochangia mada ya Amani na Utulivu: kuhakikisha Heshima ya Binadamu na Usalama wa Binadamu kwenye sehemu ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ngazi ya Mawaziri unaofanyika nchini Japan tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

Ameipongeza Japan kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki katika jitihada za kimataifa na kuwaomba washirika wengine wa kimataifa kuiga mfano huo na kuongeza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa ushiriki sawa na ujumuishaji wa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana katika kuhakikisha amani na usalama vinatamalaki.

 

Amesema kutokana na umuhimu huo Tanzania iko katika hatua za mwisho za kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji (NAP) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2000. 

 

Amesema siku zote Tanzania imekuwa na mchango muhimu katika  harakati za upatanishi, mazungumzo ya amani na njia nyingine za kidiplomasia katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa ndani na nje ya mipaka yake na ndio maana imefanikiwa kuondoa mizizi ya vita vya kikabila na migogoro kwa kuunganisha makabila takriban 126 na kutumia lugha moja ya Kiswahili kama lugha ya Taifa.

 

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania imeendelea na utamaduni wa kuwapatia hifadhi mamia ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka nchi jirani na zaidi na kwa sasa Tanzania inahifadhi wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi wapatao 237,997 huku wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

 

Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe.Yoko Kamikawa umehudhuriwa na Mawaziri, washirika wa TICAD, wawakilishi na waandaaji wenza -Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Benki ya Dunia, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na mashirika ya Kimataifa na kikanda, sekta binafsi na  Kiraia kutoka Japan na Afrika.

 

 

 

 

 

 

 

 






Friday, August 23, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAPAN

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji alipofika ofisini kwake jijini Tokyo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Tisa wa ngazi ya Mawaziri wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika utakaofanyika nchini huko tarehe 24-25 Agosti, 2024


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji alipomtembelea ofisini kwake jijini Tokyo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Tisa wa ngazi ya Mawaziri wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika utakaofanyika nchini huko tarehe 24-25 Agosti, 2024


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akizungumza alipomtembelea Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji ofisini kwake jijini Tokyo. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akifuatilia mazungumzo hayo


Mazungumzo yakiendelea






Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb) amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Kyoto Tsuji ofisini kwake jijini Tokyo.

Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan kwa manufaa ya pande mbili.

 
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Chumi aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, uwekezaji, elimu, na afya.

Amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha inaongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati yake na Japan na hivyo kuchochea ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya pande zote mbili.

Naye, Mhe. Tsuji ameelezea utayari wa Japan kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya nchi hizo.

Amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuongeza biashara na bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana.

Mhe. Chumia yuko nchini Japan kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ngazi ya Mawaziri utakaofanyika jijini Tokyo tarehe 24-25 Agosti 2024.

 

TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA WA TOKYO KUHUSU MAENDELEO YA AFRIKA




 

Thursday, August 22, 2024

BALOZI KOMBO AKIPONGEZA KITUO CHA DKT SALIM AHMED SALIM KWA KUTOA MAFUNZO YA STADI ZA UONGOZI NA MAJADILIANO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekipongeza Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa kutoa mafunzo yenye lengo la kuwanoa vijana katika masuala ya uongozi hususan kwenye stadi za Uongozi na Majadiliano. 

 

Mhe. Balozi Kombo ametoa pongezi hizo leo Agosti 22, 2025 alipokitembelea Kituo hicho ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kujitambulisha, kufahamu majukumu yake pamoja na kuangalia maendeleo ya mradi wa jengo la vyumba vya mihadhara.


Akizungumza na wanafunzi kutoka Taasisi za Umma na Sekta binafsi wanaoshiriki mafunzo ya muda mfupi kuhusu stadi za Uongozi na Majadiliano chuoni hapo, Mhe. Waziri Kombo amewataka kuzingatia mafunzo hayo ambayo yatawajenga katika masuala ya uongozi, uzalendo na majadiliano, fani ambazo ni muhimu katika ulimwengu wa sasa wa kutumia diplomasia na uhusiano na mataifa mbalimbali kunufaika kiuchumi.


Amesema washiriki hao wana bahati kubwa kupatiwa mafunzo katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ambacho pia baadhi ya wakufunzi wake ni Mabalozi na Wanadiplomasia wabobevu  kwenye masuala ya uhusiano wa kimataifa na Diplomasia kwa ujumla.


