Sunday, October 11, 2015

Silaha za maangamizi zisiishie mikononi mwa makundi ya kihalifu –Tanzania

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzani katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi, akichangia majadiliano kuhusu upokonyaji wa silaha na usalama wa kimataifa  mwishoni mwa wiki, ambapo ametoa wito wa jumuiya   ya kimataifa  kushirikiana katika kuhakikisha kuwa silaha za maangamizi haziishii mikononi mwa makundi ya kihalifu.


Na Mwandishi Maalum, New York

TANZANIA imetoa  wito Kwa    Jumuiya ya Kimataifa wa kuhakikisha  inashirikiana  kuhakikisha kwamba silaha za maangamizi  zikiwamo za nyukilia  haziiangukii  mikono ya  makundi ya kihalifu.

Wito huo  umetelewa mwishoni mwa wiki na  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika  Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi,wakati wa Mkutano kuhusu masuala ya   uponyaji wa silaha na  usalama wa kimataifa.

Katika  mkutakno  huo  wazungumzaji wengi walieleza wasiwasi wa  kuwapo kwa  ushirikiano wa karibu kati ya nchi ambazo zina  silaha za nyukilia na zile ambazo hazina, lakini huku zile ambazo zinamiliki silaha hizo zikiendelea kuziboresha na kujilimbikizia.

 “Ni jambo la kusikitisha, badala ya   kuzipungua silaha hizi na hatimaye kuzitokomeza kabisa,  nchi zinazolimiki silaha za nyukilia zinaendelea na kasi ya kuziboresha , kuzifufua na  kujilimbikiza”. Akasema  Balozi Manongi.

Akabainisha kuwa  mbaya Zaidi hata zile  nchi ambazo hazina silaha hizo nazo sasa zinatafuta kila maarifa ya kuwa nazo. Jambao  ambalo  amesema  ni  tishio kwa usalama wa mwanadamu.

Amesisitiza  kuwa ingawa ni  miongo saba imekwisha kupita lakini madhara ya matukio  ya Hiroshima na Nagasaki bado  yanaendelea na yapo  hai  miongoni mwetu.

Balozi  Manongi akaongeza kuwa ni muhimu basi utokomezaji wa  silaha za  nyukilia na teknolojia inayoambatana nazo likaendelea kupewa  kipaumbele pamoja na kuwa na mikataba ya kisheria itakayosimamia  jambo hilo.

Akasema  kutoka na  ongezeko la  ulimbikizaji wa silaha za nyukilia,  Jumuia ya kimataifa inawajibu wa kushirikiana kuhakikisha kwamba silaha hizo na nyingine za maangamizi haziangukii mikononi mwa  makundi ya kigaidi na  kihalifu.

Pamoja na ukweli kwamba silaha za nyukili na zingine za maangamizi  bado ni tishio kubwa kwa uhai wa mwanadamu. Balozi Manongi akasema kwa nchi zinazoendelea  tatizo la usaambaji na matumizi holela ya silaha ndogo na nyepesi  zinaendelea kuwa janga kubwa kwa ustawi na maendeleo ya bara hili  na  kwingineko.

Akimnukuu  Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa  Kofi Annan kwamba  madhara yatokanayo na  matumizi  holela ya silaha  ndogo na nyepesi yameendelea kuwa makubwa sana   na madhara yake  ni makubwa  pengine  kuzidi   mabomu ya atomic yaliyoiangamizia  Hiroshima na  Nagasaki.

Akizungumzia zidi kuhusu matumizi holela ya silaha ndogo na nyepesi,   Mwakilishi huyo wa Tanzania  anasema  mirindimo ya risasi  na   hata  matumizi ya silaha kali zikiwamo za maangamizi,  haiwezi  au haitamhakikishia   mwananchi   maisha yenye hadhi, utu, ustawi na maendeleo.

Akasema kuna uhusiano  mkubwa baina ya  Amani, usalama na utekelezaji wa Malengo ya maendeleo endelevu y (Agenda 2030) malengo yanayojikita katika kumaliza  umaskini pasipo kumwacha yoyote nyuma pamoja na kuilinda sayari dunia.

Akasema  itakuwa   vigumu kuyatekeleza malengo  mapya ya maendeleo   kama kiwango cha gharama za kujilimbikiza silaha kitaendelea ambapo inakadiriwa kuwa  mataifa hasa yale makubwa  yanatumia Zaidi ya dola za  kimarekani trillion 1.7 kwa mwaka  kwa matumizi ya silaha.

Akasema  matumizi ya kiasi hicho cha fedha kujilimbikizia silaha katika maghara mbalimbali duniani   huku mamilioni ya watu wakiendelea kuishi katika umaskini  uliopindukia, na maelfu ya watoto wakiathirika kwa utapia mlo na wengine wakipoteza maisha kwa kukosa  chakula na huduma nyingine za msingi ni jambo lisilo kubalika.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.