Thursday, October 8, 2015

Kaimu Katibu Mkuu azungumza na waandishi wa Habari kuhusu Wiki ya Umoja wa Mataifa

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Simba Yahaya (wa pili kutoka kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa. Pamoja kwenye picha ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi.Mindi Kasiga (wa pili kulia). Mwingine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Celestine Mushy (wa kwanza kulia) 
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez, naye akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani). 
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Maafisa wa Umoja wa Mataifa nao wakifuatilia mkutano huo pamoja na waandishi wa Habari (hawapo pichani)
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi.Mindi Kasiga (kulia) akiwafafanulia jambo waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mkutano ukiendelea.

Picha na Reginald Philip


Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, Watanzania wamehimizwa kuweka mbele suala la amani kuliko kitu kingine chochote. Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Simba Yahaya na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Mataifa ambapo kwa Tanzania, kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Siku ya Jumanne tarehe 13 Oktoba 2015.



Kwa upande wake, Bw. Rodriguez alieleza kuwa wakati Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 70 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1945, dunia imeshuhudia kuidhinishwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)  na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja huo  ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Milenia (MDGs) yanayofikia kikomo mwaka huu.



“Utekelezaji wa malengo hayo ambao utaanza mwaka 2016 na kukamilika mwaka 2030, unatarajiwa kumaliza umasikini nchini Tanzania  na duniani kwa ujumla”. Bw. Rodriguez alisikika akisema. Aidha, alisema kuwa UN Tanzania itasaidia utekelezaji wa malengo hayo kupitia Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo wa Awamu ya Pili (United Nations Development Assistance Plan- UNDAP II). Mpango huo pamoja na mambo mengine, unalenga kusaidia ukuaji wa uchumi shirikishi, kuhamasisha demokrasia, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendeleza huduma za kijamii.



Hivyo, Mratibu Mkazi wa UN aliwaomba waandishi wa habari kuelimisha umma wa Tanzania kuhusu SDGs na kuwasihi kuandika habari zitakazodumisha na kuendeleza amani nchini Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Hassan Simba Yahaya naye aliungana na Mratibu Mkazi wa UN kusisitiza umuhimu wa kutunza amani. Alisema kuwa bila ya amani hakuna kitu chochote cha maendeleo kinachoweza kufanywa. Alitoa mfano wa nchi ambazo zimetekeleza MDGs kwa mafanikio makubwa lakini nchi hizo sasa zimerudi nyuma kwa kukosa amani. 

Vilevile aliwafahamisha waandishi jinsi Tanzania ilivyoshiriki kuandaa malengo hayo ambayo yamezingatia pale yalipoishia malengo ya milenia. Amesema Serikali imeshayawekea mpango wa utekelezaji ambao umezingatia mpango wa maendelea wa miaka mitano wa Serikali.

Aliongeza kuwa lengo la 16 la Maendeleo Endelevu linalozungumza kuhusu amani ndio msingi mkubwa wa vipaumbele vya nchi ya Tanzania. 

"Nafarijika kuona kuwa wengi wenu mliohudhuria mkutano wa leo ni vijana, na hii dunia tunayoitaka kwenye malengo haya ni yenu, ni wajibu wenu kuitunza na sio kuibomoa" alisema na kuongeza kuwa utekelezaji wa SDGs una faida kubwa kwa vijana na taifa kwa ujumla.
Description: https://blogger.googleusercontent.com/img/proxy/AVvXsEifwmjYKS-gMfl_aN9z6GJdGmF04LrzwSY57xswSgnf6JIjFGu8jqWxjD6KtulC3AYA2xtAczb5j-PanN8N3O05RH8fehgpRg8sRRGHDDlPZnKuqBFYy2uJEepBKXXLBONwgygu3Nsi7rVanNtcUK2fs9uY7MR-HM_PZ-Im=s0-d-e1-ft

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.