Monday, July 29, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: UJIO WA WAZIRI MKUU WA THAILAND


220px-Coat of arms of Tanzania.svg f1f71


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, anatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam kesho, tarehe 30 Julai, 2013 mchana kwa ziara ya siku tatu nchini Tanzania  kwa mwaliko wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Bibi Shinawatra, ambaye atatokea Msumbiji, atalakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na mwenyeji wake, Rais Kikwete, na kupigiwa  mizinga 19 kwa heshima yake.

Wakati wa adhuhuri, Waziri Mkuu wa Thailand atafanya mazungumzo rasmi na Rais Kikwete, Ikulu na baadaye kutia saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Thailand.

Kabla ya kuhudhuria dhifa ya Taifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake, Ikulu, Bibi Shinawatra, ambaye anafuatana na ujumbe wa wafanyabiashara takriban 70 wa Thailand, atahutubia mkutano wa Uwekezaji wa Biashara kati ya Thailand na Tanzania kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, ambao utahudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Thailand na wawekezaji wa ndani (Tanzania), Wanadiplomasia, Wasomi na Viongozi mbalimbali kutoka serikalini. Katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Thailand ataelezea sera ya uchumi ya nchi yake kwa Tanzania na Bara la Afrika. Baada ya hapo, Waziri Mkuu huyo atazuru maonyesho ya biashara hotelini hapo.

Katika siku ya pili ya Ziara yake, Mgeni huyo wa Taifa atatembelea Mbuga ya Wanyama ya Serengeti mkoani Mara, ambako atajifunza namna Mamlaka za Tanzania zinavyosimamia na kutunza Hifadhi za Taifa za Wanyamapori. Waziri Mkuu Shinawatra atakabidhi Vifaa mbalimbali vya kupambana na majangili kwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi za Wanyama (TANAPA).

Mgeni huyo atarejea Dar es Salaam tarehe 1 Agosti na kuagwa na mwenyeji wake, Rais Kikwete kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kuelekea nchini Uganda.

IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
DAR ES SALAAM
Julai 29, 2013


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.