“Kwenu ninyi washiriki wa mafunzo haya mna bahati kubwa ya kufundishwa na wanadiplomasia nguli akiwemo Balozi Modest Mero ambaye ni miongoni mwa wanadiplomasia waliowahi kuhudumu kwa nafasi ya kuiwakilisha nchi yetu katika Umoja wa Mataifa nchini Marekani. Hivyo, Balozi Mero kwa wasifu wake ni fursa kubwa kwenu washiriki kupokea elimu ya masuala ya stadi za uongozi na majadiliano”, amesema Mhe. Kombo.


Wakati wa ziara hii Mhe.Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo hicho, Mhe. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dkt. Felix Wandwe ndc, baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Kituo hicho na Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.


 

Wednesday, August 21, 2024

WAZIRI KOMBO AAGANA NA BALOZI WA UFARANSA NA USWIS HAPA NCHINI.

Waziri wa Mambo ya Nje ma Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameagana na aliyekuwa Balozi wa Ufaransa Mhe. Nabil Hajlaoui na Balozi wa Uswisi Mhe. Didier Chassot ambao wamemaliza muda wao wa uwakilishi hapa nchini.


Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwa nyakati tofauti katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam Mhe. Balozi Kombo amempongeza Mhe. Nabil Hajlaoui kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.


“Mhe. Balozi Hajlaoui nakupongeza sana kwa kazi kubwa, nzuri na ya mfano, uliyoifanya hapa nchini, hasa katika eneo la kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa, kwakweli hongera sana na nikutakile kila la heri huko uendako,” alisema Balozi.


Naye Mhe. Balozi Hajlaoui ameshukuru kwa ushirikiano alioupata wakati wote alipokuwa nchini na hivyo kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi bila ya kikwazo chochote na kuahidi kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania huko aendako.


Katika tukio lingine akiagana na Balozi wa Uswisi anayemaliza muda wake nchini Mhe. Didier Chassot Balozi Kombo amemshukuru na kumpongeza kwa kushiriki kikamilifu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi katika kipindi chake cha uwakilishi.


Amemuahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa ushirikiano kwa ajaye na kuendelea na kukamilisha masuala mbalimbali ya ushirikiano aliyoyaanzisha.


Naye Mhe. Chassot ameishukuru Wizara kwa ushirikiano mzuri iliyompatia wakati wote wa uwakilishi wake hapa nchini na kuahidi kuwa atayaendelea mazuri yote alyojifunza alipokuwepo hapa nchini.


 

Tuesday, August 20, 2024

WAZIRI KOMBO APOKEA MWALIKO WA RAIS SAMIA KUSHIRIKI JUKWAA LA FOCAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amepokea mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushiriki Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping utakaofanyika mwezi Septemba 2024 jijini Beijing nchini China. 


Mwaliko huo umewasilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, pia umeainisha  nafasi ya kipekee kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzungumza katika kikao cha ufunguzi kwa niaba ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na kuzungumza Katika Mkutano wa Ngazi ya Juu utakaojadili mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa.


Akipokea mwaliko huo kwa niaba ya Mhe. Rais, Mhe. Balozi Kombo ameelezea kuwa nafasi ya Mhe. Rais kushiriki na kuzungumza katika Jukwaa hilo itaipa nchi fursa ya kuangazia uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla,  hali ambayo itasaidia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania ni kinara na kiongozi wa kupigiwa mfano kwenye Jumuiya hiyo kongwe Afrika.


Aidha Balozi Kombo amemhakikishia Balozi Chen ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC ambapo Tamko la FOCAC na Mpango Kazi wa FOCAC itakuwa ni moja ya Matokeo ya Mkutano huo. 


Naye Balozi wa China Mhe. Chen ameelezea kufurahishwa kwa China kutokana na kupokelewa kwa mwaliko wa kuhudhuria Mkutano na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na China.


Amesema China inaona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na kuahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania. 


Jukwaa la Focac lilianzishwa kwa lengo la kukuza ushirikiano kati ya China na Afrika ili kuchagiza maendeleo kupitia sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. 


FOCAC limekuwa jukwaa linalotoa fursa sawa kwa pande zote mbili kujadili masuala muhimu ya kimaendeleo na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo amani na usalama na mabadiliko ya tabia nchi.





