Wednesday, October 7, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
 


Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600         

              

 

                   
       20 KIVUKONI FRONT,
 P.O. BOX 9000,
      11466 DAR ES SALAAM, 
              Tanzania.

 


Taarifa zaidi ya Mahujaji kutoka Tanzania huko Saudi Arabia

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa masikitiko makubwa imepokea majina mengine matatu ya Mahujaji kutoka Tanzania waliofariki dunia kufuatia tukio la mkanyagano wa Mahujaji lililotokea eneo la Mina, Makkah tarehe 24 Septemba, 2015. Vifo vya Mahujaji hao vinafanya idadi ya Watanzania waliofariki kufuatia tukio hilo kufikia watu kumi na moja (11) hadi sasa.

Majina ya Mahujaji hao ambao wametambulika baada ya kupitia taarifa zao za vidole zilizotolewa na Serikali ya Saudi Arabia ni Bw. Yusuf Ismail Yusuf kutoka kikundi cha Khidmat Islamiya, Bi. Rahma Salim Suweid kutoka kikundi cha Ahlu Daawa na Bw. Issa Amir Faki.

Aidha, Ubalozi unaendelea kushughulikia taratibu za mazishi kwa mahujaji ambao wamefariki dunia na miili yao kutambuliwa. Tunapenda kufafanua kuwa mali za marehemu ikiwemo mizigo waliyokuwa nayo wakati wa Hijah zitawasilishwa nyumbani Tanzania na vikundi walivyokuja navyo na kukabidhiwa kwa jamaa wa marehemu.

Vile vile, Ubalozi unaendelea kufuatilia orodha mpya ya taarifa za vidole iliyotolewa na Serikali ya Saudi Arabia kwa ajili ya kuwabaini Mahujai wa Tanzania ambao bado hawajatambuliwa.

Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Saudi Arabia inaendelea kukamilisha zoezi la kuchukua taarifa za vinasaba (DNA) vya Mahujaji wote waliokufa na kujeruhiwa katika ajali hiyo na imeshauri wale wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao kupima vinasaba (DNA) ili kuwabaini jamaa zao.

Pia, kwa vile mchakato wa kuwatambua wahanga wa ajali hiyo ni mgumu na unachukua muda, Wizara inawaomba Watanzania kuwa na subira katika kipindi hiki ambapo taarifa zaidi kuhusu wapendwa wetu zikiendelea kutolewa.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
07 Oktoba, 2015


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.