Thursday, October 22, 2015

Taarifa kwa Vyonbo vya Habari


Taarifa zaidi kuhusu Mahujaji kutoka Tanzania waliofariki au kujeruhiwa huko Saudi Arabia

Mahujaji wengine wawili kutoka Tanzania ambao walikuwa hawaonekani tokea ajali ya kukanyagana kwa mahujaji ilipotokea Makkah nchini Saudi Arabia tarehe 24 Septemba 2015 wametambuliwa kuwa, ni miongoni mwa mahujaji waliofariki  dunia. Kutambuliwa kwa mahujaji hao kunafanya idadi ya mahujaji wa Tanzania waliopoteza maisha katika ajali hiyo kufikia ishirini na saba (27). Majina kamili ya mahujaji hao ni Bw. Juma Yussuf Bakula na Bw. Ahmad Awadh Namongo kutoka Kikundi cha Ahlu Dawaa.
Hadi sasa mahujaji kumi na tatu (13) kutoka Tanzania bado hawajulikani walipo na jitihada za kuwatafuta bado zinaendelea.

Kwa upande wa mahujaji wanne ambao walikuwa wanapatiwa matibabu kutokana na kuugua au kujeruhiwa, mmoja wao ni Bw. Mustafa Ali Mchina ambaye alikuwa amelezwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika mji wa Maddinah alifariki dunia tarehe 17 Oktoba 2015 na kuzikwa Maddinah siku hiyo hiyo. Bi. Mahjabin Taslim Khan ambaye alijeruhiwa katika ajali hiyo na kusababisha kukatwa mguu wake amepata nafuu na alirejea nchini tarehe 20 Oktoba 2015. Mwingine ni Bi. Hidaya Mchomvu ambaye alijeruhiwa pia bado yupo hospitali akiendelea kupatiwa matibabu. Hujaji wanne ni Bw. Ahmed Abdallah Jusab ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo alifanyiwa upasuaji wa kumuwekea kifaa cha kuongeza mapigo ya moyo tarehe 19 Oktoba 2015 na alitarajiwa kurejea nchini tarehe 21 Oktoba 2015.
 
Serikali ya Saudi Arabia inaendelea kutoa taarifa zaidi za kuwatambua mahujaji waliofariki dunia au kujeruhiwa katika ajali hiyo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu wahanga wa ajali hiyo kadri itakapokuwa inazipokea.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
22 Oktoba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.