Monday, August 19, 2024

RAIS MNANGAGWA AKABIDHI ENEO LA UJENZI WA MAKUMBUSHO YA UKOMBOZI WA AFRIKA


Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa amezindua ujenzi wa Makumbusho ya Urithi wa Afrika na kukabidhi eneo la hekta moja (1) kwa ajili ya uhifadhi wa historia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika linalotambulika kama Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC au “SADC Liberation Square” 


Mhe. Mnangagwa alikabidhi Kituo hicho rasmi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, ambapo kilipokelewa kwa niaba na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi na kueleza kuwa Kituo hiko kitachangia juhudi za Kanda za kuenzi michango ya Wapigania uhuru katika harakati za ukombozi na pia ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kuenzi Waanzilishi wa SADC.


Kwa upande wake, Mhe. Mnangagwa alikiri kuwa Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC kitachangia uhifadhi wa historia muhimu za ukombozi ambazo zinaendelea kuandaliwa chini ya mpango wa kujenga Makumbusho ya SADC jijini Gaborone na ule wa kujenga Makumbusho ya Urithi wa Afrika nchini Tanzania. Hali kadhalika, Mhe. Mnangagwa alizialika nchi wanachama za SADC kuchangia katika kuboresha Kituo hicho kwa kuwasilisha zana za Sanaa kutoka nchini mwao zinazoelezea historia ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.


Makabidhiano ya eneo hilo yameenda sambamba na ziara ya kutembelea eneo la mradi pamoja na zoezi la kupanda mti ambao ulipandwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Magosi na kushuhudiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki ziara hiyo akiwemo, Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mtukufu Mswati III, Mfalme wa Eswatini, Mhe. Andry Rajoelina, Rais wa Jamhuri ya Madagascar, na Mhe. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Jamhuri ya Botswana.


Ziara hiyo ilikuwa ni muendelezo wa ratiba ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 Agosti 2024. Akihutubia katika hafla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuwaenzi wanaharakati wa kweli na wana wa Afrika waliojitoa muhanga katika kupigania ukombozi wa nchi zao. Hivyo, ni heshima kubwa kwa mataifa yetu kutambua mchango wao na kuona fahari kuienzi historia yetu.


Aidha, Wakuu hao wa nchi na Serikali walitembelea pia Kituo cha uchakataji taka cha Geo Pomona cha jijini Harare ambacho awali kilikuwa dampo na baadae  kuanza kuchakata taka kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme sambamba na kutoa ajira mbalimbali kupitia shughuli za kituo hicho.


Mradi huo una uwezo wa kukusanya taka ngumu zenye uzito wa tani 1000 na kuzaliwa kiasi cha Megawati 16 hadi 22 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya Taifa kwa matumizi ya umma wa Zimbabwe.


Akihutubia katika uzinduzi huo, Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa eneo hilo awali lilikuwa limekithiri kwa uchafu na wingi wa taka na hivyo kupatikana kwa teknolojia bora na ya kisasa ya kuchakata taka imesaidia kutunza mazingira kwa kuteketeza taka hatarishi pasipo kuleta madhara ya kiafya kwa bianadamu, mimea, wanyama na mazingira kwa ujumla.


“Zimbabwe imeweka ahadi ya kukiendeleza na kukisimamia kituo hiki ili kiwe cha mfano katika kuitengeneza kanda ya kijani kwa kutunza mazingira na kuzalisha umeme” alisema Mhe. Mnangagwa.


Aidha, alieleza kuwa miradi kama hii ni sehemu ya jitihada za ubunifu unaohitajika ili kuiletea Jumuiya ya SADC maendeleo na akasisitiza ni vyema kuendelea kuwa wabunifu katika kila sekta kwa kuwa ni wazi kuwa kila nchi itajengwa na wenye nchi na sio kinyume chake.

====================================

Habari katika picha; Matukio yaliyojiri wakati wa uzinduzi wa eneo la Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika

Sehemu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walioshiriki katika ziara ya kutembelea eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika na Kituo cha kuchakata taka vilivyopo Harare, Zimbabwe tarehe 8 Agosti, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa akihutubia katika ziara ya ujumbe wa SADC kwenye kituo cha kuchakata taka tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe

Mhe. Mnangagwa akimkabidhi Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi eneo la ujenzi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika ambaye alipokea kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Mhe. Magosi akipanda mti katika eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika.


Mratibu wa Masuala ya SADC kitaifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akimwagilia mti uliopandwa katika eneo hilo la mradi unaoashirikia "umoja na mshikamano katika kanda" wakati wa hafla ya uzinduzi wa eneo hilo.


Matukio mengine yaliyojiri katika kituo cha kuchakata taka