Friday, October 23, 2015

Tanzania na Malawi zawasilisha Rasimu ya Azimio kuhusu Watu wenye Ualbino

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa  Balozi Tuvako Manongi akifurahia jambo na Bi Ikponwosa Ero mwenye Ualibino mara  baada ya mazungumzo yao  ambapo walibadilisha mawazo kuhusu pamoja na mambo mengine,   changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino na namna gani jumuiya ya kimatifa inaweza kushirikiana katika kuzikabili changamoto hizo. Bi Ikponwosa  aliteuliwa mwezi Agosti Mwaka huu na  Kamisheni ya  Haki za Binadamu  ya Umoja wa Mataifa kama  Mtaalamu huru anayeendesha kampeni,  uhamasishaji, uelimishaji  na  uwezeshaji kuhusu watu wenye ualibino na changamoto  zinazowakabili  watu wenye ualibino. Bi Ero ni   Mzaliwa wa Nigeria mwenye uraia wa Canada.
 
Na  Mwandishi Maalum, New York

Kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ualibino, Wakilishi za Kudumu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi katika Umoja wa Mataifa, zimewasilisha rasimu ya azimo kuhusu watu wenye ualibino.

Rasimu ya azimio hilo inalenga katika kuzishawishi na kuzitaka Jumuiya ya Kimataifa kuendelea na juhudi za kutetea haki na ustawi wa watu wenye ualibino ikiwa ni pamoja na kuliwanda.

Azimio hilo limewasilishwa kupitia Kamati ya Tatu ya Utamaduni,  Haki za Binadamu na Jamii ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  na ambalo limekwisha kusambazwa kwa nchi wanachama na wadau wengine kwa ajili ya kupata maoni na kuungwa mkono.

Azimio hilo linajielekeza pia katika kusisitiza upatikanaji wa fursa za elimu, huduma za afya na ajira kwa watu wenye ualibino, maeneo ambayo ni changamoto kubwa kwa watu hao.

Kupitia azimio hilo, Tanzania na Malawi,  zinaitaka Jukumuiya ya Kimataifa kuunga  mkono jitihada zinazofanywa na nchi ambazo tayari zimejiwekea sera, sheria na mipango ya pamoja na  mambo mengine, kuwalinda watu wenye ualbino na kuwapatia fursa mbalimbali za maendeleo kama raia wengine.

Vile vile, azimio hilo linamwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  kuwasilisha taarifa kuhusu hali za watu wenye ualibino mkazo ukiwa katika changamoto wanazokabiliana nazo,  na juhudi ambazo zimechukuliwa na nchi wanachama katika kuzikabili.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu inaombwa kuwasilishwa wakati wa Mkutano wa  71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chini ya ajenda ya Maendeleo ya Jamii.

Azimio hilo pia linasisitiza haja na umuhimu wa kutambua juhudi zinazofanywa katika ngazi ya nchi na Ki- Kanda, na hivyo Katibu Mkuu anaombwa kuwasilisha katika Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa,  mapendekezo ya namna ya kuimarisha uwezo na juhudi za nchi husika katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la  watu wenye ualibino kwa kadri nchi hizo zitakavyoomba.

Katika sehemu ya utangulizi wa Azimio, Azimio linatambua juhudi mbalimbali na taarifa za vyombo vingine kama Vile Baraza la Haki za Binadamu, Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuhusu haki za watu ,kuzuia vitendo viovu na ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino.

Azimio linaeleza hofu dhidi ya uovu wanaofanyiwa watu wenye ualibino wakiwamo wanawake na watoto.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.